Mgogoro mkubwa wa ardhi kati ya wilaya ya Kibaha na Kisarawe – Vita ya wakulima na wafugaji yafukuta

Ni muda mrefu sasa kumekuwa na mgogoro wa mpaka kati ya wilaya hizi mbili za Kibaha na Kisarawe. Mgogoro huu ni wa zamani kidogo tangu mwaka 2006.

Juhudi za kutatua mgogoro huu zilifanyika mwaka 2014, na wataalam kutoka wizara ya ardhi makao makuu Dar es Salaam walienda kusuluhisha mgogoro huu kwa kushirikiana na viongozi wa pande zote mbili za Kibaha na Kisarawe.

Wataalam hao walitakiwa kuchora upya mpaka kati ya wilaya hizo za Kibaha na Kisarawe na kuweka mawe ya mipaka ili kumaliza kabisa mgogoro huo.

Lakini tangu mwaka huo wa 2014 hakuna jitihada zozote zilizofanyika ili kukamilisha utatuzi wa mgogoro huo, hivyo kutoa mwanya kwa watu wachache kuuendeleza mgogoro huo kwa manufaa yao binafsi.

Ni hivi karibuni tu mnamo mwezi wa November 2016 mgogoro huu uliibuka kwa kishindo kikubwa sana pale wafugaji kutoka kijiji cha Mafizi wilaya ya Kisarawe walipojichukulia sheria mikononi mwao na kujipa mamlaka ya kuweka mipaka kati ya wilaya hizo mbili.

Wafugaji hao walijipa mamlaka hiyo na kuamua kupeleka bulldozer ambalo walilitumia kuweka alama za mpaka kati ya wilaya hizo mbili.

Uwekaji huo wa mipaka hii uliofanywa na wafugaji kutoka kijiji cha Mafizi wilaya ya Kisarawe, ulimega eneo kubwa sana la kijiji cha Kitomondo kilicho katika wilaya ya Kibaha na kuliweka upande wa wilaya ya Kisarawe.

Viongozi wa kijiji cha Kitomondo ambacho eneo lake lilimegwa walipohoji uhalali wa zoezi hilo walijibiwa kuwa wafugaji ndio wameweka alama hizo za mipaka, na kuwa huo ndio mpaka rasmi wa wilaya hizo.

Cha kushangaza zaidi ni kuwa uwekaji huo wa mipaka ya wilaya uliofanywa na wafugaji hao ulipata baraka zote za viongozi wa wilaya ya Kisarawe akiwemo mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mh. Happiness William.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kisarawe katika kikao chake na viongozi wenzake kilichofanyika tarehe 16th November 2016 katika kijiji cha Mafizi wilaya ya Kisarawe, alitamka kuwa anatambua rasmi mpaka huo kati ya wilaya yake ya Kisarawe na wilaya ya Kibaha, mpaka ambao uliwekwa na wafugaji kutoka wilaya yake ya Kisarawe.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kisarawe alisisitiza kuwa kitendo cha wafugaji hao kuweka mpaka huo wa wilaya ni sahihi kabisa, na kwamba wakulima wote walioko kwenye eneo lililoporwa na wafugaji hao wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.

Hivyo, mkuu huyo wa wilaya ya Kisarawe Mh. Happiness William akatoa agizo kuwa mpaka huo ndio mpaka rasmi kati ya wilaya yake ya Kisarawe na wilaya ya Kibaha, na kuwaagiza wafugaji hao kuweka uzio kwa kutumia mapipa, nguzo na waya kwenye mpaka huo, ili kuzuia mifugo na watu wasiweze kupita kwenye mpaka huo uliowekwa na wafugaji.

Wafugaji hao sasa wamewazuia kabisa wakulima wa kijiji cha Kitomondo kwenda kwenye mashamba yao ambayo yapo kwenye eneo lililoporwa na wafugaji hao. Wafugaji hao wameweka vijana wao ambao wanalinda mpaka huo ili kuwazuia wakulima kwenda mashambani kwao.

Hali hii imechochea uhasama kati ya wakulima wa kijiji cha Kitomondo kilicho wilaya ya Kibaha dhidi ya wafugaji wa Kisarawe, kwani eneo la wakulima hao limemegwa na wafugaji, na sasa wakulima hao hawana eneo kwa ajili mashamba yao.

Mbaya zaidi, ni kitendo cha mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mh. Happiness William kubariki uporaji huo wa ardhi ya wakulima wa kijiji cha Kitomondo wilaya ya Kibaha, na kuamrisha wafugaji waweke uzio ili kuwazuia wakulima wa kijiji cha Kitomondo wasiweze kwenda kwenye maeneo ya mashamba yao.


Maoni yangu:-

· Hali ya watu kuchukua sheria mikononi na kuweka mipaka ya wilaya inaweza kuzusha vita maana kila mtu ataweka mipaka anavyotaka yeye.

· Viongozi wasitumike na upande mmoja kukandamiza upande mwingine wa wananchi. Sisi wote ni watanzania wenye haki sawa.

· Uporaji kama huu wa ardhi ndio chanzo kikubwa sana cha migogoro ya ardhi, na migogoro kama hii inachochewa na viongozi.


Swali:-

Ni nani mwenye mamlaka ya kuweka mipaka ya wilaya? Au kila mtu akiamua anaweza kwenda kuweka mipaka ya wilaya mahali anapotaka yeye?
Miaka 50 ya taifa ni mingi tunafanikiwa mambo mengi kitaifa,ni wakati sasa kufuta huu usemi wa migogoro ya wakulima na wafugaji binafsi Napata shida kutamka mgogoro kwa kuwa mkulima ni mfugaji,na mfugaji ni mkulima
 
Miaka 50 ya taifa ni mingi tunafanikiwa mambo mengi kitaifa,ni wakati sasa kufuta huu usemi wa migogoro ya wakulima na wafugaji binafsi Napata shida kutamka mgogoro kwa kuwa mkulima ni mfugaji,na mfugaji ni mkulima

Migogoro hii ipo, ma kwa kiasi kikubwa inachochewa na viongozi, kwa mfano mgogoro unaozungumziwa hapa.
Wafugaji wanahujumu sana wakulima kwa kuharibu sana mazao ya wakulima kwa makusudi.
Wafugaji mara nyingi ndio wavamizi kwenye mashamba ya wakulima.
Mifugo ndio inayopelekwa kwenye mashamba ya wakulima, na sio kwamba mazao ya wakulima yanapelekwa kwenye mifugo ya wafugaji..!!
Kwenye sataka hili hapa, mkuu wa wilaya ya Kisarawe yuko pamoja na wafugaji akiwapa support ya uporaji wa eneo kubwa sana la wakulima wa kijiji cha Kitomondo.
Hapo ndipo mgogoro ulipojikita.
Iwapo mkuu huyo wa wilaya angetaka, angeweza kuepusha mgogoro huu, lakini yeye ameamua kuwapa support wafugaji wavamizi-waporaji ardhi ya wakulima.
 
Tunamuomba Mheshimiwa Rais atuangalie na sisi huku kwetu wilaya ya Kibaha wakulima wananyanyaswa, kuporwa ardhi yao na kufukuzwa kwenye ardhi yao na wafugaji wachache wenye pesa.
Dhuluma hii inafanana kabisa na dhuluma waliofanyiwa wamachinga wa Mwanza.
 
Reminder .........
Tunamuomba Mheshimiwa Rais mtetezi wa wanyonge atuangalie na sisi huku kwetu wilaya ya Kibaha wakulima wananyanyaswa, kuporwa ardhi yao na kufukuzwa kwenye ardhi yao na wafugaji wachache wenye pesa.
Dhuluma hii inafanana kabisa na dhuluma waliofanyiwa wamachinga wa Mwanza.
 
Back
Top Bottom