Miaka miwili Kikwete Ikulu, tumaini lililopotea

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,791
288,003
Miaka miwili Kikwete Ikulu, tumaini lililopotea

M.M. Mwanakijiji
Tanzania Daima

IJUMAA ya Desemba 21, wiki hii, Rais Jakaya Kikwete, anatimiza miaka miwili madarakani.

Pamoja na fanikio hili binafsi kwake na anguko kwa wananchi, miaka miwili ya Kikwete inaacha maswali mengi kuliko majibu.

Mwaka 2005 akiwa kwao Chalinze, Kikwete aliitangazia dunia alivyokuwa na nia na mikakati ya kuikomboa nchi yetu iliyokuwa imetopea kwenye ufisadi na ubabaishaji.

Aliibuka na kauli mbiumali yenye kuvutia na kushawishi kiasi cha hatimaye kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Rais wa Awamu ya Nne.

Alibuni kaulimbiu - Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya - iliyowapa matumaini mapya watanzania hasa wapiga kura.

Kipindi cha kuelekea uchaguzi, Kikwete na wapambe wake waligeuka gumzo kiasi cha kumfunika Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye umma uliishamchoka na kumchukia kutokana na ubabe wake, kutokidhi matarajio ya umma na kutokuwa na falsafa maalumu ya kuongoza nchi.

Umma ulichoka kuburuzwa na kupuuzwa kiasi cha Kikwete kufanikiwa kuwalaghai wananchi kwa kumlinganisha Mkapa na Farao huku yeye akijilinganisha na Nabii Musa. Rejea ahadi ya kuwapeleka watu Kanani, nchi ya maziwa na asali ambayo baada ya miaka miwili imegeuka kuwa shubiri!

Tathmini yangu ya utawala wa Kikwete inaanza na hitimisho kuwa ni utawala uliofeli linapokuja suala la kukidhi matarajio ya umma na kutimiza ahadi zake huku ukifanikiwa kuwaghilibu wananchi.

Tutatoa sababu. Kwanza Kikwete aliahadi kutengeneza ajira zipatazo 500,000 ndani ya mwaka mmoja. Sasa miaka miwili imeyoyoma ajira hizi hazijatengenezwa wala hakuna dalili ya kufanya hivyo.

Kama Kikwete amefanikiwa kuunda ajira basi ni zile za marafiki zake ambao aliwapa uwaziri, ukatibu wa wizara, ukuu wa mikoa na wilaya huku akijipinga kwa kuunda baraza kubwa la mawaziri tofauti na ahadi yake ya kuunda serikali ndogo na safi.

Kwenye hili Kikwete amefanikiwa kujizungushia marafiki zake ambao mara zote amekuwa akiwalinda wanapoboronga.

Rejea kuendelea kuwamo madarakani kwa mawaziri wanaokabiliwa na shutuma za ufisadi kama Andrew Chenge (mikataba ya uwekezaji hasa kwenye sekta ya nishati na madini), Nazir Karamagi (Buzwagi), Profesa Peter Msolwa (SUA na mikopo ya wanafunzi), Profesa Juma Kapuya (matumizi mabaya ya ndege ya jeshi), Basil Mramba (kuidhinisha malipo ya rada na ndege feki ya Rais) na wengine waliotajwa na Dk. Wilbroad Slaa kwenye mkutano wa hadhara wa wapinzani katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke.

Pili, Kikwete aliahidi angekomesha ufisadi uliokuwa umetamalaki chini ya Mkapa. 'Madudu' kama ANBEN, Fosnik, Tanpower na mengine yalifanywa.

Bila woga, Kikwete amekula yamini kumkingia kifua Mkapa na wenzake huku akiendelea kutapatapa kuwalinda watu wanaotuhumiwa kutumia madaraka kifisadi.

Rejea majina ya watajwa hapo juu bila kusahau makatibu wa wizara (wakurugenzi wa Deep Green), kampuni inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha Hazina na kuyaficha nje ya nchi kwa kushirikiana na Gavana wa Benki Kuu mwenye kila aina ya utatanishi, Daudi Ballali.

Tatu, Kikwete aliahidi angefufua na kuboresha uchumi wetu. Je, uchumi wetu uko wapi baada ya Kikwete kuingia madarakani?
Matumizi ya serikali kubwa na isiyo na nidhamu ya kimatumizi na maadili yamekuwa ndiyo sala ya kila siku. Rejea ripoti ya Mhasibu Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya hivi karibuni juu ya kupotea kwa takriban shilingi trilioni moja za matumizi ya Serikali Kuu na za Wilaya.

Nne, Kikwete aliahidi kutatua mgogoro wa Zanzibar ambao hadi tunaandika makala hii haujulikani mwelekeo wake.

Tano, Kikwete aliahidi Watanzania maisha bora ambayo kwa sasa ni 'bora maisha'. Maana kila uchao hali za watu wetu zinazidi kuwa dhaifu huku sarafu yetu ikizidi kuporomoka ikilinganishwa na zile za majirani zetu ambao hawana hata nusu ya raslimali kama zetu.

Rejea kuvushwa kwa madini yetu hata michanga na kukithiri kwa mikataba yenye utata ya uwekezaji kwenye sekta za madini na nishati.

Rejea ahadi ya kurekebisha mikataba ya madini ambayo imekuwa ikipigwa danadana hadi kuundiwa zaidi ya tume tano za kuirekebisha zisifanye hivyo zaidi ya kula pesa ya umma.

Rejea kauli ya suto na kejeli ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, ambaye hakumung'unya maneno kwa kumwambia Kikwete wazi kuwa asilaumu Canada bali sheria mbovu za utawala wake zinazowezesha kuwapo wa wizi na ufisadi kwenye madini.

Mkapa alilaumiwa sana kwa kupenda kusafiri nje akiandamana na kundi la watu.

Kikwete baada ya kuingia madarakani, watu walitarajia angejifunza kutoka kwa mtangulizi wake kuachana na tabia hii yenye kulitia taifa hasara.

Katika ripoti ya CAG juu ya matumizi mabaya ya serikali iligundulika kuwa ziara za rais na mkewe nje vilisababisha upoteaji wa fedha nyingi. Rejea ziara ya Kikwete mkewe na watoto wake kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Mataifa katikati ya mwaka huu huko New York, Marekani.

Rejea ziara za hasara za kujitambulisha kwenye nchi mbalimbali huku akifanya hivyo hata kabla ya kujitambulisha kwa wapiga kura waliomchagua kwa kishindo cha tsunami iliyogeuka kuwa tsunami ya kimaisha kwa Watanzania.

Sita, Kikwete amefanikiwa kuwaingiza kwenye nafasi za ulaji marafiki zake na hata na ndugu zake, jambo linaloonyesha uchakavu na kutojiamini kisiasa.

Umma umekuwa ukihoji uhalali wa kumteua rafiki yake wa siku nyingi, Edward Lowassa kuwa waziri mkuu, huku wengi wakiwa waasisi wa chama chake (CCM) wakiwa na shaka juu ya udhu alionao kushika wadhifa kama huo.

Waandishi wengi kama Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Happiness Katabazi na wengine walikwishaandika kulalamikia kadhia hii bila Kikwete hata kushituka.

Wachambuzi wengi wameshauri Kikwete avunje baraza la mawaziri na kuunda jingine dogo na lenye udhu na ari ya kuweza kuaminika na kuendesha nchi, lakini amepuuzia!

Baada ya miaka miwili madarakani, Kikwete amefanikiwa kumuua Kikwete kipenzi cha watu aliyechaguliwa kwa kishindo na kumuhuisha yule ambaye hata kura za taasisi ya Redet inayojulikana kulalia upande wa serikali kushtuka, na kuja na matokeo ya kura za maoni zinazoonyesha kuporomoka kwa Kikwete kutoka kuungwa mkono kwa asilimia zaidi ya 80 kuja kwenye 40!

Hili si jambo dogo wala jema kwa Kikwete na nchi. Hii inatafsirika kama kushindwa vibaya kwa utawala wa Kikwete unaosifika kwa kutoa ahadi nyingi hewa, kulindana, kujuana, kutoambilika na zaidi kutofanya lolote.

Miaka miwili ya Kikwete madarakani imefanikiwa kumwibua Kikwete wa kweli ambaye alifichwa wakati wa kampeni. Imefanikiwa kumweka mbele ya hadhira Kikwete mtatanishi asiyejali na anayeweza kusema lolote leo na kesho akalikana.

Kama kuna kitu Kikwete amefanikiwa kufanya ndani ya miaka yake miwili Ikulu ambayo akina Joseph Butiku na Jenerali Ulimwengu wamekiri kuwa imekuwa pango la wezi na watafuta ngawira, si jingine bali kujiangusha na kuwaangusha Watanzania.

Ila bado hajachelewa kama ataamua kuelewa. Akitaka yaliyoorodheshwa hapo juu yasiendelee kumtafuna, basi afanye yafuatayo:

Awatimue marafiki zake wote wanaokabiliwa na shutuma za ufisadi, aache wachunguzwe na tume na vyombo huru na kufikishwa mbele ya sheria.

Avunje baraza lake la mawaziri na kuunda jipya dogo na lenye hadhi na ithibati ya kuikwamua nchi inayozidi kuzama.

Asikilize ushauri wa Watanzania bila kujali itikadi wala nafasi zao kisiasa.

Awe muwazi na mkweli huku akijitahidi kutimiza ahadi zake ambazo zimekuwa chanzo kikuu cha aibu na maanguko yake.

Aanze kushika hatamu badala ya kukiachia chama na marafiki wachache kuendesha nchi kwa maslahi yao huku ya umma yakihujumiwa.

Na mwisho akubali kujifunza kutokana na utawala wa mtangulizi wake ambaye kwa sasa anaishi maisha ya kujificha nyuma ya joho la ulinzi na fadhila za urais huku akiandamwa na kashfa na aibu lukuki.
Mwisho wa yote ajue kuwa urais ni koti la muda ambalo kuendelea kulichafua na kulitoboa baadaye kunaweza kumletea hata kesi za jinai ambazo kama jamii itaamua kubadilika na kusimamia haki na mustakabali wake, vinaweza kumwacha pabaya huko tuendako.

Tathmini yangu ya miaka miwili ya utawala wa Kikwete ni ya maanguko. Mantiki niliyotumia ni baya moja kufuta mabaya mia.

Pia falsafa niliyotumia ni ile ya mwanzilishi wa taifa hili, Mwalimu JK Nyerere, aliyeacha usia kuwa akudanganyae hukufanya mpumbavu. Je, Kikwete ataridhika na kuendelea kuudanganya umma asichelee matokeo yake?

Nkwazigatsha@yahoo.com www.mpayukaji.blogspot.
 
Hii article inajumuisha miaka miwili ya awamu ya nne. Kauli mbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya imeshasahaulika.
I'm less optimistic, kama mabadiliko hayajatokea sasa, they will never happen. There is neither the will nor interest to bring change as long the status quo benefits those are supposed to initiate and supervise the changes on our behalf.
 
Mwanakijiji umenikumbusha mtu anayeitwa Prince Bagenda, ndiye aliyeandika kitabu juu ya muungwana JK mara tu baada ya kuteuliwa kugombea urais, akakiita "Tumaini Lililorejea". Wale walionunua kitabu hicho inafaa wakamdai awarejeshee fedha zao! Mwanakijiji ukimwona Bagenda muulize, lile tumaini liko wapi? Pengine anayo majibu. Hivi bado ni mpinzani ama asharejea "kundini" a.k.a "Buzwagi"?
 
Siku za mwisho wa utawala wa Kikwete zinakaribia. Jinsi siku hizo zinavyokwenda, ndio imedhihirika wazi kuwa hakuna matumaini yeyote yale kwa Watanzania walio wengi. Ni Watanzania wachache mno ambao wamenufaika na utawala huo, na ni hao wachachache wanaowarubuni Watanzania wengine kuunga mkono ccm. Hata hivyo Watanzania sasa wameona wenyewe na wanasubiri kwa hamu kuuondoa utawala wa ccm.
 
  • Thanks
Reactions: BAK
Back
Top Bottom