Mchango wa Mhe.Cheyo.

Mpaka Kieleweke

JF-Expert Member
Feb 27, 2007
4,132
1,575
MHE. JOHN M. CHEYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, nitumie nafasi hii, kumpongeza sana Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, kwa kutoa angalau mwelekeo wa matumaini kwa Watanzania; imekuwa ni Bajeti nzuri sana ya upande wa Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimefurahishwa sana mwaka huu na jinsi ambavyo Kamati ya Fedha na Uchumi, ilivyoweka mchango wake katika Bajeti hii. Matumaini yangu ni kwamba, Serikali itayachukulia maoni haya kwa uzito wake na kuweza kuchukua kama somo labda kwa Bajeti inayofuata. Pia niwashukuru wengine, lakini labda niseme, nimefurahishwa sana na mchango wa ndugu yangu hapa nyuma, Mheshimiwa Kabwe Zitto, kwa kufanya kazi nzuri; naona kuchelewa kidogo kumemsaidia. Sasa baada ya hapo naomba kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ambayo ningependa kuizungumzia ni juu ya Mapato ya Wakulima. Kwa kuwa mimi natoka kule ambako pamba inalimwa, hapa hoja ni pamba. Kwanza, nimesikitishwa na bei ya shilingi 400 kwa kilo ya pamba, nilitegemea ingeanzia shilingi 500. Kwa kuwa sisi wakulima wa pamba tunafahamu, mwanzoni bei inakuwa ndogo na baadae inapanda, kwa mfano; mwaka jana ilianza kwa shilingi 275 ikapanda mpaka karibu shilingi 500, basi ushauri wangu kwa wakulima, wafanye kama tunavyofanya, kila wakati tusubiri wakati muafaka ambapo wanunuzi watahitaji hiyo pamba yetu na tutawauzia kwa bei angalau ya shilingi 500. Hilo ni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la kufurahisha zaidi, mwaka huu wakulima wa pamba, kilio chetu cha kuibiwa kwa kupitia kitabu cha pembejeo kimekwisha. Mwaka huu kitabu hicho kimefutwa na kusema kwamba, mambo ya kila siku kuwa na kitabu kinachowaibia wakulima kwamba wanakukata mwaka huu shilingi 100,000 lakini pembejeo unayopata ni ya shilingi 50,000; kilio hicho kimekwisha sasa. Hii haimaanishi kwamba, hatuhitaji fedha za pembejeo. Bado mimi ningewashauri wakulima, kwa hivi sasa kwanza wanapopokea fedha zao za pamba, waweze kuweka akiba kwa ajili ya kujinunulia pembejeo.

Vilevile ningependa kuishauri Serikali, iweke kama vile tunavyoshindana sehemu nyingine; kwa nini pasiwepo na ushindani katika kuuza dawa za pamba, badala ya kutegemea muuzaji mmoja tu. Kwa hiyo, kama tunakubali kabisa kwamba mfumo wa ushindani ndiyo unaoleta ufanisi katika biashara, basi ningeshauri kwamba, pawepo na ushindani mkubwa katika kuleta dawa mbalimbali kwa ajili ya pamba ili watu waweze kununua kwa bei nafuu. Naomba kushauri kuwa ruzuku ya pamba iendelee, kwa sababu kwa mfano, msimu wa mwaka 2005 ilikuwa ya kwanza katika kutoa fedha za kigeni kwa takriban milioni 101 USD.

Sasa tusibabaishwe na fedha zinazotoka kwenye madini; bilioni 822, ambazo nyingi zake zinakaa nje, zinatokana na mazao yetu na ndiyo zinatusaidia kununua bidhaa mbalimbali. Ninaiomba Serikali iwaone wakulima hawa kuwa ni wachangiaji wakubwa sana katika Bajeti ya Serikali na zaidi katika fedha za kigeni. Kwa hiyo, ruzuku kwa pembejeo iendelee, tusiende kwenye upande mmoja tu wa mbolea. Najua ni ya maana, lakini pembejeo kwa hawa watu ni ya maana pia. Wakulima jiandaeni na tumieni fedha zenu vizuri. Hilo limeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ni Bajeti ya Serikali. Hapa najikita zaidi kwenye takwimu za Bajeti ya Serikali. Ukichukua hiki kitabu katika ukurasa wa 48, tuanzie ukurasa wa 47 kitu kimoja kinanitatanisha; Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, katika Bajeti hii atapata trilioni 4.729 kama mapato ya ndani, lakini ukichukua kitabu ambacho ametupa na natumai ndicho kitabu rasmi, unashangaa kuona fedha anazosema zitapatikana ndani ni trilioni 4.786, yaani kuna tofauti ya bilioni 60. Sasa hizi bilioni 60 mbona hazimo katika Bajeti hii? Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, kutoka kwa Wafadhili tutapata trilioni 2.249, lakini ukiangalia katika kitabu hiki ambacho ametupa, unaona kwamba tutapata trilioni 2.36 nako tena kuna tofauti ya bilioni 60. Halafu si hivyo tu, hata ile fedha ambayo ameitaja ya MCC, ametuambia tutapata bilioni 68 lakini kitabu kinazungumzia bilioni 79. Haiishii hapo, ukiangalia katika mizania ambayo ametupa, ukurasa wa 48 anatuambia kwamba, mapato ya ndani ambayo nimeyasoma ya trilioni 4.728, ndiyo yatatumika, kweli nakubalina na ni jambo zuri katika matumizi ya kawaida ambayo ni trilioni 4.726 inabakia kama bilioni 1.9 tu.

Sasa anapokuja kutuambia kwamba, fedha za ndani atatupa bilioni 938, hizo anazipata wapi? Umebakiwa na bilioni moja na pointi, unasema utatumia bilioni 938; sasa hizo zinatoka wapi?

Kwa hiyo, sioni tunazungumza Bajeti gani, kwa sababu Bajeti ni takwimu. Sasa kama takwimu ya kitabu hiki ambacho ndicho rasmi hazifanani na Bajeti tunapewa na Mheshimiwa Waziri; sasa tuulize, tutakapopiga kura tunapigia kura hesabu za vitabu hivi rasmi au Hotuba ya Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni la maana na linaleta shaka juu ya hesabu ambazo tunapewa. Pili, Wazungu wanasema hakuna credibility, unapokuwa na kitabu kimoja kinasema hivi na kitabu kingine kina takwimu hii; sasa watu waamini nini? Sisi tunajua kwamba, maana ya Bajeti ni mkataba kati ya Watanzania na Serikali yao na mkataba wao unasema kwamba, nipeni fedha hizi kwa mapato nitazitumia. Sasa tukiangalia hapa mara tunakosa bilioni 56; tunazungumzia Bajeti gani?

Napenda Mheshimiwa Waziri, aliangalie hili jambo ili tuweze kujua tunapitisha nini Ijumaa. Kama vitabu vimekosewa basi virekebishwe na kama ni hotuba ndiyo iliyokosewa basi irekebishwe, lakini takwimu hizi hazionyeshi uhalisia wa Bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni juu ya fedha za wafadhili. Sasa sijui nitamke figure gani; nitatumia figure ambayo aliizungumzia Waziri ambayo ni trilioni 2.429. Katika fedha hizi, ningeshukuru zaidi kama kila tunapopata Bajeti, angeweza kutuwekea mchanganuo kama asilimia ngapi ni mikopo na asilimia ngapi ni misaada? Hii ni kwa sababu, ukisema hatutaki kutegemea wafadhali na unaweka fedha trilioni 2.429, ambazo asilimia 40 ya hizo fedha ni mikopo; huwezi kusema ni fedha za wafadhili tena! Kama unaenda kukopa World Bank siyo fedha ya Mfadhili; hukufadhiliwa utailipa. Tunalipa madeni na tunaweka fedha nyingi sana kwa ajili ya kulipa madeni. Kwa hiyo ni vizuri Watanzania tukafahamu fedha zipi ni msaada na zipi ni za mikopo. Zaidi kinachonigusa kwa wafadhili ni jambo moja kwamba, siku hizi kwa maana ya hizi Kamati za LAAC, POC na PAC tulishangazwa sana. Tulipokaa na hili group ambalo linaitwa Development Partiners, tulishangaa kuona kwamba, kumbe Serikali inapopokea hizi fedha, inafanya mkataba wa mambo mbalimbali ya kutimiza katika mwaka huo.

Mambo hayo hayajulikani Bungeni, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, anaposema mwaka huu atapata trilioni mbili kutoka kwa wafadhili ni vyema basi akalifanyia haki Bunge hili, akaliambia ni kwa masharti gani? Baadhi ya masharti tumeona kwa mfano, pawepo na uhuru wa vyombo vya habari; sasa uhuru wa vyombo vya habari unahusiana vipi na 2.4 trilioni? Pawe na Serikali iwafunge na iwapeleke mahakamani mafisadi watano kila mwaka na hili wasipolitimiza wasipate hizi fedha. Sasa tunapoambiwa juu ya fedha hizi, basi tuambiwe na masharti ambayo wamekubaliana na wafadhili ili na sisi tuweze kufuatilia; kwa sababu kukosa fedha hizi maana yake ni kukosa barabara, fedha za elimu na fedha za maji. Sasa unatupa Bajeti au unatupa Bajeti halisi, kwa sababu kama yale masharti hayafikiwi ndiyo kusema kwamba, hatuna bajeti ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kukazia mambo yafuatayo: Mimi bado nasema ni vyema Tanzania tukaenda kwa hatua ya kujitegemea na kwa hili naipongeza Serikali. Hatua ya kusema kwamba, tunataka kujitegemea ni jambo zuri sana, lakini mbona hatufanyi juhudi katika sehemu ambazo zinaweza kutupa fedha? Nimeangalia sana katika Wizara ya Utalii, tutakachopata sasa kwa watalii ambapo mapato yanayotajwa kwenye Kitabu cha Nne, yanazungumzia 1.2 triolioni. Ukiangalia kutoka kwenye utalii tunapa bilioni moja; ni vipi? Hoteli zote ambazo tumeambiwa na Mheshimiwa Waziri kwamba, hoteli moja tunapata milioni 35 kwa siku; sasa mbona hatupati hizo fedha? Hilo ni eneo la kukazia.

Ukiangalia kwenye madini madini; dhahabu peke na vito vingine ni dola milioni 884, lakini Wizara ya Madini inapata bilioni 50; kwa vipi? Nasisitiza hapa kama Mjumbe wa Kamati ya Madini ya Rais; yale mapendekezo tuliyotoa kwa Mheshimiwa Rais, pamoja na Tume nyingine ili kuimarisha mapato kutoka kwenye Sekta hii, naomba yafuatiliwe ili tupate tunachostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
 
Back
Top Bottom