Mh Nyanganyi ASOMEWA DUWA na mahujaji wa ATC!!!

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,138
Mnayakumbuka haya;mahujaji kadhaa wameamua kuswali kwa ajili ya yote aliehusika na matatizo na usumbufu wa mahujaji waliolala pale airport ya dar es salaam;
kazi kwelikweli

Makala
Nakala chapishi
Mtumie mwenzio
Jiandikishe utaarifiwe



Bodi ya ATCL yamkandamiza Balozi Nyang’anyi

Mwandishi Wetu Disemba 26, 2007




Kwa siku 12 Mahujaji wa Tanzania na baadhi ya wengine kutoka nchi jirani, walikwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, baada ya taratibu za kuwasafirisha hadi Saudia kukwama. Hatimaye, walisafiri lakini baada ya Serikali kuingilia kati. Sasa jitihada zinafanyika waweze kurejea bila matatizo makubwa. Baada ya sakata hiyo, Serikali iliagiza ipewe taarifa ya hali ya mambo. Raia Mwema imefanikiwa kupata nakala ya taarifa hiyo ya Bodi ya ATCL na inaichapisha kwa faida ya wasomaji.

1.0 UTANGULIZI

Kuanzia Desemba 10 , 2007 hadi Desemba 14, 2007 Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilikuwa katika msukosuko mkubwa. Hiyo ilitokana na matatizo ya kukwama kwa Mahujaji kwenda Hijja Saudi Arabia. Tatizo hilo lilianza kama tukio la kawaida la kiutendaji, lakini taratibu lilianza kuchukua sura mpya kiasi cha kuihusisha Serikali wakiwamo viongozi wa juu kabisa wa nchi.

Tatizo hilo kwa kiasi kikubwa limeleta usumbufu usio kifani kwa Mahujaji ikiwamo aibu na fedheha kwa shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Taifa kwa ujumla, Serikali na viongozi wake wakuu.

Kutokana na hayo, Mheshimiwa Andrew Chenge (Mb), Waziri wa Miundombinu, aliiagiza Bodi kwa kupitia barua yake Kumb. Na. MC 62/2270/01 ya Desemba 17, 2007, kwamba iundwe kamati ya Bodi ya ATCL kufanya uchunguzi juu ya suala la kukwama kwa Mahujaji, na kutoa taarifa yake siku ya Ijumaa, 21 Desemba, 2007.

1.1 UAANDAAJI WA TAARIFA

Kamati ya Bodi katika maandalizi ya taarifa yake ilizingatia yafuatayo:-

Maelezo ya mdomo ya wahusika wakuu wakiwamo wafuatao:-
- Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL
- Mkurugenzi Mkuu, ATCL na
- Manager Flight Operations

maelezo yaliyotolewa katika kikao cha dharura cha 14 cha Bodi ya Wakurugenzi cha Desemba 17, 2007

Maelezo ya maandishi ya wahusika muhimu katika suala hili yaliwahusu wafuatao:-
Mwenyekiti wa Bodi – ATCL (Balozi M. Nyang’anyi)
Mkurugenzi Mtendaji - ATCL (D. Mattaka)
Manager, Flight Operations – (M. Manji)
Kaimu Mkurugenzi wa Operations (Capt. S. Muze)
Afisa Masoko - (J. Kagirwa)
Katibu Muhtasi – (M. El-Hady)
Mwanasheria wa Kampuni – (A. Mziray)
Maoni ya Wajumbe wa Bodi ya ATCL
2.0 MAELEZO YA AWALI (BACK GROUND)

Kufuatana na maelezo ya Menejimenti ya ATCL, mnamo mwezi Julai, 2007, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, aliwaomba viongozi mbalimbali wa Jumuiya za Kiislamu zinazoshughulika na safari za Mahujaji kulipatia shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) biashara ya kusafirisha Mahujaji kwenda Makka na Madina, Saudi Arabia (Lakini Mwenyekiti anasema ni viongozi wa Mahujaji ndio waliomfuata na kumuomba).

Mnamo Julai 19, 2007 Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL alimwita ofisini kwake Mkurugenzi wa Uendeshaji, Capt. Sadiki Muze, na kumtambulisha kwa viongozi mbalimbali wa Taasisi za Kiislamu, na kumueleza kwamba mwaka huu ATCL itaandaa safari za Mahujaji. Mkurugenzi huyo alitoa taarifa hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL kuhusu maongezi yake na Mwenyekiti wa Bodi. Baada ya majadiliano marefu na wataalamu wahusika kwenye Shirika ilionekana kuwa shirika halina uwezo (ndege) wa kuandaa safari hizo.

2.1 HATUA ZILIZOFUATIA

Mkurugenzi Mkuu aliandika barua kwa Mwenyekiti wa HAJJ Trust, ya Julai 26, 2007, ikimuelezea kuwa ATCL haina uwezo wa kuandaa safari za Hijja. Hata hivyo barua hiyo haikupelekwa kwa walengwa, kwani wakati Katibu Muhtasi anatafuta ofisi za Hajj Trust ili barua iwasilishwe huko, Mwenyekiti wa Bodi aliagiza kuwa barua hiyo isipelekwe mpaka afanye mawasiliano na Menejimenti. Katibu Muhtasi aliwajulisha Mkurugenzi Mtendaji na Mkurugenzi wa Uendeshaji (Capt. Muze) kuwa barua haikupelekwa kutokana na maagizo ya Mwenyekiti wa Bodi.

Mwenyekiti wa Bodi aliwasiliana na Mkurugenzi wa Uendeshaji na kumhakikishia kwamba ATCL ingeliweza kufanya safari hizo, kwani ndege zingeweza kupatikana, hususan kutoka katika kampuni ya RAK Leasing ya Dubai. Pia Mwenyekiti alimpatia Mkurugenzi wa Uendeshaji jina na namba ya simu za mhusika ili awasiliane naye kuhusu upatikanaji wa ndege.

Captain Muze aliwasiliana na kampuni ya RAK Leasing ambao walimwambia kuwa wanayo ndege aina ya Boeing 747-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 489, ambayo kwa wakati huo ilikuwa katika matengenezo ya Check “C” na kwamba ingekuwa tayari mwezi wa Septemba, 2007. Capt. Muze aliwaomba wamletee “Documents” za ndege hiyo ili aweze kufanya maandalizi ya kupata vibali muhimu, zikiwemo “slots”. Pia aliwasiliana na kampuni ya Al-Wassam ambao ni “Ground Handling Agent” wa Makka na Madina (ambao hapo zamani walikuwa wana “handle flights” za Hijja za Air Tanzania Corporation) ili wafanye matayarisho muhimu, ikiwamo utafutaji wa “slots”.

Hata hivyo, “documents” za ndege zilichelewa kufika na ilibainika kuwa zilikuwa zinaisha muda wake Novemba 30, 2007, na hivyo zisingefaa kutumika kuombea vibali pamoja na “slots”. Kampuni ya RAK Leasing iliahidi kuwa ingepata “documents” zingine na kuahidi kuitafutia ATCL kampuni nyingine za “ku-handle” ATCL. Pamoja na ahadi hizo kampuni hiyo haikufanya hivyo.

Wakati huo huo Capt. Muze alisafiri kikazi kwa muda mrefu na kumuachia shughuli hii Afisa Masoko, Josephat Kagirwa.

Kadiri muda ulivyopita, na safari za Mahujaji kukaribia ilidhihirika kuwa ndege isingepatikana kutoka kampuni ya RAK Leasing. Hii ilithibitika baada ya wafanyakazi wa ATCL, akiwamo mwanasheria wa ATCL Mziray kwenda Dubai, na kurudi mikono mitupu bila mikataba na au “documents” za ndege ya RAK Leasing na hiyo ilikuwa mwishoni mwa mwezi Novemba, 2007, zikiwa zimebakia siku chache mno kabla ya safari za Mahujaji kuanza.

Baada ya hapo Mwenyekiti wa Bodi na Capt. Muze walianza kufanya mipango mipya ya kutafuta ndege nyingine. Walifanikiwa kupata ndege kupitia msaada wa Al-Wassam, wa Jeddah. Ndege hiyo ni aina ya DC 10 inayomilikiwa na Global Aviation ya Afrika Kusini. Hata hivyo, ndege hiyo ilipatikana kupitia kwa wakala mwingine ambaye ni SAMEK Aviation Services wa Jeddah, (Ground Handling Agent).

Katika mikataba ATCL iliyoingia na SAMEK AVIATION ilijumuisha pia kuipatia ATCL “slots” za ndege hiyo. Mkataba huo ilibidi usainiwe Saudi Arabia na Balozi Hamis Msumi kwa niaba ya ATCL, kutokana na ucheleweshaji wa maandalizi na ufupi wa muda. Wakati haya yanakamilika ilikuwa 6/12/07 na tayari Mahujaji kutoka sehemu mbali mbali walikwisha kuwasili ikizingatiwa kuwa ratiba ya awali ya Mahujaji ingelikuwa 4/12/07.

SAMEK Aviation Services, waliahidi kuwa safari za Hijja zingeanza 8/12/07, na ahadi hii ilithibitishwa kwa Balozi wetu nchini Saudi Arabia, kwamba ndege husika ilikuwa inakuja. Kwa bahati mbaya haikufika kama ilivyoahidiwa, pamoja na ATCL kutimiza masharti yote, ikiwamo kulipa malipo ya awali ya Dola za Kimarekani 550,000.

Kufuatia kutowasili ndege hiyo kama ilivyokuwa imetarajiwa, na Mahujaji kuzidi kusongamana uwanja wa ndege wakati wanasubiri ndege ambayo haikuwa na uhakika, ndipo hali ya wasiwasi na mtafaruku kwa Mahujaji ilitanda na kuanza kuongelewa na vyombo mbalimbali vya habari, hadi Serikali kufahamu kuwa kulikuwa na tatizo.

Kuanzia 9/12/07 Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mtendaji, ilibidi wahamie uwanja wa ndege ili kuwafariji Mahujaji na kutafuta ufumbuzi kadri hali ilivyokuwa ikijitokeza. Hata hivyo, ndege haikufika kati ya tarehe 9 na 10/12/07 kama ilivyo ahidiwa na SAMEK Aviation Services kwa visingizio mbalimbali. Baadaye iligundulika kuwa sababu za ucheleweshaji wa ndege hii ni kwamba:-

Ndege hiyo ilikuwa inaendelea kufanya kazi nyingine za kusafirisha Mahujaji kutoka Baghdad kwenda Saudi Arabia.
Mawakala waliokodisha ndege hiyo walishindwa kupata “Slots”.
Hatimaye ndege hiyo ilifika nchini 11/12/2007 bila kuwa na “slots” kama ilivyotarajiwa.

3.0 UUZAJI WA TIKETI KWA MAHUJAJI

Mnamo 20/08/07 Capt. Muze kwa niaba ya Menejimenti aliwasiliana na Taasisi ya Waislam, Tanzania, akiwafahamisha upatikanani wa ndege aina ya Boeing 747-200 na nauli ya kiasi cha dola za Marekani 950 ambayo kila abiria angetakiwa kulipa.

Baada ya majadiliano baina ya ATCL na viongozi wa Taasisi ya Waislam Tanzania, mambo yafuatayo yaliendelea kufanyika:-

Alichaguliwa Afisa Masoko ili ku-“coordinate” uuzaji wa tiketi kwa Mahujaji
Viongozi wa Mahujaji walimchagua Wakala FAST TRACK kuwa wakala wao wa usafiri, hivyo fedha zote kwa mauzo ya Dar es Salaam zilipitia FAST TRACK.
Afisa Masoko alipata kibali toka kwa Mkurugenzi wa Masoko, Ajay, kuingiza ratiba ya safari za Mahujaji kwenye mtandao (Reservation System).
Afisa Masoko alipata kibali kingine kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Eliasaph, cha kuuza tiketi kwa Mahujaji.
Nauli halisi iliyopokelewa na ATCL ilikuwa ni Dola za kimarekani 870 kwa kila Hujaji na pesa taslimu kwa Mahujaji wote ni Dola za Kimarekani 1,248,013 kiasi ambacho ni baada ya makato yote (commission).
Kuweka ratiba ya Hajj Charters kwenye mtandao (Reservation System) ni kuwezesha safari hizi kuuzwa mahali popote ndani na nje ya nchi, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Comoro, Malawi na kadhalika.
3.1 MAPUNGUFU YA NAULI

Baada ya kukosekana kwa ndege toka kampuni ya RAK Leasing, ndege ya DC10 ambayo ilisafirisha Mahujaji imegharimu dola za kimarekani, 1,450 kwa kila Hujaji, wakati nauli iliyotozwa na ATCL ilikuwa ni dola za Kimarekani 870 kwa kila Hujaji. Kwa sababu hiyo, ulitokea upungufu wa dola za Kimarekani 580 kwa kila Hujaji. Baada ya majadiliano kati ya Mwenyekiti wa Bodi na Viongozi wa Mahujaji walikubaliana kwamba Mahujaji walipie dola za Marekani 230 kila mmoja na zilizobaki zitafidiwa na ATCL. Hata hivyo, Mahujaji waliahidi kwamba fedha hizo watazilipa watakaporudi kutoka kwenye Hijja.
Imedhihirika kwamba upo utata katika mkataba kati ya SAMEK AVIATION SERVICES na ATCL kuhusu gharama za nauli. Upande wa ATCL imeeleweka kuwa gharama za nauli ni za kwenda na kurudi, japo katika mkataba suala hilo halijawekwa wazi. ATCL kwa ushirikiano na ubalozi wetu nchini Saudi Arabia wanawasiliana ili kuhakikisha swala hili linaeleweka vizuri kabla ya safari za kurudi kuanza.
4.0 SERIKALI KUINGILIA KATI

Baada ya ndege kuwasili 11/12/07, Manager Flight Operations, Mark Manji aliwasiliana na mwakilishi wa SAMEK AVIATION SERVICES kuhusu suala la “Slots” na alihakikishiwa kuwa “slots” zipo. Wakati wanatayarisha utaratibu wa ndege kuondoka Mark Manji vile vile aliwasiliana na kapteni wa ndege ambaye alimjulisha kuwa kila kitu kilikuwa tayari.

Mark Manji aliwajulisha viongozi wenzake wa ATCL kuwa ndege ilikuwa tayari na abiria waruhusiwe kupanda kwa ajili ya safari. Kabla ya hapo muwakilishi wa SAMEK AVIATION SERVICES, alidai na kukabidhiwa fedha kiasi cha dola za Marekani 160,000 kama malipo ya ziada ya safari ya kwanza.

Abiria walipopanda kwenye ndege uongozi wa ATCL uligundua kwamba ndege hiyo haikuwa na kibali “slots” cha kutua Saudi Arabia. Suala hili lilipojitokeza ungozi wa ATCL haukuwa na namna nyingine yeyote ila kuwashusha abiria waliokuwa wamepanda kwenye ndege. Itakumbukwa kwamba tukio hili lilitokea baada ya Rais na Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine wa Serikali kuwaaga Mahujaji ambao tayari walikwisha hakikishiwa kuwa safari ingekuwapo.

Kadri muda ulivyopita ilidhihirika kuwa SAMEK AVIATION SERVICES walikuwa na mikakati ya ubabaishaji kuhusu upatikanaji wa “slots” na hivyo Serikali iliamua kuingilia kati suala hili. Hatimaye “slots” zilipatikana na ndege ya kwanza iliondoka na kundi la kwanza la Mahujai 11/12/2007.

Bahati mbaya kundi la pili halikuweza kuondoka kwa muda uliopangwa kutokana na ndege kuharibika ilipotokea Madina. Hata hivyo, kundi hilo liliondoka 12/12/2007 saa 11.30 jioni badala ya saa 1.30 asubuhi. Kundi la tatu lilisafiri 14/12/2007 mnamo saa 3.30 asubuhi.

5.0 USHIRIKI WA BODI

Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL ilipanga kuwa na kikao chake cha 16 cha kawaida kuanzia 9/12/07 huko Bagamoyo. Tarehe 10/12/07 asubuhi baadhi ya wajumbe walipokutana iligundulika kwamba Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji hawakuwapo. Wajumbe walifahamishwa kwamba kulikuwa na tatizo kubwa lililohusu kukwama kwa Mahujaji uwanja wa ndege, hivyo Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Menejimenti walikuwa uwanja wa ndege wa Mwl. Nyerere wakishughulikia suala hilo. Wajumbe walifanya kikao cha dharura chini ya uenyekiti wa Balozi (Ami) Mpungwe na kuamua yafuatayo:-

Kuahirishwa kikao cha kawaida cha 16 kutokana na dharura hiyo na hivyo kurudi Dar es Salaam.
Kuagiza Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mtendaji waitishe kikao cha dharura, siku iliyofuata yaani 11/12/2007 ili Bodi ipewe maelezo juu ya suala hilo, ambalo wajumbe wa Bodi walikuwa hawana taarifa yeyote; na
Wajumbe walikubaliana kwa kuwa suala hili walikuwa hawalijui, wasiliongelee popote, hasa kwenye vyombo vya habari.
Kikao hicho cha dharura hakikuweza kuitishwa kutokana na hali halisi ilivyokuwa, hadi ilipofika 17/12/2007.

6.0 ATHARI ZA KIUTENDAJI KWA ATCL

Kutokana na sakata hili la ATCL na Mahujaji, maneno mengi ya kejeli na kashfa dhidi ya Uongozi wa ATCL yamekuwa yakitolewa na baadhi ya Viongozi wa Mahujaji ambayo yanatia dosari kwa Shirika hili.
Kuanzia 10/12/2007 vyombo vya habari vimekuwa vikitoa maoni na maneno yasemwayo na Mahujaji. Mifano michache ni pamoja na:-
- Katibu wa kundi la Mahujaji la AL-BIZ Abdallah Mohamed alikaririwa akisema “Safari hii imeandaliwa na kundi la kisanii – kisanii …. Tutadai haki na fidia kwa ATC”

- Kiongozi wa Taasisi ya MUSLIM Hajj Trust Juma Nchia alisema “watu waliotenda kosa kubwa wanapaswa kukatwa kichwa kwa mujibu wa Dini yao ……….. tutajadili hukumu yake baada ya safari hii kushidikana kabisa”.

- Katibu wa Taasisi ya Alh-Bir Abdallah Harith Mohamed alisema kuwa “waliingia mkataba na ATC baada ya Nyang’anyi ambaye ni Muislamu mwenzetu na mtu aliyewahi kuwa Balozi wa Saudia Arabia, ambaye aliwaomba Waislam wasafiri na ndege yao….”

Aliendelea kusema “sisi tulikuwa tumeachana na Shirika hili kwa miaka 10 … Taasisi zote ziliambiwa kuwa ATC ina ndege ya kukodi Boeing 747-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 480”.
Akalalamika kuwa ATC imewatia hasara kubwa na lazima walipe gharama zote hizi pamoja na fidia ya usumbufu.

- Uzembe huu wa ATC ulitaka kuwasha moto wa hasira ya maandamano kwenye RUN WAY ya ndege ili kuzuia ndege zozote zisiondoke wala kutua uwanjani hapo.

Yote haya yanaashiria kuwa bado Mahujaji kupitia viongozi wao wanatarajia kufanya mamabo yafuatayo:-
Kudai fidia na gharama ya usumbufu.
` (ii) Kuishitaki ATCL kwa kukiuka mkataba.

Kuitaka Serikali kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na kuvuruga safari yao ya Hijja.
Serikali kuwaomba radhi Hadharani kwa usumbufu wowote ule uliotokea.
Kuitaka ATCL kupitia Serikali kuwahakikishia kuwa kosa hili halitarudiwa tena wakati wa kuwarejesha nyumbani Mahujaji.
7.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA BODI

Katika kikao cha dharura kilichofanyika 10/12/2007 huko Bagamoyo na baadaye kuhitimishwa kwa pamoja 17/12/2007 katika Ofisi za ATCL Dar es Salaam, Wajumbe wa Bodi walimtaka Mwenyekiti na Menejimenti ya ATC itoe maelezo ya kina kuhusiana na sakata lote hili kuanzia mwanzo lilipojitokeza hadi tarehe ya kikao hicho. Pia Bodi ilitakiwa kutoa majibu ya masuala yaliyojitokeza kama barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu ilivyokuwa imeelekeza Menejimenti na Bodi kufuatilia kwa undani nini kiliathiri mpango mzima wa safari za Hijja.

7.1 MAELEZO YA MWENYEKITI WA BODI

Bodi ilipata maelezo ya kina toka kwa Mwenyekiti wa Bodi Balozi Mustafa Nyang’anyi na baadaye akayaweka kwenye maandishi.

