Mei Mosi Mwanza: Rais Samia ahutubia, aahidi kuongeza mishahara kuanzia mwakani, agusia mafao ya wastaafu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,796
11,959
1619869985966.png

Kutoka jijini Mwanza tunawaletea taarifa za moja kwa moja, maadhimisho ya sherehe ya siku ya wafanyakazi duniani,ambayo kitaifa yanafanyika hapa.

Mgeni rasmi anatarajiwa kua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mama Samia Suluhu Hassan, ambapo atapokea maandamano ya wafanyakazi mbalimbali Tanzania.

Hali ya hewa ni tulivu kabisa,uwanja umepambwa vyema,barabara za jiji zimesafishwa safi huku zikichagizwa na mabango yenye ujumbe wa hapa na pale.

Wananchi wameanza kumiminika viwanjani hapa.

Karibuni.....
============
Updates.
Tayari uwanja wa CCM Kiruma umeanza kufurika huku ukipendezeshwa na sare mbalimbali za tishirts na kofia za vyama vya wafanyakazi wa sekta binafsi, serikali kuu, mashirika ya umma, serikal za mitaa na Chama cha Walimu, nyuso za wafanyakazi zinaonyesha tabasamu lililojaa matumaini tofauti na mei mosi za miaka 5 iliyopita.

Viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya wafanyakazi wameanza kuwasili uwanjani.
Namuona Makamu wa Rais,Dr.Mpango,Waziri Mkuu Majaliwa,Katibu Mkuu Kiongozi,Spika wa bunge na makamu wake.
Screenshot_2021-05-01-09-31-37-1.png

Updates
Tayari msafara wa Rais Mama Samia umewasili uwanja wa CCM Kirumba tayari kwa shughuli za Mei Mosi kuanza rasmi,shangwe na nderemo zinashamiri uwanjani hapa wananchi wakimshangilia Rais wetu.

======
Maandamano yanaanza baada ya Rais Samia kuwasili jukwaani,takribani vyama 17 vya wafanyakazi vitashiriki maandamano haya.

Screenshot_20210501-113924.png

Updates
Fuatilia matangazo live kupitia link ya Ikulu Mawasiliano



HOTUBA RAIS SAMIA
Rais Samia:
Hakuna Nchi iliyosonga mbele kimaendeleo bila kuwategemea Wafanyakazi. Ndiyo wanajenga miundombinu na kutoa huduma mbalimbali za kijami. Natambua mishahara haijapandishwa kwa muda mrefu. Miaka nane kwa Sekta Binafsi na miaka sita kwa Sekta ya Umma.

Rais Samia: Kuna usemi unasema ‘mafanikio ya Nchi yoyote hutokana na nguvu ya Wafanyakazi wake’, hakuna Nchi iliyoendelea bila Wafanyakazi. Mwaka jana Taifa letu limeingia Uchumi wa Kati, tumefikia hapo sababu ya Wafanyakazi, nawapongeza sana Wafanyakazi wote.

Rais Samia: Leo hii tunapoadhimisha Siku ya Wafanyakazi naomba niwapongeze na kutambua kazi nzuri ambazo mnaendelea kuzifanya. Natamani kuona Mtu aliyestaafu analipwa mara moja na sio kuzungushwa muda mrefu. Nimeelekeza Mifuko kuwalipa haraka Wastaafu.

KUPUNGUZA KODI P.A.Y.E
Rais Samia:
Serikali imesikia ombi la kupunguza kodi ya mishahara na tumepunguza asilimia moja - Tumeamua kupungzua 1% ya P.A.Y.E. Mimi pamoja na nyinyi Wafanyakazi wenzangu tutakatwa 8% badala ya ile 9% ya awali.

Hii imetokana na ombi la Katibu Mkuu wa TUCTA kuomba kupunguziwa kodi hiyo kwenye mishahara.

BIMA YA AFYA, MADENI YA WAFANYAKAZI NA MAKATO YA BODI YA MIKOPO
Rais Samia:
Kuhusu Bima ya Afya, Mtoto wa miaka 18 bado ni mtegemezi kwa Wazazi wake - Tumeamua kuongeza umri wa Mtegemezi kutoka miaka 18 hadi 21 ambapo tunakusudia maamuzi haya kuyaweka kwenye marekebisho ya Sheria ya Bima ya Afya

Rais Samia: Kuhusu suala la Watumishi wa darasa la saba waliositishiwa ajira najua wapo ambao hawajalipwa kwa kisingizio kuwa Serikali haijatoa mwongozo. Naagiza Waajiri wote waliokuwa na Wafanyakazi wa aina hii wafanye kila linalowezekana wawalipe haki zao.

“Kuhusu madeni ya Watumishi Serikali inajitahidi kulipa, kipindi cha July mwaka jana hadi April mwaka huu Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya Tsh Bil. 74 kwa Watumishi 36,126 na tutaendelea kulipa madeni yote ya Watumishi”

Rais Samia: Kuhusu Makato ya bodi ya mikopo, kwenye changamoto hii tumeamua kubakia kwenye asilimia 15 ya sasa na Serikali imefuta asilimia sita iliyokuwa ikikatwa - Lakini nasisitiza, waliokopa wahakikishe wanalipa.

KUHUSU MISHAHARA
Rais Samia:
Mimi ni Mama, Mama ni mlezi. Kuna msemo wa Kiswahili unasema Masikini hapendi mwana - Hata kama unataka mwanao apendeze, lakini huna uwezo wa kumfanya apendeze. Ni kweli mishahara haijaongezwa miaka mingi, lakini kutokana na sababu mbalimbali, nimeshindwa kuongeza.

Mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, Mimi binafsi natamani kuongeza mishahara mwaka huu ila kwasababu mbalimbali nimeshindwa. Uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka 6.9% hadi 4.7% kwasababu ya Corona, mwakani siku kama ya leo nitapandisha mishahara.

=====

FULL TEXT HOTUBA YA RAIS SAMIA SULUHU M

======

HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI MKOANI MWANZA, TAREHE 1 MEI, 2021

Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Ndugu Tumaini Nyamhokya, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;


Waheshimiwa Mawaziri wengine mliopo;


Mheshimiwa Balozi Hussein Athman Kattanga,
Katibu Mkuu Kiongozi;


Mheshimiwa John Mongela, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Wakuu wa Mikoa wengine mliopo;

Mheshimiwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi na Waheshimiwa Majaji mliopo;

Ndugu Makatibu Wakuu mliopo;


Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO),
Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

Ndugu Said Wamba, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi;

Ndugu Pendo Berege, Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri;


Ndugu Jayne Nyimbo, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);

Viongozi wengine wa Vyama vya Wafanyakazi; Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo; Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo; Waheshimiwa Viongozi wa Dini;

Ndugu Wafanyakazi, Ndugu Wananchi; Mabibi na Mabwana;


Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…!!!

Mshikamano…………….Solidarity………!!!


Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyetujalia uhai, afya njema na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nawashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) kwa kunikaribisha katika Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi Duniani. Nimepata fursa ya kushiriki sherehe hizi mara kadhaa ila leo ni mara yangu ya kwanza kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho haya. Hivyo basi, nawashukuru sana TUCTA kwa imani kubwa mliyoionesha kwangu na kwa Serikali.

Nitumie fursa hii pia, kwa niaba ya Serikali, kuwashukuru sana kwa salamu zenu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wetu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Msiba huu ulikuwa wetu sote; hivyo basi, nami nawapa pole na kuwashukuru kwa namna wafanyakazi nchini walivyoshiriki kikamilifu katika kuaga na hatimaye mazishi ya aliyekuwa Kiongozi wetu. Nawaomba wote tusimame kwa dakika moja kumkumbuka. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi. Amina.

Kwa namna ya pekee, nawashukuru sana kwa salamu zenu za pongezi kwangu kufuatia kukabidhiwa dhamana hii kubwa ya kuliongoza Taifa letu. Nimefarijika kwa ahadi yenu ya kuniunga mkono na kuiunga mkono Serikali kwa moyo wa dhati katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati. Niwahakikishie kuwa, miradi yote ya kimkakati tutaitekeleza na kuibua mingine mipya. Kwa bahati nzuri, miradi yote ya kimkakati tayari tumeijumuisha kwenye Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) ambao tutaanza kuutekeleza mwezi Julai 2021. Hivyo basi, nina uhakika, miradi hiyo itatekelezwa kama ilivyopangwa, tena kwa ufanisi huku tukizingatia matumizi mazuri ya rasilimali fedha. Niwaombe nanyi mfanye kwa upande wenu kwa kuwa ninyi ndiyo hasa watekelezaji wa miradi hiyo.

Ndugu Wafanyakazi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Upo usemi wa Kiingereza usemao “Every nation owes its success to its labourers”. Usemi huu una maana kwamba, mafanikio ya Taifa lolote hutokana na juhudi za wafanyakazi wake. Hakuna nchi iliyoweza kupiga hatua za kimaendeleo bila kutegemea wafanyakazi wake. Wafanyakazi ndiyo wazalishaji viwandani na mashambani. Wafanyakazi ndiyo wanajenga miundombinu; wafanyakazi ndiyo wanatoa huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo afya, elimu na huduma ya maji safi na salama.

Mwaka jana, Taifa letu limeingia kwenye Kundi la Nchi za Uchumi wa Kati. Tumeweza kufikia hatua hiyo kutokana na mchango mkubwa sana uliotolewa nanyi wafanyakazi. Ni kwa msingi huo, leo, tunapoiadhimisha Siku hii ya Wafanyakazi, napenda niwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya ya kuliletea maendeleo Taifa letu. Kwa hakika, nawapongeza sana wafanyakazi wa Tanzania.

Ndugu Viongozi wa TUCTA; Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

Pamoja na mchango mkubwa mnaoutoa kwa Taifa letu, natambua kwamba bado mnakabiliwa na changamoto nyingi. Na changamoto ya kwanza mmeieleza vizuri kwenye kaulimbiu yenu mwaka huu, ambayo inasema “Maslahi Bora, Mishahara Juu, Kazi Iendelee”. Kaulimbiu hii inatoa ujumbe kwa Serikali kuhusu umuhimu wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kupandisha mishahara yao, ambayo natambua kuwa haijapandishwa kwa muda mrefu (takriban miaka 6 kwa sekta ya umma na miaka 8 sekta binafsi). Mbali na changamoto hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Ndugu Said Wamba, ametaja changamoto nyingine ambazo ni:

Kutokufanya Kazi kwa Bodi za Mishahara - Kwenye changamoto hii, nilishaelekeza Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) akae na vyama vya Wafanyakazi waone jinsi ya kuzifufua Bodi hizo ili ziweze kufanya kazi inayopaswa.

Kodi kubwa katika Mishahara na Marupurupu Mengine.
Nataka niwaambie kwamba Serikali imesikia

ombi la Wafanyakazi la kutaka kupunguziwa kodi inayotozwa kwenye mshahara au PAYE, na pia kutokatwa kodi kwenye malipo ya stahiki nyengine zisizokuwa mshahara. Serikali imeliona jambo hili, na tumeamua kupunguza asilimia moja (1%) ya makato ya PAYE kutoka asilimia 9 ya sasa kufikia asilimia 8. Aidha, tutaendelea kulitazama suala la makato katika malipo yasiyo ya mshahara.

Urasimu katika Kujadili, Kufunga na Kuidhinisha Mikataba ya Hali Bora Kazini - Lengo la Mikataba ya namna hii ni kuwapa motisha watumishi kwa kuongeza mishahara, kutoa marupurupu, kuboresha mazingira ya kazi, kutoa mafunzo, makazi, huduma za afya, na mengine mengi. Hata hivyo, kwenye Mashirika na Taasisi nyingi, Mikataba ya Hali Bora Kazini imekuwa ikijikita zaidi kwenye masuala ya posho na marupurupu bila kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya nchi yetu, na wakati mwingine, kuwasilisha Mikataba isiyozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Hali hii ndiyo inafanya Serikali kuwa makini kabla ya kupitisha Mikataba ya Hali Bora Kazini. Hata hivyo, nimeiagiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuongeza kasi katika kuidhinisha Mikataba hiyo. Kwa hiyo kazi inaendelea ya kuidhinisha Mikataba.

Ucheleweshaji wa Mafao kwa Wastaafu - Nakiri kuwa tatizo hili ni kweli lipo na linanisikitisha sana. Binafsi, natamani kuona, mtu akistaafu analipwa mara moja badala ya kuzungushwa zungushwa. Nimeielekeza Mifuko kuhakikisha wanalipa mafao ya Wastaafu ambao wameendelea kusubiri kwa miezi kadhaa. Na katika hilo, nataka nitoe taarifa ya faraja, kwamba, kwa wastaafu waliosubiri mafao yao kwa mrefu, tutaanza kuwalipa kuanzia mwezi huu wa Mei. Na naahidi tutakuwa tukilipa kila mwezi mpaka tumalize mlundikano uliopo.

Madeni mbalimbali ya Watumishi - Kuhusu suala la Madeni au Madai ya Watumishi, kama mnavyofahamu, Serikali imekuwa ikijitahidi sana kulipa madeni ya watumishi. Kwa mfano, katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Aprili 2021, Serikali imelipa malipo ya malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 74.12 kwa watumishi 36,126. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 32.669 zimelipwa kwa walimu 11,272. Aidha, atika kipindi hicho, Serikali imelipa madeni yasiyo ya kimshahara yenye thamani ya shilingi bilioni 18.22; na uhakiki wa madeni ya kimshahara ya watumishi 8,334 unaendelea. Nataka niwahakikishie ndugu zangu Wafanyakazi kuwa, Serikali itaendelea kulipa madeni yote inayodaiwa na watumishi.

Lakini nitumie fursa hii, kuwaonya Viongozi wa Taasisi mbalimbali kuacha tabia ya kuzalisha madeni mapya bila sababu za msingi, ikiwemo kuwahamisha watumishi bila kuwa na bajeti za kuwalipa. Aidha, nawasihi watumishi kuacha kutengeneza madeni hewa. Wakati mwingine Serikali inachelewa kulipa madeni kutokana na uwepo wa madeni hewa. Mathalan, ipo taasisi moja ilileta madeni ya watumishi yenye thamani ya shilingi bilioni 40; lakini baada ya kuhakikiwa madeni yaliyostahili kulipwa yalikuwa yana thamani ya shilingi bilioni 1 tu.

Bima ya Afya - Serikali imeona mantiki ya pendekezo lililowasilishwa na TUCTA kwamba mtoto mwenye umri wa miaka 18 bado ni tegemezi. Hivyo basi, tumeamua kuongeza umri wa Mtoto Tegemezi kutoka miaka 18 hadi miaka 21; na maamuzi hayo tutayajumuisha kwenye Marekebisho ya Sheria ya Bima. Vilevile, kwa kuzingatia Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko ambayo tunatarajia kuifanya mwezi Juni 2021, Serikali itaangalia uwezekano wa kugharamia Kundi la Wastaafu bila kuzingatia kigezo cha uchangiaji wa miaka 10. Ila kwa sasa, tutaendelea kutoa fursa kwa wastaafu kuendelea kujazia miaka iliyopungua ili kukidhi kigezo hicho. Katika hatua za muda mrefu, kama mnavyofahamu, tayari Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote.

Makato ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu - Kuhusu changamoto hii, Serikali imeamua kuifuta tozo ya asilimia 6 iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo (yaani Value Retention Fee) na kubakisha kodi ya asilimia 15 iliyokuwepo zamani. Aidha, naiagiza Bodi ya Mikopo kuhakikisha inazihakiki taarifa za madeni ya wanufaika ili kuondoa sintofahamu inayojitokeza mara kwa mara kati yao na wanufaika. Lakini, nataka nitumie fursa hii kuipongeza Bodi ya Mikopo kwa kazi kubwa wanayofanya. Pamoja na changamoto zilizopo, katika miaka ya hivi karibuni, kasi ya ukusanyaji madeni imeongezeka kutoka shilingi bilioni 28.21 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 192 mwaka 2019/2020. Hii imewezesha kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 373 mwaka 2014/2015 ambayo iliwanufaisha wanafunzi 98,300 hadi kufikia shilingi bilioni 464 mwaka 2020/2021 na kuwanufaisha wanafunzi 149,389. Hivyo basi, sina budi kuipongeza Bodi ya Mikopo na kuendelea kuwasihi wanufaika kulipa madeni yao kwa hiari ili watu wengi zaidi waweze kunufaika.

Suala la Watumishi wa Darasa la Saba Waliositishiwa Ajira - Kuhusiana na suala la Watumishi hawa, kama mnavyokumbuka, Serikali ilitoa msamaha na kuwarejesha kazini watumishi walioajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei, 2004 ambao hawakufanya udanganyifu wa vyeti pamoja na watumishi waliojiendeleza na kujipatia sifa stahiki kwa mujibu wa miundo ya Utumishi wa Umma. Kupitia Msamaha huo, ninafahamu kuwa watumishi 4,380 wamerejeshwa kazini. Hata hivyo, napenda kutumia fursa hii kurudia maelekezo ya Serikali kwa Waajiri kuhusu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kuhitimisha Ajira za Watumishi walioajiriwa kwa Elimu ya Darasa la Saba na wale walioghushi vyeti. Najua wapo Waajiriwa wa Darasa la saba waliostaafishwa na kulipwa mafao yao kisheria; na vile vile, wapo ambao hawajalipwa kutokana na madai ya kutokuwepo kwa muongozo
makhsusi kutoka Serikalini; na wapo ambao hawajalipwa kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu za ajira zao. Sasa hapa nataka niwaagize Waajiri wote waliokuwa na wafanyakazi wa aina hii, wafanye inavyowezeka, ili kila mwenye haki aweze kupatiwa haki yake. Natambua kwamba wafanyakazi hawa walikuwa wakikatwa michango kwenda Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hivyo, naitaka Ofisi yangu ya Utumishi na Utawala Bora kusimamia zoezi hili.

Ndugu Wafanyakazi;

Changamoto nyingine zilizoelezwa ni kuhusu Mabaraza ya Wafanyakazi Sehemu za Kazi; Uhuru wa Vyama vya Wafanyakazi; Ajira za Raia wa Kigeni; pamoja na Unyanyasaji na Udhalilishaji Wafanyakazi Kazini. Kimsingi, changamoto hizi ni za kiutendaji. Sheria zipo; kinachohitajika ni usimamizi na utekelezaji wa Sheria zilizopo. Hivyo basi, naziagiza mamlaka husika, hususan Wizara inayosimamia masuala ya Ajira na Kazi kuhakikisha wanasimamia masuala hayo kwa mujibu wa sheria, lakini pia kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Nafahamu kuwa Taasisi za Umma 40 hazijaunda Mabaraza ya Wafanyakazi. Naziagiza Taasisi hizo kuunda Mabaraza hayo mara moja. Kwa upande wa Sekta Binafsi, natambua kuwa Sheria haiwalazimishi. Lakini, nawahimiza kuyaanzisha kwa vile faida zake ni kubwa. Panapokuwa na Mabaraza ya Wafanyakazi tija inaongezeka, maslahi ya wafanyakazi yanalindwa na migogoro kupungua.

Aidha, nawakumbusha Waajiri kwamba suala la kuanzisha Vyama vya Wafanyakazi na Uhuru wa Vyama hivyo sio la hisani bali lipo Kisheria. Hivyo, natoa wito kwa Waajiri kuruhusu wafanyakazi kuanzisha Vyama vyao kwa Uhuru. Vilevile, ningependa kutoa rai kwa viongozi wa vyama hivyo kuhakikisha haviwi chanzo cha migogoro sehemu za kazi. Nawasihi pia Viongozi wa Vyama Vya Wafanyakazi kuhakikisha wanawasilisha Serikalini taarifa za unyanyasaji na udhalilishaji unaotokea kwenye maeneo yao ya kazi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Kuhusu suala la Vibali vya Ajira za Wageni; hili nilishalitolea maelezo wakati nikiwaapisha Makatibu Wakuu. Lakini, ninachotaka kusisitiza ni kwamba, Vibali kwa Raia wa Kigeni kisiwe kikwazo kwenye shughuli za uwekezaji. Vibali vitolewe kwa kuzingatia sheria, lakini pia kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Kama nilivyosema, nchi yetu inawahitaji wawekezaji wa ndani na wa nje ili kuchochea ukuaji uchumi. Lakini, sambamba na suala hilo la Vibali kwa Wageni, naiagiza Wizara inayosimamia Kazi na Ajira kuliangalia vizuri suala la Mawakala wa Ajira, ambao wamejiegeuza kuwa Waajiri na kusababisha migogoro kwenye maeneo mengi ya kazi.

Ndugu Wafanyakazi;

Mimi ni mfanyakazi mwenzenu. Changamoto hizi zote mlizotaja ni za kweli na ni za msingi. Hivyo basi, nataka niwaahidi kuwa, katika kipindi changu cha Uongozi, nitashirikiana nanyi kwa karibu katika kuhakikisha tunazishughulikia kwa lengo la kuzipunguza kama sio kuzimaliza kabisa.

Ndugu Viongozi wa Wafanyakazi; Ndugu Wafanyakazi;

Mabibi na Mabwana;

Naomba sasa nizungumzie suala lililokuwa linasubiriwa kwa hamu kuhusu Mishahara. Ndugu zangu, mimi ni mama, na mama wakati wote ni mlezi. Hata hivyo, upo usemi wa Kiswahili unaosema “Masikini hapendi mwana”. Usemi huu una maana kwamba, ukiwa masikini, hata kama utatamani kumpendezesha mwanao, utashindwa; na hivyo, kuonekana humpendi. Hivyo basi, kama nilivyosema awali, dai la kuongezewa mshahara ni la msingi na ni kweli mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu. Binafsi natamani sana kuona kuwa, mwaka huu, mishahara ya watumishi inaongezwa. Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, nimeshindwa kutimiza matamanio yangu.

Kama mnavyofahamu, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, kasi ya ukuaji uchumi duniani imeshuka sana. Kwetu sisi Tanzania, kasi ya ukuaji wa uchumi imepungua kutoka wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka hadi asilimia 4.7 mwaka jana (2020). Hii ina maana kuwa uchumi umeshuka. Zaidi ya hapo, kama nilivyoahidi, tumepanga kuchukua hatua za kurekebisha mfumo wa viwango vya kodi. Hatua hii tunatarajia itapunguza mapato ya Serikali katika kipindi cha mpito. Hivyo, kwa kuzingatia hayo yote, imekuwa vigumu kwetu kuongeza mishahara kwenye mwaka huu; na hasa kutokana na ukweli kuwa nimeingia madarakani hivi karibuni.

Lakini, pamoja na ukweli huo; kwa kutambua umuhimu wa wafanyakazi, tunakusudia kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwenye Mwaka ujao wa Fedha. Kwanza, tumepanga kuwapandisha vyeo kati ya watumishi 85,000 hadi 91,000 ambao wataigharimu Serikali takriban shilingi bilioni 449. Tunakusudia pia kulipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 60; kufanya mabadiliko ya kimuundo wa utumishi yatakayotugharimu takriban shilingi bilioni 120 na pia kuajiri watumishi wapya takriban 40,000 ili kupunguzia mzigo kwa watumishi waliopo, hususan kwenye aelimu na afya. Ajira hizi mpya zinatarajia kuigharimu Serikali shilingi bilioni 239.

Sambamba na hayo, kama nilivyosema awali, mwaka huu, tutapunguza viwango vya kodi za mishahara kwa watumishi kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8. Aidha, tutaendeleza jitihada za kudhibiti Mfumko wa Bei ili kupunguza kasi ya kupanda kwa bei ya bidhaa. Ni matumaini yangu kuwa, jitihada hizi zitasaidia kupunguza ukali wa maisha kwa watumishi. Niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa, penye Majaliwa, mwakani siku kama ya leo, nitakuja na zawadi nzuri ya kuwapandisha mishahara watumishi, ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa sekta ya Umma na Sekta binafsi. Na katika hilo, narudia agizo langu kuhusu kuundwa haraka kwa Bodi za Mishahara ili waianze kazi hii mara moja na hatimaye nikija mwakani nijue niwapandisha kwa kiwango gani.

Ndugu Wafanyakazi;

Nimeeleza mengi; lakini kabla sijahitimisha naomba mnivumilie nieleze masuala mawili ya mwisho. Jambo la kwanza, ni lile lililozungumzwa na Rais wa TUCTA kuhusu Bodi ya Kitaalam ya Walimu. Nilifanya kikao na Viongozi wa TUCTA niliwaeleza kuwa, Mtoto akililia wembe, mpatie. Bodi hii ilitokana na ombi la walimu wenyewe; lakini sasa baada ya kuianzisha, Walimu wameikataa. Serikali imesikia malalamiko ya walimu kuhusu utendaji wa Bodi ya Walimu. Tumeanza kuchukua hatua, ambapo tarehe 28 Aprili, 2021 tulikutana na Kamati ya Bunge ya Sheria kwa lengo la kujadili suala hilo. Nina imani, majadiliano hayo yatatuwezesha kupata ufumbuzi kulingana na matakwa ya walimu. Pamoja na kwamba Bodi hii imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria, lakini hatuwezi kuwa watumwa wa Sheria tulizozitunga wenyewe.

Jambo la pili ambalo ningependa kulizungumza ni kwamba hii ni mara yangu ya kwanza kuja Mwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; na tangu nimekabidhiwa dhamana ya kuliongoza Taifa letu mwezi Machi mwaka huu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wana-Mwanza kwa ushindi mkubwa mliokipatia Chama changu (CCM). Nataka niwahakikishie kuwa tutayatekeleza yote tuliyoyaahidi kwa wananchi wa Mwanza. Tutakamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Mkoa huu, ikiwemo Daraja la Kigongo - Busisi; ujenzi na ukarabati wa meli kwenye Ziwa Victoria; Jengo la Abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza; na pia kuanza ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka. Tutaendelea pia kuboresha huduma za elimu, maji na afya, ikiwemo kukamilisha upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure. Ni imani yangu kuwa, hatua hizi zitalifanya Jiji la Mwanza kuwa Kitovu cha Biashara kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, kama tulivyoahidi wakati wa Kampeni. Wito wangu kwa wana-Mwanza, endeleeni kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano; kuchapa kazi kwa bidii; na bila kusahau kulipa kodi, tukifahamu fika kwamba kodi ndiyo maendeleo yetu.

Ndugu Viongozi wa Wafanyakazi; Ndugu Wafanyakazi;

Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia tena kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kwa kunialika kwenye Maadhimisho haya ya Siku ya Wafanyakazi. Nimefurahi kuungana nanyi; na nataka niwapongeze kwa Maandalizi mazuri ya Sherehe hizi. Kwa hakika, Sherehe zimefana sana. Nawapongeza wana-Kwaya pamoja na vikundi vyote vya burudani vilivyotuburudisha. Wito wangu kwa Wafanyakazi tuendelee kushirikiana, kushikamana na kusisitiza uwajibikaji na uadilifu mahali pa kazi. Narudia tena uadilifu mahali pa kazi. Waajiri wamekuwa wakilalamikia suala la uadilifu na uaminifu. Najua maslahi ni madogo lakini tukiwa waadilifu na kufanyakazi kwa kujituma tija itaongezeka na kupata uwezo wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wote. Hivyo basi, hatuna budi kuiondoa kasoro hiyo ya uadilifu. Tukumbuke kila wakati kuwa, sisi sote tunajenga nyumba moja.

Baada ya kusema hayo:

Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania

Mungu Ibariki Tanzania!

Nawasalimu tena kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”
 
Mara paa aongeze Misharaha na kupandisha watu madaraja..

Hapo mama tayari kashaingizwa kwa kumbukumbu za Maisha kwenye vichwa vya watu na vizazi vijao kwa kutoa historia kuwa tulisimama miaka 6 hakuna kitu kama hicho basi Mungu akamleta mteule na kumpa kijiti nae akawaonea huruma wafanyakazi wake.

Ila pia ninaona harufu ya katiba mpya kama mama anaendelea hadi 2030 na hii ndo itakuwa legency haswa achana na hizo za ku lazimishiwa tunazopigiwa mapambio na watu sa hivi
 
Mama hatataja kuongeza mshahara Ila atatoa kauli ya kuwa wahusika wangalie namna ya kuongeza maslahi kwa watumishi kwa kuzingatia muda ambao hawajafanyiwa hivyo. Ataomba busara kwa watumishi wampe muda kupitia idara husika wakamilishe mchakato japo ni ndani ya mwaka huu huu
 
Acha Asante kwa taarifa Mkuu,tuna imani na mama mh SSH....Tunategemea habari njema za umate umate kupanda.
Acha uoga wa maisha wewe, asipowaongeza utafanya nini utaacha kazi?, maana unajilizaliza mbaka unatia huruma,hapo unakazi lakini muogawamaisha ungekuwa huna kazi sindio unge pata kisukari wewe.

Tumia akilizako kujiingezea kipato ukitegemea serikali kiasihicho kunasiku utakuja kulia mbele za watoto wako kama zwazwa, Magu angekuwepo mngetia akilinyie.

R.I.P Jembe.
 
Hotuba ya leo.. itasikilizwa na wananchi wengi.. kwa sababu wengi wanataka kusikia habari za....

Mimi alipo nipo kumsikiliza Rais wetu
 
Acha uoga wa maisha wewe, asipowaongeza utafanya nini utaacha kazi?, maana unajilizaliza mbaka unatia huruma,hapo unakazi lakini muogawamaisha ungekuwa huna kazi sindio unge pata kisukari wewe....
Mkuu sifanyi kazi serikalini mkuu napiga mbishe zangu tu porini na nikiwa mjini napiga udalali na ujenzi,naongelea in general kwamba kwa miaka 6 wafanyakazi wa serikali hawajapandishwa salary ni muda muhafaka mama ssh akaanza kuwapa tabasamu jipya....Mnaona mama akipandisha salary atavuruga legasi ya jiwe.
 
Back
Top Bottom