Membe: Vyama vya siasa vimeshindwa kutetea wananchi

Mtanzania

JF-Expert Member
May 4, 2006
4,816
678
Membe: Vyama vya siasa vimeshindwa kutetea wananchi (Kutoka Majira)

Habari Zinazoshabihiana
• Wapinzani wasema kwa sasa hawaungani 09.05.2007 [Soma]
• Membe ziarani Mashariki ya Mbali 12.05.2007 [Soma]
• Miaka 43 ya Mapinduzi Z'bar 12.01.2007 [Soma]

*Asema nafasi yao imechukuliwa na asasi zisizo za Serikali
*Anena baada ya uchaguzi hujiingiza kwenye malumbano

Na Said Mwishehe, Dodoma

VYAMA vya siasa vimeshindwa kutetea maslahi ya wananchi na kusababisha asasi za kijamii (NGOs) kuchukua nafasi hiyo.

Hayo yalisemwa mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa vya Afrika Mashariki unaojadili majukumu ya vyama hivyo kwenye uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Bw. Membe alisema viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshindwa uchaguzi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekuwa wakiacha majukumu yao baada ya uchaguzi na kuamua kuanzisha malumbano yenye lengo la kuvunja amani.

Alisema amani inapotoweka, vyama hivyo vimekuwa vikishindwa kusaidia kuirejesha na hivyo kulazimu mashirika yasiyo ya kiserikali, kuingilia kati kuchukua majukumu ambayo yalipaswa kutekelezwa na vyama vya siasa.

Alibainisha kuwa wakati wananchi wa Afrika Mashariki wamekuwa wakijenga ushirikiano kupitia biashara na shughuli za utamaduni, inasikitisha kuona vyama vya siasa vya Upinzani vimeshindwa kuona fursa wanayoiona wananchi na kubaki kutetea maslahi ya watu wachache ya kutafuta madaraka.

Alifananisha vitendo vya vyama vya upinzani kuweka kipaumbele kwenye kutetea maslahi ya watu binafsi na vitendo vya urasimu wa madaraka usioonekana.

Kutokana na hali ya kutetea maslahi ya watu wachache, wanaopenda madaraka, Bw. Membe alishauri vyama hivyo virudi kwenye majukumu makubwa ya vyama vya siasa ambayo ni kuwakilisha na kutetea maslahi ya wengi.

Ili kuwasilisha maslahi ya wengi, Bw. Membe alivishauri vyama hivyo kubadilisha mitazamo na sera zao, ambazo zitaacha kung'ang'ania maslahi ya watu wachache au ya sekta chache na kuongeza wigo wa maslahi ya watu, uguse watu wa kanda ya Afrika Mashariki ili vionekane kuwa na agenda za watu wengi.

Alionya kwamba kama vyama hivyo vitashindwa kuwakilisha na kutetea maslahi ya wengi, na kugusa watu wa Afrika Mashariki vitajikuta vikikosa umuhimu mbele ya watu, kutelekezwa kwenye michakato ya kisiasa na mwishowe nafasi zao kuchukuliwa na asasi zisizo za kijamii.

Alitahadharisha kuwa baadaye vyama hivyo vitasukumwa nje ya ulingo wa siasa wa kutengeneza hoja na kubakia kuwa wasindikizaji na wapiga kelele wasiokuwa na uwezo wa kutengeneza hoja.

Akielezea uzoefu wa siasa kwa Tanzania akihusisha pande mbili za Muungano, Bw. Membe alisema vyama vilivyoshindwa kuwakilisha maslahi ya wengi kutoka pande mbili za Muungano, vimejikuta nje ya ulingo wa siasa, na kwamba hali ya uwakilishi wa vyama hivyo ndani ya Bunge inaelezea hali hiyo.

Bw. Membe alisema hali hiyo si nzuri, lakini ndio ukweli na ni malipo kwa vyama vinavyoshindwa kuwakilisha maslahi ya wengi.

Kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, Bw. Membe alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kuunga mkono dhana ya Shirikisho la Afrika Mashariki, linalojumuisha sekta zote na kuongeza kwamba mafanikio ya shirikisho hilo yatategemea mawazo, mtazamo, utamaduni wa siasa na sura moja ya watu wa Afrika Mashariki.

Vyama vilivyoshiriki ni CCM, CHADEMA na UDP kutoka Tanzania. Kutoka Kenya ni KANU, FORD Kenya, DP Kenya, LND na UNDA. Kutoka Uganda ni NRM na UPC, kutoka Burundi ni FRODEBU, UPRONA na FDD. Kutoka Rwanda ni RPR na kutoka Ujerumani ni chama cha SPD.
 
Mbona hapa anawasema CCM? Naona anachoongelea kinawahusu CCM zaidi ya upinzani.

Hizi hotuba zinakuwa na maana yoyote? Au mtu anatoa tu kwasababu ametoa.

Huyu naye anataka kuwa rais?

Next time, mtu akitaka kuwa rais, tumwulize kafanya nini kwenye jimbo lake? Haya mambo ya kuleta watu wanasema watajenga Tanzania, wakati wameshindwa hata kujenga majimbo yao ndio yanatuletea Wasanii.
 
LOL!...Madudu yote yanayofanywa na CCM hayaoni! anayaona ya vyama vya upinzani ambavyo CCM imefanya kila njia viendelee kudumaa! ama kweli nyani haoni kundule!
 
Hivi huyu jamaa kafanya nini kule jimboni kwake? Kama sikosei sasa ni kipindi cha pili, je amefanya nini la maana kwa wanajimbo wake?
 
Mbona hapa anawasema CCM? Naona anachoongelea kinawahusu CCM zaidi ya upinzani.

Hizi hotuba zinakuwa na maana yoyote? Au mtu anatoa tu kwasababu ametoa.

Huyu naye anataka kuwa rais?

Next time, mtu akitaka kuwa rais, tumwulize kafanya nini kwenye jimbo lake? Haya mambo ya kuleta watu wanasema watajenga Tanzania, wakati wameshindwa hata kujenga majimbo yao ndio yanatuletea Wasanii.

Kwa msingi huu napendekeza Mohammed Dewji awe Rais maana amejenga zahanati, mashule, barabara, nk ktk jimbo lake..
 
Membe: Vyama vya siasa vimeshindwa kutetea wananchi.....


Alitahadharisha kuwa baadaye vyama hivyo vitasukumwa nje ya ulingo wa siasa wa kutengeneza hoja na kubakia kuwa wasindikizaji na wapiga kelele wasiokuwa na uwezo wa kutengeneza hoja.
Maneno mazito haya...
 
Back
Top Bottom