Mchango wa Bongo Flava kwenye istilahi ya Kiswahili

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
705
Waungwana,

Leo nawaombeni tujadili na tuichambue michango ya muziki wa Bongo Flava kwenye istilahi na misamiati ya lugha ya Kiswahili, kama ifuatavyo:

1) Mtoto wa Geti Kali - Msamiati huu ulianza kutumika mara tu baada ya wimbo uliopendwa sana wa Inspekta Haroun, kwa jina hilo hilo. Mojawapo ya mfano wa msamiati huu unaweza kuwa, "Umemwona huyo? Mtoto wa geti kali huyo!" Au, "Siku hizi naona umekuwa mtoto wa geti kali... hata huonekani." Maana ya msamiati huu inaeleweka kwa wote... asiyejua aulize, ataelezwa.

2) Mzee wa Busara - Sikumbuki wimbo huu uliimbwa na nani. Alikuwa Juma Nature au msanii gani? Hapa, kwa kweli, sanaa ilifanya kazi kubwa, ya kubadilisha na kugeuza kabisa maana ya maneno "Mzee" na "Busara". Kwa wimbo huu, msanii alileta sura mpya kwenye maneno haya, na kuufanya msamiati huu ueleweke kwamba mtajwa ni mtu mshirikina au mchawi. Kwa kawaida, wazee wanajulikana ni watu ambao wana busara na hekima. Kwa matumizi ya msamiati wa "mzee wa busara", si tu kwamba msanii hakuwalenga wazee peke yao, bali aliwalenga watu wote ambao wanatuhumiwa kujihusisha na imani za nguvu za giza, yaani, ushirikina.

3) Habari ndio hiyo - Huu ni msamiati mpya kabisa kwenye istilahi ya lugha ya Kiswahili. Msamiati huu umeenea sana hapa jijini Dar es Salaam, na umeanza kutumiwa na vijana na hata watu wazima pia, wakiweka msisitizo wakati wanapotoa taarifa nzuri au mbaya kwa mtu wanayeongea naye, au hata kwenye maongezi ya kawaida ya kila siku. Msamiati huu umetokea kwenye wimbo wa msanii wa Bongo Flava Ambwenye Yesaya, maarufu kwa jina la A.Y., ambaye amewashirikisha baadhi ya wasanii maarufu wa mtindo huo (Bongo Flava ni mtindo, si fani...), kama vile (sina uhakika na hili), Mwana Falsafa, kwa jina lingine, Mwana FA.

4) Dar Mpaka Moro - Hiki ni kiitikio cha utani, ambacho kimetoka kwenye jina la wimbo wa TMK Wanaume Halisi, unaoitwa "Dar Mpaka Moro". Kiitikio hiki, kama kawaida, kimeanzia 'mitaani' kwa vijana, na sasa kimekubalika kwa watu wa rika mbali mbali. Ni kiitikio cha swali lolote linalotumia neno "wapi", kama kinavyotumika kwenye wimbo huo wa TMK Wanaume Halisi. Usishangae, siku hizi, ukipita mtaani na kuuliza swali lenye neno "wapi", kama vile, "Samahani, unaweza kunionesha wapi nitakwenda kujisadia haja ndogo?" na kujikuta ukajibiwa, "Dar Mpaka Moro, ni nyuma ya ile nyumba, ukiingia kwenye uchochoro ule pale".

Kwa leo ninaishia hapa waungwana. Yeyote mwenye kuweza kutoa mchango wake kwenye mjadala huu anaombwa kuongezea hapa nilipofikia. Mchango wangu unaweza pia kuwa na makosa fulani fulani, kama vile majina ya wasanii waliotajwa kuhusika na nyimbo zilizochangia kwenye istilahi na misamiati ya Kiswahili. Nawaombeni mnisahihishe pale nilipokosea.

Asanteni.

./MwanaHaki
 
Wasanii wamesaidia sana kama FID Q,FROF J,MWANA FA,SOLOTHANG, WAGOSI
 
Back
Top Bottom