Mheshimiwa rais: Amua sasa! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mheshimiwa rais: Amua sasa!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Msanii, Oct 25, 2009.

 1. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #1
  Oct 25, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  BUTU BUTUA

  Nilisoma insha ya Rev. Kishoka inayokwenda kwa jina la AJIZI YA KIBUGE. Nimekuwa naipitia mara kwa mara ili kujua mtunzi au mwandishi alikuwa analenga msomaji wake apate maudhui gani hasa. Inawezekana mkuu KISHOKA alishaisahau hoja yake hiyo kwani ni mchangiaji ambaye anakuja na hoja tunduizi kila uchao.

  Hapa sitaki kumjadili Kishoka na KIBUGE wake bali nalitumia andiko lake kama mrejesho wa hali halisi ya leo, Si bure kwamba KIBUGE anayemsema katika insha yake ni vasco da gama wetu ambaye amejitia kibwebwe kuubeba mzigo mzito wa masaibu yetu ili aambulie siagi ya adidu-rejeza.

  Nimehamasika kuamini kwamba katika zama hizi hakuna kiongozi wala mtawala ambaye ana nia njema kwa Taifa na watu wake. Kila mmoja anajijengea uhalali wa kuchukua nafasi na anajitweza kwamba ni mtumishi inagwa akishaukwaa ukwasi atatumikiwa na SISI. Haiyumkiniki kwamba mshika usukani wetu anahangaika huku na kule akitafuta uhalali wa sura njema huku akiwa amehifadhi huzuni na fadhaa za kushindwa kutimiza malengo na ahadi alizojitutumua kuzitekeleza akiwa anajinadi kwa hadhira miaka kadhaa hapo awali. Uholela wa utendaji pamoja na mashinikizo ya utekelezaji ni dalili tosha kwamba hali si shwari, pia udhaifu wa mawasiliano na ushirikiano kati ya mihimili ya kiutawala umejenga ufa mpana zaidi katika taifa letu adili.

  Watanzania wenzangu msifikirie kwamba kuna siku ambayo mkaazi mkuu wa Oval Office pale Washington DC anatekeleza mipango na sera zake kwa target ya kuwapendezesha watu wa dunia ya nje seuse Tanzania. Kila anachopanga na kufanya anatekeleza kwa lengo la Marekani KWANZA. Ndo maana wanafikia kukataa kusaini mikataba kuntu kama mkataba wa KYOTO kuhusu upunguzaji wa joto duniani kwa kisa kwamba mkataba huo utaathiri Marekani kiuchumi.

  Nasema hivyo kwa sababu SISI tumeamua kuuza UTU wetu na heshima yetu kwa minajili ya kuwavutia wawekezaji wanaokuja kuchota kwa jasho letu. Nakumbuka Mwalimu Nyerere katika moja ya nasaha zake alitabainisha kwamba hakuna mwekezaji atakayekuja kuwekeza kwetu kwa minajili ya kutuendeleza sisi na vizazi vyetu. Hivyo suala la sisi kuimba wimbo wa kuvutia wawekezaji huku tunawadhalilisha wapiga kura wa Tanzania ni UJUHA usiopimika

  Napenda kutambua uwepo wa watani zangu REDET ambao kila wanapopiga tarumbeta lao wanakuja na takwimu zisizo na mashiko kuhusu umaarufu na harufu za turufu. Haiingii akilini kwamba MTU mmoja anakuwa maarufu zaidi ya wasaidizi wake eti kisa hawamsaidii katika utekelezaji wa shughuli wanazopaswa kufanya. Sidhani na siamini kwamba REDET ndio walioiteua kamati ya kikabati (kabinet), watambue kwamba aliyeiteua ndiye aliyeona wanafaa na mpaka sasa wanamfaa sana kwani hakuna jipya la kiutendaji lililobadilika tangu hawa wapiga filimbi wa Hamelin (REDET) wajifarague na tafiti zao. Tafakuri na tafiti nyingi zimekuwa zikigusia namna ambavyo maadili ya Taifa yanavyohujumiwa na wapigiwa kura, haiyumkiniki kwamba hizi kelele zinazopigwa na jamii kuhusu uhalisia wa UFAKAMIZI ni kama kelele za mlango zisizozuia usingizi poyoyo wa PONO. Je tumlaumu nani kwa haya yanayotokea? Ingawa kuna wachawi wengi walioturoga mpaka hapa tulipo ila mchawi mmoja mbaya kabisa ni UJINGA wetu. Tangu TAIFA lilipoamua kupiga hatua kadhaa nyuma kielimu ndipo tulipojitwisha nira ya KUYUMBA na kupepesuka kimaadili.

  Sina ujuvi sana katika masuala ya kisiasa kama walivyo nguli wengine (mwanakijiji, Kishoka, WomanOf Substance, Invisible, Mchambuzi, Bubu, MTM, Zitto, Dr, Slaa, Halisi, to name few) ila hapa nataka kuchambua nionavyo katika mfumo wa Tanzania na kama ningekabidhiwa nchi ningeanzia wapi.

  Usalama wa Taifa:-
  Hawa wazalendo wapo kama hawapo vile. Kuna kila dalili kwamba taasisi hii imekuwa tofauti sana na jinsi inavyoshughulika na ulinzi na ustawi wa Taifa letu. Tumesikia sana (lisemwalo lipo au laja) kwamba watawala wengi tulionao wamepitia au kutumika katika taasisi hii adhimu hivyo basi ni dhahiri hawa wanatuangusha kwani huwezi kuwa moyo halafu ukajipa majukumu ya kichwa at a time. Taasisi hii iboreshwe iwe ya kisasa zaidi na ya kimkakati ambapo badala ya kuanza kufukuzana na vijitu vidogo vidogo kama MSANII wangewekeza katika kufanya tafiti na utekelezaji wa mikakati ya TAIFA kujiimarisha kimaendeleo.

  Najiuliza kwamba walikuwa wapi wakati mabilion ya EPA yanakwibwa? Au walikuwa katika sayari ipi wakati nchi inaingia mikataba ya KIHULKA ya madini au walikuwa wapi kuthibitisha uhalali/uwepo wa kampuni tapeli ya Richmond? Walikuwa wanacheza ngoma gani wakati wa ununuzi wa rada kwa bei mruko? Je nashawishika kuamini kuwa uwepo wao ni kwa ajili ya usalama wa viongozi (bila kujali wayatendayo) na si usalama wa TAIFA (wananchi wanyonge)? Kuhusu madhila yanayowapata Watanzania wenzetu kule North Mara (utiririshwaji wa kemikali katika mto) hawa jamaa wamefanya nini kulinda usalama wa taifa?

  Nauliza hivi kwa sababu kuna baadhi ya mipaka ambapo polisi wa kawaida kwa upeo wa kazi yake hawezi kuvuka na itahitajika njia ya ziada. Ila nijuacho mimi ni kwamba kila senti wanayolipwa hawa wazalendo inatokana na KODI yangu na Mtanzania mwingine na haitokani na michango ya viongozi ambao wanaila keki ya taifa bila kuilipia kodi. Nawaasa wasikubali kutumika vibaya na ninaamini kwamba ndani ya taasisi hii wapo wazalendo wa kweli ambao wanalitakia mema taifa letu.

  Hivyo basi badala yake, ingelikuwa vyema Taasisi hii ingeangalia maeneo mengine zaidi hasa namna na mbinu za kupenya mipaka ya kiuchumi na ustawi ili Watanzania waweze kuwekeza nje na hata nchi kufaidika na kila fursa au fununu njema kwa mjengo wa uimarishaji kiuchumi. Ni budi tuondokane na huu utamaduni wa kuwavutia wawekezaji badala yake iwe ni kuwahimiza na kuwawezesha watanzania kuwekeza nje. Pia ni budi kila mwekezaji achunguzwe usafi wake huko atokapo kwa kupitia chujio maalum ambapo itapunguza queries za kizembe wanazozisababisha baada ya kujikita nchini.

  Maboresho ya mbalimbali na katiba: -
  Pamoja na marekebisho mengine yaliyopendekeza na wadau wengine kuhusu mabadiliko ya katiba, ningependa pia Katiba itamke bayana idadi na majina ya wizara zitakazoundwa na kiongozi mkuu aliyeko madarakani ili kuondokana na mpangaranyiko wa ubunifu wa wizara kwenye kila awamu inapokuja. Pia katiba itamke bayana kwamba kiongozi mkuu atamteua Mtanzania aonaye anafaa kushika wadhifa wa uwaziri na nitaondoa cheo cha waziri mkuu kwani makamu wangu atanisaidia katika kusimamia majukumu ya wizara mbalimbali na mawaziri wote watawajibika kwa Bunge.

  Kwenye Katiba nitashawishi iwepo clause inayotamka kwamba waziri wa fedha, mambo ya Nje, ulinzi na utumishi (kama zitakuwepo) lazima uteuzi wao uthibitishwe na bunge. Kiongozi mkuu apewe mamlaka ya kuanzisha idara/ vitengo maalumu katika wizara endapo atashawishika kufanya hivyo. Suala la upunguzaji madaraka ya rais ni kuntu na halina mjadala tofauti. Pia kupunguza kinga ya raisi kwani sidhani kama tulimfuata na kum-bembeleza atuongoze, alijipanga, na kwa utashi wake aliamua kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea, hivyo basi kwa kuwa aliingia kwa utashi basi anapaswa pia kufahamu kwamba akienda kombo lazma atawajibika kwa kila pindo atakalosababisha. Hii itajenga maadili kwa kiongozi mkuu ambaye pia atasimamia vyema walio chini yake kwa maslahi ya Taifa.

  Katiba itakataza mtu kujirundikia vyeo lukuki ilhali kuna Watanzania wengi wenye uwezo kushika nafasi hizo, nafasi moja mtu mmoja hakuna mbunge and same time mkuu wa mkoa. Pia katiba itatamka bayana kuhusu sera ya elimu ya taifa katika kuainisha mambo muhimu ambayo kila kiongozi atawajibika kufuata, ambapo itakuwa ni dhambi ya kukufuru kwa kiongozi au afisa wa daraja la Fulani serikalini kumsomesha mwanae nje ya mfumo wa elimu itolewayo na serikali. Hii itasaidia kutunga sera na utekelezaji wake kuwa mzuri wa kuboresha elimu yetu.

  Huwezi kupika chakula usichoweza kula labda uwe umeweka sumu ndani yake. Elimu itatolewa bure (kwa kuwa nitaboresha uchumi) kwa kila mwenye uwezo wa kusoma, ila elimu ya msingi na sekondari itakuwa ni ya LAZIMA kwa kila mtu. Shule yeyote (ya umma au binafsi) itakayojengwa bila ya kuwa na maabara na maktaba itageuzwa kuwa community centre, na wahandisi/ wakandarasi waliobuni na kusimamia ujenzi watawajibishwa na mamlaka husika. Pia ishu ya watoto wa mitaani na yatima watatunzwa katika kambi za serikali ili wapate haki zao za msingi na elimu.

  Wazazi WATALAZIMIKA kuhudhuria mafunzo ya mara kwa mara yatakayokuwa yanatolewa na ofisi za ustawi wa jamii nchi nzima kuhusu masuala muhimu ya malezi ya familia na watoto. Napendekeza hivyo kwa sababu katika katiba kutakuwa na vipengele vinavyoainisha collective responsibility ya malezi ya watoto na ustawi wa familia, naamini hii itapunguza kasi ya wabongo kuwa makini katika masuala ya uzazi. Kama kawaida kila agizo litakuwa na penal code yake ili kuleta order.

  Kuhusu kupunguza wasomi wanaokariri badala ya kuelewa, nitaelekeza mamlaka za mitihani kuboresha mitihani ambayo itapima uwezo wa mtu kuelewa ishuz na si ufundi wa kukariri ili kujibu mitihani. Hivyo basi mtu atatahiniwa uwezo wa darasani na kuoanisha uwezo wa ufahamu wake kwa kupitia njia nyingine (ambayo siitaji hapa mpaka mninunulie popcorn). Pia maslahi ya walimu yataboreshwa SANA kwani kuanzia day one pale mtaa wa Luthuli nitasign badiliko la wataoteuliwa kujiunga na vyuo vya ualimu. Wale watakaokuwa wanapata alama hafifu watakuwa automically wamepoteza sifa za kujiunga na ualimu. Daraja la kwanza na pili ndio watakaopewa kipaumbele cha kuchaguliwa kwenda ualimu (na italipa). Uhuishaji wa utamaduni wa kujisomea utakuwa ni kampeni ya nchi nzima kama ilivyo kampeni dhidi ya maambukizi ya ukimwi.

  Nitatunga sheria inayoamrisha utekelezwaji wa sheria zote zilizotungwa kwa minajili ya kuheshimu na kulinda katiba na sheria zilizopo, nayo itakuwa na penal code yake.

  Hospitali zote za umma zitatoa huduma bila malipo kwani serikali itawajibika kuboresha huduma na maslahi ya wafanyakazi wa hospitali hizi. Serikali itaanzisha vituo na vyuo vya kutafiti tiba na madawa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kila kunapokucha. Pia kuhakikisha viwanda vya dawa vinaanzishwa nchini kukabiliana na upungufu wa dawa kwenye hospitali za umma. Pia nitahakikisha kwamba hospitali za kijeshi zinaendesha tafiti na majaribio ya kina katika matibabu.

  Kuanzisha na kuboreshamaabara za kisayansi na teknolojia ili kuhakikisha kila teknolojia inayoingia nchini inakidhi mahitaji yetu. Kuwachechemiza wabunifu wa Tanzania kuzitumia maabara hizi kuchalenji ubunifu wao hasa katika uboreshaji.

  Umeme ukikatika nitamfuta kazi waziri mwenye dhamana ya umeme pamoja na watendaji wote husika. Kila waziri atakayeapishwa atasaini mkataba maalumu wa utumishi wa wizara atakayoongoza sambamba na kupewa mwongozo wa kiutendaji. Na waziri atawajibika kuwa mfano wa utendaji wa kuleta tija. Zile ishu za watu wanaokimbilia kwa rais ili awatatulie matatizo yao ya ardhi na zagazaga nyingine, itakuwa ni kitanzi kwa wizara na idara husika kwamba hakuna tija wala utekelezaji wa maazimio ya hudumatija kwa watu.

  Katika maboresho ya katiba itatamka bayana kwamba mtanzania yeyote atakayechaguliwa kwa kura kuwa kiongozi mkuu wa nchi atawajibika kuachia ngazi ya/za uongozi katika chama chake ili kumpatia fursa ya kutimiza majukumu yake ya uongozi kimaadili na si kichama. Hii ni kupunguza mgongano wa kimaslahi hasa kuchanganya masuala ya chama katika uongozi wan chi. Atawajibika kutekeleza kikamilifu sera za chama chake kilichoshinda. Hivyo mtanzania yeyote atakayeingia katika uongozi wa nchi anapoteza sifa ya kuongoza chama alichotoka, wanachama watachagua viongozi wengine wa chama

  Katika sheria ya uanzishwaji wa SUMATRA kuna clause inayomkataza kamishna au mwanabodi yeyote wa taasisi hiyo kujiingiza katika biashara ya usafirishaji mpaka miezi mingi kadhaa baada ya kustaafu, hivyo pia nitaweka uwigo wa kuingiza ndugu na jamaa za watawala katika safu za kiutawala maana hakuna definition yeyote hapo zaidi ya RUSHWA ya kimadaraka. Kwani endapo nitakuwa kiongozi mkuu halafu wakatokea ndugu jamaa zangu kujipenyeza kushika baadhi ya nyadhifa ni sawa na kuunda taifa la kisultani au kifalme yaani kuwakoloni watanzania. Hivyo kila kiongozi ataingia mkataba wa kimaadili unaoelekeza kuepuka kutumia mgongo wake kuwapenyeza jamaa zake katika utawala (hata wakiwa na uwezo kiuongozi). Wasubiri muda Fulani upite baada ya ndugu yao kutoka madarakani ndipo nao waingie ktk kinyang’anyiro kwa nguvu na utashi wa muda huo. Kwa kuwa Usalama wa Taifa itakuwa imeboreka itakuwa ni kazi nyepesi kudhibiti uroho na undugulaizesheni.

  Endapo maamuzi au utekelezaji wa maamuzi ya kisera yataathiri ustawi wa watu na taifa, katiba itatamka bayana aina ya uwajibikaji utakaofanyika dhidi ya uzembe wa kimakusudi utakaotokana na kiburi na uzembe wa kutekeleza shughuli za kiserikali.

  Hivi wadau ili tuondokane na hakimiliki za majimbo tufanyaje? Ingawa nadhani kuna haja ya kubuni njia chanya ya kuweka ukomo wa ubunge, pia kila kiongozi atalipa kodi kwa kila kipato atakachoingiza ingawa kutakuwa na unafuu (si sana)

  Mhimili wa mahakama nitauondoa kutoka kuwa idara ya mahakama na kuipa mamlaka kamili kimhimili. Yaani katika katiba itawekwa clause inayotamka bayana majukumu na nafasi ya mahakama kama mhimili wa serikali na si kama idara. Ingawa executives watakuwa ndiyo mhimili unaoongoza nchi lakini mihimili mingine ya bunge na mahakama itakuwa na nafasi na majukumu yake bayana. Raisi atateua jaji mkuu ambaye atapitia chujio la bunge kabla ya kuapishwa, jaji mkuu atasaidiana na rais katika kuteua majaji. Mahakama itaweka mfumo wake wa kuajiri watumishi wa ngazi mbalimbali za mahakama kwa ushirikiano na idara ya utumishi serikali kuu.

  Vivyo hivyo spika wa bunge atachaguliwa na wabunge na kuapishwa na rais ila katibu wa bunge atapatikana kutokana na mchakato wa ajira ya bunge na kuapishwa kwa utaratibu utakaoundwa na bunge. Nitaidhinisha sheria zitakazotungwa na bunge na si executives. Ila nitatoa (executives) mapendekezo ya uundwaji wa sheria ili bunge liweze kuunda sheria hizo. Kazi asili ya tafsiri ya sheria itaachiwa mahakama. Kwa hiyo mwanasheria mkuu wa serikali atakuwa ni kiungo muhimu kati ya mhimili wa watawala na mahakama. Mwanasheria huyu hatoingia bungeni kwani waziri mwenye dhamana na idara yake atakuwa ndiye mwakilishi wake bungeni. Nitapendekeza utaratibu utakaotumika na mahakama katika kuwasilisha bajeti na masuala ya mhimili huo katika bunge.

  Pamoja na kuboresha sheria nyinginezo, sheria inayosimamia udhitibi wa uozo (corruption) serikalini na mali ya umma. Itakuwa kwamba pamoja na adhabu nyingine endapo mhusika atatiwa hatiani, atataifishwa mali zake ili iwe fundisho kwani mwizi hukamatwa siku ya arobaini. Na hapa SFO ya bongo lazma iingie kazini kuunganisha mali za mtuhumiwa (endapo amezisambaza ktk vivuli vingi) ili endapo akitiwa hatiani na kuhukumiwa basi kutaifishwa ni adhabu itakayoenda sambamba na adhabu nyingine yeyote ambayo hakimu au jaji ataridhia kumzawadia. Kuhusu rushwa kama nilivyosema hapo juu mnaweza kutazama avatar yangu hapo juu mjue aina ya jicho litakalomwangalia bazazi atakayethubutu kuniharibia kazi ambayo nilipewa kwa kuwapigia magoti wabongo.

  Katiba itatamka bayana muundo wa tume huru ya uchaguzi na makamishna wake (mseto) watakavyopatikana. Chaguzi zote za kiserikali zitasimamiwa na tume ninamaanisha hata hizi chaguzi za serikali za mitaa.

  Ustawi na uchumi wa taifa: -
  Hapo ni kasheshe, kwani kila mkataba nchi utakaoingia bila ya kuthibitishwa na bunge (kwa koram) utakuwa ni batili. Pia nitarudisha kila yodi ya shirika la umma lililouzwa (kisa limekufa/ limeuawa) ili taifa liweze kuajiri na kuzalisha. Nadhani viongozi wetu (wajuvi) wanafahamu fika kwamba hizi sera za akina world bak na IMF kwamba serikali isifanye biashara ilihali mataifa yanayounda haya mashirika yaliyojipa ukiranja wa uchumi walifanya biashara kwa zaidi ya miaka 600 mpaka kufikia hapo walipo na hawatatetereka kwani walishaweka misingi, hivyo sisi ambao hata nusu ya karne moja hatujafikia, hatuwezi kujitia nira ya kukimbizana nao hivyo siwezi kukubaliana na kila upuuzi wanaousema eti kisa watatunyima misaada (ambayo kiutekelezaji wanachota hela zote wanazotupatia na kutuachia double deni).

  Kama mfanyakazi yeyote katika serikali yangu hataonesha tija atakuwa amejiwekea kigingi cha kupata maslahi bora au kupanda daraja kazini. Positive productivity ndiyo itakayokuwa ni dira yangu ya uchumi. Na kodi itatozwa kutokana na levo za walipaji. Kila mwekezaji atawajibika kufungua akaunti ya mtaji katika benki za hapa nchini na ataruhusiwa kuhifadhi sehemu ya faida ya mwaka katika benki za nje. Pia kila mwekezaji mgeni atapewa nafasi finyu za kuajiri kutoka nje ila asilimia 85 ya kila daraja la ajira (utawala, vitengo na idara) itakuwa ni nafasi kwa watanzania.

  Kufufua au kuanzisha viwanda vya usindikaji kwa minajili ya kuboresha mazao ya biashara kabla ya kusafirisha nje. Kuboresha miundombinu ya kilimo (siyo porojo) hasa kilimo cha kisasa na kuanzisha maghala ya kitaifa na kutafuta masoko shindani kwa bidhaa za wakulima badala ya kuwabana kuuza katika masoko yanayopunja na kuwanyonya wakulima. Kwa faida za kiuchumi nitatenganisha majukumu ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa wilaya ili kuwepo na uwajibikaji wa kimaendeleo zaidi ya uwajibikaji wa kiutawala. (hili siwaambii kiundani zaidi kuwa nitafanyaje labda mpaka mnipe mji).

  Sanaa na utamaduni:-
  Nihimiza uanzishwaji wa national galleries na vituo kadhaa kwa minajili ya uboreshaji wa sanaa zizalishwazo kwa minajili ya kuingia soko la ushindani. Pia kutakuwa na mtaala wa sanaa na utamaduni utakaoingizwa katika ngazi zote za elimu pamoja na teachers colleges. Sayansi ya sanaa pamoja na teknolojia zake zote (industrial arts and design, interior design, animation, film, folklore na zagazaga zote) vitakuwa katika mfumo wa mtaala ili kuhuisha innovation and arts marketing. Naona serikali hii imethubutu cultural tourism lakini hawana dira ya nini kifanyike hadi sasa ndo maana hakuna maendeleo makubwa ya cultural tourism zaidi ya kutangaza mbuga zetu na wamasai (ohooo msielewe vibaya wazazi wangu) ingawa nina nasaba ya kimasai pia.

  Nikiamua kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa top post nitawatoa jasho. Hapo bado sijaja na sera, nimeleta wazo tu la aina ya serikali iliyopo katika ndoto zangu za mchana.

  Ingawa hoja zipo shaghalabaghala ndo nimewasilisha ivo!


  Mabandiko yataendelea…….
   
 2. Tiba

  Tiba JF-Expert Member

  #2
  Oct 25, 2009
  Joined: Jul 15, 2008
  Messages: 4,511
  Likes Received: 95
  Trophy Points: 145
  Mkuu, nimekusoma lakini kupanga ni suala moja na kutekeleza ni suala lingine. Nini mikakati ya kutekeleza hayo uliyoyaota?

  Tiba
   
 3. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #3
  Oct 25, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  Mkuu thanx kwa dukuduku lako.
  Ingawa kutakuwa na kalenda ya utekelezaji wa mipango hii, na mipango mingine itatekelezwa katika kuweka misingi ili ajaye aweze kuendeleza. Ila asilimia 80 ya mipango inatekelezeka hata kwa sehemu katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza. safari hii viongozi ndio watakaofunga mikanda kama hutako OUT!
   
 4. Rev. Kishoka

  Rev. Kishoka JF-Expert Member

  #4
  Oct 25, 2009
  Joined: Mar 7, 2006
  Messages: 4,470
  Likes Received: 277
  Trophy Points: 180
  Msanii,

  Kama ingekuwa ni kufaulu mitihani ya masuala ya siasa na jamii kutumia yanayotokea sasa hivi, wengi wetu tungeshakuwa na PHD 10!

  Nimekueleza kisa cha Kibuge Mwinyi Fuadi kule kwenye Ilani ya CCM 2010, jinsi alivyofunga barabara kwa saa 2 kisa anarudi Dar kutoka Msoga!

  Sijasahau nilichoandika na ndio maana hata hili la kijana Mamvi Eddo, naendelea kucheka huku wengine mapovu na Misukule ikiwatoka!

  Keep it up, Unguli nawe unao na hii imetulia!
   
 5. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #5
  Oct 25, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,593
  Likes Received: 3,887
  Trophy Points: 280
  Hivi nyie hamjachoka tu kumpa JK ushauri? kisiki kile kiondolewe basi
   
 6. M

  Mkandara Verified User

  #6
  Oct 26, 2009
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Msanii,
  Mkuu samahani sana napenda kuuliza. Hivi umeandika wewe kitu hii au macho yangu.. Sii kwamba nakudharau ama kukebehi lakini kitu imetulia sana kiasi kwamba nachelea kusema kwamba wewe ni mwandishi mmoja wa hali ya juu sana. Lugha unaiweza na unajua kupanga vitu kama vile umeviunda..
  Kifupi, mkuu wangu hiki ni kipaji wala sii zaidi.. nakuomba sana weka mabandiko kama haya magazetini..
   
 7. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #7
  Oct 26, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  Mkuu wangu Mkandara
  mimi si kitu kabisa ktk siasa za Bongo ila lazma niseme kwamba ninyi ndio mlini-influece niweze kufikiri. Mie huwa nawasoma sana ninyi ktk debate zenu. anyway nashukuru kwa kunipa changamoto.

  Ila inatia hasira na huzuni kweli kwa namna mambo yanavyokwenda kana kwamba nchi haina usukani au mshika usukani vile.

  Ila kitu kimoja dhahiri ni kwamba am an artist just a man with his brushes....
   
 8. M

  Mkandara Verified User

  #8
  Oct 27, 2009
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Damn, U good! jitahidi uingie fani nyingine ya Uandishi...
   
 9. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #9
  Oct 27, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  thanx mkuu,
  tudumishe utamaduni wa kuelimisha umma
   
Loading...