Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar: Wafanyakazi wa serikali kuneemeka kwa mishahara minono

FikraPevu

JF-Expert Member
Jan 2, 2010
303
236
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuanzia Aprili mwaka huu serikali yake itaanza kuwalipa wafanyakazi wa umma kima cha chini cha mshahara cha shilingi 300,000 kutoka 150,000 za awali ikiwa ni mkakati wa kuboresha maisha ya wananchi wa visiwa vya Zanzibar.

Rais Dk. Shein ametoa ahadi hiyo wakati akihutubia wananchi katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Aman mjini Zanzibar ambapo amesema mkakati huo wa serikali utaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo.

“Katika kipindi hiki mipango yote imekamilika ya kuwalipa wafanyakazi wa serikali kima cha chini cha mshahara kutoka 150,000 cha sasa hadi sh. 300,000. Kiwango hichi kimeongezeka kwa asilimia 100, mshahara utaanza kulipwa mwezi Aprili hivi karibuni”, amesema Dk. Shein.

Amesema nia ya serikali ni kuongeza hali kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, kuongeza uzalishaji na utolewaji wa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi.

Amebainisha kuwa serikali yake haitasita kuwachukulia hatua baadhi ya wafanyakazi ambao wameshindwa kuwajibika kwenye nafasi zao licha ya serikali kuboresha utolewaji wa mishahara na posho mahali pa kazi ambapo amewataka kuheshimu sheria na miiko ya dhamana walizopewa.

“Serikali katika mwaka 2016 imelishughulikia suala la nidhamu kwa wafanyakazi kwa mujibu wa sheria namba 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011 ya kanuni za kazi”, amesema Dk. Shein na kuongeza kuwa,

“Wapo wafanyakazi wameondoshwa kwenye dhamana za uteuzi kwa kukiuka maadili ya kazi, vilevile wapo waliosimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma na wanaendelea kuchunguzwa na kushughulikiwa na taasisi zinazohusika”.

Ameongeza kuwa serikali yake itahakikisha wananchi wote bila kujali nafasi zao wananufaika na rasilimali za nchi ikiwemo kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana na wanawake ambao hawako katika sekta rasmi ili kuwawezesha kiuchumi.

Wakati huo huo, Dk. Shein amezungumzia suala kupambana na ufisadi na kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli za kupambana na vitendo vya rushwa huku akiwataka wananchi na viongozi wa serikali kutambua juhudi hizo ili kujenga muungano wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Pia katika hutuba yake hakuacha kuwasifu na kuwaenzi waasisi wa Tanzania akiwemo rais Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume kwa kufanikisha uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Kudumisha na kuimarisha muungano ambao umeifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu kwa wananchi wote.

Zaidi, soma => Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar: Dk. Shein ahimiza uwazi, uwajibikaji serikalini | FikraPevu
 
Back
Top Bottom