Mgogoro wa ardhi sasa wapambanisha wageni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mgogoro wa ardhi sasa wapambanisha wageni

Discussion in 'Jamii Intelligence' started by BabuK, May 3, 2012.

 1. BabuK

  BabuK JF-Expert Member

  #1
  May 3, 2012
  Joined: Jul 30, 2008
  Messages: 1,847
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 145
  RAIA wa Trinidad & Tobago, Sohooba Keith Smith, aliyewahi kufungwa nchini na baadaye kuachiwa huru lakini akipigwa marufuku kurejea tena Tanzania (Prohibited Immigrant-PI), mali yake ambalo ni shamba kubwa mjini Arusha limeuzwa katika mazingira ya kutatanisha kwa raia wa Ujerumani, Peter Kersten, taarifa za Serikali ya Trinidad & Tobago zinaeleza.

  Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Trinidad & Tobago, Knowlson Gift pamoja na waziri mwingine mpya aliyeteuliwa baada ya Gift, Arnold Piggott, wote kwa pamoja wamekuwa wakifuatilia kadhia hiyo kwa miaka kadhaa sasa bila mafanikio. Raia huyo wa Trinidad alikuwa akimiliki shamba lililokuwa likijulikana kwa jina la Ndamakai Estates Limited ambalo kwa sasa linaitwa Acacia Hills Company likidaiwa kuuzwa kwa raia wa Ujerumani, katika mazingira ambayo Serikali ya Trinidad & Tobago inaamini ni ya utata yanayopora haki ya raia wa nchi yao.

  Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limezipata, Agosti 29, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Trinidad & Tobago, Knowlson Gift, alimwandikia barua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Dk. Asha-Rose Migiro akipendekeza Serikali ya Tanzania ichukue hatua kushughulikia haki za raia wao. "Kwa heshima nakuandikia kuhusu suala la raia wetu wa Trinidad & Tobago, Sohooba Keith ambaye rekodi zinaonyesha amewahi kufungwa na kutumikia kifungo hicho huko Tanzania katika mazingira ya utata.

  "Rekodi zaidi zinaonyesha kuwa kifungo chake kilisitishwa na kuondolewa Tanzania kwa msaada wa Serikali ya Trinidad & Tobago. Serikali ya Trinidad inaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumwachia huru raia wetu, hata hivyo, tunaomba ufanyike uchunguzi kuhusu kuuzwa kwa shamba la Sohooba kwa raia wa Ujerumani katika wakati ambao yeye akiwa jela, tupo tayari kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo," inaeleza barua ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Trinidad, Knowlson.

  Takriban miezi mitano baadaye, Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Trinidad & Tobago, Arnold Piggott, naye alimwandikia barua kuhusu suala hilo Waziri mpya wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe. Katika barua hiyo Waziri Piggott anaeleza; "Smith akiwa jela, mali yake iliuzwa kinyemela kwa raia wa Ujerumani Peter Kersen, tunaendelea kuomba msaada wa Serikali ya Tanzania katika kupata haki ya raia wetu, ofisi yangu imekuwa ikisumbuliwa kupata majibu kuhusu suala hili kutoka Serikali ya Tanzania, na tangu kuandika barua ya kuomba uchunguzi kwa Waziri Migiro, hakuna majibu tuliyopata, ni matumaini yangu kuna juhudi zinafanyika na utaziendeleza ili kukamilisha suala hili," inaeleza barua ya Waziri Piggott.

  Katika kuonyesha kuwa suala hilo ni la muda mrefu likiwa bado kupata ufumbuzi, mwaka 1994, ofisi ya ubalozi wa Trinidad & Tobago, Lagos nchini Nigeria, ofisa wake alifanya mawasiliano na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Meja Jenerali Silas Mayunga.
  Kilichojiri katika mawasiliano kati ya Meja Jenerali Mayunga na balozi huyo kinabainishwa na balozi huyo mwenyewe katika barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Tanzania, ya Oktoba 18, mwaka 1994.

  Ofisa huyo anaeleza katika barua yake; "Balozi (Mayunga) hakuweza kunipa majibu isipokuwa ameeleza amewasilisha suala hilo Dar es Salaam na hakuna majibu yaliyorudishwa kwake," "Lakini kuna jambo linanitia wasiwasi na kwa kweli nimepata mtazamo kwamba katika mazungumzo yetu na Meja Jenerali Mayunga kuhusu suala hili ni kama anapendekeza Smith asifuatilie mali yake kwa kushinikiza na angalau ashukuru hadi sasa yupo hai."

  Kutokana na hali hiyo, mwandishi wetu alifanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuambiwa kuwa suala hilo lipo mikononi mwa Waziri Membe na tayari limefanyiwa kazi katika hali ya kuridhisha. Mawasiliano kati ya mwandishi wetu na Waziri Membe yalishindikana kutokana na kuelezwa na maofisa wa wizara kuwa yupo nje ya nchi kikazi. Juhudi za kuwasiliana na Waziri Membe zinaendelea.

  Hata hivyo, taarifa zisizothibitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje zinaeleza kuwa maofisa wa Wizara hiyo wamewahi kukutana na Sohooba na kufanya naye mazungumzo na kubaini kuwa utatuzi wa suala lake unategemea zaidi mkondo binafsi na si wa kiserikali, ikidaiwa kuwa mtu aliyehusika kwenye kuuza eneo shamba lake wakati yeye akiwa jela ni mmoja wa watu wake wa karibu, ambaye anadaiwa kuwa na nyaraka muhimu za kufanya mauzo hayo.
   
Loading...