7.2 MAONI YA BODI

Wajumbe pamoja na kukubaliana na Mwenyekiti kukubali kuwajibika kwa kushawishi Menejimenti kuidhinisha kuingia Mkataba wa ukodishaji wa ndege; Wajumbe waliona kuwa ilikuwa ni kosa kwa kuwaingiza watendaji katika mikataba mizito kama hii, bila Bodi kuhusishwa.

Pamoja na nia nzuri ya Mwenyekiti kutaka kufanikisha safari hii, lakini wasiwasi wa kuwatumia mawakala wa ndege za kukodi bila kutumia taratibu zetu za nchi na Sheria za manunuzi n.k. zinatia dosari utendaji wa Bodi katika kusimamia taratibu hizi.

Ni kutokana na hilo Bodi inaona kuwa Mwenyekiti anastahili kuwajibika na kutoa maelezo hayo kwa chombo cha uteuzi wake ili kusisafisha Bodi na Wajumbe wake ambao hawakuhusika kabisa katika sakata zima la ukiukaji wa taratibu zote za maandalizi ya safari za Hijja.

7.3 MAELEZO YA MKURUGENZI MTENDAJI

Pamoja na maelezo ya kina yaliyojitokeza kama ilivyoainishwa kwenye taarifa yake, kama Mtendaji Mkuu wa Shirika na Mshauri Mkuu wa Bodi, angeweza kukataa ushauri wa Mwenyekiti na kuleta suala hili kwenye Bodi kwa maamuzi. Inaonekana hakufanya hilo na badala yake alikubaliana waendelee na utekelezaji wa ushauri huo kinyume cha sheria, kanuni na maelekezo ya Bodi.

Tatizo hili lilichukua sura mbaya baada ya ATCL kuendelea kuvurugwa na ratiba za ndege hizo za kukodi hata bila Bodi kuwa na taarifa.. Maji yalikuwa yamefika shingoni, hakukuwa na nafasi ya kukwepa mzigo huu.
Mkurugenzi Mtendaji kwa hili, pamoja na barua ya awali ya kutaka kupinga ATCL isijihusishe katika ukodishaji wa ndege za Mahujaji, hawezi kukataa kuwajibika kwa kuwa alikuwa na kila sababu ya kuwajulisha Wajumbe wa Bodi kuhusu mapatano hayo ambayo kiutaratibu yalitakiwa yapate kibali cha Bodi.
Pamoja na uwezo wake mzuri wa kikazi lakini kwa hili anastahili kukiri kosa kwa tabia kama hii.

8.0 MAJUKUMU YA BODI

Kwa mujibu wa majukumu ya Bodi kama yalivyoainishwa kwenye Waraka wenye Kumb. Na. SHC/B.40/6/21 imedhihirika kuwa Menejimenti imesahau na pengine haikufuatilia maelekezo kwenye waraka huo ambao ulifafanua yafuatayo:-

Majukumu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
Majukumu ya Wakurugenzi wa Bodi
Majukumu ya Watendaji Wakuu


Imedhihirika kuwa, wajumbe wamesahau na pengine hawakuyafuatilia maelekezo yaliyomo katika waraka huo. Matukio ya hivi karibuni ya SAKATA la ATCL na Mahujaji, yamedhihirisha udhaifu huo kwa kutozingatia maelekezo na utendaji wa kazi za kila siku.

Bado hatujachelewa, hili ni fundisho kubwa kwa Shirika letu la ATCL katika kusimamia maelekezo yale yote yaliyomo kwenye waraka huo.

9.0 MAJUMUISHO

Katika sakata hili, Bodi imebaini kuwa:-

Utaratibu mzima wa kushughulikia suala hili ulikosewa baada ya Mwenyekiti kuanza kujiingiza kwenye utendaji.
Mkurugenzi Mtendaji hakuwajibika ipasavyo baada ya kuandika barua ya kutoridhia maombi ya Mahujaji na kushindwa kuhakikisha kwamba maamuzi yake ya awali ya kukataa yanatekelezwa.
Uongozi wa ATCL haukuwajibika ipasavyo kwa kuliacha suala hili liwe “one man show” badala ya kushughulikiwa na kamati maalum ya Hijja, yaani “Hijja Committee” ambayo ingehusisha idara ya Masoko, Uendeshaji, (Operations) Fedha na Mwanasheria wa Shirika. Kamati hii ingesaidia sana kugundua mapema kasoro za upatikanaji wa ndege “slots” na vibali vingine na kutafuta mipango mbadala ya kuokoa hali hiyo.
Makabidhiano yaliyofanyika kati ya Mkurugenzi wa Uendeshaji na Afisa Masoko hayakuzingatia taratibu za kiutawala. Kazi hii muhimu ilipaswa ikabidhiwe kwa Mkurugenzi Masoko, ambaye angeweza yeye kwa wadhifa wake kutumia maafisa wengine waliochini yao.
Mwenyekiti wa Bodi alikosea kukutana na Mahujaji na kuwaahidi kuwa ATCL itabeba mzigo wa kutoa ruzuku bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi. Jambo hili lina athari ya kifedha na Bodi ndiyo yenye maamuzi ya mwisho juu ya masuala ya fedha na haswa ambayo hayamo kwenye Bajeti ya Shirika.
10.0 MAPENDEKEZO

Bodi inasisitiza kuwa mamlaka yake ya kiutendaji yasiingilie kamwe shughuli za uendeshaji wa Shirika kama ilivyoainishwa katika Waraka wenye Kumb. Na. SHC/B.40/6/21 wa tarehe 28/3/1994.
Vile vile na Menejimenti isijichukulie mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya Bodi.

Kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa Shirika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria (kushitakiwa) na Mahujaji ni vyema ifanywe mikakati ya kukutana na uongozi wa Mahujaji walioko nchini ili kutafuta muafaka mapema kabla Mahujaji hawajarudi nchini.
Shirika lisijihusishe tena na usafirishaji wa Mahujaji hadi hapo litakapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo baada ya kupata idhini ya Bodi ya ATCL na Serikali.
Kutokana na uzito wa suala lenyewe lilivyojitokeza kwa umma wa Tanzania na ulimwengu kwa ujumla Bodi inapendekeza kuwa Mwenyekiti alitolee maelezo bayana kwa umma kwa jinsi alivyohusika.
Kutokana na kutosimamia kikamilifu suala hili Bodi inapendekeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL apewe karipio ili iwe fundisho kwake.
Bodi itachukua hatua itakazoona zinafaa kwa kuwawajibisha waliohusika katika Menejimenti.
11.0 MWISHO

Bodi ya ATCL inaishukuru Serikali ambayo ndiye mwenye hisa zote za Shirika hili kwa jinsi walivyoingilia kati.

Shukurani ziende kwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa Kamati rasmi ya Komandi ya kuokoa ATCL, Dr. Enos Bukuku kwa kazi nzuri sana waliyoifanya kupunguza aibu ambayo ingetupata.

Tunawapongeza na kuwashukuru Viongozi wa dini ya Kiislamu na Mahujaji wote kwa utulivu na uelewa waliouonyesha wakati wote huu wa usumbufu wa safari yao ya Hijja. Tunaiomba Serikali kwa wakati huu ambao Bodi inajaribu kusawazisha athari hizi mbele ya watumishi na mbele ya Umma wote wa Tanzania, iendelee na Kamati yake (Command Post) hadi Mahujaji watakaporejea.

Ni ukweli usiopingika kuwa Bodi nzima imechafuliwa mbele ya uso wa Watanzania; ni kweli pia Mwenyekiti wa Bodi aliwatenga wajumbe wa Bodi kutowahusisha katika maamuzi makubwa kama haya. Ni kweli pia Mkurugenzi Mtendaji alishindwa kumkatalia Mwenyekiti wa Bodi juu ya ATCL kutokuwa na uwezo wa kuingia katika mikataba ya ukodishaji wa ndege kwa ajili ya Mahujaji.

Lakini ni kweli pia katika hali hii wajumbe wamesononeshwa na kitendo hiki cha Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji kwa kutokutoa taarifa yeyote hata sakata lilipoanza hadi lilipotolewa na vyombo vya habari. Ni matarajio yetu kuwa Serikali italifafanua suala hili vizuri ili UKUNGU uliotanda mbele ya uso wa ATCL uondolewe.
 
Back
Top Bottom