SoC01 Michezo ya kupeana hela ilivyomnufaisha Isa mchoma mishikaki wa Ufukwe wa Coco

Stories of Change - 2021 Competition

Uchumi wa Mifugo

JF-Expert Member
May 20, 2021
345
575
Asubuhi ya jumatatu ya tarehe 26 Julai 2021 ilinikuta nikiwa kwenye ufukwe wa Coco,macho yangu yalikuwa yanaitazama fukwe hiyo maarufu nchini huku upepo mkali ukivuma kutokea baharini,meli na boti zikikatiza nyingine zikitokea usawa wa bandari ya Dar es salaam na nyingine zikielekea, pia zipo zilizokuwa zimetia nanga wakati huo ambapo maji yalikuwa yamekupwa.

Upande mwingine kwenye mchanga niliwaona watoto sita waliokuwa wanacheza mpira muda ambao walikuwa wanatakiwa wawe darasani,walipomaliza kucheza mpira walielekea kuogelea,walipomaliza kuogelea walivaa sare zao wakapita karibu yangu nikawaita nikawauliza mbona hawakwenda shule?walinipa majibu ya ubabaishaji nikawaacha.

Pembeni yangu alikuwepo Isa Sospeter kijana mchoma mishikaki wa hapo Coco akaniambia mimi nilipenda sana kusoma lakini mazingira ya nyumbani kwa baba yalinikwamisha nikamuuliza ilikuwaje?
Isa aliamua kunisimulia safari ya maisha yake kwa kirefu;
Isa mkazi wa Msasani na mzaliwa wa Ilemela mkoani Mwanza alizaliwa mwaka 1997 mama yake ana watoto watatu lakini kila mtoto ana baba yake Isa ndiye kifungua mimba. Alipokuwa na miaka minne wazazi wake waliachana, Isa alibaki na mama yake baba yake alielekea Musoma. Tangu hapo maisha ya Isa na mama yake yalikuwa magumu lakini mama yake alipambana na kuhakikisha Isa anakua na anapata elimu yake ya msingi. Baada ya kumaliza darasa la saba katika shule ya msingi Nyamwilolelwa baba yake Isa alimfuata na kumtaka aende Musoma ambako angemtafutia shule ya upili,Isa na mama yake hawakuwa na kipingamizi kwani Isa alitaka kusoma.

Isa alivyofika Musoma alikutana na mama wa kambo ,Isa alikaa mwaka mmoja bila kwenda shule mama wa kambo alitia ngumu Isa kusoma kwa sababu kazi za nyumbani kama kupika,kufua,kufanya usafi zisingefanyika.Isa ilibidi aende kushtaki kwa rafiki wa baba yake kuwa alienda Musoma kwa ajili ya kusoma lakini mwaka umekatika bila kupelekwa shule.Rafiki huyo wa baba yake aliingilia kati na Isa akapelekwa shule ya kutwa lakini alikuwa anatakiwa aamke saa kumi na moja asubuhi afanye kazi zote za nyumbani kama kupika,kufua nguo za mdogo wake,nguo za baba yake na nguo za mama yake ndiyo aende shule. Isa alikuwa kama mtumishi wa ndani ambaye alikuwa hapewi ujira wake.

Pia alikuwa anaenda shule bila kupata kifungua kinywa na wala alikuwa hapewi hela yoyote ya kununulia angalau andazi,Isa alikuwa anashinda siku nzima shuleni bila tumboni kutia kitu chochote.Maisha hayo yalimfanya Isa awe mchovu na darasani alikuwa analala muda wote.

Alipofika kidato cha pili alisoma kwa miezi miwili tu chokochoko zilianza mama wa kambo alimuambia baba yake Isa kuwa hataki kusikia habari za shule na kama anataka Isa asome basi amtafutie sehemu ya kuishi,Isa anasema wakati huo mama wa kambo anataka yeye asisome lakini baba yake alikuwa anamsomesha mtoto wa huyo mama ambaye alimkuta ,mtoto huyo alikuwa anasoma shule ya bweni.

Huo ulikuwa mwanzo wa Isa kuishi maisha ya kuhangaika na kutaabika kwani ukawa mwanzo wa yeye kuwa mtumishi wa ndani kwa kufanya kazi zote za ndani kutengeneza barafu na ubuyu na kwenda kuuza.Maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wake hali iliyomfanya mwaka 2011 atoroke na kuelekea Nyamagana Mwanza kwa rafiki yake aitwaye Kulwa ambaye alikuwa fundi umeme.Aliishi kwa Kulwa huku akimsaidia kazi yake ya umeme mpaka alipokutana na Jamila mkazi wa Msasani Dar es salaam.Isa alikuwa anamfahamu Jamila muda mrefu kwani mama yake Jamila ni mkazi wa Mwanza,Jamila alikuwa ameenda Mwanza kumsalimia mama yake ndipo alipokutana na Isa.

Jamila alimuahidi Isa kuwa kama angekubali kwenda naye Dar es salaam angempa kazi ya kuuza duka mshahara ungekuwa shilingi 150,000 kwa mwezi pamoja na kumpeleka chuo cha ufundi kujifunza ufundi na udereva wa magari.Lakini haikuwa hivyo Isa alikuwa mtumishi wa ndani wa Jamila kwa mshahara wa shilingi 50,000 kwa mwezi.Baada ya kufanya kazi kwa Jamila kwa muda aliamua kuacha na kwenda kufanya kazi kwa mama mwingine aitwaye mama Salum ambako alikuwa anafanya kazi ya kupika kwenye mgahawa ulioko Msasani, mshahara wake ukiwa shilingi 60,000 kwa mwezi lakini nako hakufanya kazi kwa raha kwani alikuwa anapata matatizo ya kuumwa mara kwa mara akaamua kuondoka na kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine akiwa hana pa kulala.

Isa aliniambia kuwa alipoondoka kwa mama Salum alikuwa analala nje ya geti la Don Bosco na wakati mwingine karibu na baa ya Coco wanakokodisha maboya ya kuogelea. Nilimuuliza walinzi walikuwa hawakufukuzi?Isa anasema ilibidi ajenge mazoea na walinzi na wao walikuwa wanamuacha alale.Maisha ya kulala nje Don Bosco na Coco yaliendelea mpaka alipopata kazi kwenye nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na mzee Ubuga iliyopo Msasani ambako alikuwa analipwa shilingi 5000 kwa siku kazi yake ilikuwa kufua mashuka na kazi nyingine za usafi. Lakini nako mambo hayakwenda vizuri kwani alisingiziwa kuwa ameiba simu za wateja ikabidi afikishwe kituo cha Polisi cha Oysterbay ambako alilala kituoni kwa siku saba mpaka rafiki yake Abel alipokwenda kumuwekea dhamana.Isa alisema hakuiba simu ila watoto wa mzee Ubuga hawakupenda yeye afanye kazi pale kwa sababu walimuona kikwazo kwa wao kuiba hela za mzee wao hivyo ikabidi wamtengenezee zengwe na wakafanikiwa.Baada ya kutoka kwa mzee Ubuga Isa alikuwa hana pa kulala ilibidi arudie makazi yake ya Don Bosco na Coco.

Katika kuhangaika huku na kule alibahatika kupata kazi ya
kusaidia kuchoma mishikaki kwa Saleh aliyekuwa anachoma mishikaki kwenye ufukwe wa Coco ambako alikuwa analipwa shilingi 10,000 kwa siku za kawaida na shilingi 12,000 kwa siku za sikukuu na mwisho wa juma,kwa kawaida Coco kunakuwa na wateja wengi siku za sikukuu na mwisho wa juma hivyo malipo kwa mfanyakazi nayo yanaongezeka kwani huwa wanachoma mishikaki mingi tofauti na siku za kawaida.
Baada ya kufanya kazi kwa muda kwa Saleh aliamua kuacha kulala nje Don Bosco na Coco na hivyo kutafuta chumba Msasani.

Baada ya kufanya kazi kwa Saleh na kupata uzoefu wa kutosha wa kuchoma mishikaki Isa alimuomba Saleh amtafutie sehemu ya kuchoma mishikaki ili aweze kuchoma mishikaki yake mwenyewe Saleh hakuwa na kinyongo kwani alimuambia Isa kuwa yeye atamuachia eneo lake kwa sababu alikuwa na mpango wa kuacha kazi ya kuchoma mishikaki na kuondoka Dar es salaam,baada ya muda walikabidhiana eneo kupitia ofisi ya mtendaji wa eneo lao na Isa akaanza kuchoma mishikaki yake.Isa aliniambia hakupata shida ya wateja kwa sababu aliwarithi wateja wa Saleh ambao walikuwa wanamfahamu.

Nilimuambia Isa kuwa Saleh alikuwa mtu mzuri sana kwake kwa sababu alimfundisha kuchoma mishikaki pia alimuachia eneo lake la biashara,Isa alinijibu "Niliweka bidii sana ya kazi pia nilikuwa nawahi sana kazini kwa ajili ya kufanya usafi na maandalizi mengine pia nilimuheshimu sana Saleh,heshima na nidhamu ndiyo kila kitu na hiyo ndiyo sababu Saleh alinipenda na kuniachia eneo lake kirahisi kwani angeweza kumpa mtu mwingine" Isa anachoma mishikaki ya kilo tatu,kilo moja nyama ya nundu na kilo mbili nyama ya steki kwa siku za kawaida, ananunua steki sh.10,000 na nundu shilingi 13,000 kwa kila kilo moja,pia ananunua mkaa wa shilingi 3000, tangawizi,mafuta ya kula,chumvi na ndimu za shilingi 3500,bunda saba za sitiki za kuchomea mishikaki kwa shilingi 7000.Kwenye kilo tatu anapata mishikaki 600,kila mshikaki anauza shilingi 300,analipa mfanyakazi shilingi 10,000,analipa wafanya usafi shilingi 3000 kwa kila juma pia walinzi wanalipwa shilingi 15,000 kila juma.Isa aliniambia kwenye kilo tatu anapata faida ya shilingi 120,000.Alivyoniambia hivyo nilistuka nikamuuliza inawezekana vipi nyama za shilingi 33,000 apate faida ya 120,000.
Isa alisema anakata vipande vidogo vidogo vinavyotoa mishikaki 200 kwa kila kilo moja na kila mshikaki unakuwa na vipande vidogo vitatu,alivyonionyesha mishikaki yake niliamini.

Siku za sikukuu,jumamosi na jumapili Isa anachoma hadi kilo tano za nyama.

Isa pia anacheza mchezo wa kupeana hela ambapo kila siku anatoa shilingi 10,000 na wapo watu 100,Isa aliniambia mchezo huo umemnufaisha sana kwani ameweza kumpa mama yake shilingi 1,000,000 kwa ajili ya kufanya biashara ya kuuza dagaa na samaki Mwanza na pia ameweza kununua viwanja viwili vilivyopo Ilemela na ana mpango mwezi wa tisa kununua kiwanja kingine Chanika au Kisarawe kwa ajili ya kujenga nyumba yake ya kuishi.Isa aliniambia kuwa mchezo huo wa kupeana hela kila siku umemfanya awe makini na biashara yake na pia awe na matumizi mazuri ya fedha zake kwani hataki kukosa hata siku moja kutoa hela za mchezo.

Pamoja na mafanikio hayo madogo Isa hajamsahau mama yake anasema huwa anamtumia shilingi 40,000 kila juma kwa ajili ya matumizi ,nilimuuliza inakuwaje anamtumia hela wakati alimpa mtaji,Isa alisema anafanya hivyo ili mama yake asitumie hela za biashara ,anataka azihifadhi kwani ana malengo nazo.

Isa pia anafanya biashara ya kuuza matunda iliyopo Gongolamboto stendi ambako ameajiri kijana wa kumuuzia,matunda ananunulia kwenye soko la Temeke sterio na mengine ananunua kwenye soko la Buguruni.Isa alisema aliamua kufungua biashara ya matunda baada ya soko la mishikaki kuyumba baada ya kuingia kwa ugonjwa wa Korona kwani baadhi ya wateja wao ni wageni wanaotoka nje ya nchi pamoja na baadhi ya Watanzania walikata mguu kwenda Coco kwa kuogopa ugonjwa huo hatari.Lakini kwa sasa Isa anasema angalau kuna nafuu ingawa kabla ya ujio wa Korona walikuwa wanauza kilo tano mpaka sita za nyama kwa siku za kawaida na siku za sikukuu,jumamosi na jumapili walikuwa wanauza hadi kilo nane za nyama.
Biashara zote mbili za matunda na nyama zimemuwezesha Isa kusaidia ndugu zake,kupiga hatua kimaendeleo na kuajiri vijana wenzake wawili.

Isa alisema hakuna biashara au kazi yoyote inayoingiza fedha isiyo na changamoto,alisema kuna wakati mishikaki inalala "unaanda mishikaki 600 ambayo unategemea kupata shilingi 180,000 lakini unauza mishikaki 100 unaishia kupata shilingi 30,000 inapotokea hivyo unapata hasara ingawa hali hiyo haitokei mara kwa mara.Pia changamoto nyingine ni wateja wakorofi wakitukuta hapa tunapigwa na vumbi na jua wanajua tuna njaa sana,kuna watu wanadharau sana hasa wasichana wanaoendesha magari na vijana wasomi na wengine wanafunzi wa vyuo, wengine wakija hapa na magari yao ukiwakimbilia kwa ajili ya kuwakaribisha wanakutukana" Namuambia lakini ndiyo wateja wenu hao inabidi muwavumilie Isa alisema"Ndiyo hivyo tunawavumilia kwa sababu mimi nataka hela yake tu,wewe njoo na dharau zako lakini nipe hela yangu.Kuna wateja wengine wanakuja wanakula halafu hawataki kulipa au wanalipa hela pungufu,kwahiyo changamoto zipo lakini tunazikabili".

