Mchakato Wa Katiba Na Kisa Cha Mtema Kuni! (Makala MWANCHI Jumapili) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mchakato Wa Katiba Na Kisa Cha Mtema Kuni! (Makala MWANCHI Jumapili)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Dec 4, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Dec 4, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Ndugu zangu,

  Kwenye hili la mchakato wa kupata katiba mpya bado nasimama kwenye kauli yangu ya tangu mwezi Aprili mwaka huu, kuwa tumeanza na mguu mbaya lakini naamini kuwa bado tuna nafasi ya kujisahihisha.


  Ndio, tukitanguliza hekima na busara tunaweza kuinusuru nchi yetu tuliyozaliwa kwa madhara ya muda mrefu yatakayotokana na makosa tunayotaka kuyafanya kwa makusudi kwa kutanguliza zaidi maslahi ya kisiasa ya muda mfupi.

  Matukio ya hivi karibuni

  Niwe mkweli kwa nchi yangu, katika hili la mchakato wa katiba naanza kuziona dalili za uwepo wa mizengwe ya kisiasa inayouzunguka mchakato wenyewe.

  Ni mizengwe inayozingua akili za Watanzania kuliko kuzituliza. Na katika dunia ya sasa, nchi itakayounda katiba yake itakayotokana na mizengwe ya kisiasa badala ya hoja za msingi za kitaifa, kamwe haiwezi kuwa na hakika ya kubaki salama.

  Tayari, kwenye muswada uliokwishatiwa saini na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kuna vifungu vya adhabu kwa Mtanzania kwenda jela kama atatoa maoni yake yenye kukiuka masharti yaliyowekwa katika kutoa maoni juu ya katiba mpya kwenye baadhi ya vipengele.

  Naam, Watanzania tumeshaambiwa ;‘ Mtakiona cha mtemakuni kama…’. Na hapo ndipo utawajua Watanzania walivyo. Kila Mtanzania aliyezaliwa na kukulia Tanzania anajua maana ya ’ kukioona cha mtema kuni!’

  Na ajabu si Watanzania wengi wenye kukifahamu kisa kilichomkuta mtema kuni, lakini, wanaijua usemi wa ’kukiona cha mtema kuni!’

  Mtema kuni ina maana ya mkata kuni. Afrika kwenda kukata kuni porini ni kazi ya hatari sana. Porini kuna wanyama wakali, kuna nyoka na miiba mikali pia. Moja ya simulizi za Mtema kuni nilizosimuliwa utotoni ni pale aliporudi nyumbani bila kuni lakini na jeraha la kuchomwa na mwiba mkali.

  Kunahitajika kazi ya ziada kuwafanya Watanzania wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru kwenye mchakato wa jambo lililochanganyika na hofu ya kupatwa na ’ Kilichompata mtema kuni’, au hata ’ kilichomtoa kanga manyoya!’.

  Naam, hofu ya kushiriki mchakato wa kutoa maoni lakini wenye adhabu ndani yake kama maoni hayo yatagusa jambo fulani ambalo walioandaa mchakato wameweka marufuku ya kuliongelea.

  Kingine kinachojitokeza sasa ni hali ya kutoaminiana hususan baina ya vyama viwili vikubwa vyenye wafuasi wengi miongoni mwa Watanzania. Ni vyama vinavyovutana kisiasa kwa sasa, CCM na Chadema.
  Ukweli wa uwepo wa mvutano huo na CHADEMA kutangaza kujiweka kando, kunaufanya mchakato huo kuchangia kwenye kuwagawa Watanzania na hata kuufanya mchakato wenyewe uonekane wenye sura ya chama tawala zaidi kwa maana ya CCM, hivyo kupunguza matumaini ya uwepo wa muafaka wa kitaifa katika kupata katiba mpya. Kwa mazingira haya, sote tutakuwa tumeshindwa.


  Katika wakati huu kuna haja kubwa kwa viongozi wa siasa, kidini na wanaharakati kutanguliza hekima na busara. Kuweka mbele maslahi mapana na ya muda mrefu ya nchi yetu. Tufanye hima kuisafisha njia ya mazungumzo katika kufikia muafaka wa kitaifa juu ya jambo hili kubwa kwa nchi yetu, yaani Katiba.


  Nimepata kuandika hapa, kuwa ni kwa njia hii ya mazungumzo na kupata muafaka wa kitaifa ndipo tutaepuka wingi huu wa manung’uniko ambao kimsingi yatazaa katiba ya manung’uniko, itakayotupelekea kwenye uchaguzi wa manung’uniko , utakaozaa matokeo ya manung’uniko. Hivyo basi, tutakuwa tumeandaa katiba ya kutuletea vurugu katika nchi yetu.


  Maana, katika kuongezeka kwa hali ya kukata tamaa na hata kupoteza imani yao kwa CCM na Serikali yao, Watanzania wengi kwa sasa wanaiona katiba mpya kuwa ni tumaini jipya. Tutafanya makosa makubwa kuwaburuza Watanzania katika mchakato huu wa katiba.

  Mathalan kule Igunga Watanzania tulishaziona ishara mbaya, kuwa kama nchi yetu itakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 bila kuufanyia mabadiliko ya kimsingi mfumo wetu wa uchaguzi ikiwamo uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, bila kuwa na katiba itakayolifanya Jeshi la Polisi kutenda haki kwa raia na vyama vyote vya siasa kwa wakati wote na bila kuwa na vyombo huru vya habari hatuhitaji kuwa na maarifa ya elimu ya nyota kuweza kutabiri machafuko ya kisiasa yakayopelekea madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa nchi yetu.

  Maana, Watanzania kwa asili ni watu watulivu na wenye kupenda amani. Watanzania hawa kwa kawaida watakwenda kwenye mikutano ya siasa na watawasikiliza wanasiasa. Na siku ya kupiga kura watakwenda kupiga kura kwa amani.
  Ni vyama vya siasa na baadhi ya wanasiasa ndio wenye kutumia hila , ghilba na hata , kwa kutumia fedha, hutokea wakagharamia vurugu ili baadae kwa kuvilipa vyombo vya habari na hata baadhi ya wana habari, watajenga taswira ya uongo juu ya uwepo wa vurugu na hata kusukuma lawama kwa wapinzani wao wa kisiasa.


  Jeshi la Polisi nalo kwa ama kutojiamini kwa baadhi ya viongozi wa jeshi hilo au kusukumwa kisiasa, nao wataingia kwenye mapambano na wafuasi wa vyama na hata viongozi wa vyama, hapo ndipo chuki inapozaa chuki na silaha inapozaa silaha, ni balaa.

  Uwepo wa Tume ya Uchaguzi isiyo huru unapelekea tume kuwa na viongozi wasiojiamini hivyo kuendesha shughuli za uchaguzi katika hali ya mashaka na hata kuegemea upande mmoja.


  Katika nchi zetu hizi siku zote tabu inakuja kwenye shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo. Joseph Stalin wa Urusi ya zamani alipata kutamka ‘Katika uchaguzi wowote ule, mpiga kura si anayeamua matokeo, bali mhesabu kura’’

  Tunachojifunza kwenye kauli hiyo ya Stalin ni ukweli, kuwa kikubwa katika mchakato wa uchaguzi ni uwepo wa imani kwa wanaondesha mchakato huo.

  Kama vyama vya siasa na hata wapiga kura watakosa imani na aliyeteuliwa kuendesha mchakato na hata kuhesabu kura zao, basi, matokeo ya chaguzi yanaweza kuwa chanzo cha vurugu za kisiasa.

  Hivyo basi, waTanzania wapenda amani watapenda hata kabla ya kupata katiba mpya ijayo, itungwe sheria itakayosimamia uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoanza na kazi ya kusimamia zoezi la kura za maoni ya ama kuikubali au kuikataa rasimu ya katiba itakayoletwa kwa wananchi baada ya Tume ya Katiba na Bunge la Katiba kumaliza kazi yake.

  Hilo la mwisho linawezekana, kama tuna dhamira za kweli za kisiasa. Kama tuna mapenzi ya kweli kwa nchi yetu tuliyozaliwa. Nahitimisha.

  Mungu Ibariki Afrika!
  Mungu Ibariki Tanzania!

  Maggid Mjengwa,
  Iringa.
  .

  ( Makala haya yamechapwa kwenye gazeti la Mwananchi leo Jumapili)
  .
   
 2. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #2
  Dec 4, 2011
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,547
  Likes Received: 18,210
  Trophy Points: 280
  Asante Maggid, well said!.
  Tusubiri kukiona "Cha mtema kuni" na " Kilichomyoa Kanga Manyoya"!.
   
 3. Domhome

  Domhome JF-Expert Member

  #3
  Dec 4, 2011
  Joined: Jun 28, 2010
  Messages: 1,986
  Likes Received: 1,043
  Trophy Points: 280
  Ni vyema msafiri yeyote yule anapokosea njia, tiba siyo kuendelea na safari ili kubahatisha kama utafika bali ni Kurudi na Kuanza Safari Upya.

  Kwenye hili la Katiba sisi tumepotea njia, tunapaswa kurudi na Kuanza Upya. Kazidi Kusonga mbele ni Kuendelea Kupotea. Tumepotea Katika hili tukubali ama tusikubali!!
   
 4. fige

  fige JF-Expert Member

  #4
  Dec 4, 2011
  Joined: Jul 4, 2010
  Messages: 376
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nanukuu

  'Wengine wanadhani kuwepo kwa katiba mpya ndiko kutakitoa ccm madarakani'
  Ben Mkapa akihojiwa na bbc jana.

  Mkuu hiyo ndiyo hofu yao kuu, kwa jinsi hiyo ndiyo maana wameamua kwa makusudi kuukwaza mchakato mzima.
   
 5. S

  SHIMBONONI Senior Member

  #5
  Dec 4, 2011
  Joined: Sep 17, 2011
  Messages: 112
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  Very analytical! Uchambuzi huu unaonesha na kudhihirisha mapenzi ya dhati ya nchi yetu. Well said Bro Maggid.
   
 6. l

  lutondwe Senior Member

  #6
  Dec 4, 2011
  Joined: Dec 20, 2010
  Messages: 150
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Natamani tuwe na waandishi wal aina ya Maggid hata hamsini tu watatufikisha pale tunapotamani kufika.Nchi yetu hii ni yetu sote bila kujali itikadi zetu kisiasa.Mimi binafsi ni shabiki na kamanda wa kweli katika moja ya vyama vya siasa hapa Tanganyika ila katika hili niwe mkweli hoja ya mwandishi Mjengwa iko juu.:director::director:
   
 7. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #7
  Dec 4, 2011
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,547
  Likes Received: 18,210
  Trophy Points: 280
  lutondwe, mbona waandishi kama hawa tunao wengi zaidi ya 100!.

  Humu tuu JF peke yake tunao zaidi ya 30!.
   
 8. Filipo

  Filipo JF-Expert Member

  #8
  Dec 4, 2011
  Joined: Jan 6, 2011
  Messages: 9,330
  Likes Received: 210
  Trophy Points: 160
  "Nchi hii ni yetu sote"
  Asante sana!
   
Loading...