Mgombea urais kwa tiketi ya TLP adaiwa kutapeli Sh mil 18 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mgombea urais kwa tiketi ya TLP adaiwa kutapeli Sh mil 18

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Quinine, Aug 18, 2010.

 1. Quinine

  Quinine JF-Expert Member

  #1
  Aug 18, 2010
  Joined: Jul 26, 2010
  Messages: 10,919
  Likes Received: 12,106
  Trophy Points: 280
  MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), Muttamwega Mgahywa, anadaiwa kutapeli Sh 18,829,500 za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

  Mgahywa anadaiwa kuwatapeli watumishi 61 kwa kuwaahidi kuwapelekea pikipiki za mkopo kutoka Japan kupitia kampuni yake ya Africa Japan Technology Motorcycle Industry Co Ltd ya Ubungo, Dar es Salaam.

  Watumishi hao wakiwemo walimu wamewasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Peter Toima.

  Watumishi wengi wanaodai kutapeliwa ni walinzi, Idara ya Afya na wahasibu.Mwenyekiti wa Kamati ya ufuatiliaji pikipiki hizo ni Prosper Maresi.Jana walikuwa na kikao cha pamoja kilichoongozwa na Toima.

  Katika kikao hicho,miongoni mwa wanaodaiwa kutapeliwa,Liberatus Kazungu, Joseph Laswai, Lucas Shayo, walidai kuwa walitoa fedha hizo mwaka 2005,na kwamba,tangu wakati huo wamekuwa wakizungushwa.

  Walidai kuwa,walitoa fedha hizo baada ya kampuni hiyo kujitambulisha kuwa imesajiliwa katika barua ya utambulisho yenye kumbukumbu Namba TSC/MARK/005 ya Agosti 12, 2005, na nambari ya akaunti benki za NMB na CRDB Rombo, pikipiki halisi kwenye gari na viambatanisho vingine kuonesha kuwa imesajiliwa jambo lililowafanya watumishi hao kuwa na uhakika wa kampuni hiyo.

  Kwa mujibu wa madai hayo, baada ya kuwa na uhakika wa kampuni hiyo, walitoa fedha hizo kwa mkataba wa kukopeshwa na kuahidiwa kupatiwa pikipiki hizo baada ya wiki tatu, makubaliano haya hayajatekelezwa hadi sasa.

  Walidai kuwa, walitakiwa watoe fedha kulingana na aina ya pikipiki walizozihitaji; walitoa kwanza Sh 100,000; Sh 200,000; Sh 300,000; Sh 500,000 na Sh 900,000 na hiyo ilikuwa ni kwa mkataba wa kukopeshwa huku wakikatwa mishahara yao, na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Rhoda Nsemwa, ambaye walidai alikuwa akiinadi kampuni hiyo.

  “Pikipiki ambazo tuliahidiwa kukopeshwa zilikuwa aina tofauti tofauti ambazo ni Toto 150 DT, Male 15XL, Life 125 TF, Tanzanite 200 DR, na Sina 125, ambazo zote ziliuzwa kwa bei ya shilingi 998,000 kwa kila moja,” walidai watumishi hao.

  Walisema wanataka pikipiki za Nagasaki na si za China, na endapo hilo halitatekelezwa warudishiwe fedha zao, ikiwa ni pamoja na fidia ya miaka mitano pamoja na gharama za usumbufu.

  Mwenyekiti wa watumishi wa halmashauri hiyo, ambaye ndiye aliyeingia mkataba na kampuni hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Pere Muganda, alisema aliagizwa na Mkurugenzi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuwafahamisha watumishi wakope pikipiki hizo.

  Muganda alisema,amekuwa akilifuatilia suala hilo bila mafanikio hivyo aliamua kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), na hakupata mafanikio yeyote.

  Toima alithibitisha kuwepo kwa madai ya watumishi hao na akaeleza kuwa kila mara wamekuwa wakilalamika wakiwamo walimu wengine kukata tamaa za kupata madai yao.

  Toima alisema suala hilo limeachwa kwa Takukuru Wilaya ambapo wamelishughulikia na kupata nyaraka zote muhimu za kuonesha ukweli wa jambo husika na namna fedha hiyo ilivyochukuliwa.

  Alisema ni vyema kampuni hiyo ikatoa pikipiki hizo kama makubaliano yalivyokuwa au kurejesha fedha za watumishi hao kama wanavyohitaji riba ya miaka mitano.

  “Huu ni utapeli wa wazi na kwamba serikali haitalinyamazia suala hili hata kidogo….lazima hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya wahusika ili kuhakikisha haki ya watumishi inapatikana bila kuangalia wadhifa wa mtu,” alisema Toima.

  Juhudi za kumpata Mgahywa hazikufanikiwa kwa njia ya simu ya mkononi baada ya simu yake kupokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwanawe na kudai baba yake ameacha simu nyumbani.

  Alisema angepatikana baada ya saa mbili, lakini baada ya muda huo simu iliita, haikupokewa.
   
Loading...