Pamoja na changamoto hizo Isa anaifurahia kazi yake na anataka siku moja arudi shule kwani ana ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa awe anapeleka bidhaa nje ya nchi "unajua bila kujua kiengereza au nikiendelea kuwa na elimu hii niliyonayo nitashindwa kufanikiwa kwenye biashara kubwa hasa za kupeleka bidhaa nje ya nchi,hivyo mipango yangu ikikaa sawa nitarudi shule" alisema Isa.

Isa anawashauri vijana hasa wasomi wasione haya kufanya biashara ndogo ndogo kwani baadhi zinataka mtaji mdogo lakini zina faida kubwa "kwenye biashara yoyote kinachotakiwa ni uzoefu na uzoefu unapatikana baada ya kuvumilia,mtaji si kitu kikubwa kwani mtaji unaweza kupewa au kukopeshwa lakini uzoefu hakuna mtu anayeweza kukupa au kukukopesha,uzoefu ni lazima ujifunze,uvumilie shida na changamoto mbalimbali.Hata biashara iwe ndogo kiasi gani lakini uzoefu ni muhimu vijana wenzangu wanatakiwa wajifunze kwanza biashara wanazotaka kuzifanya,waende hata kwa watu wajifundishe kwa kusaidia kazi,unaposaidia kazi hata kama hulipwi lakini kuna kitu kikubwa utajifunza,utajifunza jinsi biashara hiyo inavyofanyika,malighafi zinakopatikana,msimu wa biashara kwani biashara inabadilika badilika haiwezi kuwa sawa kuanzia Januari hadi Disemba kuna miezi wateja wanakuwa wengi, kuna miezi wateja wanapungua kiasi na kuna miezi wateja wanapungua sana,pia utajifunza jinsi hali ya hewa inavyoathiri biashara unayotaka kuifanya kwani wakati wa mvua ni tofauti na wakati wa kiangazi au wakati wa joto ni tofauti na wakati wa baridi.Pamoja na hayo nidhamu,uaminifu na bidii ni vitu muhimu ili ufanikiwe kwenye biashara yako"alisema Isa.

Pamoja na Isa hakupata malezi bora kutoka kwa baba yake lakini anatamani kuwa na familia na kuwa baba bora"nguvu niliyo nayo leo nataka kuitumia vizuri ili familia yangu iishi vizuri,nilipotoka napajua,naipigania leo na kesho yangu ili niwe na familia bora,sitaki watoto wangu wapate shida na changamoto nilizopitia mimi"alisema Isa.
 
Na wewe kwanini Jumatatu asubuhi haukua kazini? ?😂😂

Unabaki kuuliza watoto hawajaenda shule Na kuhoji wenzako walio kazini (Joke)

Stori nzuri kiongozi. Biashara nyingine watu wanazidharu sana ila pengine ndo zina hela kuliko maelezo
Ni kweli kabisa ,Tena hawalipi Kodi yoyote mtu anapata 100,000-120,000 kila siku lakini halipi Kodi, walikuwa wanalipa 20,000 ya vitambulisho vya Magufuli lakini sasa havipo.
 
Kujiajiri ni suluhisho la ukosefu wa ajira nchini lakini kabla ya kujiajiri ni muhimu kujifunza kwa undani kiti unachotaka kukifanya.
 
Nasema hivi kilo moja huwezi toa mishikaki 200, hata kama italingana size ya sisimizi!!huo ni uongo kiwango cha SGR, yaani vipande 600!!!hahaaa hiyo ya 500 tu, ikitoka 40, ni midogo kweli, kwa hiyo kilo moja!!!sembuse 200?!!
Tembelea Coco Beach uone ile mishikaki yao,ukubwa wake ni Kama punje ya Hindi.
 
Huu mchezo wa kupeana pesa umesaidia wengi sana. Wakati wa Ukoloni, makuli bandarini walilipwa kwa siku nao walianza mchezo wa kupeana na ndiyo uliwasaidia kupata viwanja Kariakoo, Magomeni mpaka Mwananyamala.
 
Huu mchezo wa kupeana pesa umesaidia wengi sana. Wakati wa Ukoloni, makuti bandarini walilipwa kwa siku nao walianza mchezo wa kupeana na ndiyo uliwasaidia kupata viwanja Kariakoo, Magomeni mpaka Mwananyamala.
Njia nzuri ya kuweka akiba lakini Inabidi wahusika wawe waaminifu.
 
Back
Top Bottom