Mgomo wa Madaktari hautaisha kwa vitisho na Dola; ni kwa Makubaliano tu!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,460
39,928
Kuwalazimisha madaktari kurudi kazini mara moja ama sivyo watajifukuzisha kazi hakubadilishi ukweli wa hali iliyopo. Hata kuwabembeleza warudi kazini mara moja kwa sababu “wagonjwa wanakufa” nako hakubadilishi hali iliyopo. Kwa ufupi, agizo la serikali kutaka madaktari warudi kazini mara moja linapuuzia kabisa madai yao na linatumia ubabe wa madaraka na bila ya shaka nyuma yake kuna tishio la nguvu za dola kulazimisha madaktari. Kwa vile sababu za msingi zilizosababisha mgomo hazijashughulikiwa – hata zile zinazoweza kushughulikiwa mara moja – basi sababu ya uwepo mgomo haijaondolewa au kupunguzwa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye ametoa tamko la kuwataka madaktari kurudi kazini


Serikali inaweza kulazimisha madaktari kurudi kazini?
Serikali ina uwezo wa kulazimisha watu warudi kazini lakini haina uwezo wa kulazimisha watu kufanya kazi. Kwa kutumia tishio au hata nguvu serikali inaweza kuvunja mkutano wa madaktari na kuwakamata viongozi wa mgomo huo na yumkini madaktari wanaweza “kurudi kazini”. Hata hivyo madaktari “kurudi kazini” haina maana wanarudi “kufanya kazi”. Wataweza vipi kufanya kazi yao vizuri kwa uadilifu kama msingi wa malalamiko yao umepuuziwa zaidi ya kuambiwa “madai yenu ni ya msingi na tunayafanyia kazi?”

Kwa vile serikali haiwezi kulazimisha watu kufanya kazi wazo kuwa madaktari wanalazimishwa kurudi mahospitalini katika mazingira yale yale, yakiwa na vikwazo vile vile ni wazo la hatari. Hivi ni kweli tunaamini kuwa madaktari hawa waliopuuzwa, kudharauliwa na kunyanyaswa wakirudi kuangalia wagonjwa kesho watafanya hivyo vizuri zaidi? Hivi kweli serikali inaamini kuwa maisha ya wagonjwa mikononi mwa madaktari waliopuuzwa yako salama kwa vile madaktari “wamerudi kazini”?

Mgomo wa madaktari husitishwa kwa makubaliano
Mgomo wa madaktari hauwezi kuisha kwa kulazimisha au vitisho kwani kwa kufanya hivyo serikali itajikuta inapanda mbegu za mgomo mwingine labda mkubwa zaidi kuliko wa sasa. Huko India mwishoni mwa mwaka jana (kuanzia Disemba 21) madaktari waligoma jimbo la Jaipur. Mgomo wao ulidumu kwa siku 11 na madaktari zaidi ya 10,000 walishiriki. Mwisho serikali ikawaweka ndani madaktari wapatao 500 lakini mwisho wa siku – na baada ya wagonjwa 60 kudaiwa kufa kwa sababu ya mgomo – serikali ilikubali kuwaachilia madaktari wote toka jela, na kuondoa adhabu ya sheria ya kutokugoma na kukubali kuyafanyia kazi madai ya madaktari. Tarehe 1 Januari madaktari wakarudi kazini baada ya makubaliano ya kusitisha mgomo siku moja kabla yake.

Huko Israeli nako madaktari waligoma mwaka jana kufuatia suala la maslahi vile vile. Mgomo wao ulidumu kwa siku 158 na mwisho wake mwezi Augusti ulikuwa ni makubaliano ambayo serikali ilikubali kuongeza mishahara ya madaktari na kuboresha mazingira yao ya kazi. Badala ya madaktari kusubiri kufukuzwa madaktari walijiuzulu (mass resignations) katika kuonesha kuwa hawakuwa tayari kuburuzwa na serikali. Waziri wa Fedha wa Israeli akitangaza kuishia kwa mgomo huo alikiri kuwa wamefikia makubaliano na madaktari ambayo yamemaliza “mojawapo ya migomo mikubwa zaidi katika historia ya Israeli”. Waziri Mkuu Netanyahu alijikuta akikubali kuwa matokeo ya mgomo ule ilikuwa ni kuboresha maslahi ya madaktari lakini vile vile kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa huduma za afya nchini Israeli.

Huko Kenya vile vile mgomo wa madaktari wa mwishoni mwa mwaja jana uliishia kwa kufikia makubaliano na serikali ambapo serikali ilikubali kuongeza fedha katika kuboresha miundombinu ya afya, kulipa madeni ya nyuma ya madaktari na kutenga fedha zaidi katika mafunzo n.k Mgomo wao uliodumu kwa siku 10 nao ulimalizwa kwa makubaliano.

Kwa ufupi, mgomo huu wa kitaifa wa madaktari haupaswi kumalizwa kwa vitisho, kejeli, kupuuzia au dharau. Mgomo unatakiwa kumalizwa kwa makubaliano. Ndio maana ninaamini bila makubaliano mgomo huu unaweza ukazua mgomo mkubwa zaidi kwani mambo ya msingi hayajakubaliwa. Na kwa kweli haupaswi kuisha bila kuweka makubaliano ya msingi ili kuondoa ulazima wa kugoma tena muda si mrefu ujao.

Kanuni za Makubaliano
Sasa, kuna msingi wa kusitisha mgomo ambao unategemea kanuni kadhaa. Naamini, makubaliano ya kusitisha mgomo huu lazima yazingatie lau kanuni zifuatazo.

a. Wagonjwa wapate nafuu – makubaliano yahakikishe kuwa mwisho wa siku ni wagonjwa wanaopata nafuu katika huduma, matibabu na kupona. Utakuwa ni mgomo mbovu kama baada ya makubaliano maisha ya wagonjwa wetu yanarudi pale pale. Hivyo, mambo yote yatakayokubaliwa lazima yazingatie kuwa Wagonjwa wetu wanapatiwa unafuu wa gharama, huduma, na ubora wa hali ya juu wa huduma hiyo. Nje ya hapo mgomo utakuwa umefeli.

b. Maslahi ya Madaktari ni lazima yaboreshwe na kuinuliwa. Lengo la (a) haliwezi kufikiwa kama madaktari wataendelea kufanya kazi katika miundo mbinu mibovu na hali mbovu ambazo zinawafanya wasiwe makini au waadilifu. Hata mtu anayejitolea anaweza kujitolea zaidi kama kujitolea kwake kunaonekana na kunawezekana. Hivyo, mishahara na posho za madaktari ziongezwe lau kufikia kiasi wanacholipwa Wabunge. Posho za mazingira magumu, on-call, midnight shifts etc ziongezwe mara moja. Kama tunaweza kumpa mbunge shilingi 200,000 kwa kukaa (azungumze au asizungumze) tunaweza kumlipa daktari kiasi hicho kwa zamu ya usiku au mazingira fulani fulani yatakayokubaliwa. Bila ya shaka maslahi ya wafanyakazi wote wa huduma ya afya ni lazima yaangaliwe kwa upana wake. Hili linaweza kuchukua muda mrefu kidogo kukamilika.

c. Serikali ni lazima itenge fedha za kutosha kuboresha miundo mbinu ya afya ikiwemo suala la nishati, madawa, na vitendea kazi mbalimbali. Hospitali za serikali ni lazima ziwe na kiwango fulani kisichopungua cha vifaa (minimum standard) ili hospitali ifanye kazi. Serikali ni lazima iwekeze vya kutosha kwenye huduma ya afya ili ndani ya miaka angalau mitatu hii kabla hawajaondolewa madarakani- waoneshe kuwa wamebadilisha sekta hii kwa kiasi kikubwa. Siyo kwa kuongeza “idadi” bali kwa kuongeza “ubora”! Katika kuboresha huduma wa sekta ya afya serikali ni lazima iwawabishe viongozi na watendaji ambao wamechangia kufikisha nchi mahali hapa.
Hivyo, basi kwa kuzingatia kanuni hizo tatu naweza kutoa mapendekezo ya mambo ambayo yanapaswa kukubaliwa na madaktari na serikali ili kusitisha mgomo huu mara moja.

Serikali:
1. Kufukuzwa mara moja kwa Waziri wa Afya, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Daktari Mkuu. Hili ni jambo msingi la kwanza kufanywa na serikali kwani hawa watatu walikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa madaktari hawafikii mahali pa kugoma. Ushahidi wote uliopo wazi hadi hivi sasa umetuonesha kuwa watu hawa watatu wametumia ubabe, dharau na kejeli na kulazimisha mgomo huu. NI LAZIMA WAONDOKE KABLA Mgomo haujasitishwa.

2. Kutenga fedha za kulipa madeni ya nyuma ya madaktari pamoja na kutenga fedha za kuongeza posho za msingi ambazo zinahusiana na mazingira ya kazi, na usafiri. Kwa vile tayari tunajua serikali inaweza kuongeza posho katikati ya bajeti kwa wabunge tunajua basi inawezekana kufanya hivyo kwa madaktari. Ongezeko la posho hizo liendane na ongezeko la posho walizopewa wabunge. Madaktarii wawe tayari kuahirisha kuongezewa posho hizo endapo posho za wabunge nazo zitafutwa au kupunguzwa.

3. Serikali itenge fedha sasa hivi kwa ajili ya kufanyia matengenezo vifaa ambavyo havifanyi kazi kwenye mahospitali yetu ikiwemo uagizwaji wa wa vifaa vya kisasa vya kutolea huduma. Kama serikali inaweza kuagiza magari mapya kwa watendaji mbalimbali wa serikali kila mwaka wakati umefika kwa serikali hiyo hiyo kukubali kuagiza vifaa vipya. Kwa kuanzia hospitali zote za mkoa zipatiwe CT Scan kabla ya mwisho wa mwaka huu pamoja na wataalamu wa vifaa hivyo. Hii inazingiatia kanuni ya (a). Vile vile hili linaweza kupatiwa motisha wa kodi (tax incentive). Kama kuna kodi kwenye vifaa vya afya wakati umefika kufuta kodi hizo ili kurahisisha uingizwaje wake nchini.

4. Serikali ijiwekee viwango (standard) za huduma za afya ambavyo wananchi watarajie kuona kwenye hospitali zao za umma. Hospitali za Umma lazima zionekane zina ubora wa kuweza kushindana na zile za binafsi.

5. Serikali ifanyie mabadiliko ya sheria inayowapa viongozi haki ya kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa gharama za wananchi. Kwa kadiri ya kwamba viongozi wanahaki hiyo hawawezi kuboresha sekta ya afya kwani mahospitali yetu yatakuwa ni mahali pa kupata rufaa tu za kwenda nje. Kiongozi anayetaka kwenda nje ajipeleke kwa fedha zake mwenyewe au jamaa zake au ndugu zake. Kuendelea kuruhusu hilo ni kuendelea kuruhusu kuvuja kwa fedha zetu kwenda nje ya nchi. Endapo viongozi watajua kuwa wao na watoto wao watatabiwa hapa hapa nchini wataona umuhimu na uharaka wa kuboresha hospitali zetu. Kinyume chake wao wanafikiria kuboresha “hospitali zetu” wakati wenyewe wako tayari kwenda kutibiwa kwenye “hospitali za wenzetu”.

Kama serikali haitofanya hivi ni matumaini yetu wabunge wa upinzani (ambao nao ni wanufaika wa mfumo huu) wataandaa mswada binafsi wa kuondoa hivi vipengele. Viongozi pekee ambao kwa muda wanaweza kuruhusiwa kuendelea kuangaliwa nje ni wale waliokwisha staafu na wao watapewa nafasi hiyo kwa mwaka mmoja ujao tu baada ya hapo na wao lwao!

6. Serikali iwe tayari kwa kushirikiana na madaktari kuunda a Special Task Force ambayo itapitia sera na mfumo wetu wa afya na kutoa mapendekezo ndani ya miaka mitatu ya mabadiliko makubwa ya sekta ya afya. STF hiyo iundwe na madaktari na wataalamu wa afya, wa fedha, na wanasheria ili hatimaye ije na mapendekezo ambayo yataanza kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu ili kufanyia mabadiliko makubwa mfumo wetu wa huduma za afya (major healthcare reform). Waangalie, tatizo liko wapi, fedha zinapotea wapi, nini kibadilishwe na vipi na mwananchi atanufaika vipi katika mabadiliko hayo. Mfumo wa sasa siyo endelevu ni mzigo mkubwa kwa wananchi.

Madaktari

1. Kama sehemu ya kuonesha wanajali madaktari watangaze kurudi kazini mara baada ya uongozi wa sasa wa Wizara ya Afya kujiuzulu. Mgomo huu kwa kiasi kikubwa umesababishwa na hawa viongozi kwa hiyo kuumaliza ni lazima hawa waguswe. Wafanyakazi wa afya hawawezi kufanya kazi na hawa watu tena – wamepoteza moral legitimacy kuongoza wizara hiyo hasa baada ya kuachilia vifaa vibovu vya kupima HIV kuendelea kutumika nchini na pia kudharau madai ya madaktari hadi mgomo umetokea. Ni lazima waondoke kama sharti la kwanza la madaktari kurudi kazini na kuzuia wauguzi na wataalamu wengine kujiunga kwenye mgomo huu.

2. Madaktari wawe tayari kupata ongezeko dogo katika mishahara na mafao mbalimbali wakisubiri STF ije na mapendekezo yake na bajeti mpya. Kiasi gani wakubali inategemea na ofa itakayotolewa na serikali.

3. Madaktari wawe tayari kurudi kazini mara moja endapo serikali itatenga fedha za dharura kununulia vifaa vya msingi vya huduma ya afya kwa mahospitali yote ya umma. Vitu kama maglovu, sindano, nk ni vitu ambavyo ni lazima viwepo hospitalini. Serikali ikubaliane na madaktari kuwa ndani ya miezi mitatu hospititali zote za umma na za binafsi zitatakiwa kuwa na vifaa vya msingi vya kutolea huduma ya afya. Hii ni pamoja na kutenga fedha za kuhakikisha kuwa hakuna mgonjw anayelala chini kwenye wodi yoyote ile au hospitali yoyote ile. Hii ni mojawapo ya kashfa kubwa za huduma ya afya nchini ni lazima tuondokane nayo.

4. Madaktari kwa kutumia hiyo STF waandae mapendekezo ya kuboresha elimu na ujuzi wa madaktari ili hatimaye tuweze kupata madaktari wengi zaidi kwa muda mfupi zaidi. Je, nini kinaweza kufanyika kuharakisha mafunzo ya madaktari yenye ubora wa hali ya juu? Hatuwezi kutumia mfumo wetu wa zamani wa kuandaa madaktari kwani itatuchukua muda mrefu sana kuweza kuziba pengo. Lazima tutumie uwezo wetu kubuni mfumo mzuri wa kufundisha madaktari ili kwa haraka – ikiwezekana ndani ya miaka mitano hivi tuweze kuongeza idadi ya madaktari kwa kiasi kikubwa.

Hayo ni baadhi ya mambo tu yanayoweza kukubaliwa na pande mbili ambayo matokeo yake yatakuwa ni manufaa kwa wananchi. La msingi ni kuwa hatuwezi na hatupaswi kuahirisha huu mgomo kwa vitisho isipokuwa kwa makubaliano. Kuwapa amri madaktari kurudi kazini mara moja ati kwa kufikiria kwamba wasiporudi basi wanafukuzwa kazi na Tanzania italeta madaktari kutoka nje ni kujaribu kukwepa tatizo. Kwanini?

a. Madaktari wa kigeni hawatakuja kwa kujitolea nao bado watahitaji kulipwa kwani na wenyewe wanatakiwa kuishi maisha ya utu na kufanya kazi mazingira mazuri.

b. Madaktari mbadala nao wataenda kufanya kazi kwenye mazingira yale yale. Kitakachokuwa kimebadilishwa ni madaktari tu na siyo mazingira ya kazi. Hivyo, wataweza kufanya kazi kwa siku, wiki au mwezi lakini baada ya muda na wao wenyewe watakufanya na yale yale ambayo yametufikisha hapa. Kuleta madaktari wa nje, kutazuia kuvuja kwa damu tu lakini hakutakuwa kumetoa tiba ya kidonda!

c. Madaktari wetu wenyewe ni madaktari wetu kuwafukuza kazi au kuwaweka nje kwa sababu wamekataa kurudi kazini hakutaondoa
ukweli kuwa mfumo wetu wa afya ni mbovu na watu wanakufa pasipo ulazima – bila haja ya mgomo! Madaktari wetu wanagombania kitu kikubwa zaidi hao madaktari mbadala watakuja kutibu tu lakini hawatokuja kupigania kuboresha mfumo wetu wa afya.

d. Wakileta madaktari wengine halafu wauguzi, madaktari wa meno, madaktari wa dawa ya usingizi nao wakagoma kuunga mkono madaktari wao serikali italeta wauguzi kutoka India, Misri na Israeli? Au mwisho italeta hadi wafagizi kugoka nje?
Kwa ufupi, agizo la Waziri Mkuu kuwa madaktari warudi kazini mara moja bila kufanya nayo makubaliano ni sawasawa na kujaribu kumaliza vita bila kufanya mapatano ya kumaliza mgogoro. Vita havimalizwi kwa truce bali kwa kufanya mapatano ya kumaliza vita (cessation of hostilities). Hili linaweza kufanywa ama kwa kusalimu amri (surrender agreement) ambapo mshindi anatoa terms of surrender (ndivyo inaonekana serikali inafanya) au kwa pande mbili kuona kuwa vita havilipi na hivyo wanaamua kupatana. Ninaamini, serikali inataka kulazimisha surrender bila kupatana.

Hii ni hatari kwa huduma ya afya. Ni makubaliano tu yatamaliza mgogoro, makubaliano ambayo yatazingatia madai ya madaktari, yatakubali na kuanza kutekeleza sehemu ya madai hayo kama hatua za kujenga imani na vile vile kuweka utaratibu wa kuona mambo mengine yaliyokubaliwa yanatimizwa bila kuchelewa na katika muda muafaka.

Nje ya hapo, mgomo huu utaduma na hautakoma kwa haraka au kwa vitisho kwani hata madaktari wakikubali kurudi kazini, hakuna mtu anayeweza kuwalazimisha kufanya kazi, na hata wakilazimika kufanya kazi watakuwa wamepewa sababu nyingine ya kufanya mgomo mwingine huko mbeleni. Ndugu zangu, ni bora ujue madaktari wamegoma na wamegoma kuliko kutokujua kuwa daktari anayekuhudumia amegoma moyoni.

Lakini hakuna kibaya zaidi kama kumshambulia mtu badala ya hoja. Katika vitu vya kushangaza sana Waziri Mkuu ameamua kufanya mashambulizi ya mtu – ad hominem – kwa Dr. Ulimboka katika kuonesha kuwa hoja za madaktari hazina msingi. Hivi, ni kweli kuwa Dr. Ulimboka akiacha kushiriki kwenye mgomo huu manake ni kuwa madai ya madaktari yanafutika? Serikali inaweza kabisa kushambulia watu au mtu yeyote katika kujaribu kuonesha kuwa inawajua watu hao na inaweza kuwasema vibaya vyovyote vile lakini ukweli wa hoja zao utasimama ulivyo.

Ukiona watu wanamshambulia mtu badala ya hoja zake, manake ni kuwa tayari wameshindwa hoja sasa wanataka kutumia nguvu! Kama watu wengine wanavyouliza mbona hatujaambiwa mambo ya wabunge ambao wamesimama kutetea posho? Au na yeye watu waanze kuulizia kwanini anatetea wafanyabiashara wakubwa kuchukua maeneo makubwa ya ardhi nchini? Hoja zijibiwa kwe hoja siyo viroja!

Ni hatari kwa wagonjwa.
kwa wagonjwa.
 
Mgomo wa madaktari hauwezi kumalizwa vizuri kwa vitisho au kulazimisha kwa kutumia dola. Unaweza kumalizwa kwa makubaliano tu.

Naunga mkono hoja lakini kwanza kabisa lazima wakutane! wasipokutana na kuzungumza, nothing will work out! Kwa nini leo hawakukutana?
 
Makubaliano ni muhimu sana. Lakini mbona madaktari hawakutaka kukutana na PM? Hayo makubaliano bila mazungumzo yatapatikanaje kwa njia ya kuandikiana barua?

Kimbunga, hakuna mtu aliyekataa kukutana na PM, hizo ni porojo za kisiasa za kutaka ku'win PUBLIC!!...KAma we ni msomaji mzuri wa JF updates zote zilikuwa zinatolewa humu, ni jana tu ndo walimuandikia barua (na yeye alikiri kuipata) kumwomba kwamba wakutane kesho Jtatu badala ya leo Jpili kwa sababu za msingi kabisa...Sasa kama alishajua kwamba leo hawatakuja ukumbini, alifuata nini na watu wake kibao??? HIZI ZOTE NI PROPAGANDA TU ZA KISIASA
 
Mwanakijiji M.M naomba ushauri huu au mawazo yako yaandikwe gazetini,maana nimesikiliza tamko la PM nimesoma bandiko lako nimeona mawazo yako ndio yalitakiwa ayatoe PM wakati akijadiliana na M-dr,na Tamko la PM ni kama tamko la mtu ambaye alikuwa anapiga porojo wala hakuwa amejiandaa ku-address issue kubwa kama hii,sijui tatizo liko wapi kwa viongozi wetu,sijui ni kweli kwamba wao wanaamini kila migomo inayotokea hapa nchi inakuwa backed up na Chadema?
Please mwanakijiji naomba mawazo haya yawe published soon kwenye moja ya print media.
 
In February 2008, Pinda was sworn under the oath of protecting and defending watanzania. Surprisingly, he looks helpless, whilst Tanzanians are dying as a result of an avoidable strike. We have become a ‘strike republic'.

Nchi za wenzetu madaktari wanakuna vichwa jinsi gani ya kuja na Medical Breakthroughs, sisi, wanakuna vichwa jinsi gani ya kupambana na uzembe wa serikali na siasa zake. Tatizo ni kwamba, Tanzania, sekta ya Afya inaendeshwa kisiasa, kuanzia process ya kuandaa bajeti, allocation of resources, to the management of the sector. Na mfumo wetu bado n ule ile wa enzi za welfare and developmental state.

Pinda angetumia busara zaidi kwa kusisitia umuhimu wa kubadilisha mfumo mzima wa sekta afya, ili awe ukurasa mmoja na moja ya madai ya madaktari kwamba uongozi wizarani ni mbovu. Ameshinda nini kutoa tamko kama alilotoa bungeni wakati wa sakata la Jairo? Angesema tu kwamba Rais yupo nje, akirudi, tutaliangalia hili, hasa la kubadili mfumo wa sekta ya afya. Then Rais angefanya tu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri lengo likiwa ni kubadili mfumo wa wizara uliopitwa na wakati, ili kuondoa ufisadi na siasa. Kwa ahadi hii tu, madaktari wangepata moyo kwamba wanasikilizwa, hivyo wangerudi makazini, huku serikali ikiahidi kushughulikia mengine, especially in the context of the next budget ya June 2012.

Kuanzia bajeti ijayo, serikali ingeachana tabia mbovu ya kutenga 75% of the budget kwa matumizi ya wizarani, na hospitali za rufaa na taasisi za kitaifa (humo humo ikiwa ni pamoja na posho, mishahara, tiba za wakubwa nje), huku hospitali nyingine za mikoa, wilaya, na zahanati vijijini ziikipata the remaining 25%, ambayo hata hivyo, zinaishia mikoani mifukoni mwa wachace, na baadhi ya wilaya. Ndio maana unakuta wataalam wengi wanakimbilia up the ladder (hospitali za rufaa, taasisi kadhaa za afya, na baadhi ya mikoa), kwa sababu huku ndio kuna more resources allocated, hivyo kupelekea ‘too much manpower to chase too few resources'. Many years ago, pia African Union walikubaliana kwamba kila nchi itenge 15% ya bajeti yake kwa ajili ya sekta ya Afya. Since then, Tanzania haijawahi kufikisha anything beyond 8%.

Iwapo Mizengo Pinda angeahidi haya - kufumua sekta ya afya na pia kubadilisha how resources are being allocated in the sector, hapo Pinda angekuwa in-line na kiapo chake cha to protect and defend watanzania, na sio kuachia watanzania wafe kwa mgomo unaotatulika.
 
Naunga hoja 100%,makala nzuri yenye ufafanuzi wa kina,nadhani ujumbe umefika.
 
Tusipoangalia mgomo huu utakuwa ni Richmond ya Pinda - utaondoka naye.

Hata mimi nina mashaka sana maana nimekuwa nikijaribu kuzungumza na hawa ma-dr baadhi yao waliopo hapa Dar na wengine na wengine walioko Dodoma wao wanasema kwa kauli ya Pinda hata Ermegency wanasitisha rasmi,isije kweli ikawa nae ndo Richmond yake
 
Kwa taarifa nilizonazo ambazo ni za uhakika hadi usiku huu,wale madaktari wa Intern walikuwa wanaendelea na mkutano this night,wanajadili tamko na jinsi ambavyo wamepokwa haki ya kukutana kuzungumzia mstakabali wao.
 

Ukiona watu wanamshambulia mtu badala ya hoja zake, manake ni kuwa tayari wameshindwa hoja sasa wanataka kutumia nguvu! Kama watu wengine wanavyouliza mbona hatujaambiwa mambo ya wabunge ambao wamesimama kutetea posho? Au na yeye watu waanze kuulizia kwanini anatetea wafanyabiashara wakubwa kuchukua maeneo makubwa ya ardhi nchini? Hoja zijibiwa kwe hoja siyo viroja!

Ni hatari kwa wagonjwa.
Very well said MMJ...salute you.....on top of every thing..the doctors have the moral support from the majority of Tanzanians...so they should not give up to threats from this pathetic government....even nurses will join them in this en devour..all the best docs
 
Ukiona watu wanamshambulia mtu badala ya hoja zake, manake ni kuwa tayari wameshindwa hoja sasa wanataka kutumia nguvu! Kama watu wengine wanavyouliza mbona hatujaambiwa mambo ya wabunge ambao wamesimama kutetea posho? Au na yeye watu waanze kuulizia kwanini anatetea wafanyabiashara wakubwa kuchukua maeneo makubwa ya ardhi nchini? Hoja zijibiwa kwe hoja siyo viroja!

Ni hatari kwa wagonjwa.

Kaka hapa umenena,OMBI langu naomba um faxie JK huko aliko nakala kwa Sifue na Pinda.
 
serikali ya ccm imezoe kuwatishia waalimu ambao wengine vyeti wanatumia vya ndugu zao sasa hapa inaongea na wasomi wa kuanzia level ya degree lazima serikali iweke kiburi pembeni
 
Ndugu Mwanakijiji na Mchambuzi,

Hii article itakuwa ni busara angalau zikachapwa kwenye moja ya magazeti yetu ili Pinda and Co wajue kuwa brains and thinking zao zimekuwa mfu. Watanzania majority pamoja na kunyimwa elimu lakini wanajitahidi kuwa na upeo, busara and above all kuwa well informed kwani wanaona kuwa madai ya madaktari ni ya msingi. Propaganda walizozoea kuwa zinafanyakazi miaka ya nyuma zimepitwa na wakati.
Nawasilisha.
 
Kimbunga, hakuna mtu aliyekataa kukutana na PM, hizo ni porojo za kisiasa za kutaka ku'win PUBLIC!!...KAma we ni msomaji mzuri wa JF updates zote zilikuwa zinatolewa humu, ni jana tu ndo walimuandikia barua (na yeye alikiri kuipata) kumwomba kwamba wakutane kesho Jtatu badala ya leo Jpili kwa sababu za msingi kabisa...Sasa kama alishajua kwamba leo hawatakuja ukumbini, alifuata nini na watu wake kibao??? HIZI ZOTE NI PROPAGANDA TU ZA KISIASA

Mkuu hizo upadate za JF ni tofauti na alichokisema PM. Sababu za msingi za kutokutana na PM ilikuwa ni kusubiri wenzao waliokuwa wakitoka mikoani!
 
Sasa propaganda hazitasaidia sana kwani watu wakiishafunguka ni kazi sana kuwatudisha katija utumwa kifikra.
 
PM alitakiwa kwanza kabisa kuwakemea vikali watendaji wa wizara ya afya (Waziri, Naibu na Katibu Mkuu) kwa kushindwa kuutatua mgogoro huu mpaka yeye kulazimika kuingilia kati. Lakini kinyume chake amewaachia watendaji hawa wamjaze majungu, fitina na ujinga mwingine kuhusu madaktari mpaka kufikia kuongea mambo ya ajabu badala ya kujibu hoja za msingi....Jamaa kweli ni hopeless!!
 
Kwanza huu n mgomo ambao ungeweza kuepukika mapema kweli lakini hapa ulipofikia si pazuri kabisa.
 
26 Reactions
Reply
Back
Top Bottom