Tanzania Daima said:WANANCHI mkoani hapa wamechanga sh 38,728,000, kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, ikiwa moja ya hatua ya kusogeza huduma hiyo muhimu inayolenga kuinua kiwango cha elimu.
Michango hiyo ni pesa taslimu na ahadi zilizotolewa katika harambee iliyofanyika kwenye ukumbi wa Oceanic Hotel, hapa, mwishoni mwa wiki. Harambee hiyo iliongozwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Gaudensia Kabaka.
Katika harambee hiyo, wananchi wa mkoa huo walichanga papo hapo kiasi cha sh 14,293,000 wakati sh 24,435,000 ni ahadi zilizotolewa na watu mbalimbali, mashirika na taasisi za umma na Serikali na wadau wengine wa maendeleo wa mkoa huo.
Katika uchangiaji huo, Kabaka na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, na marafi zake - Mbunge wa Lindi Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Abdulaziz - kila moja alichangia sh 1,000,000.
Wengine ni kampuni ya Bioshape Limited yenye makao yake wilayani Kilwa, inayojishughulisha na ulimaji wa mibono kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya dizeli, kupitia taasisi yake ya Bioshape Benefits Foundation, Ruvuma Construction pamoja na Jamal Malinzi, kila moja wakichangia sh 1,000,000.
Ofisi za wakuu wa wilaya zote tano za Lindi, Nachingwea, Ruangwa, Kilwa na Liwale kila moja zilichangia kiasi sh 300,000, wakati ofisi tatu za wakurugenzi watendaji - Lindi Vijijini, Liwale na Ruangwa, zikitoa kiasi kama hicho kila moja, wakati Nachingwea na Kilwa zikitoa sh 200,000 na Lindi Mjini sh 100,000.
Vyama viwili vya siasa vya CCM na CUF vilijitokeza katika harambee hiyo. CCM ilichangia sh 300,000 na CUF sh 100,000.
Wachangiaji wengine - wabunge wawili wa Viti Maalumu Mkoa wa Lindi kwa tiketi ya CCM - Fatuma Mikidadi, Rulida Said - Oceanic Hotel, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kila mmoja akichangia sh 500,000. Kiasi kilichobaki kimechangiwa na taasisi za umma na watu binafsi.
Akizungumza mara baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo, Said Meck Sadiki, kutangaza mapato hayo, Kabaka aliwataka wananchi wa mkoa huo waendelee kuchangia ujenzi wa chuo hicho.
wandugu,
..wahenga walisema "safari ni hatua." naona wana-Lindi wameanza safari ya Ujenzi wa Chuo Kikuu.
..napendekeza wasikibatize chuo kikuu chao majina ya wanasiasa, badala yake wakipe jina rahisi, zuri, Lindi University.
..natoa hongera kwa wananchi na viongozi wa mkoa wa Lindi kwa kuleta wazo hili la maendeleo.
NB:
..ile University ya kule Bukoba inaendelea vipi? pia nakumbuka Nimrod Mkono naye ana project yake ya kujenga University karibu na Butiama.