Mfahamu Mzee Mwinyi: Mtanzania wa Kwanza Kuwa Rais Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

View attachment 2066302
Wakati naanza kuandika makala ya huyu Mzee aliyejaaliwa miaka mingi na heri hapa Duniani nikakumbuka yule dogo aliyemzaba kibao sijui yuko wapi. Kweli maisha ya mwanadamu ni hadithi tu ndiyo maana Mzee Mwinyi anapenda kusema tujitahidi kuacha hadithi nzuri hapa duniani.

Kwakweli huyu Mzee kabarikiwa vingi. Mbali na umri mrefu, Mwinyi ana roho nzuri, muungwana na mcheshi sana. Alituchekesha hadi kwenye msiba wa Magufuli. Mzee Mwinyi bana. Eti siku hizi anasahau hadi majina ya watoto wake. Halafu ana Kiswahili kitamu kweli. Siku anasubiria uteuza wa Nyerere alisema “moyo wangu ulijaa mchanganyiko wa uoga na furaha isiyoelezeka, tamaa yakupata, na hofu ya kukosa.”

Mzee Mwinyi alianza kuiongoza Tanzania Novemba 5, 1985 baada ya kufanya wonders kule Zanzibar! Wasiolijua hili utasikia wanasema Mwinyi hakuwa chaguo la Nyerere. Chaguo la Nyerere lilikuwa Salim Ahmed Salim. Haya mambo ya chaguzi haya tuyaacheni tu. Wakati mwingine ukichunguza sana utakuja ambiwa hata baba yako hakuwa chaguo la mama yako na wewe haikuwa chaguo lao uzaliwe. Ohoo! Kwani hata Jakaya siwalisema ni chaguo la Mungu?

Whether alikuwa chaguo la Nyerere au la, unachotakiwa kujua ni kwamba Mwinyi alianza siasa mwaka 1964, akiwa na umri wa miaka 39, akang'ara kitaifa na kimataifa. Kumbe siasa kukutoa siyo mpaka uanzie chipukizi kama jamaa zako wanavyowatishia na kujigana. Kwamba wanakijua chama. So what!

Unaweza kukijua chama na ukafa ni hopeless tu! Chama kinaangalia uwezo na wako na siyo umri wako ndani ya chama. Magufuli hakuwahi kuwa hata mjumbe wa nyumba kumi lakini alikuwa Mwenye Kiti wa Chama Taifa! Haya mambo tusiwe tunatishana bana! Kila mtu na nyota yake. Kama hauna nyota basi jitahidi uwe na pesa, uhonge ukamatwe ukose vyote. Kosa ni kukamatwa na siyo kuhonga!

Halafu usidhani Mwinyi aliingia kwenye siasa bila kusoma kama wengi mnavyodanganyana. Mwinyi kapiga shule mpaka nje ya nchi. Tena kasomea elimu zote; ya dini na dunia. Akiwa na umri wa miaka minne tu baba yake alimpeleka Zanzibar kwa rafiki yake Mzee Suedi Bin Mgeni kupana elimu ya dini ili baadaye aje kuwa shekhe mkubwa nchini lakini akaja kuwa kiongozi mkubwa nchini kwa sababu sisi tunapanga, Mungu anapangua. Hata mdangaji yawezekana alipanga kuwa mke wa mwanaume mmoja, leo anahudumia wanaume wengi. Uzuri zote ni huduma.

Mzee Mwinyi alipomaliza kusomea elimu ya Kurani Mabangapwani alijiunga na elimu dunia katika shule ya msingi Mangapwani akiwa na umri wa miaka nane na nusu na kuhitimu mwaka 1936. Mwaka 1937 vijana wawili tu Mwinyi na mwenzake walichaguliwa kuingia darasa la tano shule ya kati Dole Zanzibar na kumaliza mwaka 1942. Zamani walifaulu wengi, wakachaguliwa wachache kwa sababu ya uhaba wa shule. Mwaka 1943 alijiunga na Chuo cha Ualimu Dole.

Mzee Mwinyi akawa ameandika rekodi ya kupata elimu ya juu sana nchi. Kumbuka hata digrii zimeanza baada ya uhuru. Alipomaliza aliajiriwa na kupelekwa Bumbwini kusimamia ujenzi wa shule na kutafuta wanafunzi na kuwafundisha yeye mwenyewe. Zamani ukimaliza shule tu kazi imekwisha kilichofuata ni kula na kuzaa, siku hizi ukimaliza shule kazi ndio inaanza upya, full kusaga sole kutafuta ajira kusiko na ajira! Ukicheza unaweza kufa bila vyote, kazi na kuzaa! Ohooo!

Basi bwana wakati Mwinyi akipiga chaki pale Bumbwini hakuridhika na elimu aliyokuwa nayo, Aprili 1954 alikwenda zake Uingereza kuchukua Diploma ya ualimu. Zamani elimu ilikuwa ualimu, ubwana shamba na udaktari, siku hizi kuna kozi hadi za kukaanga mboga. Pale Uingereza alikuwa katika chuo kikuu cha Durham, London. Alirudi mwaka 1956 na Diploma yake mkononi. Wakati wenzake wanapigania uhuru yeye alipigania elimu. Hii niliipenda maana hakujificha maporini kama babu zetu!

Mwaka 1961 tena alikwenda zake chuo kikuu cha Hull Leicester, Uingereza baada ya kunogewa na kitabu cha nje. Hata hivyo alirudi Zenj mwaka 1962 baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu Zanzibar. Kwahiyo hadi anaingia kwenye siasa tayari alikuwa ni msomi mkubwa tu nchini! Msomi wa kiwango cha Diploma, tena Diploma ya Uingereza, miaka ya 60! Imagine alikuwa kipanga kiasi gani. Halafu elimu ya zamani ilikuwa ya kibabe kweli, ukikutana na vizee vya zamani vinajua sana! Vikilewa vinaongea Cambridge English! Hahaha, halafu vinaamini msomi ni kingereza hata kama vinalala njaa! Siku vioja vikiisha Afrika ndipo ntahama.

Halafu ile kuingia kwenye siasa ilikuwa kama vile kafungulia mvua ya baraka. Vyeo vilianza kumgombania badala ya yeye kuvigombania. Alianza na Ukatibu Mkuu Wizara ya Elimu, hajakaa sawa akala Unaibu Mkurugenzi wa Shirika la Chama cha Walima Karafuu, mara Mwenyekiti wa BAKITA, mara Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mara Mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe, mara Mwenyekiti wa Zanzibar Censorship Board, mara Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara Waziri wa Mambo ya Ndani.

Yaani kwa Mwinyi kuwa na cheo zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja ilikuwa jambo la kawaida tu. Hata Nyerere kipindi Nyerere anatafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais alimuomba Karume majina mawili kutoka Zanziba, Karume akatuma majina hayo, neema ikamdondokea Mzee Mwinyi. Mzee Mwinyi aliposikia jina lake kwenye taarifa ya habari ya usiku alisema, “Nililala Mwalimu nikaamka waziri katika Serikali ya Muungano.” Wacha kabisa watu na bahati zao. Siyo jamaa yangu, yeye alilala ndani kwake ni mwalimu ukaamkia chooni na kuomba uhamisho wamtoe kijijini. Yaani kuna vijiji vinaroga, loh!

Mwaka 75 tuliingia kwenye uchaguzi wa Rais na Wabunge, Mwinyi hakugombea lakini bado akateuliwa kuwa Mbunge na kisha Waziri wa Mambo ya Ndani, askari wa Shinyanga wakamuangusha baada ya kupiga na kutesa watu wasiokuwa na hatia kwa tuhuma za kichawi. “Kwa fedheha hii, naomba nijiudhuru mwalimu,” Mwinyi alimuandikia Mwl Nyerere kuomba ajiudhuru. Ilikuwa mwaka 1974. Leo hii nani ana ubavu wa kujiudhuru! Thubutuuu! Zamani walijiudhuru kwa sababu uongozi ulikuwa dhamana, siku hizi hawajiudhuru kwa sababu uongozi ni ulaji. Na sharti la kula lazima uliwe alisema Mzee Kikwete.

Pamoja na kujiudhuru nyota yake iliendelea kung’ara maana Afrika ukijudhuru unapotea mazima. Mwaka 1978 Mwinyi alirushiwa tonge la Ubalozi wa Tanzania nchini Misri ambako alipiga mzigo hadi Oktoba 1981, akarudi nyumbani na kudaka Uwaziri wa Maliasili na Utalii. Hajakaa sawa mwaka 1983 akadondoshewa Uwaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Muungano.

Yaani huyu Mzee alikuwa na bahati mpaka naumwa. Unajua kwa nini naumwa? Kuna watu wamelala hadi makaburini kutafuta vyeo wakatoka kapa, wakaaamua kuokoa. Nawajua. Ukiwaona kama wamechanganyikiwa vile! Hasa ukiwakuta kwenye maombi ya kupokea makontena kutoka China kwa Jina la Yesu unaweza kufa. Haya ndiyo madhara ya kumfanya Yesu wa dharula lazima akufanye wa subiri ufe!

Hii dunia siielewi ujue?? Sasa hapo hujakutana na motivetional Spiker anayefokea watu kwamba kufa maskini ni uzembe wao na wakati na yeye anakaribia kufa maskini! Ukimuuliza kulikoni anakwambia hata fundi ghorofa hana ghorofa kwa hiyo sikiliza maneno yake, usiangalie matendo yangu. Huu nao ni uhuni tu.

Karne hii tunajifunza kutembea kwa kutembea, kuona kwa kuona na kula kwa kula. Sasa unanifundishaje kutembea na wakati huna miguu?
Hapa nachotaka kusema ni kwama Mzee Mwinyi hakuwa na nyota ya bundi kuchukiwa na kila mtu. Mwinyi alikuwa na nyota ya kipapatio kupendwa na kila mtu. Hebu fikiria hivi majuzi tu kwenye Birthday yake kapewa Benzi la milioni sijui 250 na wakati wengine hapa magari yametung'ang'ania utadhani figo, tangu tumeyanunua ni miaka imepita na hakuna dalili za kubadilisha.

Mzee alipewa Benzi hadi Prof. Shivji akashtuka! Prof bana! Kwamba aliwahi hudhuria birthday ya Nyerere mwaka 1992, hakumbuki kama alipewa zawadi yoyote. Hata kukata keki alifanya kwa mzaha. Zawadi ya Benz kwa Mzee wetu ikamshitua sana Shivji. Zama zimebadilika. Hata Yesu akirudi leo hatapokelewa kwa punda, atapokelewa kwa benzi kama la Mzee Mwinyi.

Halafu tukumbukeni iliishaandikwa aliyenacho huongezewa. Mwinyi anaongezewa kila siku. Hivi unajua kaongezewa Rais kwenye familia yake? Anaitwa Dr. Hussein Mwinyi. Ndio Rais wa Zanzibar alikoanzia kazi ya Urasi baba yake Mwinyi.

Siri ya baraka za Mzee Mwinyi ni kinywa cha baba yake! Baba yake alimuita Nzasa. Yaani ardhi asiyokauka maji, waha wanaita masebhura ili Mwinyi asijekukaukiwa katika maisha yake na kweli Mwinyi hakuwahi kupungukiwa. Anakwambia hajawahi kukopa maisha yake yote. Nakama unavyojua maskini anakopa akiishiwa. Hivyo Mwinyi hajawahi kuwa maskini.

Wakati mwingine tuwe makini na majina tunayowaita watoto wetu. Jina laweza kuwa neema au noma. Unamuita mwanao Tabu za Dunia ! Akiwapa taabu mnasema ni kazi ya Mungu. Anyway wacha Mungu aendelee kuitwa Mungu maana unaweza kumuita mwanao Baraka akaja kuwaletea balaa ukoo mzima mkajuta. Nenda mahakamani utakutana na kina Musa na Petro wana kesi za ukabaji.

Halafu huyu Mzee Mwinyi amebarikiwa hata umahiri katika kuongea ndiyo maana si rahisi kusikia baada ya hotuba zake akishambuliwa. Anajua aongee nini,wakati gani,mahali gani na mbele ya nani. Wakati anastaafu alisema mabaya yangu niachieni mimi lakini mazuri yangu tugawane! Hizi ndizo hekima. Unajua unaweza kuwa na akili ukakosa hekima? Lakini kwani akili ni nini yakhe!! Akili ni kuujua ukweli wa jambo, hekima ni kujua ni wakati gani uuseme ukweli huo. Kuzungumza ukweli sehemu isiyokuwa sahihi ni ukosefu wa hekima. Utaambiwa acha kuropoka.

Mzee Mwinyi yeye amepewa vyote, akili na hekima. Katika utawala wake alikumbana na mengi lakini hatukuwahi kusikia akijibu hadharani. Amewahi kuambiwa anaendesha nchi kwa fikra na mawazo ya mke wake utadhani wanawake ndiyo watu wasiokuwa na akili. Haya mbona hao walioendeshe nchi kwa fikra za kiume uchumi uliwabinua?

Mwinyi amechukua nchi hii watu wanakula kwa foleni lakini ameondoka bidhaa zinatafuta watu. Huyo ndiyo Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mzee asitaka makuu na mtu. Hata siku ile January Makamba ametumbuliwa na kuandika mitandaoni kwamba anakubaliana na maamuzi ya JPM, halafu chini kaweka picha yuko na Mzee Mwinyi wanacheeeeeka kweli, Mwinyi hakupenda hadi kusema alichofanya January baada ya mambo kukorogeka.

Historia nzuri inambeba huyu Baba wa Mageuzi, na ni baba wa mageuzi kweli maana nikikumbuka tulipotoka, sina hamu. Tulikula ugali wa yanga maarufu kama chakula cha farasi. Tulipanga foleni kununua huduma. Mtu alitumia masaa hadi manne kupanga foleni ili apate kibaba cha mafuta ya kula, mche mmoja wa sabuni na kilo ya sukari. Unaweza kaa kwenye foleni tangu asubuhi mara mnaambiwa "unga umeisha". Dah!

Foleni zilikuwa za kusukumana. Watu walikuwa wengi kuliko bidhaa. Kupanga foleni haikuwa guarantii ya kupata huduma. Ndiyo kusema, wengine walirudi nyumbani mikono mitupu baada ya jitihada za kulifikia dirisha la duka kushindikana. Wengine walizirai kwenye foleni! Waulize wazee wako maana enzi hizo ndio walikuwa vijana matozi.

Watu tulivaa viraka. Mafundi cherehani walipata kipato kwa kushona viraka. Suruali la baba lilikatwa kaptura za watoto na chupi kadhaa za mama. Watu tulipiga mswaki kwa mkaa. Watu tulivaa kata mbuga. Miguu ilijaa funza wakubwa utadhani mbaazi. Tulikwenda chooni peku, tena wakati wa mvua na hatukuugua. Baada ya kujisaidia tulitumia gunzi la muhindi au kona ya ukuta. Hakuna maji chooni wala bafuni. Kujisaidia vichakani ilikuwa bora kuliko chooni. Tulimwagia majivu chooni kila siku asubuhi kupunguza harufu na kuua wadudu.

Enzi hizo watu walikuwa na chawa kichwani acha kabisa. Mayai yake yalizunguka kichwa kizima. Watu tuliishi chumba kimoja na mifugo, bata, mbuzi, kuku, sungura, panya, nge na tulisavaivu. Tulitandika magunia na tulilala juu ya mavi ya kuku, mbuzi, kondoo, ila shukrani kwa mungu kwa ulizi wake wote mpaka leo hii.

Watu tulienda shule pekupeku, uku tukibeba , mifagio, madumu, vifuniko vya soda, njiti, huku kaptura ya shule ikiwa imechanika kwa nyuma imebakiza uzi wa katikati,hapo ndani hakuna chupi!

Tulioga mtoni kama wachawi. Kukutana na baba yako anaoga mtoni uchi wa nyama ilikuwa jambo la kawaida maana mito mingi ilikuwa njiani. Mkosi ulioje kuona viungo vya baba yake? Kiafrika hii haikubaliki. Nchi ilikuwa na hali mbaya hii jamani acheni tu! Vijijini watu walivaa magunia na mifuko ya simenti, kunguni na chawa vilikuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu hadi tukavitungia na methali kabisa kwamba kidole kimoja hakivunji chawa na kitanda usichokilalia utajuaje kunguni wake?

Tulikula mdundiko na kitumbo kutoka Japan. Hii ilikuwa aina ya mchele. Kuna watu walifungwa kwa kudhaniwa wahujumu uchumi kisa tu wamekutwa na vyakula kutoka nje ya nchi! Home mkinywa chai na mkate mnaoneka matajiriii! Wali uliliwa Jumamos kuamkia Jumapili ili mpate wa chai kabla ya kwenda kanisani. Wali tuliita kicheka na watoto. Siku ya wali watoto mlioga mapemaaaa,bila kusukumwa. Nayaeleza haya ili mjue tulikotoka!

Tulikuwa tunanunua tisheti za mikono mifupi, ukilifua mara mbili linakuwa mikono mirefu, na kola inalegea utadhani unanyonyesha. Halafu mtu alilivaa tisheti hilo hadi mgongoni linakuwa kama nyavu. Enzi zile mtumba ulikuwa unapita hapo bandarini Dar es Salaam unakwenda Burundi halafu unarudi Tanzania kwa njia ya magendo.

Madingi zetu walishinda vichakani kukwepa kodi ya kichwa. Wakati mnaenda shule mnaweza kukutana na baba yako amejificha juu ya mti kuwakwepa mgambo. Mgambo walikuwa wanoko hao! Kodi ya shilingi tano ilimtoa jasho babu yako. Leo anaibuka mtoto wa juzi anasema nchi hii ameifia. Umeifia nchi na wakati hujawahi kwenda chooni peku, tena choo cha shimo wakati wa mvua halafu hakijaezekwa.

Dhiki na umasikini wa kunuka Tanzania ulianza mwaka 1967 mara tu baada ya kutangazwa Azimio la Arusha, wahuni wakalihujumu. Tunapokwambia wahuni siyo watu wazuri mnatakiwa muelewe ili muwashughulikie. Nyerere na Sokoine wake walikomaa na ujamaa hadi wakasema poo. Sema na wao kuna sehemu walibugi, maana walianza kukamata watu wenye pesa kuwa ni wahujumu uchumi. Matajiri wakasema isiwe taabu. Wakaanza kuficha pesa porini, maana ukiweka benki ulifuatiliwaaaaaaa hadi kero.

Nyerere alifanikiwa sana katika kutujengea uzalendo lakini katika uchumi alisalimu amri akasema nang'atuka, neno ambalo hata kwenye kamusi ya Kiswahili halikuwepo, labda liwe limeingizwa siku hizi. Mchakato wa kumtafuta mrithi wake ukaanza. Mezani yakawekwa majina matatu. Ali Hassan Mwinyi; Dk Salim Ahmed Salim; na Rashid Mfaume Kawawa. Mnyukano wa hoja ukapigwa, mara Kawawa akajitoa. Yakabaki majabali mawili. Zikaendelea kupigwa. Hatimaye Mwinyi akaibuka kidedea kutokana na sifa yake ya kutokuwa na makundi. Yeye anasema kundi lake ilikuwa Zanzibar.

Hata mabadiliko makubwa aliyoyafanya Zanzibar yalimuongezea CV ya kupewa Urais wa Tanzania. Nakumbuka akiwa Rais wa Zanzibar kilikuwa ni kipindi bora kabisa kiuchumi tokea kuanguka kwa bei ya karafuu na baada ya vita ya Kagera. Aligeza mikanda iliyokuwa imewakaza wananchi, bidhaa kutoka kila kona ya dunia zikaanza kumiminika Zenj. Zenj ikawa Dubai ya Afrika Mashariki na Kati. Wazanzibar wakawa na unafuu wa maisha hadi tukawaonea gere. Bara tulikwenda kununua vitu Zanzibar kwa bei chee. Hali iko hivyo hadi leo. Nani asiyejua unafuu wa TV zenj? Wakisikia uko Zenj watu watakuagiza vitu kibao kama tunavyoagizana vitenge kwa bei ya chee kutoka Kigoma.

