Migomo hii isiyoisha kwanini ufumbuzi unashindikana?

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
Migomo imekuwa inaitesa sana Serikali yetu hasa katika miaka hii ya karibuni. Migomo imetikisa sekta ya Elimu na Afya na pia imeligusa kundi la wafanyakazi kwa ujumla wao, madai makuu yakiwa haki zao za msingi zikiwemo posho,

nyongeza za mishahara na marupurupu mengine kulingana na mikataba ya kazi na kwa mujibu wa sheria.
Misukosuko hii kila inapojitokeza, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kufanyia kazi madai hayo ili kuweza kumaliza

mambo hayo kwa njia ya amani. Lakini bado tunajiuliza, kama kweli suluhisho la kudumu linatafutwa, mbona halipatikani? Na kama ahadi zipo katika kutatua madai ya watumishi hawa, kwanini hazitekelezwi?

Tunafikia hatua kuuliza maswali hayo kwa sababu pamoja na matatizo ya kada hizi kujulikana na kuwekwa mezani, bado utekelezaji wake unasuasua jambo ambalo linasababisha migomo kulipuka na kuleta athari kubwa hasa kwa watu

wasio na hatia wakiwemo wagonjwa mahospitalini na wale wanaofuatilia tiba pasipo mafanikio.
Mgomo mkubwa wa madaktari ulilipuka mwezi Februari mwaka huu. Wakati bado wananchi hawajasahau machungu ya

mgomo ule ambao ulileta mtafaruku nchi nzima na hata kupoteza maisha ya watu, tayari mgomo mwingine umetangazwa na sasa umeanza kimya kimya.
Ni kweli kwamba katika mgomo wa awali Serikali ilikubaliana na madai yote nane ya madaktari ikiwemo nyongeza ya

mishahara, posho katika mazingira magumu, posho za nyumba na mikopo ya magari. Mazungumzo juu ya utekelezaji wa madai hayo bado yanaendelea kupitia kamati teule ya madaktari na Serikali.

Kama kweli mambo yanakwenda sawa katika majadiliano hayo, kwanini mgomo mwingine tena katika muda mfupi kiasi hiki? Kwa mfano, katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, jana walionekana wauguzi wakitoa huduma hasa kitengo cha

wagonjwa wa dharura huku wengine wakiwaagiza wagonjwa wanaosubiri upasuaji wale chakula kwa kuwa shughuli hiyo haitafanyika. Madaktari hawakuonekana.

Hii ikiashiria kuwepo kwa mgomo baridi ingawa Serikali imewatahadharisha madaktari nchini kuacha kugoma kwa kuwa inashughulikia madai yao. Pia imewakumbusha madaktari kuhusu adha wanayopata wagonjwa na wananchi kwa jumla

pale wanapogoma kutoa huduma mahospitalini kinyume na kiapo cha kazi yao.
Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi akitoa kauli ya Mawaziri Bungeni wiki hii, ameeleza kwa kina mgomo wa madaktari uliopita na hatua iliyofikiwa na Serikali katika kushughulikia madai yao.

Lakini inavyoonekana, bado wanataaluma hao hawajaridhika na utekelezaji uliofikiwa. Hata hivyo, pamoja na kuwasihi madaktari wetu wavute subira, Serikali pia inapaswa kuliona suala hilo kuwa ni dharura hasa ikielewa kuwa watakaoumia katika mgomo huu ni wananchi wasio na hatia na ndio walioiweka madarakani. Lazima ifanye hima kuokoa jahazi hili kunusuru maisha ya ndugu zetu.

Hii ni dosari kubwa ndani ya Serikali yetu. Wakati hili la madaktari likichemka, tayari walimu nao wanapiga kelele na Shirikisho la Wafanyakazi nchini(TUCTA) limetishia kuitisha mgomo nchi nzima kushinikiza Serikali kupunguza kodi ya

pato kwenye mshahara(Paye) na kupandisha kima cha chini hadi kufikia 200,000 kwa mwezi.
Zimwi hili la migomo nchini mwetu yafaa litokomezwe sasa. Kwanini ufumbuzi ushindikane na nchi ina rasilimali tele? Serikali yetu inatakiwa ijipange vema kuangalia njia sahihi ya kuepuka migomo hii. Kama inakubali kuwa madai ya

watumishi hawa ni ya msingi, basi ifanye hima kuhakikisha kuwa ufumbuzi wa haraka unapatikana ili kelele hizi ziishe.
Taifa linakuwa halina afya kama kelele za aina hii zinasikika halafu hazipatiwi ufumbuzi wa kudumu. Katika bajeti yake

ya maendeleo, Serikali inatakiwa itenge fedha za kutosha katika sekta nyeti kama Afya na Elimu ili kuondoa matatizo kama migomo hii inayoathiri sekta zingine za maendeleo.

Ifikie wakati sasa tukatae migomo hii isiyo na tija kwa taifa letu. Vinginevyo italijengea taswira mbaya taifa kwamba ni sehemu ya maisha kumbe ni mambo yanayopaswa kuzuiwa kabla ya kutokea. Tusirithishe kizazi chetu kasumba ya

migomo hasa baada ya kuona madhara yake kwa uchumi na taifa kwa jumla. Migomo inadhoofisha nguvu kazi ya taifa na hivyo kuzorotesha maendeleo, tuizuie.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom