Mgogoro wa kisiasa nchini Ethiopia

Ngamanya Kitangalala

JF-Expert Member
Sep 24, 2012
501
1,214
Ethiopia ni nchi inayopatikana mashariki ya bara la AfriKa, kwenye eneo maarufu linalojulikana kama pembe ya AfriKa( Horn of Africa) , Ethiopia ni nchi ya 12 kwa kuwa na idadi ya watu wengi zaidi duniani, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, iliyofanyika mwaka 2018, Ethiopia inakadiriwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 109, hii inaifanya nchi hiyo kuwa ya pili kwa kuwa na idadi ya watu wengi zaidi barani Africa baada ya nchi ya Nige,na pia ndio nchi yenye watu wengi zaidi duniani miongoni mwa nchi ambazo hazijapakana na bahari( Landlocked countless).

Ethiopia ndio nchi inayoongoza kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika,kwa mujibu wa benki ya dunia( World Bank), kutoka mwaka 2008/ 2009 mpaka mwaka 2018/2019, wastani wa ukuaji wa uchumi ( Economic growth) kwa nchi ya Ethiopia ilikuwa ni asilimia 9.8.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Trading Economics,thamani ya shughuli za kiuchumi( Gros domestic product) katika nchi ya Ethiopia, inakadiliwa kuwa ni dola za kimarekani bilioni 96.11 kwa mwaka 2019 pekee, thamani ya shughuli za kiuchumi kwa nchi yetu ya Tanzania ni dola za kimarekani bilioni 61 kwa mwaka 2019.

Kiwango hicho cha GDP kwa nchi ya Ethiopia, ni sawa na asilimia 0.08 ya GDP yote ya dunia( Global Economy).

Lakini pamoja na mafanikio hayo makubwa kwenye eneo la uchumi, nchi ya Ethiopia ni moja ya nchi maskini kabisa duniani, kwa maana ya wastani wa pato la mwananchi( per capita income) ni dola za kimarekani 850 kwa mwaka, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020, kutoka shirika la fedha duniani ( IMF), na kwamba inakadiliwa kuwa nchi ya Ethiopia itafikia uchumi wa kati mwaka 2025( Tanzania tumefanikiwa kuingia kwenye nchi za uchumi wa kati mwaka huu 2020).

Kiutawala nchi ya Ethiopia, imegawanyika katika serikali za majimbo ya kimkoa ( Regional states) ambayo jumla yake yapo kumi, ugawaji huo umefanywa kwa kuzingatia misingi ya jamii za watu( Ethnic groups), na kila jimbo lina serikali yake na bunge lake na kila jimbo lina mamlaka yake kamili ya ndani juu ya uendeshaji wa jimbo lao, tofauti kabisa na serikali ya shirikisho( Federal Democratic Republic of Ethiopia), na kwa Ethiopia wao wamekwenda mbali zaidi kwa kila jimbo kuwa jeshi lake la ndani( Regional special forces).

Nchini Ethiopia kuna jamii nne za watu( Ethnic groups)kubwa zaidi, ambazo ni Oromia ambao wao ni asilimia 34.6 ya watu wote nchini Ethiopia, Amhara wao asilimia 27.1 , Somali wao ni asilimia 6.1 na Tigraya wao pia ni asilimia 6.1, japokuwa zipo jamii nyingine ndogo ndogo.

CHANZO CHA MGOGORO WA SASA UNAOENDELEA NCHINI ETHIOPIA
Kwa takribani wiki mbili sasa kumekuwa na mapigano makali sana kaskazini mwa nchi ya Ethiopia,kwenye jimbo la Tigray, kati ya majeshi ya jimbo la Tigray( Tigray Special forces) chini ya chama cha Tigray People's Liberation Front) na majeshi ya Ethiopia ( Ethiopia National Defence Forces) yanayoshirikiana kwa pamoja na majeshi ya jimbo la Amhara( Amhara special Forces), Amhara ni jimbo mojawapo kubwa nchini Ethiopia, ambapo wanapatikana watu wa jamiii ya Amhara, ambao wanashika nafasi ya pili kwa uwingi nchini humo,baada ya watu wa jamii ya Oromo ambao ndio wengi zaidi nchini Ethiopia.

Mwezi machi mwaka huu wa 2020, bodi ya taifa ya uchaguzi nchini Ethiopia ( National Election Board of Ethiopia) ilisimamisha kwa muda uchaguzi wa wabunge, katika bunge la taifa la nchi hiyo( House of People's Representatives) katika majimbo yote nchini humo ikiwemo na jimbo la Tigray kutokana na tishio la ugonjwa wa COVID-19 ulioikumba dunia.

Lakini kama ilivyotarajiwa na wachambuzi wa siasa za nchini Ethiopia, uamuzi huo wa bodi ya taifa ya uchaguzi ulipingwa vikali sana na viongozi wa jimbo la Tigray wakiongozwa na Rais wa jimbo hilo Debretsion G. Michael, ambaye pia ndio mwenyekiti wa chama cha Tigray People's Liberation Front( TPLF), ambapo kwa kuonyesha msimamo wa pamoja, kupinga hatua hiyo wabunge wote kutoka jimbo la Tigray akiwemo na Spika wa bunge la juu la nchi hiyo( upper house) walijiondoa kwenye bunge la taifa la nchi hiyo( National Parliament).

Mwezi Septemba mwaka huu 2020, serikali ya jimbo la Tigray iliitisha uchaguzi mkuu jimboni humo kinyume kabisa na msimamo wa hapo awali wa serikali ya shirikisho la Ethiopia ( Ethiopia Federal Government), ambapo chama cha Tigray People's Liberation Front ( TPLF) walijitangaza washindi kwa asilimia 98 ya kura zote( popular vote), huku uchaguzi huo ukishutumiwa vikali na serikali ya shirikisho,kwa kukosekana na waangalizi kutoka nje ya jimbo la Tigray.

Serikali ya shirikisho ya Ethiopia, waligoma kutambua matokeo hayo, yaliupa ushindi mkubwa chama cha TPLF,hatua iliyofuatiwa na kusitishwa kwa mgawo wa fedha kutoka serikali kuu( Federal Funding) kwenda katika serikali ya jimbo la Tigray , hatua hiyo ilichukuliwa kama tangazo la vita( declaration of war) na serikali ya jimbo la Tigray.

Usiku wa tarehe 04 mwezi huu wa Novemba, majeshi ya jimbo Tigray, yalivamia kambi ya majeshi ya Ethiopia( Ethiopia National Military Base) iliyopo jimboni humo na kuua baadhi ya askari wa jeshi la Ethiopia wasio na asili ya Tigriya, kitendo hicho kulichukuliwa na serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed kama ni kuvuka mstari mwekundu, kwa katiba ya Ethiopia, waziri mkuu ni kiongozi mkuu wa serikali ( Head of the government) na pia ndiye amiri jeshi mkuu( Commander in chief) wa majeshi ya Ethiopia.

Baada ya hapo kumekuwa na mapigano makali sana kwenye eneo hilo la Tigray, ambapo mpaka sasa inakadiriwa watu wapatao 600 kufariki dunia na watu zaidi ya 25,000 kukimbia makazi yao na kwenda kuonba hifadhi kama wakinbizi kwenye nchi jirani ya Sudan.

NINI MSINGI WA SITOFAHAMU KATI YA SERIKALI YA ADIS ABABA NA SERIKALI YA JIMBO LA TIGRAY?
Mara baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia ( Ethiopia civil war) mwaka 1991, vita iliyopelekea kuangushwa kwa utawala wa kijamaa wa chama kimoja cha People's Democratic Republic of Ethiopia, chini ya mfumo wa Derg, uliongozwa na Rais dikteta Mengistu Haile Mariamu.

Chama chama cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front ( EPRDF) kilichukua madaraka ya nchi hiyo, chama hicho kilikuwa ni muunganiko wa vyama vifuatavyo, Tigray People's Liberation Front( TPLF) kutoka watu wa jamii ya Tigraya, Amhara Democratic Party( ADP) kutoka jamii ya watu wa Amhara, Oromo Democratic Party( ODP) kutoka jamii ya watu wa Oromia na Southern Ethiopian People's Democratic Movement( SEPDM) kutoka watu wa jamii ya Wolayta kusini mwa Ethiopia.

Marehemu Meles Zenawi kutoka chama cha TPLF cha watu kutoka jamii ya Tigriya,alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama cha EPRDF na kuwa Rais wa serikali ya mpito ya Ethiopia mpaka mwaka 1995 ambapo Ethiopia walibadili katiba ya nchi yao, kutoka kwenye utaratibu wa serikali ya mfumo wa Urais( Presidential type of government) na kwenda kwenye mfumo wa serikali ya mfumo wa kibunge ( Parliamentary type of government) ambapo Meles Zenawi alishinda uchaguzi huo na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo.

Kutoka mwaka 1991 mpaka mwaka 2012 baada ya kifo cha waziri mkuu Meles Zenawi, watu kutoka jamii ya Tigriya ndio wamek uwa wakitawala siasa za Ethiopia kwa kiwango kikubwa sana.

Hata baada ya kifo cha waziri mkuu Meles Zenawi mwaka 2012, na nafasi yake kuchukuliwa na Hailemariam Desalegn kutoka watu wa jamii ya Wolayta kutoka kusini mwa Ethiopia, bado watu wa jamii ya Tigriya waliendelea kuwa na ushawiahi makubwa kwenye siasa za Aidis Ababa na Ethiopia ndani ya serikali ya shirikisho.

Mwaka 2018 watu wa jamii ya Oromo na Amhara ambao kimsingi ndio jamii kubwa zaidi nchini Ethiopia kwa idadi ya watu, walianziaha maandamo makubwa yasio na ukomo nchi nzima, kupinga utawala wa waziri mkuu Hailemariam Desalegn, sababu kubwa ya maandamano hayo ni kupinga kile walichokiita utawala wa chuma wa serikali ya EPRDF chini ya waziri mkuu Hailemariam Desalegn, kwa takribani miaka 27, watu wa jamii za Oromia na Ahmara walijiona kutengwa na serikali ya Adis Ababa na siasa hizo kutawaliwa zaidi na watu wa jamii ya Tigriya.

Hatimaye mwezi Aprili mwaka 2018 baada ya maandamano kupamba moto kwenye maeneo mengi nchini humo,waziri mkuu Hailemariam Desalegn, alijiuzuru nafasi yake kama waziri mkuu wa Ethiopia na pia kama mwenyekiti wa chama cha EPRDF.

Baada ya waziri mkuu Hailemariam Desalegn kujiuzuru, nafasi yake ilichukuliwa na kijana Abiy Ahmed kutoka jamii ya watu wa Oromia, ambaye kabla ya hapo ndio alikuwa mwenyekiti wa chama cha Oromo Democratic Party(ODP).

Mara tu baada ya waziri mkuu Abiy Ahmed kushika madaraka, alianza kufanya mageuzi makubwa sana kwenye maeneo kadhaa ndani ya serikali , kwenye chama cha EPRDF na hata ndani ya jeshi la nchi hiyo( ENDF), ambapo kwa kiwango kikubwa maeneo hayo yalikuwa yametawaliwa zaidi na watu kutoka jamii ya Tigriya, ambapo takribani majenerali wa juu 160 wa jamii ya Tigriya waliondolewa jeshini na maofisa kadhaa wa ngazi za chini wa jamii ya hiyo nao waliondolewa jeshini.

Hatua hiyo ya waziri mkuu Abiy Ahmed, ilitafsiriwa na watu wa Tigriya, hasa viongozi wa chama cha TPLF kama ni njia mojawapo ya waziri mkuu Abiy Ahmed kuwakandamiza watu wa jamii ya Tigriya.

Novemba mwaka 2019, waziri mkuu Abiy Ahmed, katika jitihada zake za kuleta mageuzi nchini Ethiopia, aliamua kuunganisha muungano wa vyama vinavyounda chama cha EPRDF, na kutengeneza chama kimoja kikubwa kinachoitwa Prosperity Party, hatua hiyo ilipingwa vikali sana na viongozi wa jimbo la Tigray chini ya chama chao TPLF ( Tigray People's Liberation Front).

Kwa maana hiyo, msingi wa mgogoro huo unaondelea kushika kasi nchiji Ethiopia, kugombea ushawiahi wa siasa za Ethiopia, kati ya jamii kubwa za Oromia na Amhara kwa upande mmoja na jamii ya Tigriya kwa upande wa pili.

Binafsi kama mzalendo kutoka Isansa, Mbozi naomba kutoa wito kwa jumuia za kimataifa hasa umoja wa Africa( AU) kuutazama mgogoro huu kwa namna ya pekee kabisa.

Endapo mgogoro huu utaendelea, ipo hatari kubwa sana ya kutokea madhara makubwa zaidi kwa binadamu na hatimaye kuleta athari kubwa sana kwa uchumi wa bara zima la Africa, hasa kwa kuzingatia nafasi ya Ethiopia kwenye uchumi wa bara letu hili

Ngamanya Kitangalala Mwaswala.
0756 669494.
Kngamanya@yahoo.com
 
Mkuu umetiririka vyema Sana, utawala wa majimbo Kwa nchi masikini ni taabu mno , Kwa vyovyote vile utahusisha ukabila , ila Ethiopia kuna watoto wa kike wazur daah
 
Tatizo sio utawala wa majimbo kama baadhi ya watu wanavyodai ila tatizo kubwa ni ukabila uliokithiri na kila kabila kujiona lina haki zaidi kuliko wengine.

Kama utawala wa majimbo ni tatizo basi hata Marekani,Urusi na hata China kungekua na machafuko.

Nigeria pia inautawala wa majimbo ila ukabili (rejea Biafra), udini(Kaskazini na Kusini) na Sasa ugaidi ndio matatizo makubwa yanayowasumbua na sio muundo wa utawala.
 
Utawala wa majimbo unapouanzisha ni vyema kuzingatia misingi ya taifa husika, desturi na historia ya taifa vinginevyo itakuwa balaa.
 
eti mnatolea mifano ya majimbo ,mmeona hapo tu
ufisadi na uchu wa madaraka kama hapa tz hamjauona,
 
Back
Top Bottom