Kenya 2022 Mfahamu George wajackoyah: Mgombea urais Kenya anayesisimua kwa Bangi na sumu ya Nyoka

Kenya 2022 General Election

mtwa mkulu

JF-Expert Member
Sep 11, 2013
5,555
4,947
george Wajackoyah

Mgombea George Wajackoyah

Wakati mmoja alikuwa mtoto wa kurandaranda mitaani nchini Kenya na wakati mwengine akawa mchimba kaburi nchini Uingereza, George Wajackoyah amekuwa kivutio cha kisiasa kwa kugombea urais wa Kenya kupitia ahadi ya kuligeuza taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa muuzaji mkubwa wa bangi, sumu ya nyoka na korodani za fisi, ingawaje wengi wanahoji uwezekano wa mipango yake.

Profesa huyo mwenye umri wa miaka 63, ambaye ana taaluma ya sheria, ameonekana kuwa mgombea mwenye maono tofauti kati ya wagombea wanne wa urais walioshiriki uchaguzi wa Agosti 9.

Kura za maoni zimemweka mgombea wa Chama cha Roots katika nafasi ya tatu duni - kura ya hivi punde zaidi, iliyotolewa tarehe 11 Julai, inampa asilimia 4% ya kura.

Lakini wadadisi wanasema kuwa kwa kuwa mgombea wa mara ya kwanza anafanya vyema na wagombea wawili wakuu watakuwa na wasiwasi wa kupoteza kura hata moja huku kura hiyo ikitabiri ushaindani mkali kati ya kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga kwa 43% na Naibu Rais William Ruto mwenye asilimia 39.

‘’Wajackoyah anawania wadhfa huo kupitia ujumbe ambao ungepuuzwa na wengi mjini , lakini bila shaka ameteka hisia na maono ya vijana wengi wenye hasira katika maeneo ya mashambani na mjini nchini kenya , bila kujali kabila , eneo wanalotoka na misingi ya kisiasa’’, anasema Macharia Gaitho, mwandishi wa gazeti la Daily Nation nchini Kenya.

Akiwa katika kampeni zake Wajackoyah anapendelea kuvalia ‘tracksuit’ , Tishati Pamoja na kitambaa cha kichwa badala ya makoti yanayoonesha haiba ya hali ya juu – ili kuonesha kwamba yeye sio mmoja ya walio katika uongozi wa Kenya ambao anawatuhumu kwa ufisadi.

Pia mara nyengine huonyesha ishara ya mtu anayevuta bangi na anapocheza nyimbo za reggae huwafurahisha na kuwavutia wengi.

Prof Wajackoyah anasema iwapo atashinda atapitisha sheria za kudhibiti ukulima na uzalishaji wa bangi kwa matumizi ya viwandani na kimatibabu, ili kusaidia kutatua matatizo mawili makubwa nchini Kenya - ukosefu wa ajira na deni la taifa linalozidi kuongezeka.

Anadai kuwa inaweza kuipatai Kenya zaidi ya shilingi trilioni tisa ($76bn; £64bn) kila mwaka, na serikali "haitalazimika kukopa hata shilingi moja" .

"Nchi za magharibi zimehalalisha bangi [bangi]; kwa nini sisi tusihalalishe?" anaongeza.

george wajackoyah

Wajackoyah anakosolewa na wapinzani wake kwa kufanya kampeni za kuwafurahisha raia

Ijapokuwa hajaunga mkono hoja yake na utafiti wa kina, uhalalaishaji wa bangi kwa matumizi ya viwandani na matibabu ndio hoja kuu ya kampeni zake.

Tovuti ya Africa Check imetaja mipango yake kuwa ya kupotosha.

Hata hivyo, imemfanya kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, na amewasisimua vijana wengi, ambao wameathiriwa vibaya na ukosefu wa ajira

Iwapo pendekezo la Prof Wajackoyah litaidhinishwa, Kenya itajiunga na mataifa mengine ya Afrika - ikiwa ni pamoja na Lesotho, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe - ambayo yanatafuta kuingia katika soko la kimataifa la bangi, ambayo, kulingana na makadirio, inatarajiwa kuwa na thamani karibu $70bn kufikia 2028.

Prof Wajackoyah anasema hajawahi kuvuta bangi, lakini atakuwa mtu wa kwanza kufanya hivyo katika kushererehekea kuhalalishwa kwa bangi nchini.

“Hakuna ubaya kuivuta wakati imehalalishwa na vyombo vya udhibiti vimeidhinisha ivutwe,” anasema.

Maoni ya Prof Wajackoyah yamekashifiwa na Kanisa Katoliki la Kenya, linalosema kuwa utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana utaongezeka iwapo bangi itahalalishwa.

"Misingi ya familia inatishiwa na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kusababisha kuvunjika kwa mahusiano, vurugu na hata vifo wakati mwingine," Askofu James Maria Wainaina alisema.

Prof Wajackoyah pia ameahidi kukaguliwa upya kwa kandarasi zote zilizotolewa kwa kampuni za Uchina na serikali ya Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.

China inachangia 21% ya deni la nje la Kenya hali inayosababisha kilio nchini humo hususan kutokana na masharti ya kandarasi hizo za ujenzi wa miundombinu, kama barabara na reli kwasababu masharti yake hayajawekwa wazi.

Prof Wajackoyah anaona ufugaji wa nyoka kuwa nguzo nyingine kuu ya uchumi wa Kenya.

Sumu ya nyoka

Nyoka aina ya Green Mamba yenye sumu kali hupatikana sehemu za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika

Anasema sumu ya nyoka, ambayo anadai ni "ghali kuliko dhahabu", itatolewa ili kuzalisha dawa ya kuzuia sumu ya nyoka, wakati nyama ya nyoka itasafirishwa kwenda nchi kama China, ambako inachukuliwa kuwa mlo mtamu .

"Tunaweza kuwa na dola bilioni kila mwaka kuendeleza uchumi," Prof Wajackoyah anasema, bila kutoa ushahidi wowote kuunga mkono takwimu anazotoa.

Anasema pia kuwa Kenya inafaa kusafirisha nje ya nchi korodani za za fisi zinazotumika kwa matibabu nchini Uchina, akisema hilo linaweza kuleta mapato zaidi ya bangi.

Vikundi vya wanyamapori na Muungano wa Madaktari wa Mifugo nchini Kenya wamelalamikia wazo hilo.

"Biashara ya nyoka na korodani za fisi hairuhusiwi na ni tishio kwa uwepo wa wanyama pori," muungano wa madaktari wa mifugo unasema kwenye Taarifa yake.

Inaongeza kuwa pendekezo hilo ni "kichocheo cha janga jingine" kwa sababu linaweza kusababisha kuenea kwa virusi, bakteria na vimelea kutoka kwa fisi na nyoka hadi kwa wanadamu.

Mnyama aina ya fisi

Mnyama aina ya fisi ni kivuti kikuu cha utalii nchini Kenya

Licha ya kulaaniwa kwa kile ambacho wakosoaji wanakiita kampeni za uchochezi, wafuasi wa Prof Wajackoyah wanampenda kwa kupitia hali ngumu maishani ili kuwania urais.

Alikulia mshambani katika eneo la magharibi mwa Kenya, na baada ya wazazi wake kutengana aliishia kuishi katika mitaa ya mji mkuu, wa Nairobi.

Aliokolewa na wumini wa hekalu la dini ya Hare Krishna , ambao walikuwa wakiwasaidia watu wasio na makao.
Prof Wajackoyah aliishi katika hekalu hilo na kuwa muhubiri wa hare Krishna.

Alifadhiliwa kukamilisha elimu yake ya upili na baadaye kujiunga na kitengo cha polisi wa kenya kabla ya kupanda ngazi na kuhudumu katika kitengo cha kijasusi.

Ijapokuwa amekuwa mchache wa maelezo yake , profesa Wajackoyah anasema kwamba alijipata katika shida baada ya kupata taarifa muhimu kuhusu moja ya mauaji ya watu mashuhuri nchini Kenya, yale ya Waziri wa Mambo ya Nje Robert Ouko mwaka 1990.

Prof Wajackoyah anasema alikamatwa na kuteswa na baada ya kuachiliwa alitoroka Kenya kwa usaidizi wa ubalozi wa Marekani jijini Nairobi.

Mauaji ya Bw Ouko yalisalia kuwa kitendawili kwa umma hadi uchunguzi wa bunge mwaka wa 2010 ulipofichua kwamba aliuawa katika mojawapo ya makao rasmi ya aliyekuwa Rais wa wakati huo Daniel arap Moi.

Baada ya kutoroka Kenya, Prof Wajackoyah alielekea Uingereza ambako alifanya kazi duni na kutafuta elimu katika Chuo Kikuu cha Soas cha London, Chuo Kikuu cha Warwick na Chuo Kikuu cha Wolverhampton.

Alipokuwa akisoma huko Wolverhampton pia alifanya kazi kama mlinzi, mchimba kaburi na kuosha maiti ili kujipatia riziki.

Kazi hizo "zilimnyenyekeza na kumkomaza," aliambia gazeti la Daily Nation.

Anasema hatua yake ya kufanya kazi na wakati huohuo kusoma kulimwezesha kupata daraja la tatu ya shahada ya sheria.

Haizingatiwi kwamba alifuzu kwa kiwango cha juu.

Alihusika katika kampeni za kisiasa nchini Uingereza kushinikiza mabadiliko katika sehemu mbalimbali za dunia - na alishirikiana na na Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings, ambaye alichukua mamlaka kupitia mapinduzi mwaka 1981 na kutawala hadi 2000.

Prof Wajackoyah baadaye alihamia Marekani, ambako alikutana na mke wake mwenye asili ya Kiafrika. Inasemekana wanandoa hao wana watoto watatu.

Pia amesoma katika taasisi mbalimbali za Marekani, ikiwa ni pamoja na kupata shahada ya uzamifu kutoka Chuo Kikuu cha Walden akisomea mtandaoni.

Anadai kuwa na jumla ya digrii 17, nyingi zikiwa za uhamiaji, sheria za kimataifa na wakimbizi, jambo ambalo lilimfanya Gaitho kumekejeli kwamba anajivunia "shahada nyingi za chuo kikuu kuliko muda unaohitajika kumaliza kozi zote hizo".

Prof Wajackoyah alirejea Kenya mwaka wa 2010, na kutangaza kuwa anataka kuwania wadhfa wa urais.

Aliachana na azma yake wakati huo, na kuifufua tena katika uchaguzi huu na kuwa kile ambacho gazeti moja kuu nchini Kenya, The Standard, limetaja kuwa "msisimuko katika kampeni".

Katika ahadi nyingine zenye utata katika kampeni yake, Prof Wajackoyah anasema ataboresha uwiano wa maisha ya kazi kwa kuanzisha siku nne za kufanya kazi nchini ili kuwapa Waislamu likizo ya kuabudu Ijumaa, Waadventist Jumamosi na Wakristo wengine Jumapili.

Prof Wajackoyah pia ameahidi kurudisha hukumu ya kifo, na anasema wale watakaopatikana na hatia ya ufisadi watakuwa na chaguo la kuuawa kwa kupigwa risasi au kunyongwa "baada ya kula ugali .

Source: Evelyn Musambi BBC Swahili
 
0 Reactions
Reply
Top Bottom