Mgonjwa mwenye 'high cholestral' atumie mafuta gani yasiyoongeza tatizo??

kunguni wa ulaya

JF-Expert Member
Mar 16, 2014
4,132
6,100
Habari wakuu,
Kuna mtu ana matatizo ya high cholestral yanayosababishwa na kula mafuta ya viwandani
swali langu je ni mafuta aina gani ambayo anaweza kutumia ambayo hayatamletea madhara? na hapo awali alikua anatumia sana nazi kwenye kupikia kwa kuzani kuwa hayana matatizo.

Ila kuna mtaalam mmoja anadai nazi zina high cholestral. Je ukweli ni upi kuwa zina madhara au hazina?
Asanteni..
 
Ajifunze kula mchemsho, olive oil ni nzuri lakini ale in moderation kama kunyunyiza juu ya salad. Kuna dawa za regulate cholesterol.
Asante sana.
Na je vipi kuhusu mafuta ya Alizeti na mawese yana madhara kwake?
 
mkuu hili somo ni pana sana na ukitaka elimu yake nipo tayari kukusaidia kwa kina zaidi. ila kiufupi elimu ya lishe ni pana na kunawatu walifanya tafiti wakizaminiwa na baadhi ya viwanda na leo hii wanasema product zao ni nzuri zaid ila si kweli ila kunakitu kimefishwa, na lehemu haisababishwi na mafuta tuu bali vitu lukuki
 
Asante sana.
Na je vipi kuhusu mafuta ya Alizeti na mawese yana madhara kwake?
kulingana na elimu niliyopata mimi alizeti si nzuri ila mafuta ya wanyama, nazi,oliver oil, najua hapo kwenye mafuta ya nyama utapata ukakasi kunielewa ila nipo tayari kufanya uelewe
 
kulingana na elimu niliyopata mimi alizeti si nzuri ila mafuta ya wanyama, nazi,oliver oil, najua hapo kwenye mafuta ya nyama utapata ukakasi kunielewa ila nipo tayari kufanya uelewe
tufahamishe kwa niaba ya wengi
 
Lazima atumie dawa za kutoa mafuta mimi natumia pia zinaitwa LIPISTAD 10 MG
 
Lazima atumie dawa za kutoa mafuta mimi natumia pia zinaitwa LIPISTAD 10 MG
ukipiga zoezi kisha uka switch kutoka kula vyakula vilivyo andaliwa kwa mafuta mpaka vilivyotiwa chumvi tu na viungo vingine pasipo mafuta je haitasaidia? nauliza hivyo kwasabb sipendi vidonge
 
Kuna aina mbili za cholesterol: bad and good cholesterol. LDL (low density lipoprotein) and HDL (high density lipoprotein)

Pure coconut oil has "good cholestrol" i.e HDL
Lakini kumbuka siyo mafuta pekee yanayopandisha cholesterol level above 200mg/dl. Kuna vyakula vingi tu vinasababisha haya majanga.
Plse google utapata elimu pana sana kuhusu hilo tatizo
 
ukipiga zoezi kisha uka switch kutoka kula vyakula vilivyo andaliwa kwa mafuta mpaka vilivyotiwa chumvi tu na viungo vingine pasipo mafuta je haitasaidia? nauliza hivyo kwasabb sipendi vidonge
yes unaweza mbonga za mayani samaki yes you can
 
MAKALA HII YA CHOLESTRO IMEANDALIWA NA Dr BOAZ MKUMBO MD NA KUANDIKWA NA Dr Naha Isaac MD AMBAYE NI RAFIKI YAKE NA BOAZ.

CHOLESTEROL SIO ADUI YETU TENA BILA KOLESTERO HAKUNA UHAI!

Cholesterol( ikitamkwa 'kolesterol') sio neno geni kwa watu wengi. Hata wewe huenda umewahi kuambiwa kuwa cholesterol ni hatari kwa afya yako, hasa ikihusianishwa na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu kwa ujumla. Na watu wengi tumekuwa waaminifu sana wakati mwngine katika kuchagua vyakula na mafuta tunayotumia ili kupunguza kiasi cha cholesterol tunachokula, jambo ambalo ni zuri kabisa; *_kujali afya_*, namimi nalipongeza sana. Lakini kwa bahati mbaya watu wengi sana (wengine wakiwa ni madaktari) hatuna elimu sahihi kuhusu hii Cholesterol: Hivi kwanza cholesterol ni nini? Ni kweli kwamba Cholesterol ni adui mkubwa kwa afya Yangu ama je, ninahitaji cholesterol mwilini mwangu? Vyakula gani vina cholesterol na ninahitaji kula kiasi gani?? Kula cholesterol nyingi kutanisababishia kuwa na cholesterol nyingi mwilini? Kuna uhusiano gani kati ya cholesterol na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu kwa ujumla?
Ni Nani hasa ambaye ndiye adui halisi kwa kadri ambavyo afya ya moyo inahusika? Vipi kuhusu tafiti juu ya hii cholesterol, zinatuambia nini? Vipimo vya maabara kuhusu cholesterol kwenye damu yangu vinasemaje na vina maana gani? Na vipi kuhusu dawa za kupunguza cholesterol; zina msaada gani na je, ni hatari gani zinazomkabili mtumiaji wa hizi dawa? Je, ninaweza kupunguza kiwango cha cholesterol kwenye damu yangu pasi na kutumia dawa yoyote? Haya na mengne mengi ningependa tujifunze pamoja kupitia makala hii ya *Cholesterol Facts*. Ninajua Siwezi kuzungumza kila kitu kuhusu cholesterol, hasa sayansi yake lakini nitatumia lugha rahisi kuelezea mambo ambayo ni ya msingi na ni muhimu kuyazingatia na kuyafahamu.

*_Cholesterol ni nini_?*
Cholesterol ni aina ya mafuta kwa lugha rahisi, kikemikali ina umbo kama linaloonekana hapo juu (Hauhitaji kukumbuka huu mchoro). Mafuta(lipids) yapo ktk namna tofauti japo tumezoea zaid kuyaita mafuta yote _fat_. Cholesterol sio fat,na kuna tofauti kubwa tu kati ya hivi vitu. Kwa mfano ukila _fat_ itameng'enywa mwilini mwako, lakini binadamu hatuna uwezo wa kumeng'enya cholesterol. Tunakula cholesterol, tunaitumia vile ilivyo, na kama hatuitumii, tunaihifadhi; na pia tunaitoa nje ya mwili( we excret it) kama hatuihitaji, lakini hatuimeng'enyi. Hapa swala la muhimu sana kukumbuka ni kuwa cholesterol sio 'fat', ni aina nyingine ya mafuta ambayo ina matumizi tofauti kabisa mwilini.

*_Je, Cholesterol ina umuhimu wowote mwilini?_*
Jibu rahisi ni NDIYO. Kwa ufupi ni kuwa mtu hawez kuishi bila cholesterol (no cholesterol, no Life). Najua utashangaa kusikia hivyo lakini ndio ukweli; ngoja nikupe mifano michache tu ya kazi za cholesterol katika mwili wako:
1. Mwili wako umetengenezwa na muunganiko wa chembechembe ndogo zinazoitwa seli(cell). Hizi ndizo zinakutengeneza wewe, na michakato yote mwilini mwako hutokea ndani ya seli, ukila chakula ni kwa ajili ya seli; usipokula kwa mda mrefu, seli zinakufa. Hakuna kiumbe hai chochote bila seli. Seli ndio uhai( _a cell is th basic unit of life_). Sasa kila seli mwilini mwako inahitaji cholesterol ktk ukuta wake.. bila cholesterol seli haziwez kuhimili mabadiliko joto ktk mwili wako; na uimara wa seli unategemea sana hii cholesterol. Kila unapotengeneza seli mpya unahitaji cholesterol na seli hutengenezwa kila siku mwilini. Bila choleterol hakuna seli na bila seli hakuna uhai.
2. Cholesterol hutumika kutengeneza homoni mbalimbali mwilini ambazo huratibu michakato mbalimbali. Mfano ni homoni iitwayo Calcitrol ambayo huratibu kiwango cha madini ya calcium mwilini. Madini ya Calcium ni muhimu sana kwa uimara wa meno na mifupa. Pia kusinyaa na kutanuka kwa misuli(muscles) ya mwili hutegemea haya madini ya Calcium. Bila hii homoni mifupa na meno vingeyeyuka na sehem kubwa ya mfumo wa fahamu ingeshindwa kufanya kazi. Misuli yote ingesimama bila calcium, hii ni pamoja na misuli ya moyo. Unafikiri nini kinafuata baada ya moyo kusimama? Uko sahihi; ni Kifo.
Homoni zingine zinazotegemea cholesterol ktk utengenezaji wake ni Aldosterone, testoterone, estrogen, progesteron, Cortisol na nyingne nyingi ambazo hatuwez kutaja kila moja kazi zake.
3. Cholesterol ni mojawapo ya malighafi muhumu katika utengenezaji wa nyongo. Nyongo ni muhimu sana katka umeng'enyaji(digestion) wa vyakula vya mafuta aina ya Fat. Na Karibu asilimia sitini (60%) ya ubongo wako ni Fat. Bila cholesterol fat haiwezi meng'enywa na ubongo utakosa fat, na hatimaye Maisha hayatawezekana.
4. Ubongo hutumia karibu 20% ya cholesterol yote mwilini mwako. Kiwango kidogo cha cholesterol kweny ubongo kimehusianishwa na uwezo mdogo wa ubongo kufanya kazi kama vile kupoteza kumbukumbu na uwezo mdogo wa utambuzi (cognitive functions). Pia mawasiliano ktk ubongo (synaptic connections) huhitaji cholesterol. Seli maalum za ubongo ziitwazo _glial cells_ zimepewa uwezo wa kutengeneza cholesterol kwasababu hii.
5. Cholesterol inasaidia katika kupambana na baadhi ya maambukizi (inflammatory infections) mwilini inapokuwa katika kiwango cha kutosha.

Hii ni mifano michache ya matumizi mengi ya cholesterol mwilini mwako.
Kitu kikubwa cha kujifunza leo ni kuwa Cholesterol ni aina ya mafuta ambayo ni muhimu sana katika mwili wa binadamu yeyote. Maisha hayawezekani bila chilesterol. Na huu sio mtizamo wangu, ni ukweli ambao umethibitishwa kwa majaribio na tafiti za kisayansi.

***** **** **** ******
Lakini kwanini kwa miaka mingi tumefundishwa kuwa cholesterol ni mbaya na ni hatari?
Vyanzo vya cholesterol ni vipi na je tunahitaji kula kiasi gani ili tupate cholesterol ya kutosha, hasa baada ya kuwa tumeona umuhimu wake? Je miili yetu ina uwezo wa kutengeneza cholesterol? Kuna uhusiano gani kati ya cholesterol iliyoko mwilini mwako na chakula kinachotoka jikoni kwako au hoteli au cafe au kwa mama ntilie; kiwe protein, wanga au mafuta?Kula cholesterol nyingi je, kutanisababishia kuwa na cholesterol nyingi mwilini mwangu? Kwani ni nini sababu ya kuwa na kiasi kikubwa cha cholesterol mwilini? Kuna hatari yoyote kuwa na kiasi kikubwa cha cholesterol mwilini??

Tutajikita katika kuangalia vyanzo vya cholesterol na uhusiano uliopo kati ya cholesterol iliyoko mwilini na ile iliyoko kwenye chakula. Je ni kweli kuwa kula Choleaterol nyingi ni hatari kama tulivyoaminishwa kwa miaka mingi?

Kabla hatujaingia hasa katika somo, napenda nielekeze jambo fupi ambalo litatusaidia sana hapo baadae, Japo haya maelezo yako 'technical' kuliko ambavyo ningependa yawe, lakini ni sehemu muhimu sana itakayotuwezesha kuelewa mambo mengi baadaye:
Cholesterol ipo katika namna mbili mwilini: kwanza; inaweza kuwa _huru_(free/ Unesterified Cholesterol[UC], ambapo huwa peke yake bila kuungana na kitu chochote; na pili huweza kuwa katika muungano na molekuli zingine(Esterified Cholesterol, ama Cholesterol Ester [CE]).
Ni hii Cholesterol Huru(UC) ambayo inaweza kuyonzwa na kuingia mwilini.

Ukishaielewa dhana hii iweke akiba, kisha tuendelee:

*_Vyanzo vya Cholesterol Mwilini ni vipi?_*

Tunapata Cholesterol mwilini kupitia namna mbili: katika chakula tunachokula na mwili kujitengenezea Cholesterol wenyewe. Watu wengi hawajui kuwa sehemu kubwa ya Cholesterol katika mwili wetu( zaidi ya 75%) ni ile inayotengenezwa na mwili, sio ile inayoliwa katika chakula.

A: _Vyakula gani vina Cholesterol?_
Kila chakula kinachotokana na wanyama ni chanzo cha Cholesterol. Kumbuka kuwa kila mnyama ana cholesterol katika seli zake. Baadhi ya vyakula hata hivyo, mfano maini, kiini cha yai, ubongo na mafuta(cream) ya maziwa, vina kiwango kikubwa zaidi cha Cholesterol.

HAKUNA KABISA CHOLESTEROL KATIKA VYAKULA VITOKANAVYO NA MIMEA. Niliwahi kusikia mahali fulani wakina mama wakielekezana kupunguza ama kuepuka kabisa matumizi ya nazi kwa kuwa ina Cholesterol nyingi. Huenda hata wewe unafahamu hivyo au umewahi kusikia hivyo. Hii si kweli. Badala yake katika mimea kuna kemikali iitwayo _phytosterol_, ambayo naweza kusema ndio 'mbadala' wa cholesterol katika mimea. Phytosterol haina kazi yeyote katika mwili wa binadamu na hivyo inapoliwa hutoka bila kufyonzwa.

