Mchungaji Mtikila ashinda kesi ya kumkashifu rais Kikwete

Kwa hiyo yote yaliyosemwa ni kweli kabisa. ama kweli mnyika naye alinena. Kwa hiyo kesho mtu alisema maneno kama ya mtikila hakuna kesi
 
Kwa hiyo yote yaliyosemwa ni kweli kabisa. ama kweli mnyika naye alinena "dhaifu". Kwa hiyo kesho mtu akisema maneno kama ya Mtikila hakuna kesi. Mtikila ni noma
 
Wadau mara baada ya Kushinda kesi yake leo kutokana na hukumu. Kuna askari alitaka kumkamata yamkini kuna kesi nyingine akamwambia,

"Kwa cheo chako huwezi kunikamata mimi ni kiongozi wa kitaifa".

Akamjibu wote sawa mbele ya sheria. Hata hivyo walishindwa kumkamata akafanikiwa kuondoka.

Nami nimejiuliza kama wote ni sawa unaweza kumkamata Rais. Wanajamvi mnasemaje watu wenye nyadhifa za kitaifa kuna utaratibu wa kuwakamata. Nimependa mch. alipomwambia mie kama kuna kesi naambiwa naenda kujisalimisha.

Karibuni kwa hoja ili tukosoane, tusahishane, tujenge hoja kuelewa mwisho tusamehane,

Source: Mahakamani na Habari ktk Tv
 
so amesema nn kuhusu kushinda kesi?
serikali haijakata rufaa?
hajafungua madai ya fidia
 
Kuna taarifa kuwa ameachiwa chini ya kifungu kidogo ambapo upande wa Serikali ungeweza kumkamata akiwa eneo la mahakama na kufunguliwa upya mashtaka yaliyokuwa yakimkabili. Tatizo upande wa Serikali hawakutegemea maamuzi hayo (Doubts)
 
mtikila ndo hapo ninapompendeaga,
anawajua dhaifu, so hababaiki.

yaan yy kesi tu, ikitoka hii anaweka nyingine.

so kama ameshinda so maneno aliyoyasema juu serikali na raisi ni UKWELI MTUPU?
 
Kamchimba biti jamaa kamaki ameduwaa tu wala asijue la kufanya!!!!! Nasubiri Mtikila atoke na kesi nyingine manake nna hakika hautapita mwezi atanyanyuka tena!!!!!
 
Mie sielewi kabisa hapo maelezo ya waraka na kukiri kwa mtikila ni wazi kabisa kaonyesha udini na uchochezi hivyo wakristo wamuweke rais wa kikristo ikulu ili na yeye aweke nin kwenye katiba? Maneno hayo angeyasema ponda nadhani angefungwa na kushambuliwa na vyombo vyote vya habari. Hii ni wazi watendaji walio wengi wamekumbatia udini na hii ndio waislam wanasema mfumo kristo
 
Mch. Chrstopher Mtikila ashinda kesi


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili.

Akizungumza baada ya kushinda kesi hiyo, Mtikila amesema, "Ushindi huu niliutarajia maana hata asubuhi kabla ya kuja mahakamani niliongea na Yesu na sasa amenijibu".

Mara baada ya kushinda kesi hiyo lilizuka timbwili lingine baada ya mtu mmoja kujitokeza akiwa na RB (Report Book) akimtuhumu Mchungaji Mtikila kuwa alimtishia kumuua na ni mwizi wa viwanja. Baada ya kutaka kukamatwa na polisi mmoja aliyekuwa na cheo cha Koplo, Mchungaji alikataa kwa madai kuwa yeye ni kiongozi wa kitaifa hivyo hawezi kukamatwa na polisi mwenye cheo cha Koplo, labda polisi mwenye cheo cha SSP (Senior Superintendent of Police). Kwa kauli hiyo polisi alishindwa kumtia nguvuni.

TAARIFA KWA KINA, (kutoka: Happiness Katabazi - blog, HabariLeo, na Mwananchi)

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemfutia kesi ya uchochezi ya kuchapisha na kumiliki waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila badaa ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha kesi hiyo.

