tpaul
JF-Expert Member
- Feb 3, 2008
- 23,519
- 21,549
NA RAMADHAN LIBENANGA, MOROGORO
MBUNGE wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood (CCM), amezuia uvunjwaji wa nyumba tisa za wakazi wa Mtaa wa Nyerere, Manispaa ya Morogoro kwa kile kilichodaiwa wananchi hao wamevamia eneo hilo.
Akizungumza na wananchi hao jana, Abood alisema amesitisha ubomoaji kwa kuwa hakuna taratibu zilizofuatwa kabla ya kubomoa nyumba hizo.
“Hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika bila kufuata sheria na taratibu zake. Wananchi hawakuwa na taarifa yoyote kuhusu zoezi hilo, hivyo itabidi wahusika wasitishe mpaka mwafaka utakapopatikana,” alisema Abood.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mafisa, Rajabu Wanyamage, alisema hakuna taarifa zozote ofisini kwake kuhusu mgogoro huo na kwamba wameshangaa nyumba hizo kutaka kubomolewa bila wao kushirikishwa huku Jeshi la Polisi likisimamia.
Wakizungumza katika eneo hilo, mmoja wa wananchi wanaomiliki nyumba iliyotaka kubomolewa, Maria Bakar, alisema alishangaa kuona nyumba yake ikitaka kubomolewa bila yeye kupewa taarifa.
“Nilikuwa nimekaa na familia yangu nikasikia greda lipo nje linataka kubomoa nyumba kwa madai kwamba nimevamia kiwanja cha Temba.
“Mimi nipo hapa kwa miaka zaidi ya kumi na sijapewa taarifa yoyote ile kuhusu kuwepo kwa mgogoro wa eneo hili, kwa hiyo sikubaliani na ubomoaji huo,” alisema Bakar.
“Kitendo hiki wanachotaka kutufanyia ni uonevu kwa sababu nilinunua eneo hili zamani na kuanza ujenzi pamoja na wenzangu,” alisema.
CHANZO: MTANZANIA