B: *_Uhusiano kati ya Cholesterol iliyoko mwilini mwako na Cholesterol unayokula_*: _Je, kula Cholesterol nyingi kunaweza kunifanya niwe na Cholesterol nyingi mwilini?_

Kila seli mwilini ina uwezo wa kutengeneza Cholesterol lakini ni seli za ini pekee zenye uwezo wa kutengeneza Cholesterol nyingi kuliko mahitaji yake. Ini linatengeneza 20% ya Cholesterol yote unayoitengeneza kila siku.
Pia mwili una namna ya kudhibiti Cholesterol na kuhakikisha kuwa ipo katika kiwango sahihi. Tujifunze sayansi hii kidogo:

Cholesterol hufyonzwa katika utumbo mwembamba kupitia molekuli(molecule) zinazoitwa NPC1L1( huhitaji kukariri). Kama mwili hauhitaji Cholesterol,mathalani kinapokuwa kimefyonzwa kiwango kingi kuliko mahitaji; molekuli ziitwazo ABCG5/8 (huhitaji pia kuikariri) huirudisha katika mfumo wa chakula ili iweze kutolewa nje kama uchafu. *_Hii ndio sababu kubwa kwanini haiwezekani mtu akawa na cholesterol nyingi mwilini kutokana na kula chakula chenye cholseterol nyingi._*
Lakini kuna point nyingine hapa: mwili huweza kufyonza Cholesterol huru pekee(free/unesterified Cholesterol,UC). Rejea maelezo niliyokwambia uyatunze kama akiba maana ni kiini katika somo la leo. Zaidi ya 70% ya cholesterol iliyoko kwenye chakula sio _free cholesterol_ , ni ile _Esterified cholesterol_hivyo haitafyonzwa kuingia mwilini.
Vilevile, kiwango kikubwa cha hii _free Cholesterol_ iliyopo kwenye mfumo wetu wa chakula ni ile iliotengenezwa mwilini na kuletwa kwenye ini, kisha katika mfumo wa chakula kwa njia ya nyongo. Zaidi ya 85% ya cholesterol inayofyonzwa toka katika mfumo wa chakula ni hii tuliotengeneza wenyewe, Sio tuliyokula.

*_Je, Cholesterol ni hatari kwa afya ya binadamu?_*
Jibu rahisi kabisa ni Hapana, kama mwili una afya kamili. Dhana ya kuwa Cholesterol ni hatari ni moja ya dhana ambazo kwa miaka mingi zimefundishwa kwa upotoshwaji mkubwa. Baadae tutaona jinsi ambavyo kuihusianisha Cholesterol na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu ni sawa na kusema gari la ambulance limesababisha ajali kwa kuwa tu limekutwa katika eneo la ajali wakati kumbe lilikuja kwa ajili ya kusaidia katika eneo la tukio. Kwa sasa itoshe tu kusema kuwa cholesterol pekee haina ubaya wala madhara kiafya katika mwili wenye afya kamili. Kama umewahi kusikia juu ya Cholesterol mbaya na nzuri, yaani LDL na HDL( kama hujawahi sikia bado hakuna kilichoharibika), tutazifafanua zaidi baadaye na kuona uwongo ama mkanganyiko uko wapi.

Makala ijayo tutajibu maswali yafuatayo:
_Kama kula cholesterol nyingi hakuweza kusababisha cholesterol nyingi mwilini, ni nini kinasababisha Cholesterol kuwa nyingi mwilini?_
_Kwanini sukari, na wanga hasa iliyokobolewa(refined carbohydrates) huathiri sana kiwango cha Cholesterol, japo havitokani na wanyama?_
_Cholesterol mbaya(LDL) Cholesterol nzuri (HDL) Je, kosa liko wapi katika tafsiri ya hivi vipimo vya maabara?_
Tukutane katika makala ijayo.

_Summary ya makala ya Leo:_
1. Cholesterol mwilini ipo katika namna mbili: Free Cholesterol (UC) na Esterified Cholesterol (EC). Ni _free Cholesterol_ pekee inayoweza kufyonzwa na kuingia mwilini
2. Sehemu kubwa ya cholesterol tunayokula ni EC, hivyo haifyonzwi na kuingia mwilini.
3. Sehemu kubwa ya cholesterol inayofyonzwa toka katika utumbo ni ile tuliyotengeneza sisi wenyewe ktk miili yetu, sio ile tunayokula
4. Kiwango cha cholesterol katika mwili wako huwekwa katika msawazo kwa ustadi wa hali ya juu. Mtu hawezi kuwa na cholesterol nyingi mwilini kwasababu tu ya cholesterol anayokula
5. Cholesterol _pekee_ sio hatari kwa afya ya binadamu.

Makala hii imeandaliwa na Dr Boaz mkumbo na ni daktari mzoefu ila nimeamua kuileta hapa kwaajili ya kusaidiana na kupeana elimu kulingana na mada na vile niliahiji jana kufanya
 
Back
Top Bottom