Meya Mstaafu Jacob: CHADEMA kukosa Wabunge kunaathiri Wananchi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,370
8,107
Meya wa zamani wa manispaa za Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob amesema kutokuwepo kwa wawakilishi wanaotokana na Chadema katika Bunge na mabaraza ya madiwani kunawaathiri zaidi wananchi.

Jacob, aliyekuwa diwani wa Ubungo kwa miaka 10, amesema anaamini Chadema ingekuwa na wabunge bungeni wasingekubali kupitishwa kwa masuala mbalimbali yanayolalamikiwa, likiwemo sakata la tozo za miamala ya simu.

Tozo hizo zilizua mjadala miongoni mwa wananchi na wadau wengine walizipinga hadi Serikali ikaamua kufuta baadhi na kupunguza kiwango kwa nyingine.

“Tunaamini Chadema ingekuwa bungeni hata masuala ya tozo yasingepitishwa, tungepambana. Na ushuru unaoanzishwa na baadhi ya halmashauri tungepinga kwa masilahi ya Taifa. Pia ukamataji holela wafanyabiashara unaofanywa na askari wa akiba usingetokea,” alisema Jacob.

Jacob alieleza hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika hivi karibuni alipotembelea ofisi za gazeti hili Tabata Relini, ambapo alizungumzia pia maisha yake nje ya siasa, akisema hivi sasa amejikita zaidi katika shughuli za ujasiriamali, hasa ufugaji kuku.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, CCM ilinyakua viti vingi vya udiwani na ubunge Tanzania bara na Zanzibar, huku Chadema iliyopinga matokeo hayo kwa ujumla wake ikiambulia jimbo moja la Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa na kata kadhaa nchini.

Vilevile, mbali na CCM, wapo wabunge kadhaa wa upinzani, wakiwemo wa ACT-Wazalendo, CUF pamoja na wale 19 wa viti maalum ambao Chadema haiwatambui.

Jacob, aliyekuwa katibu wa mameya na wenyeviti wa halmashauri zaidi ya 10 ambazo Chadema ilishinda 2015, alisema kutowepo kwa Chadema bungeni kunasababisha wananchi kukosa utetezi na ulinzi wa rasilimali za Taifa na uwajibishwaji wa Serikali iliyopo madarakani.

“Tunapoingia bungeni au katika mabaraza ya madiwani tunakuwa wasimamizi wa rasilimali za Taifa, sisi ndio au wapinzani ndio wanakuwa wanazuia masuala yasiyokuwa na tija kwa nchi,” alisema.

Jacob alifafanua kuwa aliyegombea ubunge au udiwani kupitia Chadema akikosa nafasi hawezi kuwa mwathirika na kama yupo basi atakuwa mbinafsi.

Ndoto za ubunge

Katika mazungumzo hayo, Jacob alisema bado ana ndoto za kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo, licha ya kuikosa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Profesa Kitila Mkumbo alimshinda kwa kura 63,221 dhidi ya 20,620.

Jacob, ambaye ni mjumbe wa zamani wa kamati kuu ya Chadema anasema bado hajakata tamaa katika shughuli za kisiasa, licha ya hivi sasa kujikita katika ufugaji wa kuku, uuzaji wa mayai na nafaka nje ya nchi.

“Bado nina ndoto za kuwania jimbo la Ubungo, maana nimezaliwa na kukulia hapa, changamoto nazifahamu si za kuandikiwa katika karatasi. Shida zake nazijua kabla ya kuulizwa, kama ni mtaro wa maji machafu nimeuruka tangu nikiwa mdogo.

“Naweza kuwania ubunge katika jimbo lolote, lakini ninaamini nikiwa Ubungo nitakuwa na msaada mkubwa kwa wananchi,” alisema Jacob, aliyeanza kuwania nafasi za kisiasa mwaka 2009 kwa kugombea uenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo Kisiwani bila mafanikio.

Ndani za Chadema

Wakati Chadema ikitarajia kuanza uchaguzi wa ndani mapema mwaka 2023, Jacob alisema yupo tayari kuwania nafasi yoyote atakayopangiwa na wanachama na wafuasi wake.

“Wanachama wenzangu wakiniambia kuna majukumu ya kufanya nitafanya na hivi sasa nina rasilimali kupitia miradi yangu ya ujasiriamali.Natamani nizitumie ndani ya chama, nitakubali majukumu.

“Iwe uenyekiti wa wilaya, mkoa au kanda ili mradi yawe majukumu ya chama nitayafanya. Fomu naweza kuchukua lakini wanachama ndio wenye uamuzi wa mwisho,” alisema.

Hata hivyo, alisema yupo tayari kugombea nafasi yoyote si kwa ajili ya cheo, bali ana deni kubwa la kulipa Chadema, hasa wakati huu karibia miaka mitatu ambayo hajashika wadhifa wowote ndani ya chama.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom