Mbunge wa Monduli (CCM) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbunge wa Monduli (CCM)

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Mar 30, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Mar 30, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Nimesoma na kusikiliza vyombo vya habari, Machi 9, mwaka huu, vikimkariri Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Ngoyai Lowassa, akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Loksale kilichopo jimboni humo, mkoani Arusha.
  Alikuwa akiwashukuru wananchi kwa kupiga kura zilizochangia ushindi wa Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana.
  Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu ´aliyeachia ngazi´ baada ya kufadhaika sana, kudhalilishwa sana na kuonewa sana, alizungumzia mambo mengi, kubwa zaidi ni kuhusu dhana ya uchanga wa taifa hili.
  Akakaririwa na gazeti la serikali la HabariLeo, akisema “kwa sasa kuihukumu CCM (Chama Cha Mapinduzi) ni mapema mno na hiyo sijui kama itakuwa na maana kwa jamii…”
  Akaendelea, “iwapo CCM itashindwa kutekeleza kwa vitendo yaliyoahidiwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ndipo chama hicho kinapaswa kuhukumiwa katika uchaguzi ujao na si sasa kwa maandamano.”
  Katika kuisimika dhana ya taifa bado ni changa, Lowassa akawaambia wananchi wa Monduli, wakiwa ni miongoni mwa mamilioni ya wanaokabiliwa na ‘umaskini wa kutupa’, kwamba atavalia njuga ahadi alizozitoa, zikiwemo za upatikanaji wa umeme, barabara, maji na elimu.
  Hivi kwa mtu anayeijua historia pevu ya uongozi wa Lowassa akiwa Mbunge wa siku nyingi, ana mamlaka gani ya kimaadili kuendelea ‘kuwadanganya’ wananchi hao kwa ahadi za maji, umeme, barabara na elimu?
  Si nia yangu kumjadili Lowassa ninayemheshimu kwa utumishi wake, mwanasiasa anayetajwa kuwa na mbio zenye kasi kubwa ya kuwania urais mwaka 2015. Ninaijadaili dhana yake iliyojikita katika uchanga wa taifa hili kiasi cha kuamini ni mapema mno kuihukumu CCM.
  Bila shaka, Lowassa anaposema ni mapema mno kuihukumu CCM, ana maana pana inayogusa maslahi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo kwa mujibu wa Katiba, serikali iliyopo madarakani ni mtekelezaji wake mkuu.
  Tangu nchi ilipopata uhuru Desemba 9, 1961 na baadaye Tanganyika kuungana na Zanzibar Aprili 26, 1964, CCM ama watangulizi wake (TANU na ASP), ni kiasi cha nusu karne sasa wamekuwa madarakani.
  Wameziongoza sehemu mbili za Muungano wa Tanzania huku ahadi zikizotolewa kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine; zinajirudia.
  Hivyo anapotokea mwanasiasa mwandamizi, kuwataka wananchi wasiihukumu CCM kwa kuwacheleweshea maendeleo (eti) kwa sababu ni mapema mno, inakuwa haiingii akilini. Anakuwa haeleweki, hatafsiriki, haaminiki na hakubaliki kwa namna iwayo yote!
  Hivi Lowassa anataka ipite miaka mingapi katika karne za kidunia, ndipo ikubalike kwamba watawala wetu wameshindwa kufikia matarajio ya umma?
  Vipite vizazi vingapi, ndipo dhamira za watawala ambao miongoni mwao wamegubikwa na ubinafsi, nia za uporaji wa mali na rasilimali za umma, waamini kwamba wameshindwa?
  Wananchi wanapoelezea hisia za kuihukumu CCM (ingawa kwa Lowassa anaona ni mapema mno), wanaashiria kukichoka chama hicho, kwa maana halisi ya kuchoka. Viongozi wanaweza kuwahutubia kama alivyofanya Lowassa kule Loksale, lakini wasikilizaji wakawepo kimwili tu.
  Kama wangekuwa na shughuli nyingine ya kiuchumi na kijamii, bila shaka viongozi wangekosa watu wa kuwasikiliza kiasi cha kulazimika kufanya mikutano yao ndani ya chumba cha moja ya madarasa yasiyokuwa na madawati katika maeneo yao.
  Hali hiyo inaashiria kuwa watawala wanapaswa kuepuka kauli danganyifu, badala yake waguswe na umaskini ama kadhia zinazowakabili watoto wa kike na kiume, wanawake na wanaume wa nchi hii.
  Vijana walio mamilioni kwa hesabu yao hapa nchini, maarufu kama wamachinga, hawatokani na kukosa uwezo, bali fursa ambazo kama wangezipata ikiwa pangekuwa na usawa katika matumizi ya rasilimali zilizopo, wangekuwa hazina ya taifa.
  Kwa mfano miongoni mwa hao, nina uhakika wapo wenye uwezo kuwazidi ama kulingana na Fred Lowassa au Ridhiwan Jakaya Kikwete. Wapo wenye uwezo kulingana ama kuwazidi vijana waliopo Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
  Lakini wamekosa fursa za kujiendeleza kielimu, wazazi ama walezi wao walishindwa kumudu gharama kutokana na umaskini, hata kama miongoni mwao wanaishi kandoni mwa migodi ya dhahabu, sekta ambayo kutokana na rushwa, mikataba yake ikabainika kuwa na kasoro kadha wa kadha.
  Kama watawala, tangu walipoingia madarakani na hatimaye kupokezana wakiwa ndani ya TANU, ASP na baadaye CCM, wangeendeleza dhana ya Tanzania kuwa mali ya Watanzania, ni dhahiri kwamba nchi ingepiga hatua na kauli kama ya Lowassa, zisingekuwa na nafasi ya kutamkwa hadharani.
  Yapo mataifa ambayo kumbukumbu zinaonyesha yalikuwa na hali sawa za kiuchumi na Tanzania mwaka 1961, lakini kutokana na watawala wake kuweka mbele maslahi ya umma badala ya kufikiria ubinafsi, ufisadi, ubunge na urais, hivi sasa yamekuwa wafadhili wetu!
  Hata tunapoiangalia China ambayo imeikamata Afrika kama sehemu muhimu ya soko lake la kiuchumi, haikuwa hivyo wakati tulipopata uhuru.
  Mtaalamu wa masuala ya uchumi wa China ambaye pia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Inter Region Economic Network (IREN) yenye Makao Makuu yake jijini Nairobi, Kenya, James Shikwati, anasema ili kufika hatua hiyo, China iliwekeza katika kutafuta fursa za kiuchumi kwa watu wake.
  Watawala wao wakajenga mifumo na mazingira bora ya ndani, na baadaye kupitia kwa wana-diplomasia wakiwemo mabalozi, wakatafuta fursa za nje kama vile Afrika. Hivi sasa wameenea kila pembe ya bara hili.
  Kinachoelezwa ni kwamba kila mkoa wa China umepewa nchi katika Afrika, ndio maana utakuta Wachina waliopo Tanzania hawatoki sehemu moja na waliopo Kenya, Uganda, Afrika Kusini ama popote pale…ni mkakati.
  Je, kupitia dhana kwamba ni mapema mno kukihukumu chama hicho kwa kushindwa kuchagiza kasi ya maendeleo ya Tanzania, Lowassa anataka kuwathibitishia Watanzania wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 40, kwamba itawachukua karne ngapi kwa CCM kufikia matarajio ya umma?
  Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE ambaye hivi sasa yupo nchini Kenya. Anapatikana katika simu namba +255-754+691540,
   
Loading...