Mdogo wake BALALI afichua siri kubwa

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
48,851
18,951
...Mdogo wake BALALI afichua siri kubwa


*Asema alitaka azikwe karibu na baba yake
*Kwao wadai amefanyiwa ya Sokoine, Kolimba
*CHADEMA:kweli amekufa, NCCR:hatuamini

Na Waandishi Wetu Dar, Iringa

WAKATI suala la utata juu ya kifo cha Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania ukionekana kuchukua sura mpya kwa kuvigawa vyama vya upinzani nchini, mdogo wa nane wa Gavana huyo aliyezikwa juzi nchini Marekani, Bw. Pashali Ballali, amepinga ndugu yake kuzikwa huko na kulifichulia gazeti hili wosia wake wa awali.

Paschali aliyekuwa akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili juzi kwenye kijiji cha Luganga, Mufindi, Iringa, alikozaliwa Gavana Ballali, alipinga ndugu yake kuzikwa Marekani, akisisitiza kuwa kaka yake si tu alishaagiza akifa azikwe kijiji kwao hapo, bali pia alichagua hadi sehemu ya kuzikwa.

Alisema hata siku moja marehemu hakupata kuwatamkia kuwa akifa azikwe nje ya Tanzania na akaenda mbali zaidi kwa kulihusisha suala hilo na njama ambazo hakutaka kuzifafanua.

Alisema marehemu wakati wa uhai wake alikuwa anasisitiza kuzikwa jirani na kaburi la baba yake mzazi, Mzee Timothi aliyefariki dunia April 3 mwaka 2000.

Bw. Paschali alimwonesha mwandishi wa habari hizi sehemu ambako Gavana Ballali alitaka azikwe na pia kuonesha mahali liliko kaburi la marehemu Mzee Timothi.

Kauli hiyo ya mdogo huyo wa Ballali inaonekana kupingana na taarifa za mke wa marehemu. Bibi Anna Muganda ambaye naye alieleza kuwa na wosia ulioeleza marehemu kutaka kuzikwa huko ughaibuni.

Akionekana kuguswa na namna msiba wa kaka yake ulivyofichwa na mambo kwenda kinyume na matakwa ya wanafamilia akiwemo mama yao mzazi, ambaye yuko Dar es Salaam, Paschali aliitaka Serikali iwape pia taarifa za kina kuhusu sababu za kifo cha ndugu yao.

Akizungumzia pengo la kifo cha ndugui yao huyo Pashali alisema: "Lakini hatuna la kusema zaidi kwani pamoja na kuwa sisi tulimpenda sana kaka yetu Mungu kampenda zaidi na hivyo tunasema jina la Bwana lihimidiwe."

Nao wanakijiji wa mahali hapo alipozaliwa marehemu Ballali, Bi. Sevelanda Ngameni na Bw. Carlosy Luhumba hawakusita kueleza moja kwa moja hisia zao za kuwepo hujuma katika kifo cha Ballali.

Wakizungumza kijijini hapo walikifananisha kifo hicho na cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine na pia cha Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, hayati, Horace Kolimba.

Mazingira ya vifo vya wanasiasa hao bado ni kitendawili hata sasa ikiwa ni miaka mingi tangu walipofariki, Sokoine kwa ajli ya gari, Kolimba kwa kuumwa ghafla alipokuwa akihojiwa kufuatia matamshi yake kuwa CCM haina dira.

Lakini wakati ndugu huyo na majirani hao wa marehemu Ballali, wakionesha wasiwasi wao kuhusu kifo hicho, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini ambavyo ndivyo vilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibua kashfa ya ufisadi kwenye taasisi ambayo marehemu alikuwa akiiongoza nao wameonekana kuwa na mitazamo inayokinzana.

Jana, wakizungumza na waandishi wa habari katika matukio tofauti Dar es Salaam, viongozi waandamizi wa vyama vya NCCR-Mageuzi na CHADEMA, walitofautiana kuhusu ukweli wa kifo hicho.

Mwandishi Wetu anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Bw. Faustin Sungura, alidai kuwa chama hicho hakiamini kuwa Gavana Ballali amefariki.

Bw. Sungura alidai chama hicho kina inaamini Dkt. Ballali yupo hai kwa sababu kuu tatu. Alitaja sababu hizo akidai katika mila na tamaduni za kiafrika suala la kifo halijawahi kuwa jambo la siri kama ilivyotokea Dar es Salaam.

"Dkt. Ballali ni mtuhumiwa namba moja wa ufisadi wa kashfa ya EPA, ni shahidi muhimu kwa upande wa Serikali katika kujua ukweli jinsi fedha za Watanzania zilivyofujwa na mafisadi, lakini cha kushangaza Serikali haitaki kumleta ili ahojiwe," alidai Bw. Sungura.

Akadai: "Serikali ilikuwa inajua anaumwa nini, amelazwa hospitali gani na anaendeleaje lakini ghafla ilibadilika na kuanza kusema haina taarifa zozote za Ballali."

Naye Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje wa chama hicho, Bi. Nderakindo Kessy, alisema iwapo Dkt. Ballali amezikwa Marekani kwa sababu ya kuwa na uraia wa nchi hiyo, Rais Mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa, alifanya makosa makubwa kuteua raia wa nje kushika nafasi nyeti kama hiyo ya ugavana.

"Nafasi ya ugavana ni nyeti kwa nchi yoyote hivyo kama alikuwa raia wa Marekani inabidi Watanzania waelezwe kwa nini alipewa wadhifa huo," alisema.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa Mwenyekiti wa Chama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe amesema anaamini Ballali amekufa ila akatuhumu kuwa kuna watu Serikalini wanahusika na kifo hicho na kumtaka Rais Jakaya Kikwete aunde Tume huru.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa tawi dogo la chama chake katika Mtaa wa Ufipa uliopo Makao Makuu ya CHADEMA, Kinondoni, Dar es Salaam, Bw. Mbowe alidai Ballali amehujumiwa kwa sababu ya watu kutaka kuficha siri ya mafisadi wengine waliohusika na wizi wa BoT.

"Lazima kuna mkono katika kifo cha Ballali na yote ni kutaka wananchi wasifahamu ukweli kuhusu ufisadi uliofanywa na Serikali kwa kuwa hakula fedha peke yake bali wapo viongozi wengine nyuma yake," alisema Bw. Mbowe.

*Imeandikwa na Francis Godwin, Iringa na Reuben Kagaruki na Said Mwishehe, Dar es Salaam.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom