Membe 'awauzia' mabalozi uamuzi wa Butiama

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,082
Posted Date::4/5/2008
Membe 'awauzia' mabalozi uamuzi wa Butiama
Na Muhibu Said
Mwananchi

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jana alikutana na mabalozi wa nje wanaoziwakilisha nchi zao nchini, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili kuhusu hatima ya Mwafaka wa kisiasa kati ya vyama vya CCM na CUF visiwani Zanzibar.

Hatua hiyo imefikiwa na Waziri Membe ikiwa ni siku mbili baada ya maafisa waandamizi wa CUF, kuziandikia barua na tamko la chama balozi zote nchini Jumatano wiki hii, kueleza kilio chao namna CCM ilivyorudisha nyuma jitihada za kupatikana kwa mwafaka huo.

Kikao hicho cha Waziri Membe na mabalozi, kimefanyika siku moja baada ya maofisa wanaoshughulikia masuala ya siasa wa Jumuiya ya Ulaya (EU), kukutana juzi mchana, jijini Dar es Salaam kujadili suala hilo.

Habari kutoka wizarani hapo, zilizothibitishwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa wizara hiyo, zinaeleza kuwa katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana asubuhi, Waziri Membe na mabalozi hao, pia walijadili kuhusu hali ya kisiasa na kidiplomasia ilivyo hivi sasa nchini Zimbabwe.

Ingawa hakuna kiongozi yeyote wa wizara hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo na juhudi mbalimbali zilizofanywa na gazeti hili kuwapata wasemaji wa wizara ziligonga ukuta.

Chanzo chetu cha habari kiliarifu kuwa, katika kikao hicho kilichodumu kwa saa kadhaa, Waziri Membe alitumia kila aina ya ufundi wa kisiasa na kidiplomasia kuwashawishi mabalozi hao kukubaliana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC-CCM), uliofikiwa katika kikao chake kilichofanyika katika kijiji cha Butiama, mkoani Mara, Machi 29-30, mwaka huu, lakini uligonga mwamba.

Katika uamuzi wake huo, pamoja na mambo mengine, NEC ilitaka ifanyike kura ya maoni Zanzibar ili kupata ridhaa ya wananchi ya ama kuundwa au kutoundwa kwa serikali shirikishi, maarufu kama "serikali ya mseto" visiwani humo.

Uamuzi mwingine uliofikiwa na NEC katika kikao chake hicho cha Butiama ambao ulitetewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwa nguvu zote Jumatano wiki hii, unahusu kutaka marekebisho yafanyike katika baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Mazungumzo za Vyama hivyo ya kutafuta mwafaka huo.

"Membe aliwaeleza mabalozi kuwa barua ambayo (Yusufu) Makamba (Katibu Mkuu wa CCM) aliyomwandikia Maalim Seif (Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF) juzi kutaka warejee kwenye mazungumzo ya mwafaka, ilieleza kwa kina na kwa ufasaha juu ya uamuzi uliofikiwa na NEC Butiama, lakini mabalozi hawakuridhishwa kabisa na ushawishi wake," kilisema chanzo chetu cha habari kutoka wizarani hapo.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, katika kupinga ushawishi wa Waziri Membe kwao, baadhi ya mabalozi walihoji sababu za CCM kutojadili na wenzao wa CUF katika mazungumzo yao ya mwafaka hoja ya kutaka ifanyike kura ya maoni Zanzibar ili kupata ridhaa ya wananchi ya ama kuundwa au kutoundwa kwa serikali ya mseto visiwani humo, badala yake wakaamua kwenda kuiibua katika kikao chao cha Butiama.

Juhudi za kuwapata viongozi wa Wizara hiyo, kuelezea kikao hicho kati ya Membe na mabalozi hao, ziligonga ukuta baada ya baadhi ya maofisa, kuweka vizingiti vya kuwaona wasemaji katika kile kinachoonekana kuwa ni maelekezo maalum kutoka kwa mabosi wao.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika katika Kitengo cha Habari cha wizara hiyo kupata taarifa kuhusu suala hilo, alipokewa na mmoja wa maafisa ambaye licha ya kuthibitisha waziri huyo, kukutana na mabalozi jana asubuhi, alibadili lugha baada ya kutoka ofisini kwake.

Ofisa huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alirejea na msimamo huo baada ya kumtaka mwandishi amsubiri nje ili aitikie wito wa waziri ofisini kwake ambapo kabla ya kuingia ofisini kwa waziri huyo alichukua majina na chombo alichotoka mwandishi huyo.

" Nilipokuaga kwamba nimeitwa na waziri, nilikwenda, lakini nikakuta aliyeniita ni mtu mwingine, siyo waziri, hivyo, nakushauri uende ukamwone Katibu Mkuu ndiye msemaji, kwani waziri ana kazi nyingi," alisema Ofisa huyo.

Baada ya maelekezo hayo, mwandishi alikwenda mapokezi kwa nia ya kuonana na Katibu Mkuu, Balozi Patrick Mombo, lakini juhudi hizo ziligonga ukuta baada ya Katibu Muhtasi wake kumtaka mwandishi asubiri ili awasiliane naye, lakini dakika chache baada ya kusubiri, ghafla akapiga simu mapokezi na kusema kuwa bosi wake huyo hayupo.
 
Back
Top Bottom