Mei 23, Maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani: Waziri wa Afya ahimiza wanawake wenye matatizo kwenda Hospitali na Kutibiwa

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
1590239143512.png

Waziri wa Afya amesema Wanawake wenye matatizo ya Fistula nchini wanatakiwa kuacha tabia ya kujifungia ndani na badala yake amewataka kwenda kupata matibabu katika Hospitali zilizoainishwa na Serikali bila gharama yeyote. Leo ni Siku ya Fistula duniani Tarehe 23 Mei 2020.

Waziri Ummy Mwalimu amesema takwimu za WHO mwaka 2018 zinaonyesha kuna wanawake takribani millioni mbili wanaoishi na Fistula Duniani kote. Inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya kati ya 50,000 na 100,000 hupatikana kila mwaka, juhudi za kutibu Fistula huishia kutibu wagonjwa 20,000 tu.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Afya amesema inakadiriwa kuwa na wanawake takribani 2500 ambao wanapata fistula kila mwaka, huku idadi ya wanaopatiwa matibabu ikiwa ni takribani wanawake 1,000 na kuongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika matibabu haya.

"Katika kipindi cha miaka Mitano kuanzia 2015 hadi Disemba, 2019 wanawake zaidi ya 5,500 wametibiwa Fistula. Mafanikio haya yanatokana na kampeni iliyoendeshwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na Wadau ambayo imeweka Mabalozi wa Fistula zaidi ya 3,000 nchi nzima" Amesema Ummy.

Waziri Ummy ametaja takwimu zinazoonyesha kuwa idadi ya Wanawake wanaojitokeza kutibiwa Fistula kwenye Hospitaii za CCBRT, Bugando,Nkinga na Kuvulini Maternity Center imepungua kwa zaidi ya 30% kuanzia mwaka 2015-2019. Mwaka 2015 wanawake 1337 walipatiwa matibabu ya Fistula.

Mwaka 2016 walikuwa 1356, mwaka 2017 idadi hiyo ikashuka na kufikia 1060, mwaka 2018 ikashuka tena na kufikia idadi ya wanawake 900, na mwaka 2019 ikashuka zaidi na kufikia wanawake 852. Hii imetokana na kuimarika kwa huduma za Afya ya mama wajawazito chini ya awamu ya Tano.

"Mama mjamzito endapo atawahi kliniki mapema kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na mtoto na kuhakikisha anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya atapunguza uwezekano wa kupata tatizo la Fistula". Waziri.

Huduma za Fistula nchini zinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, CCBRT, Bugando, Hospitali ya Kanda ya Rufaa-Mbeya, Hospitali ya Nkinga Tabora, KCMC na Kivulini Maternity Center iliyoko Arusha. Tuna wataalamu waliobobea kwenye tiba ya Fistula kwenye Hospitali hizi.

Waziri amesema ili kutokomeza Fistula nchini kunahitajika juhudi za pamoja za wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa Afya kwenye ngazi zote, Wizara mbalimbali,wadau wa Maendeleo,Wanahabari na Mashirika ambayo yamekuwa yakijihusisha na uhamasishaji wa matibabu ya Fistula.
 
Back
Top Bottom