Mdahalo kati ya daktari na mgonjwa aliyekwenda kupima VVU

RIGHT MARKER

Senior Member
Apr 30, 2018
150
520
DOKTA: "Kabla ya kukupatia majibu ya vipimo vyako vya VVU, naomba kwanza nikupe ushauri nasaha".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Lo! Neema ushaniambukiza ugonjwa wako. Kama sio Neema ni Halima".

DOKTA: "UKIMWI ni kifupi cha Upungufu wa Kinga Mwilini. Zipo njia kadhaa zinazoweza kuambukizwa ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "He! nimekumbuka, nahisi ni yule barmaid Grace ndiye ameniambukiza maana si kwa homa hizi, lazima nitakuwa naumwa VVU".

DOKTA: "Unaweza kuambukizwa VVU kwa kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa - hususan damu, manii, majimaji ya uke, maziwa ya mama".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Au atakuwa ni yule Rehema wa kule Sinza niliyekutana nae mwezi uliopita. Lakini mbona aliniambia kuwa yeye huwa anapima VVU kila mwisho wa mwezi."

DOKTA: "Unaweza kupata VVU kwa kushiriki ngono bila kinga na mtu aliyeambukizwa. Pia kwa kushiriki sindano na mtu aliyeambukizwa".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Kama aliyeniambukiza sio Rehema wa Sinza, basi atakuwa ni yule mshenzi Fatuma niliyedate nae mara nne, kwa maana alikuwa na vipele vingi mwilini".

DOKTA: "Watu wengi hawapati dalili mara moja. Ndani ya wiki 1 hadi 4 baada ya kupata VVU, unaweza kupata dalili kama vile homa, upele, uvimbe kwenye shingo, makwapa, au kwenye kinena chako".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Ehe! nimekumbuka sio Fatuma, atakuwa ni Paulina wa Mbagala niliyekutana nae Facebook. Au ni Dorothea wa Instagram ambaye nilidate nae kule makaburini?".

DOKTA: "Ikiwa mtu atagundulika na maambukizi , ataanzishiwa dawa za kupunguza makali ya virusi ambazo huzuia VVU visijirudufishe na kupunguza kiwango cha VVU kwenye damu yako".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Lo! Nilimsahau Regina ambaye aliwahi kulazwa wiki mbili hospitali, sifahamu alikuwa anaumwa nini lakini atakuwa ni yeye ndiye aliyeniambukiza ugonjwa".

DOKTA: "Kwa kawaida mgonjwa wa VVU atatumia dawa 3 au zaidi za VVU kwa sababu dawa za VVU hufanya kazi vizuri zaidi zikitumiwa pamoja".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Kama si Regina basi ni Rose wa kule Keko Kurasini, kwa maana yule hajawahi kulala kwao kila siku yupo kwenye kumbi za starehe".

DOKTA: "Hata hivyo kuugua VVU sio kufa. Wapo watu ambao wanaishi na maambukizi ya VVU zaidi ya miaka 10. Kikubwa ni kufuata masharti ya dozi na ushauri wa daktari".

MGONJWA (Kimoyo moyo): "Eeh! Mungu wangu nisaidie, kama sitokuwa na maambukizi yoyote sitorudia tena kufanya uhuni. Naahidi nitaokoka, usiku na mchana nitakusifu wewe kwa kuimba mapambio".

DOKTA: "Nishamaliza naamini kwa ufupi nimeeleweka. Sasa naomba nikupe majibu yako. Upo tayari?"

MGONJWA (Kwa sauti): Mariamu wa Kibaha, Jackline wa Mbezi, Felister wa Mbeya, Sophia wa Kinondoni, Asha wa Mkuranga, Yasinta wa Chalinze na wengine nyote mmeniuwa.

DOKTA: "Punguza hofu, naomba pokea majibu yako".

MGONJWA: "Hapana daktari naogopa, Sharifa wa Kigamboni tayari ameniambukiza UKIMWI jamani".

DOKTA: "Majibu ya damu yako yameonyesha kuwa hauna maambukizi yoyote damu yako ni safi, hongera sana".

MGONJWA (Kwa mshangao): "Dokta unasemaje? Hebu rudia tena unasemaje? Ina maana Christina wa Chamanzi hakuniambukiza?".

DOKTA: "Hongera sana, pia nakusihi uwe na moyo wa kupima afya yako kila mara ili uwe unajua afya yako, ni muhimu sana kwa ajili yako. Karibu tena".

NB: Majina yaliyotumika kwenye uzi huu hayahusiani na mtu yeyote wala tukio lolote la kiafya. Uzi huu ni kwa ajili ya kuelimishana na kukumbushana kuwa UKIMWI upo, jihadhari, tumia kinga, au baki na mpenzi mmoja.

RIGHT MARKER
Dar es salaam.
 
Back
Top Bottom