Hukumu hiyo ya kesi hiyo ya jinai Na.132/2010 ilitolewa mchana wa siku ya Jumanne, Septemba 25. 2012 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ambapo alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.

Kosa la kwanza ni kusambaza waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1),(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002 na kosa la pili ni la kumiliki waraka huo wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(2) cha sheria hiyo. Hakimu Mugeta aliyasoma maelezo ya makosa hayo kuwa ilidaiwa na wakili wa serikali mwaka 2010 mahakamani hapo kuwa Novemba 1 mwaka 2009 na April 17 mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kutenda kosa la uchochezi, Mtikila alisambaza kwa umma waraka huo uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho (Kikwete Kuangamiza Kabisa Ukristo! (Wakristo wasipoungana upesi kuweka Mkristo Ikulu), huku akijua kufanya hivyo ni uchochezi.

Maelezo ya kosa la pili ni kwamba, Aprili 16 mwaka 2010 huko Mikocheni, mshitakiwa alikutwa akimiliki waraka huo wa uchochezi.

Katika utetezi wake dhidi ya kesi hiyo Mtikila alipanga kuwaita mashahidi 10 na baadaye kuishia kumuita shahidi mmoja aliyekuwa Mpigapicha Mkuu wa magazeti ya Mwananchi Communications, Mpoki Bukuku aliyepeleka kielelezo cha ushahidi ambacho ni gazeti la Mwananchi la Agosti 9 mwaka 2009, lenye kichwa cha habari "Mtikila apiga kampeni kanisani kumpinga JK... achunguzwa na polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010".

Bukuku alidai kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea mkoani Mwanza katika mkutano wa maaskofu, lengo likiwa ni kuelimisha jamii na kwamba anajiamini kuwa habari haikuwa na tatizo lolote kwa sababu polisi hawajalalamika. Baada ya hakimu kutoa hukumu ya kesi hiyo na kutoka nje ya chumba cha Mahakama Mtikila alisimama na kupaza sauti ‘Haleluya' kwa zaidi ya mara tatu huku baadhi ya watu alioongozana nao wakiitikia Amen.

Akianza kusoma hukumu yake Hakimu Mugeta ambaye alisema kwanza Mtikila katika utetezi wake alikiri kuaanda waraka huo na alikiri pia alikuwa akiumiliki waraka huo na kwamba waraka huo ulitolewa mahakamani hapo kama kielezo cha tatu na jumla ya mashahidi wanne waliletwa na upande wa Jamhuri kuthibitisha kesi hiyo wakati Mtikila akileta shahidi, alijitetea yeye mwenyewe kwa madai hakuona haja ya kuwaleta mashahidi kwa sababu endapo angefanya hivyo, angekuwa anamaliza fedha za mahakama na kupoteza muda wa mahakama bure.

Hakimu Mugeta alisema kufuatia mashitaka yanayomkabili mshitakiwa kabla ya kutoa hukumu yake alijiuliza maswali yafuatayo kuwa je ni kweli waraka huo ni wa uchochezi:


  • Je waraka huo ulileta madhara katika jamii?
  • Je waraka huo wa mshitakiwa ulikuwa ukitaka kumpindua rais Kikwete kinyume na sheria za nchini kwani ofisi ya Rais imeanzishwa kwa sheria husika?

"Mimi nimeusoma waraka huo unaodaiwa na upande wa Jamhuri kuwa ni uchochezi na nimebaini kuwa waraka huo si wa uchochezi kwani Mtikila licha ni mwanasiasa pia ni kiongozi wa kidini na waraka ule ulikuwa umejaa maneno ya kidini ambayo ndani yake Mtikila alikuwa akiwataka Wakristo wenzake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watumie haki yao ya msingi ya kumpigia kura mgombea ambaye ni Mkristo… na kumng'oa madarakani rais Kikwete kwa njia ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu siyo kosa la jinai.... Kwa kifupi, mshtakiwa anawataka Wakristo wenzake kutompigia kura Rais Kikwete na Chama Cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010."

"Kwa mtizamo wangu, kwa kitendo, neno lililozungumzwa au waraka uliochapishwa kuwa uchochezi, lazima ufuatane na matokeo…Ni mtizamo wangu kwamba machapisho matupu tu bila matokeo ya kusababisha chuki, dharau, uchochezi wa kutokuridhika, kujaribu kusababisha mabadiliko ya jambo lolote kinyume cha sheria humaanisha kuhamisha dhamira mbaya, haiwezi kuwa uchochezi."

"Kitendo ambacho mahakama hii kwa kauli moja imeona upande wa Jamhuri imeshindwa kuleta ushahidi unaonyesha Mtikila alikuwa anataka wakristo wamuondoe rais Kikwete Ikulu kwa njia haramu na pia kusambazwa kwa waraka huo na mshitakiwa kulileta madhara na kwamba wameshindwa kuleta ushahidi unaonyesha waumini wa dini ya kikristo walishawishika na waraka huo na wakajaribu kumuondoa Rais Kikwete madarakani kwa njia haramu" alisema Hakimu Mugeta.

Alisema mshitakiwa angeweza kukutwa na hatia kama ingethibitika kuwa alikuwa akitumia karata ya dini kuligawa Taifa na kuongeza kuwa mahakama hiyo imejiridhisha kuwa waraka huo haukuibia chuki mbaya baina ya waumini wa dini ya Kiislam na Kikristo na kwa sababu hiyo, "mahakama hii imemuona Mtikila hajatenda kosa la uchochezi kwa sababu hakuna madhara mabaya yaliyojitokeza katika taifa kupitia waraka huo, na kwa sababu hiyo, mahakama hii inamwachiria huru mshitakiwa..." "Ninakubali kwamba mashtaka dhidi ya mshtakiwa hayakuthibitishwa na Mahakama inamwachia huru katika mashtaka yote."

Baada ya Hakimu Mugeta kumwachiria huyu Mtikila, Mtikila alisimama kizimbani akipaza sauti akisema, "Haleluya, Haleyula… kesi hii ni ya Mungu na hakuna binadamu yoyote anayeweza kushindana na Mungu," na kuwataka Watanzania wakasome Bibilia, Waraka wa pili wa Timotheo 4:2 ambao unasema ‘fanyakazi yako wewe Mhubiri wa Injili onya, karipia na kemea dhambi'.

Mtikila akasema yeye alichokifanya katika waraka ule ni kukemea dhambi na kutangaza neno la Mungu lakini cha kushanga serikali ikamfungulia kesi hiyo ambayo ni jumla ya kesi ya jinai ya 43 amefunguliwa na serikali tangu aanze harakati zake za ukombi wa wa nchi hii, na kwamba kati ya kesi hiyo serikali ilimfunga kesi moja tu ambayo ilikuwa ni ya kutoa maneno ya uchochezi ambapo alisema CCM, ndiyo ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba. Katika kesi hiyo, aliyekuwa Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Stella Mwandu alimfunga mwaka mmoja jela.

Kabla ya Hukumu kusomwa, Mtikila alizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama ambapo alijigamba kuwa ni lazima atashinda kesi hiyo kwani alichokifanya kutangaza Injili na kesi hiyo ni ya Mungu na kwamba haogopi kufungwa.

Baada ya Mtikila kushinda kesi hiyo, hali ilikuwa ni tofauti karibu na mahabasu ya mahakama hiyo ambapo alikuja mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa mfanyabiashara anaitwa Gotem Ndunguru akiwaamrisha askari polisi wamkamate Mtikila kwa madai kuwa ana taarifa ya kumkamata iliyotolewa na kituo cha polisi Kimara yenye namba RB/10482/12 ambapo alidai Mtikila alimtishia kumuua kwa maneno.

Ndunguru anamtuhumu Mchungaji Mtikila kuwa alimtishia kumuua kwa bunduki, kuharibu mali na kuvunja nyumba yake iliyopo eneo la Kimara, Kinondoni.

Mtikila naye alitoa hati ya kumkamata Ndunguru na kuwaonyesha askari hao waliotakiwa kumkamata na kuwataka wamkamate akidai kuwa ni tapeli. Alidai kuwa Ndunguru anatakiwa kukamatwa na kupelekwa Mahakama ya Mwanzo, Kimara akidai ameidharau kwa kutohudhuria kesi yake.

Hata hivyo, askari polisi na Ndunguru walishindwa kumkamata Mtikila kwa sababu Mtikila alianza kumfokea askari polisi mmoja (ambaye hatukuweza kufanikiwa kulipata jina lake), ambaye alikuwa na cheo cha Koplo akimwambia kwa ukali kuwa hana hadi ya kumkamata yeye ana hadhi ya kukamatawa na polisi mwenye cheo cha Mrakibu wa Polisi na kwamba Nduguru ni mwizi mkubwa.

"We askari huyo Ndunguru kakuonga uje unifanyie fujo hapa. Kwa taarifa yako mimi najua sheria, wewe huna mamlaka ya kunikamata na huwezi kunikamata kihuni hivi… hata huyo bosi wako IGP-Said Mwema kabla ya kunikamata ananipigia simu kwa adabu na mimi mwenyewe ndiyo naenda polisi… sasa nawaambia hivi hauna hadhi ya kunikamata!" Alifoka Mtikila na kusababisha askari huyo kunywea na kuitwa na maaskari wenzake ambao walimtaka amwache Mtikila aende zake.

Maaskari hao walimtaka Ndunguru anyamaze asiwafundishe kazi yao.

Baadaye Ndunguru aliondoka mahakamani hapo kimya kimya.

Machi 14, mwaka huu, Mtikila alipatikana na kesi ya kujibu kwa kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Kikwete, uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake baada ya kuwaleta mashahidi watano.

Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri, amefikia uamuzi wa kumwona Mtikila ana kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa kupanda kizimbani Aprili 11, mwaka huu kuanza kujitetea.

Februari, mwaka huu, Mtikila alikiri maelezo aliyochukuliwa na ofisa wa polisi kuwa ni yake na kwamba hana pingamizi nayo na hivyo Mahakama iliyapokea kama kielezo cha upande wa Jamhuri. Katika maelezo hayo, alikiri kuwa aliuandaa waraka huo na kuusambaza lakini alisema siyo wa uchochezi ila unahusu maneno ya Mungu.

Mtikila alikiri maelezo hayo yaliyosomwa na kutolewa mahakamani kama kielelezo baada ya shahidi wa Jamhuri, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Ibeleze Mrema (54) kudai kwamba Aprili 15, 2010 akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam aliitwa na mkuu wake wa kazi na kumpa kazi ya kumhoji Mtikila kuhusu tuhuma za kukutwa na waraka wa uchochezi na alikiri kuhusika na nyaraka hizo na kwamba alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuokoa Wakristo na alisaini waraka huo.

"...Nilipomhoji walichapisha wapi hakupenda kusema, bali alidai kuwa zilikuwa nyaraka 100,000 ambazo zilisema kwamba Rais Kikwete anaangamiza Ukristo na amekuwa jasiri kuingiza Uislamu katika Katiba ya Jamhuri."

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari, 2009 na Aprili 17, 2010 Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshtakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema ‘Kikwete kuuangamiza Ukristo, Wakristo waungane kuweka mtu Ikulu.' Katika shtaka la pili, Aprili 16, 2010 eneo la Mikocheni, Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii na katika kesi hiyo alijitetea mwenyewe.




Source: wavuti.com - wavuti
 

Attachments

  • 480284948.jpg
    480284948.jpg
    40.6 KB · Views: 22
  • 608466274.jpg
    608466274.jpg
    50 KB · Views: 23
  • 999264117.jpg
    999264117.jpg
    70.3 KB · Views: 37
Kumbukumbu Mujarabu Watuhumiwa watarajiwa wajifunze namna ya kukabiliana na hizo Kesi wanazozipenda Maana Kumkashifu Raisi ni kujitakia kesi tu
 
Back
Top Bottom