Mgogoro wa ardhi wafukuta jimboni kwa Mrema

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Gama(2).jpg

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama


Wakazi wa Kijiji cha Mawala Kata ya Kahe wilayani Moshi Vijijini, wameitaka Serikali mkoani Kilimanjaro kutatua mgogoro wa ardhi unaofukuta katika maeneo yao baada ya mashamba kuuzwa kinyemela kwa baadhi ya vigogo wa serikali na matajiri.

Kauli hiyo waliitoa juzi wakati wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliotishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi hao.


Gama akiwa na timu ya wataalam na viongozi wa ngazi zote wa wilaya hiyo, alifika kijijini hapo na kuitisha mkutano huo ili kusikiliza kero za wakazi hao na malalamiko yao hayo.

Wakazi hao walionya kuwa iwapo serikali haitatatua mgogoro huo kuna uwezekano mkubwa wa kutokea uvunjifu wa amani na damu umwagika katika kijiji hicho.

Rodrick Mmari, Timotheo Severini na Daniel Kimati, walisema kutokana na ardhi ya eneo hili kuwa na rutuba na kuwepo wa kilimo cha umwagiliaji, baadhi ya viongozi wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi, ambayo wameyapata visivyo halali kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji na kata.


Walidai kuwa pia mwekezaji wa kiwanda cha sukari cha TPC, amekuwa akiwanyanyasa kwa kuwakataza kufanya usafi kwenye mfereji wa maji ambao unaanzia kwenye chanzo kikubwa cha maji cha Miwaleni na kunyonya maji yote nawao kukosa ya kumwagilia mashamba yao.


“Mwekezaji anajenga mazingira ya uadui, yeye ndio anamiliki funguo za lango la maji na anavifaa vya kisasa lakini hafanyi usafi bali
anachukua maji tu, tunapomuomba ili tufanye usafi hataki, tukifungua kwa njia zetu anatuma mtu anafungua maji kidogo, ”alidai Severini

Alisema kamwe hawatakubali kuonewa na kukandamizwa katika ardhi yao na raslimali zao.

Walisema uuzwaji wa mashamba kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wafanyabiashara, umefanywa na viongozi wa kijiji kinyemela bila kujadili katika mkutano mkuu wa kijiji.

Walisema kijiji hicho, ambacho kilianza mwaka 1976 na kusajiliwa mwaka 1977 kina zaidi ya kaya 300 za wakulima na wafugaji na
kutokana na kujua umuhimu wa kilimo na ufugaji walitenga maeneo ya shughuli hizo ambayo kwa sasa yameuzwa na viongozi wao.

Mbunge wa Moshi Vijijini (TLP), Augustine Mrema, alimtaka Gama kuchukua hatua madhubuti ili kuwaondoa wakazi hao katika unyanyaswaji ndani ya ardhi yao.


Alisema viongozi badala ya kuwatetea wakazi hao, wamegeuka wakandamizaji na kukubali kugawa mashamba ya kwa matajiri.

Mrema alisema kilimo cha mpunga kinachoendelea kwenye eneo hilo kikifanywa na matajiri huku polisi wakitumika kuwanyanyasa wananchi wanaodai haki yao.

Gama aliahirisha mkutano huo kwa kuunda tume ya wataalam kuchunguza utaratibu uliotumika kuuza mashamba hayo.

“Kwa sasa siwezi kuwasimamisha watuhumiwa kuanza kujieleza hapa, nitakachofanya nitaunda tume ya wataalam wa kila aina,

ambao watakuja kufuatilia kwa kina na kujiridhisha kisha kunishauri nini cha kufanya ili mwisho wa siku niweze kutoa uamuzi usiotiliwa mashaka na upande wowote, ”alisema

Alisema timu hiyo ya wataalam 10 inatarajia kuanza kazi hivi karibuni na kukabidhi ripoti yake Januari 15 mwaka huu kwa Mkuu huyo wa mkoa na kutoa uamuzi ambao unatarajiwa kuwa utatuzi wa mgogoro huo wa muda mrefu kijijini humo.

CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom