Mhe. Mkulo sasa azidi kubanwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
Mhe. Mkulo sasa azidi kubanwa

2008-06-18 16:25:32
Na Mwandishi wetu, Dodoma

Siku chache tu baada ya kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2008 na 2009, Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Mhe. Mustafa Mkulo, amejikuta akizidi kubanwa na hoja mbalimbali zinazotolewa na wabunge ambao leo wameendelea tena kutoa michango yao.

Mhe. Mkulo ametakiwa atoe maelezo ya kina kuhusu matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 136, ambazo matumizi yake hayakubainishwa wazi katika bajeti ya Serikali aliyoiwasilisha bungeni Alhamisi iliyopita.

Wakichangia hotuba hiyo, baadhi ya wabunge hao wametishia kuizuia bajeti hiyo endapo Waziri Mkulo hatarekebisha kasoro walizoziona.

Katika Mchango wake, Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa amesema amebaini kuwapo kwa tofauti hiyo ya bilioni 136 katika vitabu vya bajeti na hivyo akamtaka Waziri Mkullo airekebishe kabla ya kuwataka waipitishe.

Akasema kwa kawaida bajeti ya Serikali huwa na vitabu vinne vinavyopaswa kuoana kimahesabu.

Akasema tofauti hiyo ya shilingi bilioni 136 ni kubwa mno na hivyo akamtaka Waziri Mkulo airekebishe na kuchapa vitabu vingine.

``Kuna tofauti ya shilingi bilioni 136, hii ni kubwa sana na sisi tunafanya kazi ya kikatiba, lazima irekebishwe na kuchapisha vitabu vingine,`` akasema Dk. Slaa.

Mbali na hilo, pia Dk. Slaa amesema amebaini dosari nyingine ya kuonekana kwa jina la Tanzania Harbours Authority ambayo haipo kwa sasa baada ya kubadilishwa na Bunge na kuwa Tanzania Port Authority.

Naye Mbunge wa Muheza (CCM), Mhe. Herbert Mtangi, aliitaka Serikali kueleza kwenye bajeti kuhusu mchango wa mkutano wa Leon H Sullivan uliofanyika mjini Arusha hivi karibuni.

Mheshimiwa huyo alitaka wizara kuonyesha tahmini ya nini kitarajiwe kuongezeka katika pato la taifa baada ya kukamilika kwake.

Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Mjini, CHADEMA, Bw. Philemon Ndesamburo, amesema anaishangaa Serikali kila mwaka, bajeti yake inaposomwa inapandisha kodi katika bia na sigara, pasipo kutafuta vyanzo vingine vya kukuza pato lake.

``Tangu nimeanza kulisikia bunge nikiwa mdogo, wanachofanya ni kupandisha bei ya bia na sigara, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani hawa watu wanavyochangia pato la taifa...lakini itafika mahala hawa watu wasiolala bila kunywa bia mbili... wakashindwa kununua na watarudi kunywa piwa (gongo),`` akasema.

Wabunge wanaendelea kuijadili bajeti hiyo ambapo mwisho wa yote, Mhe. Mkulo anatarajiwa kutoa ufafanuzi wa maeneo mbalimbali yatokanayo na hoja zinazotolewa na wabunge ikiwemo kuhusu suala la mapesa yaliyochotwa kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje, EPA na tuhuma za ubadhirifu katika ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu, BOT kabla bajeti hiyo haijapitishwa.

SOURCE: Alasiri
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom