Uchaguzi 2020 Mgombea Urais wa Chama cha CUF, Prof Lipumba atema madini kupitia kipindi cha Dakika 45

Makala josee

JF-Expert Member
Aug 15, 2020
499
437
Ikiwa ni kipindi cha wagombea kunadi sera zao kwa wapiga kura kabla ya zoezi zima la mchakato wa kuwapata viongozi Wakuu wa kitaifa hapo Oktoba 28, Mgombea Urais kupitia Chama cha Civic United Front (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba amefanya mahojiano katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa kupitia kituo cha ITV. Mahojiano hayo yameendeshwa na mtangazaji Bi. Farhia Middle.Mtangazaji: Profesa, habari za kwako?

Prof. Lipumba: Salama. Nashukuru kwa kunikaribisha. Ahsante sana!

Mtangazaji: Unaendeleaje?

Prof. Lipumba: Mimi naendelea vizuri. Alhamdulillah!

Mtangazaji: Tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu kama ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza. Kwa mtazamo wako, tangu kuanza kwa shughuli za kampeni Agosti 26, hali ya kisiasa kwa ujumla unaionaje kwa maana umekuwa mshiriki wamasuala ya kisiasa kwa muda mrefu, Profesa?

Prof. Lipumba: Hali ya kisiasa, kwanza hali ya uchumi ya vyama hasa vya upinzani, ni hali ngumu kidogo. Tunajikuta kuweza kufanya kampeni nchi nzima inabidi kutafuta msaada toka kwa wanachama waweze kutusaidia ili tuweze kukamilisha kampeni zetu.

Mtangazaji: Ni nini kimesababisha hali ya uchumi kuwa ngumu kidogo kwa vyama, kama ambavyo umesema?

Prof. Lipumba: Kwanza hali ya uchumi kwa Watanzania kwa ujumla, hali ya fedha kwa Watanzania. Ajenda ya kusema kwamba vyuma vimekaza ni kweli n ahata wafanyabiashara pia wanakuwa na wasiwasi, mzunguko wa fedha umekuwa ni mdogo, kwahiyo michango yao kwenye vyama vya siasa unakuwa mgumu. Wengine wanaogopa tu kuwa wakifanya hivyo inaweza kuwaletea matatizo.

Mtangazaji: Profesa umesema na umeeleza hapa kwamba kwa wananchi suala la fedha kidogo limekuwa ni changamoto, lakini nyie bado munarudi kwa Watanzania na kuomba wawachangie. Sasa fedha Watanzania watatoa wapi hasa?

Prof. Lipumba: Sisi tunarudi kwa Watanzania kwasababu tunahitaji kuleta mabadiliko.Na tunahitaji kuleta mabadiliko kwasababu hali ya maisha ni ngumu. Kwahiyo kwa Mtanzania, mathalani tulitoa wito kila Mtanzania ajiwekee walau lengo la Shilingi 100 kwa siku katika siku hamsini, sitini anaweza kutuchangia Shilingi 6000.

Ikiwa watapatikana Watanzania nusu milioni watakaotuchangia Shilingi 100 kila siku kwa siku 60, maana yake ni kwamba tutapata shilingi bilioni 5, ziatutosha kufanya kampeni nchi nzima. Hata ukiwa na hali ngumu ukichangia shilingi 100 haiwezi kuongeza ugumu wa Maisha uliyo nayo. Hata mwananchi wa kawaida anaweza akajitolea shilingi 100 kwa siku, siku 50, siku 60. Maana yake ni shilingi 5000, shilingi 6000. Tukipata watu milioni moja, Watanzania milioni moja wakituchangia shilingi 100 kila siku kwa siku kwa siku 50, maana yake ni kwamba tunapata shilingi bilioni 5 na kampeni yote tutamaliza vizuri kabisa.

Lakini pia kuna wafanyabiashara wakubwa, watuchangie. Kwasababu katika chama ambacho kinahitaji waweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanya biashara, ya uwekezaji -- mazingira mazuri ya ujasiriamali – chama cha CUF kina sera ambazo zinamuwezesha mfanyabiashara aweze kufanya biashara kwa amani, alipe kodi kwa amani na mazingira ya kufanya biashara yawe mazuri.

Mtangazaji: Profesa unagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chako cha wananchi, CUF. Kwanini unautaka Urais wa JMT?

Prof. Lipumba: Mimi nagombea Urais nah ii itakuwa ni mara ya 5 kugombea Urais wa JMT. Kwasababu kwa rasilimali ambazo Tanzania tunazo na umoja wa Watanzania. Watanzania tuna lugha moja ya Kiswahili, hatuna matatizo makubwa sana ya ukabila ama udini ama ubaguzi, kwa sisis kwakweli tunapaswa kuwa taifa ambalo limepiga hatua kwa rasilimali tulizo nazo. Lakini la kusikitisha, Watanzania walio wengi ni masikini wa kutupwa. Hata tafiti za serikali na takwimu za serikali, kwa kipato ambacho wanasema kwamba Mtanzania wa kawaida katiak jiji kama la Dar es Salaam akipata shilingi 50,000 kwa mwezi, yeye siyo masikini.

Hata kwa kigezo hicho, utakuta kuna Watanzania zaidi ya milioni 14 ambao ni masikini wa kutupwa. Na ukichukuwa kigezo cha kimataifa caha kutumia dola 1 na senti 90, zaidi ya nusu ya Watanzania ni masikini wa kutupwa. Baada ya karibuni miaka 60 ya kupata uhuru wa nchi hii na miaka 56 ya Muungano, hatupaswi kuwa masikini kiasi hiki.

Na mimi fani yangu imekuwa ni kufanya utafiti na kufundisha habari ya maendeleo ya uchumi. Moja ya kitu ambacho kilinisukuma kuwa mgombea Urais ni kwamba nilipokuwa nafundisha Marekani, vijana wa Kimarekani walikuwa wanasema: ‘Mwalimu tinakusikiliza, tunakuelewa, unatoa hoja nzuri. Lakini, kwanini nchi yako bado masikini?’

Kwahiyo nimepata fursa ya chama cha CUF ambacho sera yake ya msingi ni Haki sawa kwa Wananchi Wote – haki za kiuchumi, haki za kijamii, haki za mazingira, haki za kisiasa. Nikaona hii ni fursa na niweze kufafanua hizi sera na Watanzania wakazilewa. Na kwakweli natoa wito kwa Watanzania waweze kuelewa sera zetu za Haki Sawa na Furaha kwa Wananchi Wote.

Mtangazaji: Profesa, unadhani kwako itakuwa ni rahisi, maana kuna baadhi ya watu, najua na wewe unasikia wakisema Profesa si mpinzani halisi, Profesa ana vinasaba kidogo na chama tawala. Na sasa unataka Urais wa JMT. Pengine unadhani kuna changamoto hapo katikati itajitokeza?

Prof. Lipumba: Hiyo ni propaganda na nyie pia mmesaidia kuisambaza propaganda hiyo. Kama kuna mpinzani ambaye anasimamia hoja, hakuna mtu ambaye amekuwa anaihoji CCM kwa hoja za msingi kama Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.

Mtangazaji: Prof. Lipumba umeeleza hapa kwamba sasa ni mara ya tano unagombea nafasi ya Urais wa JMT. Kwa aana kwamba ulianza mwaka 1995 ambapo Tanzania iliingia kwenye uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi, na umekuwa ukikosa kura. Pengine, 2020 hii ni nini ambacho unadhani kinakupa jeuri kwamba lazima ushiriki katika uchaguzi huu?

Prof. Lipumba: Kwanza kinachonipa jeuri hivi sasa, kama hamna vyama vya siasa ambavyo vinajenga hoja, vinawashawishi wananchi, na sisi chama chetu kinaungwa mkono na wananchi wa kawaida kwasababu ya hoja ya Haki Sawa na Furaha kwa Wananchi Wote.

Kwahiyo sisi tunakuwa tuna jukumu kubwa kwamba, kwakuwa chama tawala chenyewe si chama cha siasa, ni chama cha dola, lazima tuweze kujenga hoja, tuweze kuwafikia wananchi, wanachi watuelewe kwamba hoja zetu za msingi ni kuweza kujenga nchi inayoheshimu Haki za mwananchi wa kawaida, ambayo itatumia rasilimali na mali ya asili ya nchi hii kuweza kuboresha Maisha, kutokomeza umasikini – kuhakikisha kwamba njaa na utapiamlo, ukosefu wa lishe bora unaondoka katika nchi yetu na huduma za msingi za afya zinapatikana.

Kwahiyo, kwa hoja zetu naamini tutaweza kuwafikia wananchi na ninakushukuru kuweza kunikaribisha katika kipindi hiki kwasababu ni njia mojawapo ya kuweza kufikisha hoja zetu kwa wananchi. Hoja zetu wakizijua, wanachi watatuunga mkono, wataniunga mkono na kwenye sanduku la kura watampigia Prof. Ibrahim Haruna Lipumba

Mtangazaji: Profesa, chama tawala kinajinasibu kwamba kimefanya mambo mengi kwaajili ya maendeleo ya Watanzania katika masuala ya madaraja, katika masuala ya barabara, katika masuala ya elimu, katika masuala ya maji na mambo mengine mbalimbali. Na kwa sasa kinaendelea kujinadi kwamba kitaendelea kumalizia shuguli zile ambazo zilianzishwa lakini bado hazijakamilika, na wewe unataka Urais wa JMT. Unadhani nini hasa kati ya haya ambayo Watanzania bado hawajafanyiwa na wanataka kufanyiwa?

Prof. Lipumba: Ukitaka kukipima chama utazame zile sera ambazo wamezieleza na kuzipitisha kwenye Bunge. Ukitazama katika kipindi hiki cha awamu hii ya tano, Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miaka Mitano ulipitishwa kwenye Bungu mwaka 2016. Lakini, ukitazama katika maelezo yao yote hawaelezi wameutekelezaje Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambao ndio ulipitishwa rasmi kwenye Bunge, amabao unakamilika kwenye mwaka huu wa fedha 2020/21.

Hawaelezi. Hata kama ulikwenda kwenye mkutano wa CCM walipokuwa wanatoa maelezo yao, hawaelezi ule mpango ambao wameupitisha rasmi ndani ya Bunge na wakasema kwamba baada ya miaka miwili tutaufanyia tathmini kuona tumeutekelezaje. Hawauzungumzii kabisa. Kwahiyo hoja yangu ya msingi ni kwamba serikali ya CCM imekuwa ina sera nyingi au imekuwa na maamuzi mengi kwenye majukwaa ya siasa, lakini yale ambayo wamesema watayatekeleza, wakayaweka ndani ya mpango, hayo hayakuongeza utekelezaji wa serikali ya CCM.

Mtangazaji: Profesa, wewe ni mtaalam wa masuala ya Uchumi na ni mshauri pia wa masuala ya Uchumi. Unataka mabadiliko katika Uchumi wa Tanzania. Ni lazima ushike wadhifa wa Urais wa JMT ndipo ulete mabadiliko kwenye masuala ya Uchumi?

Prof. Lipumba: Mimi nimekuwa mshauri wa mambo ya Uchumi na baada ya kuwa mshauri nikaona ni vizuri zaidi badala ya kuwa mshauri niwe ndiye ninayeongoza jahazi hilo, kwamba kwa uzoefu nilio nao ukipata fursa hiyo ya kuongoza jahazi unakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuweza kuyatekeleza masuala haya.

Si masuala tu, bali masuala ya kujenga nchi ya kidemokrasia. Nchi ambayo wananchi wake wako huru; nchi ambayo wananchi wake hawaogopi, wanajua kuwa wakifuata sharia hawatakuwa na tatizo. Kwahiyo mambo haya ya kujenga nchi ya demokrasia nan chi ambayo ina uchumi unaokua na kuongeza ajira ni jambo ambalo ndiyo ninalifanya mimi niweze kujitokeza kugombea nafasi ya Urais wa JMT.

Mtangazaji: Kwahivyo ukiwa nje ya ofisi ya Rais wa JMT kidogo inakuwa tatizo katika suala zima la kuiletea nchi yako mabadiliko katika masuala ya Uchumi?

Prof. Lipumba: Tunatoa ushauri. Ushauri unakubaliwa au unakataliwa. Mathalani, kwa muda mrefu na zungumza kwamba ili uweze kuwa na mapinduzi ya viwanda ni lazima kwanza uweze kuwa na mapinduzi ya kilimo. Uweze kuwekeza kwenye sekta ya kilimo. Walau tuwekeze 10% mpaka 15% ya bajeti kwenye sekta ya kilimo. Wakulima wetu waweze kupata elimu ya kilimo bora. Waweze kupata pembejeo. Waweze kupata mbolea. Waweze kupata masoko ya uhakika. Waweze kupata bei nzuri. Ili kilimo kikue.

Kilimo kinapokua, kwanza unazalisha chakula kwa wingi kwahiyo gharama ya chakula inapungua. Gharama ya chakula inapopungua, unaongeza uwezekano wa kuongeza ajira katika sekta nyingine ikiwemo sekta ya viwanda. Vilevile, kilimo ndiy kibatoa malighafi ya kuingia katika sekta ya viwanda na kutengeneza chakula, kutengeneza nguo, kutengeneza viatu na bidhaa zingine za ngozi.

Mambo haya ukiyatekeleza unaweza kuwa na mapinuzi makubwa ya viwanda. Lakini serikali yetu, katika miaka hii mitano iliyopita, katika kila shilingi 100 zilizotumiwa na serikali, fedha iliyokwenda kwenye sekta ya kilimo ni chini ya shilingi 3. Na hii imo katika, ukitazama kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa. Ni chini ya Shilingi 3. Katika miaka mitano huwezi kuleta mapinduzi ya kilimo ukiwa hauwkezi kwenye kilimo. Na kama haukuwekeza kwenye kilimo hauwezi kuwa na mapinduzi ya viwanda, ukaongeza kasi ya kukua kwa viwanda na kuongeza ajira kwenye viwanda.

Kwahiyo tunasema kwamba, tunatoa ushauri na katika kushiriki katika siasa michango yetu sisi mingine inakuwa kwamba hata kabla hujawa Rais, lakini unakuwa umechangia. Tumezungumzia kwamba sisi jamani rasilimali nyingi tunatapeliwa. Kwnye madini, kwenye kila dola 100 serikali inalipwa dola 3. Hii mikataba mibovu, wakapinga CCM.

Lakini awamu hii ya 5 walau wakakubali kwamba hii ni mikataba mibovu lazima tutengeneze sharia mpya, lazima tuirejee mikataba hii.

Kwahiyo michango yetu ni kule kujenga hoja na ndiyo maana kwangu muhimu ni kule kujenga hoja, hoja ambazo hata chama kingine kikiona hizo ni hoja nzuri kuweza kuzichukua, mimi nashukuru na ninafurahi.

Mtangazaji: Ilani ya chama chako, Chama cha Wananchi – CUF, inaakisi haya ambayo unatueleza?

Prof. Lipumba: Bila shaka. Katika ilani yetu ya Uchaguzi ya chama cha CUF. Kwasababu kaulimbiu yetu ni Haki Sawa na Furaha kwa Wote. Sasa unapataje haki sawa na furaha kwa wote, tunaeleza sasa sera ambao zinaweza zikatuletea mambo hayo. Na jambo moja la msingi kaika ilani yetu, na hili naomba Watanzia walifahamu, sisis tunazungumza kwamba ikiwa mtanichagua mimi kuwa Rais, basi bila shaka nitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iweze kukamilisha Katiba yenye misingi yenye demokrasia ya kweli ambayo itawapa uhuru wa kweli Watanzania.

Tukubaliane sisi kwa pamoja kama Watanzania kwamba hii ndo inapaswa kuwa dira ya nchi yetu. Na hii ndiyo Katiba ambayo sisi sote tutaiheshimu. Tulipiga hatua fulani; Tume ya Jaji Warioba ilitoa rasimu lakini jambo hilo halikukamilishwa. Ili tulikamilishe vizuri, na vyama vingine vikikubali hii sera na mimi nitashukuru, kwamba tuunde serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuweza kuweka maridhiano kikamilifu, kupata Katiba ambayo ina misingi mizuri ya demorasia, inaheshumu Haki za Binadamu, itakayohakikisha kwamba sisis sote tunaiheshimu hiyo.

Na kwakuwa nchi hii ni ya muungano wa nchi mbili, basi pande zombe mbili za muungano ziweze kukubaliana kwamba hii ni Katiba inayoakisi yale mambo ambayo tunahitaji Ktiba iyasimamie. Kwahiyo tunahitaji Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hiyo serikali ya Umoja wa Kitaifa itasiamamia mambo gani? Sisi tunazungumzia masuala ya Haki – haki za kiuchumi, haki za kisiasa, haki za kijamii. Na mambo haya ambayo tumeyazungumza, tumeanza kuyazungumza tangu 1995. Kwa bahati hata jumuiya ya kimataifa imeweza kuyachukua na kuyafanya kuwa ni Malengo ya Maendeleo Endelevu – Sustainable Development Goals. Sisi tulikuwa tunazungumza hili tokea 1995/2000.

Ndiyo maana ilani yetu ya uchaguzi inazingatia pia utekelezaji wa sera ambazo zitahakikisha kwamba tunautokomeza umasikini, tunahakikisha kwamba elimu iliyo bora inakuwa ni haki ya kila Mtanzania. Na tunajenga misingi ya Wananchi kuweza kujielimisha katika maisha yao yote. Na hivi sasa elimu iliyopo inaendana na matumizi ya internet, matumizi ya mitandao. Tunahitaji tokea shule za msingi mpaka za sekondari Watoto wetu waweze kutumia kompyuta. Mitandao hii iweze kufikia kila shule kusudi Watoto waweze kujifundisha kutokea awali kuweza kuwa na ushindani na jumuiya ya kimataifa.

Tunahitaji kuwekeza kwenye afya, kuwekeza kwenye lishe ya kina mama wajawazito. Tunapozungumzia Hakisawa kwa wote, tunasema kwamba Haki inaanzia mtoto akiwa tumboni mwa mama yake mpaka anapokuja kuwa mzee
 

NAWATAFUNA

JF-Expert Member
Nov 14, 2019
13,306
23,826
Nipo hapa, na remote nimeishika mimi, hivi vitoto vya tamthilia visije vikahamisha chanel nikakosa madini ya prof.
 

Reykijaviki

JF-Expert Member
Aug 25, 2020
412
637
Hahahahah prof ccm wanampenda balaa! Nadhani wanamtumia katika ushauri wa mambo mbalimbali.
 

Bulesi

Platinum Member
May 14, 2008
12,619
11,297
Nipo hapa,na limoti nimeishika mimi,hivi vitoto vya tamthilia visije vikahamisha chanel nikakosa madini ya prof.

Madini atayatoa wapi na yeye hana mgodi? Pengine akawe muajiliwa wa Laizer kule Merelani!
 

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,259
8,795
Mgombea wa urais aomba kila mwananchi amchangie 100/-

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Vyama vya Upinzani vinakabiliwa na hali ngumu kiuchumi na vinafanya kampeni kwa shida.

PUMBA ED.jpg


Akihojiwa katika kipindi cha 'Dakika 45' cha ITV kilichorushwa usiku wa kuamkia leo, Profesa Lipumba alisema vyama vinaomba michango kutoka kwa wanachama na wananchi wengine ili kufanya kampeni nchi nzima.

Alisema inabidi kutafuta misaada kutoka kwa wanachama ili kusaidia kufanya kampeni na kwamba chama chake kinaomba Watanzania kukichangia walau Sh. 100 kwa kila mwananchi.

"Kwanza, hali ya uchumi ya Watanzania kwa ujumla ni mbaya, hali ya fedha, agenda ya vyuma vimekaza ni kweli, wafanyabiashara wamekuwa na wasiwasi kwamba wakifanya hivyo (kutoa mchango kwa vyama vya upinzani) inaweza kuwaletea matatizo,” alisema.

“Tunarudi kwa Watanzania kutaka kuleta mabadiliko, tunahitaji kuleta mabadiliko kwa sababu hali ya maisha ni ngumu, tumetoa wito kila Mtanzania ajiwekee Sh.100 kwa siku 50 hadi 60 watatuchangia Sh. 6,000.

"Ikiwa nusu milioni watatuchangia, tupata jumla Sh. bilioni tatu, zitatutosha kufanya kampeni nchi nzima. Hata akiwa na hali ya maisha ngumu, akituchangia Sh. 100 haiwezi kuongeza ugumu wa maisha alionao.

"Kuna wafanyabiashara watuchangie, kwa kuwa chama chetu kinaandaa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, alipe kodi kwa amani na mazingira mazuri ya biashara," aliomba.

Profesa Lipumba pia alisema anawania urais kwa kuwa Tanzania ina rasilimali, lugha ya Kiswahili inaunganisha wananchi na hakuna matatizo ya udini na ukabila.
“Tunapaswa kuwa taifa lililopiga hatua, lakini la kusikitisha hadi sasa Watanzania walio wengi ni maskini wa kutupwa. CUF sera yetu ya msingi ni haki sawa na furaha kwa wote,” alitamba.

Alipoulizwa kuhusu hoja ya kuwa yeye siyo mpinzani halisi, Profesa Lipumba alitamba kuwa yeye ndiye mpinzani pekee anayeihoji serikali bila woga, huku akitaka wananchi kupuuza propaganda zilizopo dhidi yake.

Alisema CUF ikishika madaraka ya kuongoza nchi, itawekeza kwenye kilimo ili kuleta mapinduzi ya viwanda ambavyo vitatoa ajira kwa wananchi wengi.
“Katika kila Sh. 100 iliyotumia na serikali fedha iliyokwenda kwenye kilimo ni Sh. tatu, huwezi kuleta mapinduzi ya kilimo kama huwekezi kwenye kilimo. Sisi tutaleta mabadiliko,” alitamba.

“Kaulimbiu yetu ni haki sawa na fursa kwa wote. Nikichaguliwa kuwa rais, nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kukamilisha katiba ya demokrasia yenye misingi ya kweli ambayo itakuwa dira ya nchi.

Profesa Lipumba alisema serikali ya umoja wa kitaifa wanayokusudia kuiunda, itasimamia haki za kisiasa, kiuchumi na kijamii, mambo yanayokwenda sambamba na Malengo Endelevu ya Milenia (SDGs).


IPPMedia
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom