Mchechu akana kulipwa mshahara wa shilingi milioni 36

Salary Slip

JF-Expert Member
Apr 3, 2012
48,691
149,913
Mchechu amekanusha hayo katika gazeti la Mwananchi la leo na kulaumu taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

======

Mchechu: Watanzania ni vigeugeu

Na Nuzulack Dausen, Mwananchi


Nehemiah Mchechu, moja ya majina maarufu katika nyanja za uongozi wa mashirika nchini, jina lake limeteka mitandao ya kijamii kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Ukiachana na umaarufu wa Rais John Magufuli mtandaoni kwa kazi yake ya 'kutumbua' majipu, Mchechu ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), anavuma kwa mema na ?mabaya?.

Baadhi wanasifu mafanikio yake ya kuliimarisha shirika hilo kwa kipindi cha muda mfupi, lakini wengine wanamtuhumu kulitumia kujinufaisha ikiwamo kujilipa ?mamilioni? ya shilingi kama mshahara na posho za vikao.

Tuhuma zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba bosi huyo wa NHC, anajilipa mshahara Sh36 milioni kwa mwezi na kuhudhuria vikao vingi vya bodi vinampatia posho za kutisha.

"Kiwango hicho hakina ukweli," anasema Mchechu, "mshahara wangu upo chini ya hapo," anasema.

"Pia, huwezi kujilipa. Unalipwa kwa makubaliano maalumu tangu awali kabla ya kazi kulingana na kazi unayopewa," anaongeza.

Mchechu anasema yupo NHC kulitumikia taifa kwa kuwa alipotoka sekta binafsi alikuwa akipata mshahara mkubwa, lakini alikubali kiwango kidogo serikalini kwa kuwa alikuwa akijua shirika hilo lilikuwa na hali mbaya kifedha na lilihitaji kuboreshwa.

Kuhusu vikao vya bodi na kamati mbalimbali anazotuhumiwa kushiriki na 'kuvuna fedha', Mchechu anasema kamati nyingi zinazorushwa mtandaoni siyo za kweli na hakuna fedha inayolipwa katika vikao hivyo.

"Watu wanapohoji mshahara wangu wanasahau kiwango ninachoingiza kwa Serikali. Jaribu kufikiri tumeirudisha ardhi ya Kawe Tanganyika Parkers yenye thamani ya zaidi ya Sh200 bilioni kutoka mikononi mwa aliyekuwa ameuziwa kipindi hicho, hivi ningekuwa mtu binafsi kwa kufanikisha majadiliano ya kurudisha kiwanja hicho, ningepata kiasi gani?" anasema.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni, Mchechu anaeleza kuwa Watanzania ni kigeugeu kwa kuwa wakati anaingia NHC mwaka 2010 akitokea Benki ya CBA, wengi walimuonea huruma wakieleza alikuwa anakwenda kupoteza weledi na mshahara, lakini sasa wanamzushia anapokea fedha nyingi zinazolifilisi shirika.

"Siku waajiri wangu wakigundua nalipwa mshahara mkubwa kuliko ninachofakifanya wataniondoa kwa sababu nawaletea hasara," anasema.

Bosi huyo wa zamani wa Benki ya Standard Chartered alianza kazi mwaka 2010, wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kwa kupatiwa mkataba wa miaka minne kuboresha shirika hilo lililokuwa likichechemea.

Mkataba wa awali ulimalizika mwaka jana na kusaini mwingine wa miaka mitano ambao unatarajia kumalizika mwaka 2018/2019.

Kama yalivyokuwa malengo ya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962, Mchechu, alikabidhiwa kazi ya kuendeleza sera ya kujenga makazi ya bei nafuu kwa Watanzania.

Kama ilivyokuwa kwa mashirika mengine ya umma, NHC halikuwa likipata faida kubwa ya kuwezesha kuendeleza miradi mikubwa na kwa mujibu ripoti za fedha za shirika hilo, mwaka 2010 lilikuwa limepata faida ya Sh3.1 bilioni.

Ili kulifanyia mabadiliko Shirika hilo, Mchechu anasema, ilihitajika akili na nguvu ya kutosha kwa sababu mambo yalikuwa yakiendeshwa kienyeji na kwamba baadhi ya vigogo walikuwa wakihusika kulifilisi NHC.

Anasema kuwa kuna baadhi ya vigogo serikalini na watumishi wa shirika hilo waliokuwa wakiendesha ukodishaji wa nyumba kwa mikataba ya kilaghai na NHC kwa kulipatia fedha kidogo wakati wanatoza fedha nyingi kwa wapangaji.

Kuna baadhi ya 'madalali' walikuwa wakililipa shirika kodi ya Sh700, 000 katika baadhi ya nyumba za biashara kwa mwezi wakati wao wanakusanya zaidi ya Sh5 milioni lakini mikataba hiyo ilivunjwa.

"Tumekirejesha alichokuwa akikitaka Baba wa Taifa kwa sababu kwa sasa karibu kila mkoa una nyumba za bei nafuu zilizojengwa na shirika," anasema Mchechu akieleza kuwa hadi sasa wamejenga nyumba zaidi ya 3,000 za bei ya chini.

Katika mtandao wa nyumba hizo, zilizokuwa zikiuzwa bei ya chini kuliko zote nchini ni zile zilizopo mkoani Katavi ambazo zilikuwa Sh32 milioni kwa sababu huduma za umeme na barabara zilikuwa zimesogezwa.

Anaeleza kuwa wastani wa bei ya makazi ya bei nafuu ni Sh34 milioni kwa nyumba ya vyumba viwili na Sh43 milioni kwa nyumba ya vyumba vitatu na bei hupanda kutokana na gharama za ujenzi zikiwamo kuandaa miundombinu na kodi ya ongezeko la thamani.

Pia, gharama hizo anasema zinatokana na riba kubwa ya mikopo iliyopo sokoni na kupanda kwa thamani ya Dola ya Marekani mara kwa mara.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema nyumba hizo zinauzwa ghali na kununuliwa na mabepari pekee badala ya walengwa ambao ni watu wa kipato cha chini na sehemu kubwa zinadoda kwa kukosa wateja.

Kwa Mchechu, tuhuma hizo hazimnyimi usingizi. Na kabla ya kujibu hoja hiyo, anatasabasamu kidogo.

"Kila mradi tunaoufanya huwa tunalenga watu wa kundi fulani. Hatukurupuki. Tunaangalia wa kipato cha chini, kati na cha juu. Sina sababu ya kuficha.

"Lakini nyumba zetu ni za bei ya chini kulinganisha na kampuni binafsi hivyo naomba fananisha embe kwa embe na chungwa na chungwa na si vinginevyo," anasema.

Mchechu anasema kuna baadhi ya miradi mikubwa kama ya Kawe na Morocco ni ya kibiashara zaidi na nyumba zake zinauzwa bei kubwa kwa kuwa zililenga kundi la watu ambao hukimbilia nje ya nchi kununua makazi lakini sasa wanataka wabaki nchini.

"Kama mtu ni wa malengo ya Sh50 milioni halafu anakosoa bei za mradi wa Kawe yupo sahihi kuona bei ile ni kichaa kwa sababu inaenda mara tatu hadi 10 ya kipato chake. Lakini mimi sikulenga kule," anasema.

Hata hivyo, anaeleza kwa kuwa NHC malengo yake ni kujenga nyumba za bei nafuu katika halmashauri zote nchini ambako tayari wamenunua ekari 5,600 huku nyingine 22,000 wapo kwenye mazungumzo ya kuuziana na wamiliki.

Kuhusu kudoda kwa nyumba, bosi huyo anapinga kidogo.

Anasema makazi mengi waliyoyajenga kwa bei nafuu yalinunuliwa yote na mengine kabla ya miradi yake kukamilika kupitia mikopo ambayo wananchi wanakopa benki za biashara kununua nyumba za NHC.

"Kibada, Kigamboni (Dar es Salaam) tuliuza ndani ya saa 48, mradi wa Eco Housing na Mchikichini zote zimeuzwa hata hizo za mikoani zina soko?hakuna zilizododa," anasema Mchechu.

NHC inafahamika kwa muda mrefu kuwa na nyumba za kupangisha za bei nafuu nchini lakini kwa sasa miradi yake ya kupangisha haisikiki kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, majibu ya kiongozi huyo yanashitua kidogo kwa wanasubiri kiwango kikubwa cha nyumba za kupangisha.

Anasema kuwa katika mikakati yao walipanga kujenga nyumba asilimia 70 kwa ajili ya kuuza na asilimia 30 ya kupangisha kwa watu wa hali ya chini.

Matangazo ya ukodishaji hayawi makubwa sana kama ilivyo katika uuzaji kwa kuwa wananchi wengi wanahitaji nyumba hizo, anaeleza.

"Tanzania ina upungufu mkubwa wa nyumba takriban 3.5 milioni hivyo iwapo nikisema nijenge nyumba moja kwa Sh100 milioni na kuikodisha ile fedha itasaidia familia moja tu lakini nikiuza nyumba mtaji ule nikauzungusha tunaweza kujenga zaidi ya nyumba nane za familia," anasema Mchechu.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani ameanza kubadilisha utendaji kwenye utumishi wa umma na moja ya njia ya kufanikisha hilo ni ziara za kushtukiza katika taasisi na mashirika ya umma.

Mchechu amejiandaje na ujio wa kushtukiza wa Rais?

"Sisi tayari tulikuwa tunaendesha mambo yetu kwa mwendokasi na baadaye tutaongeza zaidi kasi," anasema.

Katika uongozi wake, anaeleza aliyoyapata NHC yakiwamo kuongeza uwekezaji wa ujenzi nyumba nchini na kukuza mapato ya shirika ambayo mwaka jana yalifikia Sh130 bilioni kutoka Sh36.6 bilioni mwaka 2010 baada ya kubana matumizi na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.

"Pesa tumeikuza lakini haitosheelezi miradi hata ukichanganya na mikopo hivyo tunaendelea kutafuta fedha zaidi ili kufanikisha malengo yetu.

"Na pia niwe muwazi kabisa kama nitashindwa kutimiza malengo kwa miaka tisa niliyokaa NHC sidhani kama nitaleta kipya nikipatiwa miaka 20 hivyo baada ya hapa nitarudi sekta binafsi," anasema.
 
Mshahara yaweza kuwa siyo jambo sana,lakini je, anaweza ku justify input yake katika ku influence outcome ya shirika? That's essential.
 
asingeweza kukubali, hivi na raisi nae mshahara wake ni kiasi gani???? nae atakubali akiulizwa.
 
Hata akilipwa 40 mill sio mbaya jamaa kapiga kazi sana amelifanya NHC isimame na kuwa bora kuliko miaka 10 iliyopita jamaa ni jembe
 
Kama alipwi 36.5m analipwa ngapi? Asitake kutuongopea analipwa Hiyo Hiyo na malupulupu kibao.

Cc: NHM
 
Last edited by a moderator:
Mchechu kwanini anapotosha umma?!? Sikujua kuwa uongo ni moja ya sifa zako NKM!

Tingatinga litapita hapo NHC na nina uhakika hautasalimika.
 
Last edited by a moderator:
Kwanza akubali pesa anayolipwa ni ndefu sana lakini pili akubali yeye siyo pekee kwasasa awaachie wengine waendeleze NHC. Pumzi yake imeisha kama CCM ilivyoishiwa wakaamua kumpa Magufuli (huyu ni mwanachama wa CCM aliyeamini chama kimechoka na kuhitaji mabadiliko) tunahitaji mpya aseme NHC atakayoileta na siyo Mchechu.
 
Tumuache afanye kazi japo inabidi na yeye na NHC yake wa apply austerity measures. Mfano Kuna bosi mmoja wa NHC anapewa magari 3, Discover 4 ya kwake au VX, pickup 2.8 ya watoto kufuata shule na Mke mama wa nyumbani naye anapewa VX. Haya ni matumizi mabaya ya rasilimali hasa kwa shirika.ambalo Return on investment haijaanza kuonekana bado kama NHC.
 
Analipwa pesa ndogo sana.
Wamuongeze mara mbili. Kwa kazi nzuri ya kuimalisha shirika.
Mbona TX akija bongo kwa kazi hiyo hiyo anayoifanya mchechu mihela kibao?
 
Back
Top Bottom