Meya wa Kinondoni afanya ufisadi

hee hee JF ni hapa asemapo kwengine muungo.

sawa mkuu masatu tunakutakia safari njema

ila isije ikawa safari za usimgizini
 
Londa sasa ashauriwa ajiuzulu

na mwandishi wetu

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa anadaiwa kukaidi ushauri wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumtaka ajiuzulu.

Ushauri huo umekuja baada ya kiongozi huyo kutuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, pamoja na ufujaji wa fedha za manispaa hiyo.

Kamati ya Siasa ya CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, ilikutana Aprili 6, mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

Taarifa za uhakika zimesema kuwa, Londa (pichani chini) alipaswa kuwa amewasilisha barua ya kujiuzulu Aprili 15, lakini alikaidi ushauri huo, kwa madai kuwa hawezi kujiuzulu bila ya kuandikiwa barua na chama chake.

Taarifa zaidi zimesema kuwa, suala hilo tata la Meya Londa sasa litapelekwa kwenye vikao vya juu vya CCM, ili kupatiwa ufumbuzi.

Miongoni mwa tuhuma anazotuhumiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Meya, fedha za safari za nje, pamoja na fedha za safari za madiwani.

Kwa mujibu wa taratibu za manispaa hiyo, kuanzia mwaka 2005, Sh milioni 100 hutengwa kwa ajili ya Mfuko wa Meya, Sh milioni 100 kwa ajili ya safari za kikazi nje ya nchi, na Sh milioni 60 kwa ajili ya safari za mafunzo za madiwani.

Lakini Londa anatuhumiwa kutumia vibaya fedha hizo zaidi ya Sh milioni 700, kinyume cha malengo yaliyokusudiwa, na bila ya kuwa na vielelezo vyovyote kuonyesha jinsi zilivyotumika.

“Fedha za Mfuko wa Meya zinatakiwa kutumika kuwasaidia wananchi wanaokumbwa na maafa kama kuunguliwa nyumba, lakini hilo halijawahi kufanyika katika manispaa yetu.

“Ukiachilia mbali fedha hizo, amekuwa akisafiri nje ya nchi, lakini hakuna ripoti yoyote ya safari ambayo amewahi kuiwasilisha popote, au hata kununua kitu chochote kwa ajili ya manispaa.

“Haya fedha za safari za kikazi za madiwani, ni juzi juzi tu, ndiyo ameshituka na kutupeleka Tanga, lakini kabla ya hapo hakukuwa na kitu.

“Ukitaka kujua kuwa manispaa yetu pamoja na kuwa tajiri katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini maendeleo hakuna, barabara mbovu, ujenzi wa madarasa tunasuasua, na mengine mengi,” alisema mmoja wa madiwani katika manispaa hiyo.

Londa pia anatuhumiwa kula njama na kuchota zaidi ya Sh milioni 100 kupitia zabuni ya ununuzi wa matela ya kuzolea taka, iliyotolewa na Manispaa hiyo. Taarifa za uhakika zimesema kuwa, Julai mwaka jana, kikao cha bajeti cha Manispaa ya Kinondoni, kilipitisha uamuzi wa kununua matela 25 ya kuzolea taka.

Matela hayo 25 yalikuwa yagharimu kiasi cha Sh milioni 8 kila moja, ambapo manispaa hiyo ingelipa jumla ya Sh milioni 200.

Lakini badala yake, inadaiwa kuwa kiongozi huyo wa manispaa hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wasiokuwa waaminifu, waliamua kuyalipia matela hayo Sh milioni 12 kila moja, na wao kujipatia Sh milioni 100 kinyume cha sheria.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, baada ya kujipatia Sh milioni 100, kiongozi huyo na wenzake, walitaka kujipatia fedha zaidi, kwa kuongeza malipo hayo kutoka Sh milioni 12 kwa kila moja, hadi milioni 15, katika ununuzi wa matela mengine 25.

Hata hivyo katika jaribio la pili la mpango huo wa kujipatia Sh milioni 180 kwa kununua matela 25 kwa Sh milioni 15 kila moja badala ya Sh milioni 8, lilikwama baada ya kiongozi mwingine wa hapo kubaini na kufuta malipo hayo.

Kutokana na malipo hayo kufutwa, kampuni moja ya mjini Tanga (jina linahifadhiwa) ambayo ilishinda zabuni za kuiuzia Manispaa ya Kinondoni matela hayo, inakusudia kufungua kesi ya madai kutokana na kushindwa kufanyika biashara hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya awali.

Kampuni hiyo ya Tanga imechukua hatua hiyo baada ya Manispaa ya Kinondoni kutangaza upya zabuni ya ununuzi wa matela hayo, hatua ambayo imetokana ni njama za kutaka kuiba mamilioni ya fedha za manispaa.

Katika tuhuma nyingine, Londa anatuhumiwa kughushi nyaraka ili kumuwezesha binti yake (mkwe) kwenda Marekani, Julai mwaka jana.

Anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kumjumuisha Amina Salehe Londa, katika orodha ya madiwani vijana, ili aweze kwenda Marekani.

Madiwani vijana kutoka Manispaa ya Kinondoni walikuwa wamealikwa jimboni Florida, Marekani, mwezi Julai mwaka jana na Taasisi ya Sister Cities International.

Lakini jitihada za Londa kumpeleka mtoto wake, ziligonga ukuta, baada ya Ubalozi wa Marekani kumnyima kibali cha kuingia nchini humo (VISA), tarehe 11 ya mwezi huo.

Katika safari hiyo ambayo Alhaji Londa naye alikwenda Marekani, pia anatuhumiwa kurejea nchini na kompyuta ndongo (laptop) 20, na kuziuza kwa manispaa.

Lakini takwimu zinaonyesha kuwa, Meya huyo aliuza kompyuta hizo kwa Sh milioni 3 kila moja, bei ambayo inalalamikiwa kuwa ni kubwa, ikilinganishwa na bei ya soko.

Hata hivyo Londa alikanusha tuhuma zote hizo katika mkutano aliouitisha na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Februari mwaka huu, akisema si za kweli na kwamba zinapikwa na baadhi ya mahasimu wake wa kisiasa.

Source: Magazeti ya RA
 
Taarifa zaidi zimesema kuwa, suala hilo tata la Meya Londa sasa litapelekwa kwenye vikao vya juu vya CCM, ili kupatiwa ufumbuzi.

"vikao vya juu vya CCM, ..." Je ni zaidi ya kile cha Butiama?? Je kuna ufumbuzi wowote uliopatikana kutoka Butiama?

Nadhani sasa CCM wamebaki kutishiana tu ... ooh vikao vya juu, ooh tutaripoti kwa mkuu, ohh ...

 
"vikao vya juu vya CCM, ..." Je ni zaidi ya kile cha Butiama?? Je kuna ufumbuzi wowote uliopatikana kutoka Butiama?

Nadhani sasa CCM wamebaki kutishiana tu ... ooh vikao vya juu, ooh tutaripoti kwa mkuu, ohh ...


Huko ccm kuna mengi ila kama wameliona hili la meya basi kuna kazi imeanza kufanyika. Hivyo vikao vya juu ni mtihani mkubwa!
 
Back
Top Bottom