Basi bwana alivyopata Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama kawaida yake, Mwinyi akaanza kuigeuza Tanzania, kutoka kwenye fikra za kijamaa kwenda kwenye fikra za kibepari. Wakati wa hotuba yake ya kwanza kwa Bunge la Tanzania 1986, aliahidi kuanza mazungumzo na IMF na Benki ya Dunia kwa faida ya nchi yetu. Mwanzoni hatukuamini kama Mwinyi angeweza kuachana na sera za Nyerere kwani alikuwa mfuasi mwaminifu wake. Kumbe Baraka zote za mabadiliko zilitoka kwa Mwl. Nyerere.

Baada ya Mwinyi kukabidhiwa nchi Mwalimu aliitisha kikao cha kamati Zanzibar. Katika kikao kile akasema kwa kuwa yeye kang’atuka, basi tuendelee na mazungumzo na wahisani tuitikie makubaliano kwani hali ilikuwa mbaya sana. Baada ya hapo yalifuata mageuzi kwa kulegeza masharti ya biashara na uwekezaji. Kwa mara ya kwanza Tangu IMF na WB watimuliwe na Mwalimu tukakopa nje mkopo wa dola milioni 78.

Nchi ndio ikwa imefunguka hivyo. Watanzania wakaanza kufanya biashara na nchi nyingine, waliokwenda Kenya kupeleka machungwa, na wao kurudi na sabuni za kufulia na kuogea, waliokwenda Uganda, Burundi, waliokwenda Uarabuni, Ulaya, Marekani, alimuradi kila mmoja alikwenda alikotaka. Kibondo watu walifanya biashara ya bia za PRIMUS. Soko la bidhaa mbalimbali likashamiri. Bidhaa zikatafuta watu, siyo watu kutafuta bidhaa kwa foleni tena. Utawala wa huyu bwana ukashusha na neema kubwa kubwa na neema ndogondogo.

Nguo za dukani bwerere, mitumba bwerere, sabuni kibao, fegi bwerere, magari makubwa na madogo bwerere, televisheni kibao, Radio kibao, na ngono kwa sanaa! Mwaka 1994 Watanzania tukaangalia World Cup kwenye TV zetu wenyewe. Ruksa ikawa ruksa; jaza duka, jaza akaunti za benki utakavyo sikuulizi pesa umetoa wapi. Maduka yakajaa ghafla bidhaa, pesa za kigeni zikajaa ghafla, zimetoka wapi nobody knew and nobody cared. Mabenki yakapata pesa nyingi. Watu wakawa na pesa kama serikali ya Ghara, serikali ya Mwinyi ikawa maskini. Mzee alifungua nchi ikafunguka kweli.

Pesa ilisambaa nchini asikwambie mtu. Watu walitembea wameinamisha vichwa chini waokote pesa. Ruksa ilikuwa ruksa. Nakumbuka Show ya Kanda Bongo Man ndani ya Kilimanjaro Hotel miaka hiyo ya 90 kiingilio ilikuwa laki moja na ukumbi ulitema. Leo nani atapiga show ya laki moja ajaze. Thubutu. Mwinyi aliistaarabisha nchi hii hadi tukaachana na ushamba wa kumiliki televisheni kwamba ni uhujumu uchumi.

Hebu tupumue kidogo kwa kusoma vitabu vya Mpagaze. Kama hauna rusha 10,000 nikurushie vyote. Mpesa 0753665484. Haya twendelee!

Enzi za Mzee Mwinyi watu walishiba uhuru hadi wakaanza kuingilia uhuru wa wengine. Kuna siku alisema Kuran ibadilishwe kwa sababu inavunja haki za wanawake kwa kuruhusu mwanaume kuoa wake wengi otherwise naye atawasilisha hoja ili wanawake nao waruhusiwe kuolewa na wanaume wengi. Hii iliwakera sana Waislam wa Zanzibar, wakaandamana kupinga.

Mwinyi akamaliza mgogoro kwa kusema yalikuwa mawazo ya Sophia siyo mawazo ya chama na serikali. Unahitaji umakini mkubwa sana kujadili masuala ya dini mbele ya wenye dini zao maana wanaweza kukufanya lolote kama ilivyomtokea Mwinyi wenyewe mwaka 2009 pale alipohutubia Baraza la Maulid na kuwataka Waislamu wajikinge na maradhi hayo kwa kutumia kondom, kijana mmoja akamnasa kibao.

Mwinyi alifanya yale nchi nyingine maskini ziliishafanya kitambo kama China na kuchomoka. China chini ya utawala wa Deng Xiaoping miaka ya 1978 ilianza sera za uwazi baada ya Mao Zedong kufariki. Hii ndiyo imeifikisha China leo hapo walipo hadi kuinyima usingizi Marekani. Kipindi cha Mwinyi wafanyakazi walidharaulika. Mwinyi alishughulika na wafanyabiashara walioleta hela hadi ajira ikaonekana ni njaa tu, watu kibao wakaacha kazi serikalini. Kipindi hicho private sector ndiyo iliwika. Siku hizi private sekta njaa tupu, serikali ndio wanatamba mjini.

Hata lilie fagio alilopewa kufagia walanguzi hakulitumia tena maana walijifagia wenyewe baada ya bidhaa kupatikana kwa wingi. Watu wakasema Fagio aliondoka nalo Lyatonga Mrema pale alipojaribu kufagia pale airport akakumbana na moto hadi ufagio ukayeyuka! Alikuja kutulizwa kwa cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Stan Katabalo yeye akasema fagio lilikwenda kufagia wamasai pale Loliondo. Stan aliandika hivyo kwenye gazeti lake kwa sababu nchi ilikuwa na uhuru wa kujieleza.

Uhuru wa kujieleza ulipelekea vyombo vya habari kuchapisha bila uoga kila kashifa waliyoidaka. Waliibua hadi zile kashfa zilizotokea enzi za Nyerere ikiwa ni pamoja na kuungua kwa Benki Kuu ya Tanzania. Iliungua mwaka 1984 waziri wa fedha akiwa Kighoma Malima na Gavana Charles Nyirabu. Charles Nyirabu baadaye naskia alikuja kuanzisha benki yake, ikamshinda akawauzia Wakenya.

Nani alichoma benki? Kaitafute Ripoti ya Scotland Yard. Mie nachokumbuka tu ni kwamba Benki iliungua 17 Mei 1984 mwezi mmoja baada ya Edward Moringe Sokoine kufariki yaani 12 April mwaka 1984. Kashfa ziliendelea kuripotiwa kwenye vyombo vya habari na Mwinyi hakuzuia maana tayari aliishachukua mkopo kutoka kwa watu wanaotaka serikali itukanwe.

Kama unavyojua tena, hakuna mkopo unaokuja kizembe maana anayekukopesha siyo baba yako. Tukiendelea kukopa ipo siku tutaambiwa ushoga ruksa, hutaki tema pesa zangu. Siunataka pesa zangu? Hata Spika Ndugai ameshtuki mikopo na kuitangazia dunia kwamba nchi itapigwa mnada. Mwenye nchi akasema msitukatishe tamaa lazima tukope.

Mihimili miwili imepishania . Ukiona mke na mume wanatukanana hadharani basi ujue ndani wameishatukanana hadi wakachoka. Katika hilo la wakubwa kupishana mimi sitii neno zaidi ya kushauri tu kwamba ukiona ndugu wanagombana chukua jembe ukalime, wakipatana chukukua kapu ukavune.

Hata kujulikana kwa kashfa ya Chavda ni kwasababu ya Mzee Mwinyi aliruhusu watu waseme na wakasema kweli na hii ndiyo maana ya ruksa. Issue ya Chavda Wahenga mnaijua. Ilihusu Mfanyabiashara Vidyadhar Girdharal Chavda, maarufu kama V.G. Chavda. Huyu mwamba alikopa benki dola milioni 3.5 ili kuboresha mashamba ya mkonge ikiwa ni pamoja na makazi ya wafanyakazi, kukarabati mashine za na kulima mashamba upya ya mkonge. Walidai miradi yao ingeleta ajira 1,400 na faida ya fedha za kigeni dola milioni 42 lakini wakala kona.

Zaidi ya kashfa 86 zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari wakati wa Mzee Mwinyi. Hata ile kashifa ya kampuni ya Mohamed Enterprise kusambaza chakula ambacho hakifai kwa matumizi ya binadamu mwaka 1995 Mrema akasema angeishughulikia, lakini alibadilishwa cheo chake kuwa Waziri wa Vijana na Utamaduni kabla ya kuchukua hatua,tuliijua kupitia vyombo vya habari.

Enzi hizo Mrema naye alivuma kuliko Rais hadi Remmy Ongala akatunga kibao murua kumpongeza Mrema. Kinaitwa Mrema. Hebu kisikilize kidogo halafu tuendelee. .

Wengine waliomsumbua Mwinyi ni Maalim Seif Sharif Hamad na Mchungaji Christopher Mtikila lakini wote aliwamudu. Ukitaka kujua walimsumbuaje na aliwamudu vipi soma kitabu chake, kinaitwa Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu. Nikieleza yote hapa kitabu kitakosa soko na hivyo kumkosesha mapato. Kitafute ukisome, kina mengi sana. Humo utakutana na lile tukio na Waziri aliyemfukuza Mwinyi kwenye nyumba ya serikali kama mbwa na kumwambia arudi kwao Zanzibar, akamdhulumu na vifaa vyake vya ujenzi, mara Mwinyi akawa Rais halafu akampa uwaziri huyo bwana kwa sababu visasi si kazi yetu ni kazi ya Mungu. Kanunue kitabu hicho utaenjoy walahi.

Labda tu nikujuze kashfa moja tu iliyoisumbua serikali ya Mzee Mwinyi. Ni kashfa ya Loliondo. Ilitokea mwaka 1992. Ni ya mtoto wa Mfalme wa Kuwait kupewa ardhi ya Wamasai kihuni. Hii iliripotiwa sana na gazeti la Mfanyakazi hadi mwandishi Stan Katabalo akapoteza maisha. Stan Katabalo alipambana vita ile akiwa peke yake maskini ya Mungu na mauti yakamkuta peke yake akitumikia umma. Hili ndilo tatizo la Afrika. Mwandishi wa habari anajiita sauti ya umma lakini yakimkuta hakuna umma nyuma yake.

Stan alikubali mwaliko akaenda Nigeria, kisha alikutwa Kunduchi Beach Hotel kafa kwa shinikizo la damu. Katika makala zake za mwisho aliwahi kuandika kuwa, "Najua nitakufa na kalamu yangu ndio inaniua, lakini katika vizazi vijavyo watatamani kuona fuvu langu ili watathmini ubongo wangu umekaaje." Sasa ni muda wa kumuenzi Stan. Mimi nitamuenzi kwa kuandika historia yake kwa kina. Nikimaliza ya Stan nitawaletea ya Melek Kangero, Mwandishi aliyemsumbua Nyerere miaka ya 60.

Hata wale wabunge waliojiita G.55 walitumia demokrasia aliyoruhusu Mwinyi kudai serikali tatu. Njelu Kasaka mbunge wa Chunya enzi hizo ndiyo alijitoa muhanga kumfunga kengere paka maana kipindi hicho ukigusa muungano uligusa sharubu za Nyerere, kilichofuata Mungu ndio alijua. Nyerere aliwashauri waachane na hoja hiyo watahatarisha muungano, lakini hawakusikia. Wakafanikiwa kupeleka hoja yao bungeni kwa mbwembwe na hoja yao kuungwa mkono na wabunge zaidi ya 100 kisha hoja ikapanguliwa na hoja ya kwamba haikuanzia kwenye chama.

Baada ya hapo Nyerere akawashukia Malecela na Kolimba kwa kuruhusu hoja ya kuvunja muungano kuingia bungeni. Aliwaona ni wahaini maana hawawaonei huruma Wazanzibari. Kolimba akajibu mapigo ya Nyerere, Malecela yeye akakaa kimya maana alimjua Nyerere vizuri. Kolimba akaichana CM kwamba imepoteza dira na mwelekeo. Kumbuka Kolimba alikuwa ndio Katibu Mkuu wa CCM na Waziri wa Mipango katika serikali ya Mwinyi. Kauli yake ilisababisha mtafaruku mkali kiasi cha kufanya Kamati Kuu ya CCM imuite Dodoma kujieleza na muda mfupi baada ya kujieleza alikufa kwa shinikizo la damu. Ukaibuka usemi mtaani ukimzingua mtu anakwambia nitakukolimba.

Kwakweli enzi zile ukitaka kuijua hasira ya Nyerere gusa muungano. Rais Jumbe wa Zanzibar alipoteza kibarua chake kwa sababu ya muungano na Mwinyi alipata urais wa Zanzibar kwa sababu ya muungano. Jumbe alikuwa mrithi wa Karume. Nyerere ndo alimuweka Jumbe madarakani na kisha kumuondoa kwa sababu siasa hazina urafiki wa kudumu, siasa zina maslahi ya kudumu.

Ngoja nikusimulie kidogo walau upate picha. Baada ya kifo cha Karumr, Wazanzibar walimpendekeza Kanali Bakari kumrithi Karume, Nyerere akampenda Jumbe kwa sababu Jumbe ni kiongozi aliyeonekana kuwa na uhakika wa kuulinda muungano kutokana uzoefu wake katika mambo ya Muungano. Wakati huo alikuwa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mambo ya Muungano kwa muda mrefu. Kilichomponza Jumbe ni kujisahau.

Jumbe alipopewa nchi akawa kipenzi cha Nyerere hadi akajenga makazi yake Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na kurejea tena jioni baada ya kazi. Uwepo wake Zenj ukafifia, akili yake yote ikawa bara maana alijua ndio mrithi wa Nyerere. Jumbe akabariki hadi muungano wa ASP na CCM.

Mara mambo yakageuka, Nyerere akamteua Moringe Sokoine kuwa Waziri Mkuu, mapenzi yake yakahamia kwa Sokoine, kelele zikaanza kumtabiria urithi wa Nyerere. Matumaini ya Jumbe kuwa Rais yakaanza kufifia. Nyerere akaja na hoja ya kubadilisha Katibu tuwe na serikali moja. Wazanzibari wakachachamaa, wakamchukia Nyerere na kumuita Jumbe rafiki wa Nyerere msaliti.

Jumbe akashtuka na harakka akaamua kurudisha imani Zanzibar. Akaitisha mkutano na makatibu wakuu wote na vingunge wote waseme aina ya serikali wanayoitaka. Wote kasoro Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian Lubuva, walitaka serikali tatu.

Jumbe akamtimua Lubuva Zenj kwa sababu alionekana msaliti na nafasi yake kupewa Mghana, Alhaj Bashir K. Swanzy. Kuanzia hapo, madai ya kutaka serikali tatu na wengine wakitaka muungano uvunjwe kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto. Jumbe akawaambia msihofu hili linakwisha akaisha yeye. Jumbe akaandaa Hati ya Mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hati hiyo ikapotelea mezani kwake na kuibukia kwa Nyerere. Jumbe akaandika barua ndefu kwa Mwalimu kubainisha jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyoendelea kukiukwa na utawala wa nchi. Barua hiyo ndefu pia ikapote hata kabla hajaitia sahihi na kuibukia kwa Nyerere tena.

Kikaitishwa kikao cha dharura cha CC ya CCM mjini Dodoma kumjadili Jumbe kwa dhambi ya kuhoji muungano. Nyerere akamuuliza Jumbe, moja kujulimsha moja ni ngapi? Akasema ni mbili. Sasa kama ni mbili kwa nini unataka serikali tatu? Jumbe akavuliwa uanachama wa CCM na automatically akapoteza sifa ya kuwa Rais wa Zanzibar na kuwekwa kizuizini, Mwinyi akachukua kiti cha Urais kwa sababu kufa kufaana. Hata yule mwanasheria wake kutoka Ghana naye akapewa masaa 24 kufutika Zenj.

Ya Mwinyi yako mengi sana hadi kuna lile tukio la Michal Jackson kuja Tanzania na kupokelewa na Mwinyi. Mwinyi alimkaribisha hadi nyumbani kwake na kupiga story kama baba na mtoto. Nitakuonyesha picha yake utafurahi. Labda tu kwakuwa Mzee kaandika kitabu na kinapatikana basi kitafute, humo utaona hata jinsi Nyerere alivyompelekesha Mzee Mwinyi hadi akamtungia kitabu kwa lugha kali kabisa. Kinaitwa Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania. nimechoka!

Halafu pamoja na kutukanwa sana na Nyerere siku ya msiba wa Nyerere alisema Nyerere alikuwa kama mlima Kilimanjaro na yeye kama kichuguu. Siku ya msiba wa JPM alisema aliyoyafanya JPM kwa muda mfupi wao walishindwa kuyafanya kwa miaka 30.

Unyenyekevu na utii kwakweli vimemsaidia Mwinyi kula maisha bila kutoka jasho sana. Hata alivyopata urais wa Zanzibar ni unyenyekevu tu. Wala hakujiona mwenye akili nyingi kuliko watu wote aliowaongoza kama ilivyo kwa viongozi wengine; akipata cheo anaamini ana akili kuliko watu wote anaowaongoza. Hata kiongozi aliyesoma elimu ya siasa anajua mitambo ya umeme kuliko injinia wa TANESCO! Matokeo yake ndo haya ya maumeme kukatika kila mara.

Halafu sikumbuki kama Mzee Mwinyi alikuwa na vikundi vya kusifu na kuabudu zaidi ya kuitwa Mtukufu wakati wa Taarifa ya Habari kama Mtukufu Daniel Arap Moi.


Viva Mzee Mzee Mwinyi Viva!
Mbona Taarabu nyingi we mtu wa pwani?!
 
umefukua makaburi mengi ila shukrani sana kwa taarifa hizi.Kuna kashfa moja nadhani utawala wa Mkapa ila ya milioni900 za minofu ya samaki
 
Inaonekana ni story ya kutunga na familia ya Natepe ilikanusha hilo.
Mzee Natepe hakuwa Waziri baada ya Mwinyi kujiuzuru.

Mawaziri wa Mambo Ya Ndani:

1. Sir George Kahama (1961-62)
2. Oscar Kambona (1962-63)
3. Lawi Sijaona (1963-65)
4. Job Lusinde (1966-67)
5. Said Maswanya (1967-73)
6. Omary Muhaji (1973-74)
7. Ally H. Mwinyi (1975-76)
8. Hassan N. Moyo (1977-78)
9. Salmin Juma (1979-80)
10. Abdalah Natepe (1980-83)
11. Muhidin Kimario (1983-89)
12. Nalaira Kiula (1990-90)
13. Augustin Mrema (1990-94)
14. Ernest Nyanda (1995-95)
15. Ali Ameir (1995-99)
16. Mohamed S. Khatib (2000-2002)
17. Omar Mapuri (2003-05)
18. John Chiligati (2006-06)
19. Lau Masha (2008-2010)
20. Shamshi Nahodha (2010-12)
21. Emma Nchimbi (2012-13)
22. Emma Chikawe (2013-14)
23. Charles Kitwanga (2015-16)
24. Mwigulu Nchemba (2016-18)
25. Kangi Lugola (2018-2020)

26. GEORGE BONIFACE TAGULUVALA SIMBACHAWENE (2020-----
JF kisima Cha maarifa.
 
Back
Top Bottom