Mgaya wa TUCTA aibuka, aitisha serikali

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,073
1,250
Baada ya kimya cha muda mrefu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), limetangaza rasmi kuanza mgogoro wa kuishinikiza serikali iongeze mishahara ya wafanyakazi kuanzia mwezi ujao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nocolaus Mgaya, alipozungumza na NIPASHE muda mfupi baada ya kushiriki semina kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ambayo iliwashirikisha viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini.
Alisema Tucta haijasahu kilio cha wafanyakazi kuhusu mishahara mipya na sakata hilo lilitulia kupisha kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu na sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya na baada ya hapo mgogoro utaanza upya.
Mgaya alisema serikali iliongeza kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi kutoka Sh. 104,000 hadi Sh. 135,000, lakini bado Tucta inaona ni kidogo ikilinganishwa na hali halisi ya maisha ilivyo kwa sasa.
Aliongeza kuwa wafanyakazi waliomba kiwango hicho kifikie Sh. 315,000 na kodi inayokatwa kwenye mishahara ipunguzwe kwa asilimia sita badala ya asilimia moja iliyopunguzwa.
Alisisitiza kuwa suala la kudai nyongeza ya mishahara halitakoma mpaka hapo wafanyakazi watakaporidhika na kile wanacholipwa vingine migogoro kati ya wafanyakazi na serikali itaendelea kuwepo siku zote.
Alifafanua kuwa kuanzia mwezi ujao wataanza kudai mishahara kwa kufanya majadiliano na serikali, lakini pale yatakapokwama watatumia njia zingine ambazo alisema serikali huwa haizipendi ikiwemo migomo na maandamano.
Hata hivyo, alisema serikali mpya iliyoundwa mwezi uliopita imeonyesha matumaini kwa wafanyakazi, lakini akaonya kuwa kama itakuwa kama ile iliyopita migogoro ya wafanyakazi kudai mishahara haitaisha.
Alitoa mfano kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ameanza vizuri baada ya kuviita vyama vyote vya wafanayakazi kwa lengo la kufahamiana naye na kwamba hiyo ni hatua kubwa na yenye kuleta matumaini.
Awali, akifungua semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Edine Mangesho, aliwaambia washiriki kuwa Ukimwi ni janga la kitaifa kama wataamua wataweza kupambana nalo na kulipunguza.
Alisema Ukimwi unamaliza nguvu kazi ya wafanyakazi na kuacha mapengo hatua ambayo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kwamba kila mfanyakazi ana wajibu wa kupambana na janga hilo.
Semina hiyo ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi ilianza jana na itamalizika Desemba 11 mwaka huu ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa na kufikiwa maazimio.
CHANZO: NIPASHE
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom