Miaka saba bila Ngwair? Kasikilize ngoma yake ya mikasi...

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,438
Biti ilianza kunyongwa kama utani na Profesa Ludigo. Baada ya kufika kwenye himaya ya 'Mdachi' P Funk Majani. Akadata. Sikio la tatu la usikivu wa muziki likagundua kuna kitu kinahitajika zaidi kwenye 'biti' ile.

Akapuliza alichovuta. Akacheua alichokunywa. Kwa akili ya sanaa na kichwa chenye nywele za 'Kidachi', mwili uliochorwa chorwa kama kitenge. Akajifungia kwenye studio yake pale Bamaga. Akawasha kiyoyozi na kukamata mashine. Akainyonganyonga 'biti' ya Mikasi. Vinanda vikaimba kuliko Ferouz.
'Biti' ikaunguruma kuliko sauti ya Mchizi Mox. Kikatoka kitu tofauti na Ludigo akasahaulika ghafla. Ni kama Ludigo hakugusa kitu.

Katika wakati wake Majani, studio na kila kitu kilichokuwemo ndani yake kilimtii. Alipoamua kufanya kazi alifanya kazi.

Ilikuwa rahisi zaidi kuingia Ikulu ya Mkapa, lakini siyo kwenye geti jeusi pale Bamaga kwa Majani. Kuingia ndani ya studio yake ilikuwa ufahari kuliko kurekodi.

Ndani ya studio yake lilikuwa eneo lenye heshima tele ya Bongo Fleva kwa wakati ule. Ni sehemu iliyomfanya Joseph Haule aitwe Profesa Jay. Juma Kassim Kiroboto aitwe Sir Nature. Ndivyo ilivyokuwa kwa wengine wengi kama kina Jaymoe, kusahaulika majina yao ya asili waliyopewa na wazazi wao.

Ilikuwa nyumba ya ndoto kwa kila mwanamuziki. Kwanini usiheshimu uwepo wako ndani? Baada ya vurugu za Majani kuijaza 'biti' uzito wa tani saba. Akaitwa mtoto wa Kingoni, mzaliwa wa Moro mwenye makuzi ya mitaa ya Dodoma.

Marehemu Albert Mangweha. Ngwair. Cowbama. Mungu amrehemu. Miongoni mwa binadamu ambao kama ubongo ni ugonjwa mtu ungeomba akuambukize.

Akaachiwa uwanja. Hakufanya makosa, akatambaa nayo.
Ngwair akaitendea haki akili ya ubinifu ya Ludigo na Majani kwenye biti. Akaongelea maisha halisi ya wanamuziki wa wakati ule. Ilikuwa ngumu mwanamuziki wa Bongo Fleva kusubiri kusikiliza taarifa ya habari pindi wanapoamka na hangover za jana yake. Wakiamka ni simu kujua 'bata' iko wapi kwa siku hiyo.

Chaga Bite ilikuwa bar maarufu sana mitaa ya Makumbusho. Wasanii walipenda kukutana pale. Wanafika mapema ni supu kisha mitungi inaendelea. Ndo maisha yao yalivyoendeshwa. Wakati meza za jirani ungeona wanywaji wengine wakiwa na magazeti ya siku hiyo.

Wao ungekutana na pakti za sigara na chupa za pombe. Ilikuwa ngumu sana kukutana na mwanamuziki yuko bize na gazeti ili kujua dunia inaendeleaje. Waliishi kivyao na dunia yao. Mapema tu wengi wao akili zilivurugwa na vimiminika vinavyoongeza akili mpya.

Graveyard lilikuwa eneo tulivu lenye hadhi ya wanamuziki ambao akili na viungo vyao havifanyi kazi bila kupuliza bange. Wakati ule kila siku utasikia msanii kuwekwa ndani kwa kosa la kivuta bange hadharani.
Na Graveyard pale Makumbusho, ilikuwa kama sehemu rasmi ya kukamatwa kwa wanamuziki.

Hawakuwahi kuacha kwenda kwa sababu ya kukamatwa kila siku. Waliendelea kupatukuza kana kwamba wamefunga napo pingu ya maisha ya kuvutia bange.

Atapata wapi wazo la kuulizia kiwanja? Bei ya mfuko wa saruji? Ni ngumu sana. Wengi walipata umaarufu na pesa wakiwa wadogo. Akili ya kuwaza kesho yake ilikuwa kama kibaka na kituo cha Polisi.
Hiki siyo kitu cha kufikirika alichoimba. Ni hali halisi iliyokuwepo.

Na katika mazingira haya ilikuwa jambo la kawaida kufanya mahojiano na waandishi na watangazaji wakiwa bar.

Wengi hawakuona wala kujua umuhimu wa vyombo vya habari. Walikuwa gizani, hawana anuani rasmi ya sehemu ya kupatikana. Popote ilikuwa kambi kwao.
Mwandishi angeweza kumsaka mwanamuziki mwezi mzima ili afanye naye mahojiano.

Hana simu alipoteza kwenye ulevi. Hata mwenye simu kabadili namba kwa sababu muda wa kwenda kurudisha namba ile ile hana. Watapata wapi muda huo wakati wengi wao hata akaunti bank ulikuwa utata?

Ngwair aliimba alichokiishi yeye na wenzake wa wakati ule. Hata msanii mwenye 'singo' moja tu radioni. Bila video wala picha kwenye gazeti. Hakutaka kupanda usafiri wa umma. Tayari alijiona staa anayestahili kujificha.

Kulikuwa na ulimbukeni wa umaarufu. Bajaji wala bodaboda hazikuwepo wakati huo. Taksi ikawa ndiyo usafiri wao.
Pesa ziliteketea kwenye pombe na usafiri.

Kwa wale ambao walikuwa hawana usafiri binafsi wala washikaji wenye 'ndinga'. Ilikuwa kawaida kukodisha taksi kutoka Dar mpaka Morogoro, kwenda kwenye shoo. Hawakujali baadaye yao walichoangalia ni kile kinachowazunguka.

Pesa zao zilitoweka kama ambavyo mvuto wao ulivyotoweka kwa mashabiki. Huhitaji kusumbua kichwa kujua sababu za wasanii wa kipindi kile wengi wao kutoweka kwenye game mpaka katika maisha ya kawaida.

Kasikilize ngoma ya Mikasi ya Ngwair. Ndivyo walivyoishi na ndivyo pesa zao zilivyotoweka. Ziliishia kwenye kaunta za bar maarufu mjini na kumbi za starehe.

Ni Mitungi Branti na Mikasi. Dah!
Rest in peace Cowbama....




Credit: Dk. Levy

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom