Miaka zaidi ya kumi tokea hotuba hii itolewe – Muungano ni kero ?

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1][/h]Written by Mrfroasty (Ufundi) // 21/02/2012 // Habari // No comments


MAELEZO VA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS DKT. 0. A. JUMA,
KATIKA MAZUNGUMZO NA MABALOZI WA TANZANIA WALIOKO NCHI ZA NJE,
KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA MUUNGANO
WHITE SANDS HOTEL TAREHE 20 APRILI, 1999
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Mabalozi, Mabibi na Mabwana.
SHUKURANI NA PONGEZI
Kwanza kabisa napenda kwa dhati kukushukuru wewe Ndugu Mwenyekiti kwa
kunipa heshima ya kuja kuzungumza na Mabalozi wetu walioko nchi za nje
pamoja na viongozi wa Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, katika mkutano ambao naambiwa unafanyika baada
ya kipindi cha miaka 12 kwani mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1987. Kwa
maana hiyo pamoja na kukushukuru kwa kunishirikisha ningependa nikupongeze
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa jitihada zako zilizosaidia kuwezesha kikao
hiki kifanyike. Ni matumaini yangu kwamba pamoja na matatizo yetu ya
kiuchumi, lakini utaratibu huu wa kuwapa nafasi Mabalozi wetu walioko
nchi za nje kuja na kujifunza mambo na mabadiliko yanayotokea nchini
ni vyema uendelezwe kwani naamini unawasaidia sana Mabalozi wetu katika
kutekeleza majukumu yao makubwa kwa maslahi ya Taifa hill.
Binafsi nimefarajika sana kushiriki katika kikao hiki. Kwanza kimenipa
nafasi kwa mara ya kwanza kuonana na kujuana na Mabalozi wetu wote ambao
wengine tulikuwa hatujaonana tokea nichaguliwe kushika nafasi hii. Aidha
kwa sababu kuundwa upya Ofisi ya Makamu wa Rais ni moja kati ya mabadiliko
ambayo yametokea katika kipindi hiki ambapo hamkuwa na vikao vya aina
hii. Kwa hiyo ni nafasi nzuri ya kuwajulisha Mabalozi majukumu mapya ya
Ofisi ya Makamu wa Rais. Kuundwa ofisi mpya ya Makamu wa Rais kunatokana
na mabadiliko ya Kumi na moja (11) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ambayo yaliondoa utaratibu wa zamani wa kuwa na Makamu wa Rais wawili
na kuweka muundo wa kuwa na Makamu wa Rais mmoja katika uongozi wa nchi
yetu. Kutokana na mabadiliko haya pamoja na Makamu wa Rais kuwa Msaidizi
Mkuu wa Rais lakini Ofisi ya Makamu wa Rais pia imekabidhiwa majukumu
yafuatayo:
1. Kuratibu mikakati ya kuondosha umasikini nchini.
2. Hifadhi na Utunzaji wa Mazingira.
3. Kuratibu shughuli za vikundi visivyokuwa vya Serikali (NGOs).
4. Kuratibu shughuli za Muungano.
Ndugu Mwenyekiti,
Shughuli zote hizo zina umuhimu mkubwa kwa uhai na maendeleo ya
nchi yetu. Kutokana na uchache wa muda sikusudii kujadili mbinu
za utekelezaji wa rnajukumu hayo yote lakini ninawashauri Mabalozi
wakati wakiwa hapa waonane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
ambaye atawapa maelezo na ufafanuzi zaidi juu ya malengo na mbinu za
utekelezaji wa majukumu haya.
UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA MUUNGANO
Ndugu Mwenyekiti, Kwa vile ajenda ya utekelezaji wa shughuli za Muungano
nayo ni pana na ni vigumu kwa muda niliopewa kuzungumzia utekelezaji
wa shughuli zote za Muungano nimeona nigusie mambo ambayo yatawasaidia
Waheshimiwa Mabalozi kuelewa hali ilivyo sasa katika utekelezaji wa
shughuli za Muungano. Nitagusia mambo yafuatayo:
1. Jitihada za Serikali zote mbili kuondoa mambo yanayoleta vikwazo
katika utekelezaji wa shughuli za Muungano.
2. Taarifa ya utekelezaji wa MUAFAKA uliofikiwa na Serikali zote
mbili mwaka 1994.
3. Ufafanuzi kuhusu nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Jamhuri ya
Muungano baada ya mabadiliko ya Kumi na moja (11) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano.
4. Mchango ambao Mabalozi wa Tanzania walioko nje wanaweza kusaidia
katika kuimarisha Muungano.
5. Maoni kuhusu hatima ya Muungano wetu.
JITIHADA ZA SERIKALI ZOTE MBILI KUONDOA MAMBO YANAYOLETA VIKWAZO KATIKA
UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA MUUNGANO
Ndugu Mwenyekiti,
Naamini Waheshimiwa Mabalozi wanaelewa kwamba ingawa Muungano wetu umedumu
kwa miaka 35 sasa, lakini katika vipindi mbali mbali tokea kuasisiwa
kwa Muungano wetu kumekuwepo madai, malalamiko, manung’uniko, pamoja
na kushutumiana upande mmoja umevunja Katiba au hautekelezi mapatano ya
Muungano kama nchi mbili zilivyokubaliana. Wakati mwingine hali ilikuwa
mbaya kiasi cha kuhatarisha uhai wa Muungano wenyewe. Mengi ya kero
na malalamiko yameshughulikiwa na mengine kupatiwa ufumbuzi lakini kwa
vile matatizo bado yako na yanaendelea kulalamikiwa na pande zote mbili,
nimeona ni vyema nikumbushe yale madai na manung’uniko makubwa kutoka
pande zote mbili za Muungano:
Upande wa Zanzibar
a) Dai kubwa Ia Zanzibar ni kwamba haifaidiki ipasavyo na fursa na
haki zake za Mamlaka ya Utaifa “Sovereignty” kama inavyofaidika Serikali
ya Tanzania Bara (Tanganyika) ambayo ndiyo inayohodhi Mamlaka ya Utaifa
“Sovereignty” hiyo. Tanzania Bara inapata misaada mikopo, ruzuku kutoka
nchi rafiki na Mashirika ya Kimataifa kwa jina Ia Tanzania lakini
Zanzibar haimo. Wakati huo huo Zanzibar hairuhusiki kuwasiliana moja kwa
moja na nchi au Mashirika hayo kwa mambo yanayohitaji Mamlaka ya Utaifa
“Sovereignty”. Madai hapa ni kwamba Zanzibar ilikuwa na Mamlaka ya Utaifa
“Sovereignty” yake kabla ya Muungano, Mamlaka hayo ndio yaliyounda Mamlaka
ya Utaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikawa (One Sovereignty
Republic) Serikali ya Muungano. Kwa hiyo Zanzibar ina haki kufaidika na
Mamlaka hayo kwa mambo yote ya Muungano kama inavyofaidika Tanzania Bara.
b) Dai Ia pili Ia Zanzibar linahusu mahusiano ya kiuchumi baina
ya Serikali mbili. Uchumi si suala Ia Muungano, lakini nyenzo kubwa za
uchumi, hasa Sera za uchumi na Kifedha (Monetary and Fiscal Policies)
ni mambo ya Muungano. Hapakuwekwa utaratibu mzuri vipi uchumi wa Zanzibar
unaweza kufaidika au kufidiwa wakati zinapotokea athari zinazosababishwa
na hatua za marekebisho ya uchumi zinazochukuliwa na Tanzania Bara. Siku
za nyuma ikifanyika kwamba SMT inapunguza thamani ya sarafu ya Tanzania,
kuongeza viwango vya riba vya Mabenki, kupunguza matumizi katika sekta
ya umma au kuondoa fidia (subsidy) kwa nyenzo, vifaa na malighafi
zinazotumika sehemu zote za Muungano bila kushauriana na SMZ. Tatizo
kubwa zaidi katika masuala ya uchumi ni utata uliokuwepo kuhusu Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) na nafasi ya Zanzibar katika Benki hiyo. Sasa upo
muelekeo suala hili litapatiwa ufumbuzi mara Zanzibar itakapokubali kuwa
mteja wa Benki hiyo kwa kuweka akaunti zake za Serikali.
c) Kuhusu Mambo ya Nje, kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikidai kwamba
kilichokusudiwa kuingizwa katika Muungano ni “External Affairs” kama
ilivyo katika “Articles of Union” na kwa hiyo Uhusiano wa Kimataifa si
shughuli ya Muungano. Zanzibar kwa kutumia uhusiano wa Kimataifa ingeweza
kuwa na mahusiano na ushirikiano na nchi rafiki na kuwa mwanachama wa
Mashirika ya Kimataifa yasiyohitaji “Sovereignty” na kuwa na makubaliano
au mikataba ya Kimataifa kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano.
d) Zanzibar ilidai kwamba Katiba zote mbili za SMT na SMZ zinatambua
kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwepo Rais wa Zanzibar
basi Serikali na Rais wanahitaji kuwa na vielelezo vinavyokubalika
kimataifa (Bendera, Nembo, Wimbo wa Taifa, Rais kupigiwa mizinga 21
anaposafiri nje ya nchi na vielelezo vingine).
e) Manung’uniko mengine kutoka Zanzibar yalihusu uwakilishi katika
vyombo vya Muungano, Mashirika ya Kimataifa na Uwiano wa Mabalozi
na nafasi nyingine. Madai mengine ni pamoja na mambo ya uraia hasa
kutambuliwa kwa sheria ya Mzanzibari, uhamiaji, malalamiko kuhusu
fomula ya kuchangia mambo ya Muungano, miliki ya fedha za kigeni na
mambo mengineyo.
Upande wa Tanzania Bara
a) Hoja za Serikali ya Jamhuri ya Muungano ni kwamba madai mengi ya
Zanzibar yanahoji Mamlaka ya Utaifa “Sovereignty” wa nchi tabia ambayo
inaashiria kukiuka makubaliano ya Muungano, kuvunja Katiba na kuhatarisha
uhai wa Muungano wenyewe.
b) SMT imekuwa ikilalamika kwamba SMZ ina tabia ya kuvunja Katiba
mara kwa mara kwa visingizio ambavyo vingeweza kupatiwa ufumbuzi
katika utaratibu wa matakwa ya Katiba yenyewe (mifano kuundwa vikosi
vya SMZ ambavyo vina sura za kijeshi, kupokelewa wageni Zanzibar na
kupigiwa mizinga 21, kuingiza vifungu katika Katiba ya Zanzibar ambavyo
vinagongana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, uongozi wa Zanzibar kutoa
maagizo ya ajira au “posting” kwa nafasi za ofisi za Ubalozi na ofisi
ndogo ya Mambo ya Nje iliyopo Zanzibar kinyume na taratibu, Zanzibar
kujiunga na OIC n.k.).
c) Kuhusu mahusiano ya kiuchumi mara nyingi SMZ inakuwa haiko
tayari kufanya mageuzi ya kiuchumi inapohitajika kufanya hivyo. Kwa vile
uchumi si mambo ya Muungano, SMT haina madaraka kuingilia mambo hayo,
matokeo yake Sera za kiuchumi na fedha za Serikali mbili huwa haziendi
pamoja. Kwa muda mrefu SMZ haikuwa tayari uchumi wake ufanyiwe uchunguzi
na World Bank/IMF ili SMZ nayo ifaidike na program za Mashirika hayo,
lakini wakati huo huo ikubali masharti yanayotolewa na Mashirika hayo
ya fedha. Kuhusu SMZ kufaidika na fursa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
tatizo ni kwamba SMZ bado haikuhamishia akaunti zake za Serikali katika
Benki hiyo. Ili SMZ ipate fursa zote za BoT lazima iwe ni mteja wa Benki
hiyo kama ilivyo SMT.
d) SMT inadai kwamba mara nyingi Zanzibar inayachukulia matatizo ya
utekelezaji wa shughuli za Muungano kisiasa, wakati mambo mengi hasa ya
uchumi, fedha, mabenki ni mambo ya kitaalamu ambayo yanahitaji ushauri
wa kitaalamu. Hali hii inafanya madai mengi ya Zanzibar yafanywe na
wanasiasa ambao hutumia hoja za kisiasa badala ya utaalamu unaohitajika
kufanikisha shughuli inayolalamikiwa.
e) SMT inaamini kwamba matatizo ya kero nyingi au zote zinaweza
kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mikutano ya pamoja, mashauriano ya kidugu na
kuwepo nia nzuri “political will” ya kila upande kuelewa hoja za upande
mwingine. SMT inadhani kwamba tabia ya kulalamikia mambo ya Muungano nje
ya utaratibu (magazeti, uchochezi wa kisiasa na malumbano) kunazidisha
hali ya mvutano kwa mambo ambayo yanaweza kumalizwa kabisa.
Ndugu Mwenyekiti,
Mengi kati ya madai ya pande zote mbili ni mambo ya zamani na
yameshughulikiwa na yanaendelea kushughulikiwa na Serikali zetu kwa nia
ya kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA KUSHUGHULIKIA KERO ZA MUUNGANO
i) Katika mwaka 1977 ulianzishwa utaratibu wa mashirikiano baina
ya Serikali mbili. Wizara na taasisi zote zilitakiwa ziwe na vikao vya
mashirikiano.
ii) Kuchukua hatua za haraka sana za kudhibiti kuchafuka kwa hali
ya hewa ya Kisiasa iliyojitokeza Tanzania Zanzibar mwaka 1984.
iii) Iliteuliwa Tume ya Chama mwaka 1984 iliyoongozwa na Dr. Salmin
Amour (sasa Rais wa Zanzibar)
iv) Rais aliteua Tume ya Rais ya Mapato na Matumizi ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1991 ikiongozwa na Ndugu
E. I. M. Mtei.
v) Rais aliteua Kamati ya Wataalam ya kushughulikia mambo ambayo
ni vikwazo katika shughuli za Muungano ya mwaka 1992 ikiongozwa na Ndugu
W. H. Shellukindo.
vi) Mwaka 1993 Bunge iliishughulikia vizuri Hoja za Wabunge waliojiita
Kundi Ia G55 ambao walidai Muundo wa Serikali Tatu utakaohakikisha kuwepo
kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
vii) Ulianzishwa utaratibu wa uongozi wa Serikali zetu mbili
kukutana. Vikao hivyo viliongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano Ndugu J. S. Malecela na Waziri Kiongozi wa SMZ
Dkt. O. A. Juma. Vikao hivi ndivyo vilivyozaa MUAFAKA baina ya Serikali
mbili.
UTEKELEZAJI WA MUAFAKA
Kutokana na hali isiyoridhisha ya utekelezaji wa shughuli za Muungano
tarehe 28.07.1992 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alichaguwa
Kamati ya Wataalamu iliyongozwa na ndugu W. H. Shellukindo aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati ule, kuiongoza Tume hiyo
ambayo miongoni mwa Hadidu rejea zake ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa
kina na kushauri utaratibu mzuri wa kuondosha kero na vikwazo katika
shughuli za Muungano.
Kamati ya Ndugu Shellukindo ambayo ilikuwa na wataalamu wa juu kutoka
sehemu zote mbili za Muungano ilifanya kazi kubwa sana na ilitoa
mapendekezo ambayo ndiyo yaliyokuwa chimbuko Ia MUAFAKA uliofikiwa na
Serikali zetu mbili mwaka 1994.
Kutokana na majadiliano ya kina na uwazi, tulifikia MUAFAKA kuhusu masuala
mbali mbali ambayo kwa sababu ya uchache wa muda nitaelezea yale maeneo
muhimu tu:
1. MAMLAKA YA UTAIFA “Sovereignty”
Ilikubaliwa kuwa Mamlaka ya Utaifa “Sovereignty” ni moja na
haigawiki. Suala hili ni moja katika makubaliano muhimu sana. Kulikuwa
na mawazo kutokana na madai mengine yaliyosikika kutoka Zanzibar ambayo
nimeyaeleza hivi punde ilijengeka dhana kwamba Zanzibar inadai utaifa
wake. Baada ya mjadala mgumu ilifahamika kwamba Zanzibar haidai Mamlaka
ya Utaifa “Sovereignty” igawanywe, bali inataka iweze kufaidika na fursa
zote na haki ya Mamlaka ya Utaifa “Sovereignty” kwa mambo ya Muungano
kama inavyofaidika Serikali ya Jamhuri. Hivyo ilikubalika utengenezwe
utaratibu maalumu utakaoiwezesha Zanzibar kufaidika na fursa zote za
Mamlaka ya nchi bila kuathiri na kuingilia Mamlaka ya Utaifa “Sovereignty”
yenyewe. Ukweli utaratibu huo bado haujaandaliwa.
2. Katiba
Ilikubaliwa kwamba Katiba zote mbili zipitiwe ili kuondosha vifungu
vinavyosababisha migongano. Hili nalo halijatekelezwa kikamilifu.
3. Mambo ya Nje
Tulikubaliana uandaliwe utaratibu utakaoiwezesha Zanzibar kuwa na
mahusiano ya nchi za nje na vyombo vya kimataifa kwa mambo yasiyokuwa
ya Muungano na ilitakiwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa iandae utaratibu huo. Baada ya kufikia muwafaka kwamba
utaandaliwa utaratibu utakaoiwezesha Zanzibar kufaidika na fursa zote za
kuwa na uhusiano na nchi za nje na vyombo vya kimataifa ilikubalika kwamba
suala Ia uhusiano wa kimataifa liendelee kuwa Ia Muungano. Bahati mbaya
hadi leo utaratibu haujaandaliwa. Pia ilikubaliwa suala Ia Uwakilishi wa
Wazanzibar Makao Makuu ya Wizara, Balozi za nje nalo liwekewe utaratibu
na Ofisi ndogo ya Mambo ya Nje Zanzibar iimarishwe.
4. Mambo ya Sarafu, Fedha na Mabenki
Ulifikiwa muwafaka kwamba Tanzania ikiwa “One Sovereign State” inapaswa
kuwa na:
* Benki Kuu moja (One Central Bank)
* Sarafu moja (One Currency)
* Mamlaka moja ya Masuala ya Fedha (One Monetary Authority)
* Sera moja ya Masuala ya Fedha (One Monetary Policy)
* Udhibiti na Usimamizi wa Mabenki mmoja (Single Authority for Central and Supervision of Banks and Financial Institutions)
Hili limetekelezwa lakini bado kuna tatizo Ia Benki Kuu (BoT) kutoa
huduma kwa Serikali zote mbili, kama ilivyoelezwa hapo awali.
5. Ulinzi na Usalama
* Ilikubaliwa yaendelee kuwa mambo ya Muungano na Rais wa Jamhuri
pekee kama Amiri Jeshi Mkuu aendelee kuwa na Mamlaka ya kuunda majeshi
yote nchini.
* Kikosi cha Kuzuwiya Magendo Zanzibar yaani KMKM kiitwe “Zanzibar
Coast Guard”.
6. Ilikubaliwa Ushuru wa Forodha na Kodi ya Mapato ziendelee kuwa
shughuli za Muungano lakini viongozi wa Wizara mbili za Fedha walitakiwa
waweke utaratibu wa kudumu wa kukutana kabla ya kutangaza bajeti zao ili
wazungumzie na wakubaliane juu ya masuala ya sera na misingi ya bajeti
zao.
7. Misaada, Mikopo Nafuu na Ruzuku
Ilikubaliwa misaada igaiwe kwa kufuata fomula iliyopendekezwa na
mtalam wa IMF ambaye alishauri Zanzibar iwe ikipata asilimia ya 4.5 ya
misaada. Fomula hiyo ilikubaliwa na vikao vya pamoja. Pia ilikubaliwa
Benki ya Dunia ifanye “Sectoral Study” ili miradi ya Zanzibar nayo
iingizwe katika programu za kufufua uchumi wa Tanzania na ziwasilishwe
kwa wafadhili kupitia taratibu za kawaida. Vimejitokeza vikwazo katika
kutekeleza MUAFAKA huu, lakini hivi sasa linashughulikiwa vizuri.
8. Tume ya Pamoja ya Fedha
Ilikubaliwa suala hili ambalo ni Ia Kikatiba litekelezwe. Tume hii ndiyo
yenye uwezo wa kusawazisha matatizo mengi ya mambo ya Muungano, hasa
mahusiano ya Fedha, misaada, mikopo, mapato na matumizi ya shughuli za
Muungano. Ndio pia inayoweza kuamua kiwango cha michango ya Muungano kwa
kila upande. Sheria imeshatungwa na Bunge Ia SMT, sasa imebaki kuundwa
tu. Utekelezaji unasubiri hatua kutoka Zanzibar tu.
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa ufupi nimeona niyataje mambo hayo tu yaliyomo katika MUAFAKA
uliofikiwa baina ya Serikali zetu mbili lakini Kiambatisho Na.II kimetoa
mukhtasari wa mambo yote. Napenda nikiri kwamba manung ‘uniko na madai
yanayoendelezwa kutoka Serikali zetu mbili yanatokana na kutokutekelezwa
kikamilifu MUAFAKA uliofikiwa mwaka 1994. Kuna sababu zilizochangia
MUAFAKA huo usitekelezwe kama ilivyokusudiwa:
1. Harakati na Maandalizi ya uchaguzi wa 1995 ulifanya viongozi
na wataalamu wote washughulikie suala Ia uchaguzi kwa hiyo hapakuwa na
nafasi ya kukutana.
2. Mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa hasa kuondoshwa aliyekuwa
Waziri Mkuu Mheshimiwa J. S. Malecela na kustaafu kwa aliyekuwa Katibu
Mkuu wake Ndugu Shellukindo.
3. Mabadiliko ya Kumi na moja ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
yaliweka utaratibu mpya wa namna ya kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri
na kumtoa Rais wa Zanzibar asiwemo katika uongozi wa Muungano nab hili
limeleta kutokuridhika kwa upande wa Zanzibar ndio maana vinatokea
vikwazo kwa mambo tuliyokwisha kukubaliana.
4. Wapo baadhi ya viongozi na watendaji wa pande zote mbili za Muungano
wenye tabia ya kupenda kuendeleza malumbano na kukwamisha utekelezaji
wa mambo yaliyokubaliwa.
Ndugu Mwenyekiti,
Pamoja na hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudia katika mwaka huu
wa fedha 1999/2000 kulivalia njuga suala hili na kuhakikisha MUAFAKA
unatekelezwa.
UFAFANUZI KUHUSU NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
BAADA VA MABADILIKO YA KUMI NA MOJA NA KUMI NA MBILI YA KATIBA YA JAMHURI
YA MUUNGANO
Kwa sababu suala Ia nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muundo wa sasa
linaweza kuwa kikwazo cha utekelezaji wa MUAFAKA nimeona ni vyema
nilitolee maelezo ili waheshimiwa Mabalozi waelewe undani na ukweli wake.
Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba mabadiliko ya Kumi na moja ya
Katiba ya Jamhuri yalisababisha kuwekwa utaratibu mpya wa namna ya
kumpata Makamu wa Rais na kuweka mfumo wa kuwepo Makamu wa Rais mmoja tu
hivyo kuwaondoa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wasiwe tena Makamu wa
Rais. Chimbuko Ia mabadiliko haya yanatokana na mapendekezo ya Kamati
ya Wataalam iliyoongozwa na Jaji Mark D. Bomani iliyochaguliwa na Rais
kutazama utaratibu unaofaa kumpata Rais katika mfumo wa Demokrasia ya
vyama vingi. Miongoni mwa mapendekezo mengi iliyotoa, Kamati ya Jaji
Mark D. Bomani ilitoa mapendekezo yafuatayo kuhusu nafasi ya Makamu wa
Rais:
(a) Awepo Makamu mmoja wa Rais
(b) Makamu wa Rais achaguliwe, asiwe wa kuteuliwa
(c) Makamu wa Rais atokane na chama kile kile na Rais
(d) Makamu wa Rais achaguliwe kwa kupendekezwa na chama chake wakati
ule ule anapopendekezwa mgombea u-Rais na wapigiwe kura kwa
pamoja; Rais akichaguliwa basi na Makamu awe amechaguliwa.
(e) Makamu wa Rais asiwe Rais wa Serikali ya Zanzibar wala Waziri
Mkuu.
(f) Makamu wa Rais awe ndiye msaidizi mkuu wa Rais katika mambo yote
na hususan:
(i) atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais,
(ii) atafanya kazi zote za Rais kama Rais yuko nje ya nchi
(iii) atamsaidia Rais katika kufuatilia utekelezaji wa Mambo
ya Muungano.
(g) Makamu wa Rais awe mjumbe wa Baraza Ia Mawaziri kwa wadhifa wake.
Mapendekezo haya yalizaa mjadala mrefu pande zote mbili za
Muungano. Zanzibar ilikuwa na hoja zifuatazo:
1. Kumtoa Rais wa Zanzibar katika nafasi ya uongozi wa
Muungano ni kinyume cha mapatano na makubaliano ya Muungano
(The Articles of Union, Ibara (vi) (b)) ambayo ilitaja kuwa
Makamu wa Rais atakuwa ni Mzee Karume Rais wa Zanzibar.
2. Kumtoa Rais wa Zanzibar katika Muungano kutampa nafasi
ya kufanya kazi zake kama Rais kamili na hivyo itabidi awe na
mamlaka, madaraka na vielelezo vyote vya Urais. Hivyo itatoa sura
kuona kwamba Tanzania ina Marais wawili wenye uwezo sawa sawa.
3. Kumtoa Rais wa Zanzibar katika Muungano, Zanzibar itakosa
uwakilishi wa mtu ambaye ndiye mwenye ridhaa ya Wazanzibari
waliomchagua wenyewe.
Kulikuwa na hoja nyingine nyingi. Hoja zilizotolewa na Kamati ya Jaji
Mark Bomani ambazo ndizo zilizokubaliwa zilikuwa kama ifuatavyo:
1. Kutokana na mfumo mpya wa demokrasia ya vyama vingi upo uwezekano
mkubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar wakapatikana
kutoka vyama tofauti vya siasa. Inawezekana pia Waziri Mkuu na Waziri
Kiongozi wakapatikana kutoka vyama tofauti. Pia uwezekano wa vyama tofauti
vikashika uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hivyo hivyo kwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar upo. Huko nyuma viongozi wote walikuwa
wanatoka chama kimoja na wakitekeleza sera na itikadi moja. Kutokana na
ukweli huu halitakuwa jambo Ia busara na manufaa kwa Rais wa Zanzibar
wala Waziri Mkuu kuendelea kuwa Makamu wa Rais.
2. Katika mazingira ya mfumo wa demokrasia si vizuri kuwa na viongozi
wajuu wa nchi wanaoteuliwa. Ni vyema viongozi wa juu wawe wakuchaguliwa
na wananchi. Hivi sasa Rais wa Zanzibar anachaguliwa na wananchi wa
Zanzibar tu na si vyema kulazimisha Rais huyo achaguliwe na wananchi
wa Bara pia, kwani kufanya hivyo itaingilia uhuru na mamlaka ambayo
Wazanzibari wamepewa kikatiba. Kwa misingi hiyo ilipendekezwa Makamu
wa Rais naye awe wa kuchaguliwa na wananchi wakati ule ule wananchi
wanapomchagua Rais wa Jamhuri; Makamu wa Rais achaguliwe wakati ule ule
anapopendekezwa mgombea wa Urais na wapigiwe kura kwa pamoja (Mgombea
Mwenza). Rais akichaguliwa basi Makamu awe amechaguliwa.
3. Hoja ya tatu ilikuwa kwamba utaratibu huu hautavunja mapatano
na makubaliano ya Muungano kwani utaratibu wa kuwa na viongozi wa juu
(Rais na Makamu) utabaki vile vile. Rais akitoka sehemu moja ya Muungano
basi Makamu atatoka sehemu nyingine, kwa maana hiyo siku zote Rais
na Makamu watatoka sehemu tofauti za Muungano. Kwa maana hiyo tafsiri
ya Zanzibar si sahihi kwani tafsiri yao inamaanisha kwamba siku zote
Zanzibar atoke Makamu wa Rais tu. Ukweli ni kwamba Rais wa Jamhuri pia
anaweza kutoka Zanzibar. Zaidi ya hayo, kwa utaratibu huu siku zote
viongozi hao watatoka kutoka chama kile kile kilichotoa wagombea na
wakapigiwa kura na wananchi.
KUHUSU NAFASI VA RAIS WA ZANZIBAR KATIKA MUUNGANO
Mabadiliko ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetoa ufafanuzi wa
Ibara ya 28 ya Katiba, kuhusu viongozi wakuu wa vyombo vyenye mamlaka
ya utendaji katika Jamhuri ya Muungano vilivyotajwa katika Ibara ya Nne
(4) ya Katiba. Viongozi wakuu wanaohusika na ibara hiyo ambayo wametajwa
na Katiba ni kama wafuatao:
(a) Rais wa .Jamhuri ya Muungano
(b) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
(c) Rais wa Zanzibar na
(d) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
Hapana shaka kwamba Rais wa Zanzibar ni mmoja katika viongozi wakuu wa
Jamhuri ya Muungano kikatiba. Pia kikatiba Rais wa Zanzibar ni mjumbe
wa Baraza Ia Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muunyano. Aidha katika
MUAFAKA mambo yafuatayo tulikubaliana
1. Wizara ya Mambo ya Nje ilitakiwa iandae utaratibu wa
Itifaki ya Rais wa Zanzibar hapa nchini na anaposafiri nchi za
nje. Linashughilikiwa.
2. Kuhusu bendera anapokuwa sehemu yoyote ya Tanzania atumie
“Presidential Standard” yake na akisafiri nje ya nchi atumie Bendera
ya Jamhuri ya Muungano na atapigiwa wimbo wa Taifa. 3. Pasiwe na
pingamizi ya Zanzibar kuwa na vielelezo vyake vya Serikali kwa shughuli
zake za ndani ya Zanzibar kama inavyotamka Katiba ya Zanzibar.
4. “Consulates” zinaweza kufunguliwa Zanzibar kwa kufuata taratibu
za kawaida za kidiplomasia.
5. Zanzibar inaweza kufungua “Trade Office” nje baada ya mashauriano
na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
6. Aidha Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa ilipewa
kazi ya kuandaa utaratibu utakayoiwezesha Zanzibar kuwa na mahusiano na
nchi za nje na vyombo vya Kimataifa.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar ni mjumbe wa Baraza la Ulinzi na Usalama
na ana nafasi wakati wowote kukutana na kujadiliana na Rais wa Jamhuri
kuhusu mada yoyote.
Nimeeleza hayo kuthibitisha kwamba pamoja na ugumu wake lakini suala
hili limepatiwa ufumbuzi. Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu shughuli
za Muungano bila kuingilia uwezo na madaraka ya viongozi wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
JITIHADA ZA SERIKALI ZETU KUMALIZA KERO
ZA MUUNGANO
Katika kuendeleza jitihada za kumaliza matatizo ya Muungano, tarehe 2
Mei 1998 na tarehe 6 Agosti, 1998 ujumbe wa Serikali mbili ukiongozwa na
Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. O. A. Juma kwa upande wa SMT na Mheshimiwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Ia Mapinduzi Dkt. Salmin Amour
kwa upande wa SMZ walikutana ili kujadili mbinu za utekelezaji wa mambo
yafuatayo:
1. Mgao wa asilimia 4.5 kwa SMZ kutokana na fedha zinazotolewa na
wahisani.
2. SMZ kuanza kufaidika na huduma na fursa zote za Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
3. Kuharakishwa kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC).
4. Utaratibu wa kusawazisha madeni baina ya Serikali mbili.
5. SMZ kuiachia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ifanye kazi zake
Zanzibar kwa mujibu wa sheria za TRA.
6. Zanzibar kuanzisha utaratibu wa “Pre-Shipment Inspection” kwa
bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na wafanyabiashara binafsi.
7. Matatizo ya Bajeti ya SMZ.
8. Zanzibar kuanzisha kodi ya VAT (limetekelezwa). Mambo haya
yanaendelea kujadiliwa na Serikali zetu mbili na hapana shaka yatapatiwa
ufumbuzi.
MCHANGO WA MABALOZI WA TANZANIA
WALIOKO NJE KATIKA KUIMARISHA MUUNGANO WETU
Ndugu Mwenyekiti,
Mabalozi wetu walioko nje nao wanao mchango mkubwa wa kusaidia kuimarisha
Muungano wetu. Mna wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya pande zote
mbili za Muungano wetu hasa kwa upande wa uchumi, uwekezaji, misaada na
mikopo. Kwa maoni yangu mambo yafuatayo yanahitaji kushughulikiwa kwa
uzito wake:
1. Kwa mambo ambayo si ya Muungano – ya Zanzibar – kuyaelezea vizuri
ili nchi za nje zielewe kwamba Zanzibar inaweza kuwa na uhusiano wa moja
kwa moja na nchi za nje bila ya kupata kibali cha Hazina ya Serikali ya
Muungano wa Tanzania kwa mambo ambayo si ya Muungano. Zanzibar inaweza
kupata misaada, ruzuku kutoka nchi yoyote bila ya kuhitaji kibali cha
SMT.
2. Katika kuitangaza Tanzania hasa katika nyanja za uchumi/utalii,
uwekezaji, n.k. Sehemu zote mbili mipango yake itangazwe sawa sawa. Sasa
hivi Zanzibar inatoa kipaumbele katika azma yake ya kuifanya Zanzibar iwe
kituo cha biashara na fedha, Maeneo Huru, azma yake ya kuwa na Bandari
Huru na suala Ia kukuza utalii. Ili kuondosha malalamiko mabalozi wasaidie
kutangaza malengo hayo.
3. Itifaki ya Rais wa Zanzibar
Naamini miongoni mwenu wapo wenye uzoefu (exposure) wa taratibu za
nchi nyingine, ambazo baadhi yao zina mfumo wa ama moja au nyingine wa
muungano. Nitafurahi kikao hiki kikichangia juu ya suala Ia itifaki ya
Rais wa Zanzibar hasa kutokana na Muundo mpya wa uongozi wa Muungano
wetu.
4. Vile vile Balozi zetu za nje zisaidie kufunguliwa ofisi za
biashara au za kutangaza utalii kila pale ambapo Zanzibar inaamua kufanya
hivyo.
5. Viongozi na Maafisa wa pande zote mbili wanapotembeIea katika
maeneo yenu ya kazi wanastahiki kushughulikiwa na kukaribishwa vizuri
ili waweze kufanikisha kazi zao. Kuna manung’uniko viongozi na watendaji
kutoka Tanzania Zanzibar mara nyingine hawapewi heshima wanazostahiki
wanapokwenda katika Balozi zetu.
6. Ushauri kwa SMZ
Hivi sasa dunia inashuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi na
kibiashara. Serikali zetu zinahitaji ushauri wa mara kwa mara
kutoka ofisi zetu za ubalozi unaohusiana na mabadiliko yanayotokea
duniani. Limejitokeza suala kama Rais wa Zanzibar anaweza kuwa na
mahusiano ya moja kwa moja na ofisi hizo. Kwa maoni yangu, ni vyema
Wizara iweke utaratibu utakaomwezesha Rais wa Zanzibar kupata taarifa
anazotaka kutoka Balozi zetu kwa maslahi ya Tanzania Zanzibar.
Aidha ni vyema Balozi zetu ziwe na utaratibu wa kumpa taarifa Rais wa
Zanzibar juu ya mageuzi makubwa yanayotokea duniani katika nyanja za
uchumi, siasa, utawala bora na mtazamo wa dunia kuhusu mambo mbali mbali.
Ni matumaini yangu kwamba kikao hiki kitajadili maeneo mengine ambayo
Balozi zetu zinaweza kuchangia kuimarisha Muungano wetu.
MAONI KUHUSU HATIMA YA MUUNGANO
Ndugu Mwenyekiti,
Sasa hivi nchini kunaendelea mjadala kuhusu waraka wa Serikali Na. 1
(White Paper) na suala Ia Muundo wa Muungano limepewa nafasi ya kwanza
katika kujadiliwa sehemu zote ambapo Tume ya Rais imepita. Kitu cha kutia
moyo, Ndugu Mwenyekiti, hadi sasa hakuna taasisi, chama cha siasa, vikundi
visivyokuwa vya kiserikali (NGOs) au Mtanzania yeyote aliyesema kwamba
Hataki Muungano wa Tanzania uendeiee kuwepo au uvunjwe. Wako wanaodai
Muundo wa sasa unafaa lakini ziondoshwe kero, wako wanaodai Serikali
tatu, yuko anayetaka Serikali nne (moja ya Tanganyika, moja ya Unguja
moja ya Pemba na ya Muungano), yuko aliyetaka Serikali 26, kila mkoa
uwe na Serikali yake. Narejea tena hayuko anayetaka Muungano usiwepo.
Ni dhahiri kwamba Watanzania wanataka Muungano uwepo. Kwa hiyo ni dhahiri
kwamba hatima ya Muungano wetu ni nzuri.
Kwa maoni yangu mimi ukiacha Muungano wa muundo wa Serikali moja, ambao
hauwezi kukubalika hata siku moja kwa upande wa Zanzibar, kufanikiwa kwa
shughuli za Muungano wowote hakutegemei hata kidogo idadi ya Serikali,
muhimu ni makubaliano juu ya mambo gani yawe katika Muungano na sehemu
zote zinazohusika kukubali kwa dhati kuyatekeleza mambo hayo. Aidha ni
muhimu kuendelea kuwepo nia na dhamira ya kisiasa (political will) ya
kuwa na Muungano kama waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu
Nyerere na Hayati Mzee Karume.
Kwa maoni yangu suala Ia muundo wowote mpya utakaoongeza idadi ya
Serikali unahitaji kufanyiwa “feasibility study” kamilifu kutazama
maslahi ya kiuchumi kwa muundo huo, gharama za kuuendesha Muungano
wa aina hiyo, mgawanyo wa madaraka wa viongozi wa juu na pia ikiwa
Muundo huo unaweza ukadumishwa. Ingelikuwa vizuri wananchi wakapelekewa
miundo ambayo imeshafanyiwa uchunguzi na utafiti wa kina wa kitaalam
ili wafanye uamuzi sio kwa msingi wa kisiasa tu, bali kwa misingi ya
kiuchumi, gharama za kuuendesha, migongano inayoweza kutokea na uhalali
wa kuweza kuudumisha au wepesi wa kuvunjika. Msemo wa kiswahili unasema
“jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza”. Kutamka Serikali tatu,
nne au 26 ni rahisi, lakini kwa sasa hapana anayejua hasa maana yake
nini? Matamshi haya yanafanywa kwa jazba za kisiasa wakati mwingine kwa
hasira na malengo ya kuudhoofisha Muungano huu ambao kudumu kwake kwa
miaka 35 ni jambo Ia kujivunia kwa Watanzania wote.
HITIMISHO
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Mabalozi,
Narejea tena kwamba kwa maoni yangu hakuna muundo wowote wa Muungano
ambao hautakuwa na matatizo au kero. Kwa hiyo kuimarika kwa Muungano
hakutegemei idadi ya Serikali kama inavyodaiwa. Katika kudumisha na
kuimarisha umoja wa aina yoyote mambo yafuatayo ni muhimu:
* Kuwepo dhamira nzuri kwa pande zote mbili kuendeleza Muungano
au umoja huo.
* Kuwepo kuaminiana, kupendana na kila upande kuuheshimu upande
mwingine.
* Pande zote za Muungano kuelewa kwamba Muungano maana yake kila
upande umemega sehemu ya mamlaka yake (sovereignty) na kwa hiyo pande
zote zinastahiki kufaidika na fursa na haki za Mamlaka ya Muungano.
* Kila upande uwe na wajibu wa kutekeleza makubaliano ya Muungano,
sio yale mambo ambayo upande mmoja unayataka tu.
* Viongozi wa pande zote mbili kwa dhati na moyoni waupende
na wakubali kuimarisha Muungano, usiingizwe ubinafsi na kiburi cha
madaraka. Hisia za kila upande kutaka urejeshewe mamlaka yake ya utaifa
mara nyingi huletwa na watu wenye uchu wa madaraka.
* Katiba iheshimiwe na ifuatwe kikamilifu.
* Utaratibu wa kutatua mizozo inayotokea iwe kwa mazungumzo na
kutumia vikao sio kutumia magazeti au kuropoka ovyo tu.
* Mambo ya Muungano yasiwe nyeti na yakaendeshwa kinyemela. Wananchi
wawe huru kuuliza, kujadili, kukosoa na kutoa maoni yao kila wanapoona
haja ya kufanya hivyo.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Mabalozi,
Kwa mara nyingine tena nashukuru kwa fursa hii ya kuzungumza
nanyi. Nashukuru kwa kunisikiliza na kama nilivyosema, Ofisi yangu
inasubiri kwa hamu maoni na mapendekezo yenu juu ya njia za kuimarisha
Muungano wetu.
Ahsanteni.
 
Back
Top Bottom