Mgongano wa fikra huzaa mawazo mbadala siyo uhaini

Goliath mfalamagoha

JF-Expert Member
Aug 3, 2012
602
2,505
MGONGANO WA FIKRA HUZAA NJIA MBADALA.

Ni kweli kuwa mashaka ni mbegu imara katika mioyo ya wanadamu, Mashaka huziongoza hatua zetu kwa tahadhari katika makwazo magumu kabisa na kuyashinda.
Licha ya kutupa hatua za tahadhari lakini hutuwezesha kutupa nguvu na akili ya dhiada kuepuka viashiria vibaya na vyenye kughasi bidii na matamanio yetu.

Mtu asiye na akili ya mashaka atapotea na maisha yake yatakosa dira , matendo yake yatafananishwa na mtu anayetembea katika giza nene pasipo msaada wa chombo cha kufanyiza mwangaza.

Kiwango cha mwanadamu kukosa au kutoruhusu mawazo ya tahadhari ni kiwango kibaya kabisa, macho ni taa ya mwili na mashaka ni taa ya nafsi na akili mambo haya yapaswa kwenda kwa pamoja siku zote.

Kwani waweza kukiona kitu kwa macho lakini katika uhalisia kinaweza kikawa na sifa, tabia au maana tata zaidi ya ulivyokiona ilikuondoa utata huo mashaka huhitajika kuingilia kati ilikuzaa akili ya utafiti na udadisi kuelekea ugunduzi wa kweli.

Kwa mantiki hiyo matokeo ya udadisi na utafiti ni mazao ya fikra njema za mashaka ya mwanadamu mwenyewe.

Kwa mambo makubwa na yenye manufaa kwa umma haihitajiki mashaka ya mtu mmoja pekee kuwa ndiyo muongozo wa mafanikio na bidii zote.

Lazima kuwepo na tukundi twingi twenye kuzaa mashaka na kupitia mashaka yao ndimo ambamo watu hujitahidi kufanya udadisi wa kila tendo liibukalo kwenye jamii na kutoa kauli za tahadhari na suluhisho lake.

Katika siasa kunawatu ambao hujishughurisha na kazi za mashaka hawa huwa kama "alarm" kwa kila jambo litendwalo na wenye nguvu.

Kazi ya kuwashauri (kuwapa mashaka na tahadhari) watu wenye nguvu huhitaji nguvu vilevile kwani wengi hujihisi kudharauliwa na kushushwa thamani.

Huwenda ni kwa sababu ya ulevi wa madaraka ama ni kwa sababu ya kiwango kidogo cha hekima walicho nacho katika kufikiri ?, bado sijajua na wala sitaki kujishughurisha kujua ukweli wa jambo la pili ila la kwanza.

Ulevi wa madaraka huwafanya waathiriwa wa ulevi huo kujiona wao ni kila kitu katika nchi na bila wao nchi si chochote na wala si lolote, ulevi huu huwafanya wajione wanakiwango kikubwa na uwezo wa ajabu katika kufanya maamuzi ya busara kuliko mtu yeyote ila wao pekee.

Inapotokea mtu akajitokeza na kutowa mashaka yake kama sehemu ya kuwapa tahadhari huhisi kushushwa thamani na kudharirishwa ukuu wao hatua pekee ni kumtendea kinyama ama kupewa kifungo cha mateso na kazi ngumu.

Watu hawa badala ya kuitwa washauri huitwa wachochezi na wahaini wakubwa wasio na mema kwa mataifa yao.

Yaani kukosoa mienendo ya kiongozi hufananishwa na kuiweka rehani mihimili na uhai wa taifa huu ni ulevi mbaya wa mtu mmoja kujiona yeye ndiye nchi na nchi ndiye yeye kama ilivyokuwa kwa Mfalme Louis XVI kule ufaransa aliyejihalalisha kuwa yeye ni nchi na yeye ni sheria,ulevi mbaya huu!.

Wakati fulani aliyekuwa rais wa Congo- Zaire ya zamani dikteta Mobutu sese seko alitamka kuwa '' si daiwi chochote na nchi ila nchi inadeni na mimi kwa kila kitu".

Akimaanisha ufisadi na matendo ya anasa na rushwa alizokuwa anazifanya zilizowatia zaidi wananchi wake hasara ilikuwa ni kielelezo cha nchi kulipa deni kwake hivyo hakuhitaji kuwa mwema kwa wadeni wake ila kuwafukarisha.

Huyu alisahau kuwa yeye kwa nafasi yake ndiye mwenye deni la kuwajibika kwa raia badala yake akaigeuza nchi na raia kuwa wadeni wake binafsi pamoja na familia yake.
Na pindi alipokosolewa kwa nia ya kumrudisha kwenye mstari wa wema na wajibu wake aliwaita wachochezi na wahaini hukumu yake haikuruhusu hewa iambae puani mwao hakuchelewa dakika ileile, alitenda unyama!.

Na ulevi huu umekuwa gonjwa baya lililotapakaa kwenye akili za viongozi wengi barani Afrika hata sasa, kama si nusu yao basi zaidi ya nusu ya viongozi wapo kwenye hali ya kupepesuka kwa ulevi huu wa madaraka, inakatisha tamaa.

Kumkosoa kiongozi kwa nia ya kuonesha mashaka ya ubaya juu ya kitu fulani, kwa viongozi wetu huhesabika kama alama ya ukosefu wa uzalendo na kushuka kwa kiwango cha heshima kwao.

Uzalendo kwa Afrika ya leo ni kushangilia na kuwa mtiifu kwa kila jambo watendalo viongozi wakati viongozi kama Nyerere, Mandela na akina Kaunda waliogopa sana kusujudiwa Afrika ya sasa inapenda kusujudiwa kuliko kitu chochote.

Zao la kizazi cha Nyerere limepotea na kuwa haba sana kupatikana vizazi vya akina Idd Amin na akina Mobutu limetamaraki na kuwa tishio kuu miongoni mwa wapenda haki na demokrasia.

Aboubakar Siddiki kiongozi wa chama cha upinzani kaskazini mwa nchi ya Cameroon hivi karibuni alihukumiwa miaka 25 jela na mahakama ya kijeshi pasipo ushahidi wowote kwa kutuhuma za kuikosoa serikali.

Ipo mifano mingi inayoweza kuelezea namna viongozi wa bara hili wasivyopenda kukosolewa maisha ya vijana wenye fikra njema kwa ajili ya nchi zao yapo hatiani kila wakati.

Vyombo vya habari vingi vimegeuka kuwa wapiga zumari wa watawala habari za kufurahisha na zisizo na maono ya changamoto hupewa kipaumbele kuliko zile zenye kuonya na kutahadharisha.

Watawala wetu lazima watambue kuwa mawazo yao ni bora lakini pasipo fikra za dhiada zenye changamoto kwao ubora wa fikra zao itakuwa ni maangamizi na taabu kwa wanaowatawala.

Waswahili wanamsemo wao kuwa huwezi kujua ukubwa wa msitu ukiwa katikati ya msitu, viongozi wajue wao ni kama watu waliokatikati ya msitu kujua baya na jema au faida na athari za atua ama mawazo yao haitegemei maono yao pekee bali fikra za walio nje ya mfumo wa serikali ambao ndio waathirika wa faida na athara za mawazo yao.

Mwaka 1995 serikali ya Sani Abacha ilimnyonga mtetezi wa haki za watu wa Ogoni na mwanaharakati wa mazingira dhidi ya uchafuzi wa makampuni makubwa ya mafuta.

Kama ilivyo kwa wengine Ken alitowa tahadhari kwa viongozi lakini kwa kuwa Abacha aliihesabia akili yake kuwa alpha na omega leo hii uchafuzi wa eneo hilo madhara yake yamekuwa makubwa kuliko madhara ya uchafuzi wa sehemu yeyote duniani.

Na licha ya utajiri wa mafuta watu wa Ogoni mpaka leo wanaishi katika hali ya mashaka ya umaskini na hofu ya magonjwa ya kulipuka kwa magonjwa kutokana na uchafuzi mbaya.

Lazima viongozi wetu wa bara hili waruhusu watu kukuza hisia na fikra za mashaka na kuwa huru kuweka tahadhari zao pasipo bughuza wala ubabe na jeuri za kimabavu na pia viongozi wenyewe wawe tayari kuskiliza hatakama hawakubaliani na mawazo.

Kwani mgongano wa mawazo huzaa njia nyingi za kutimiza jambo lakini tukiruhusu kuskiliza mawazo ya wanaotuunga mkono tutabaki na njia moja pasipo kujua changamoto wala mbadala wake.

Hata mtunzi wa kitabu cha Mithali alipata kuandika kuwa "Pasipo mashauri taifa huanguka,Bali kwa wingi wa mashauri huja wokovu" Mith 11;14.

Ushauri ni kati ya mambo bora kabisa ambayo mwanadamu yeyote anapaswa kuyafurahia na kuyatii pale anapopata mwanya kuyaskia.

Hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliowahi kufanywa na kuthibitisha kuwa ushauri ni sumu iwezayo kuuwa wala hakuna ushahidi wowote wa kihistoria uliowahi kueleza kuwa mtu fulani alipata ukilema au alipoteza maisha yake pale alipothubutu kuwa mtiifu kwenye mambo ya ushauri.

Ushauri huonesha njia na hutoa tahadhari ya dira kwa mambo ya msingi na ya muhimu kutendwa, ni ukweli kuwa si kila ushauri wapaswa kufwatwa lakini hiyo haiondoi wajibu wa mtu kuuskiliza.

Utawala wa kimabavu na ubabe mwingi ulionekana kuwa bora kwa zama za zamani lakini kwa sasa wakati wake umepita na ubora wake hauna maana ila uharibifu na uchafuzi mtupu wa ustaarabu wa kidunia, amani na haki.

Kuzuia nguvu za hoja kwa mitutu ni fikra mgando na kuporomoka kwa kiwango cha uadilifu na utu kazi ya kiongozi si kuuwa watu wake bali kuwalinda, si kuwatesa bali kuwatendea kindugu busara ya jambo hili ni bora mara mia kuliko ovu lolote lile liinukalo

Tupo katika mfumo wa kidemokrasia lazima tuheshimu na tuendane na mifumo ya kidemokrasia, uongozi wa kijeshi hauheshimu haki za kiraia kwa sababu kuingia kwake haukuzingatia milango ya kiraia.

Lakini inakuwa ajabu kuona kiongozi wa kidemokrasia anatenda kama kiongozi wa kijeshi ni aibu na ni hasara kwa umma na kwa taifa muda wa kujitathimini upo Afrika inaweza kuwa njema tukiruhusu michango ya kila mtu kuwa daraja.
 
Back
Top Bottom