Mbunge: Nchi haitakalika

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Mbunge: Nchi haitakalika

Mwandishi Wetu Agosti 20, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

Vigogo kuanza kulipana fadhila

Asema Tanzania itakuwa hatari kuishi

MBUNGE wa Kishapu (CCM), Fred Tungu Mpendazoe anaamini Tanzania inaweza kuwa mahala hatari kuishi iwapo Serikali haitashughulikia kwa umakini masuala ya ufisadi na kwamba kuna hatari Rais Jakaya Kikwete aliyeko madarakani akaanza kulipa fadhila kwa matajiri waliokifadhili chama chake au yeye binafsi wakati wa uchaguzi.

Akirejea kauli ya mwanafalsafa Albert Einstein, Mpendazoe anasema: "yawezekana Tanzania patakuwa mahali pa hatari kuishi, lakini haitatokana na ufisadi bali itatokana na Serikali kuchelewa kuchukua hatua au kutochukua hatua dhidi ya ufisadi unaofanyika."

Alikuwa akichangia wiki iliyopita bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, iliyopitishwa na Bunge wiki hiyohiyo, katika mchango uliojikita zaidi katika tatizo la ufisadi.

Alisema kwamba kutokana na kuwapo na ufisadi tayari kumejionyesha mwenendo usioridhisha hususani wa kukua kwa pengo kubwa kati ya matajiri na masikini huku uendeshaji siasa ukitekwa na matajiri.

Uporwaji wa uchumi unaofanywa na kikundi cha watu wachache unatakiwa kudhibitiwa kikatiba kama tunataka nchi yetu isalimike. Katika kitabu cha uongozi wetu na hatima ya Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anasema: " Utajiri katika Tanzania unaweza kupatikana kutokana na rushwa kwa watumishi wa umma au kutokana na wafanya biashara ambao wanawania nafasi za kisiasa ili wawe wadeni wa Rais aliyeko madarakani," alisema.

Alisema tafsiri ya maneno hayo ya Mwalimu Nyerere ni kwamba Rais aliyeko madarakani, itabidi alipe fadhila kwa matajiri waliokifadhili chama chake au waliyemfadhili yeye binafsi wakati wa uchaguzi.

"Miaka 14 iliyopita Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyaona hayo na sasa ni dhahiri kuna dalili kwamba yatatokea," alisema Mpendazoe ambaye katika siku za karibuni amekuwa mmoja wa wabunge waliochachamalia tatizo la ufisadi serikalini.

Anasema kwamba ufisadi na rushwa ni vitu hatari kwenye uchaguzi, na kwamba ufisadi unaigawa nchi vipande ikiwa ni pamoja na kuwa na wananchi walio na utajiri mkubwa huku wengine wakiwa na umasikini wa kutupa wakati taifa lina rasilimali na utajiri mkubwa.


Hata hivyo, Mpendazoe anasema kuwa, si kila tajiri ni fisadi, akiongeza kuwa wapo wananchi waliotajirika kwa haki, japokuwa pia, kuwa ni kweli si kila tajiri anaweza kuongoza, kwani kwa kuwa utajiri pekee hauwezi kuwa sifa ya kuongoza kwa maana ya kuwatumikia wananchi.

"Naomba kumwuliza Waziri, Je haupo umuhimu sasa wa kuingalia Katiba yetu na sheria zetu ili tuone kama inajitosheleza kukabiliana na changamoto hizi?", alihoji Mbunge huyo.

Alisema katika mazingira ya sasa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha, na kwamba kusipokuwapo na umakini, taifa litawekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo.

"Unaweza kufadhiliwa na mtu ili anunue uongozi, ni vyema sasa tulizungumzie. Mwenendo ulioonekana kwenye chaguzi zilizopita, fedha nyingi zinatumika kwenye kampeni katika vyama vya siasa na baadhi ya wagombea," alisema Mpendazoe na kuongeza:

"Ipo haja ya kuweka utaratibu ulio wazi kwa vyanzo vya fedha na kiasi cha fedha kwa vyama vya siasa na wagombea kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza."

Alisema katika mazingira ya rushwa wanaweza kupatikana viongozi wasio na nia ya kusaidia wananchi na wasio na uwezo wa uongozi na nchi itaporomoka kiuchumi na kimaadili, na hivyo kuhoji, "je, wizara imechukua hatua gani mpaka sasa kuhusiana na mtazamo ambao Rais ameuonyesha miaka mitatu ikiwa imepita tangu mwaka 2005?"


Akimnukuu aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Jaji Joseph Sinde Warioba, kuhusu kuwapo kwa pengo kati ya matajiri na masikini, Mpendazoe alisema ni lazima Serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.

"Warioba alisema katika vyombo vya habari mwaka 2000 Aprili, naomba kunukuu. Kuna mwenendo usiopendeza wa kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya matajiri na masikini. Siasa inatekwa na matajiri. Ufisadi na rushwa ni vitu muhimu kwenye uchaguzi. Ufisadi unaigawa nchi vipande", alisema akimnukuu Jaji Warioba.

Alisema wako wananchi waliopata utajiri kwa haki, japokuwa pia ni rahisi ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuurithi ufalme wa Mungu lakini alisisitiza kwamba si kila tajiri ana uwezo wa kuongoza.

"Mheshimiwa Rais, Jakaya Kikwete alipokuwa analizindua Bunge, tarehe 30 Desemba, alisema kuhusu mawazo ya kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Tusipokuwa waangalifu nchi yetu inaweza kuweka rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Maana unaweza ukafadhiliwa na mtu ili anunue uongozi. Ni vema sasa tuizungumze hili na tulishughulikie suala hili," alisema akimnukuu Rais Kikwete alipozindua Bunge.

Alisema kuna hatari ya nchi kuwekwa rehani kwa matajiri kwa maana ya Serikali kuongozwa na matajiri wachache ambao watalinda maslahi yao bila kujali wananchi masikini walio wengi.

"Hivyo haitawajibika kwa wananchi bali italinda maslahi ya matajiri. Maana yake matajiri watanunua kila haki ya mwananchi. Ina maana demokrasia itakoma, udikiteta utaanza na wananchi watapata shida kubwa sana," alisema.

Alisema kuna mwenendo ambao ulionekana kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 ambako fedha nyingi sana zilitumika kwa vyama vya siasa na wagombea wengine.

"Ipo haja sasa ya kuweka utaratibu wa kuweka wazi kiasi cha fedha zitakazotumika kwenye uchaguzi kwa vyama vya siasa na wagombea wenyewe. Tusipofanya hivyo ni rahisi sana nchi yetu, majimbo yetu, kata zetu, tutaziweka rehani kwa matajiri," alisema.

Alisema watapatikana viongozi wasio na nia ya kuwatumikia wananchi na wasio na uwezo wa kuongoza kwa maelezo kwamba nchi itaporomoka kiuchumi na kimaadili.

"Wizara imechukua hatua gani mpaka sasa kuhusiana na mtazamo wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete tangu alipozindua Bunge miaka mitatu iliyopita?" alihoji Mpendazoe.

Akinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mpendazoe alisema, "wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka kutoka kwa wananchi na Serikali itawajibika kwa wananchi."

"Serikali inayopata madaraka kutoka kwa wananchi na Serikali inayowajibika kwa wananchi ni Serikali ya kidemokrasia. Maana yake Serikali inachaguliwa na watu, ni Serikali inayoongozwa na watu. Ni Serikali inayowajibika kwa watu. Lakini kutokana na mwenendo uliopo na unaoendelea sasa, hakika kama hatutachukua hatua madhubuti, Serikali haitachaguliwa na watu itachaguliwa na matajiri. Serikali haitawajibika kwa wananchi, itawajibika kwa matajiri," alisisitiza na kuongeza;

"Wataalam wa sayansi wanasema, kutokana na uporaji wa uchumi unaofanywa na kikundi cha watu wachache, kwa njia mbalimbali za ufisadi, ipo hatari ya kuibuka matabaka mbalimbali katika jamii. Tabaka la kwanza ni la matajiri hawa wachache wanaomiliki katika nchi yetu. Tabaka hili kwa Kigiriki linaitwa Origaki. Tabaka hili la Origaki litakuwa na watu wake wateule wanaojiona bora katika jamii. Watu ambao wameingizwa na Origaki kwenye sehemu muhimu za nchi kama mabenki na kwenye makampuni yaliyowekeza hapa nchini. Kikundi hiki cha watu wachache wanajiona ni bora katika jamii, wanaitwa aristocracy.

"Vile vile kuna tabaka jingine, kutokana na aristocracy kuna tabaka jingine litaibuka la watu ambao wana tamaa ya madaraka, wana tamaa ya makubwa. Kikundi hiki kinaitwa timocracy, timocracy ni kikundi cha watu ambao hawana msimamo wowote kwa sababu ya tamaa. Wako tayari kuunga mkono hoja zote za origaki na aristocracy. Kwa hiyo ni watu ambao ni hatari sana. Lakini kundi la mwisho ni la watu masikini. Wananchi maskini ambao wanaishi kwa matumaini ya kupata maisha bora na inawezekana wasiyapate," alisema akipigiwa makofi na wabunge.

Alisema kwa sasa wanasayansi wa jamii wanasema matabaka haya yameanza kutokea hata Tanzania kwa maana ya kwamba upo uwezekano kwa Serikali kutochaguliwa na watu na hivyo haitaoongozwa wala haitawajibika kwa watu.

Kutokana na hali hiyo, Mpendazoe alisema demokrasia itakoma na udikiteta utashamiri hali ambayo itaifanya Tanzania kuwa mahali pa hatari sana kuishi hali ambayo alisema haitokani na uovu unaotendeka lakini inatokana na watu wanaoangalia uovu ukitendeka na hawachukui hatua.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali ichukue hatua mapema na madhubuti dhidi ya ufisadi wote uliotokea nchini. Ufisadi wa EPA. Ufisadi wa MEREMETA unaotajwa na ufisadi mbalimbali ambao tumeusikia. Hatua zisipochukuliwa na za madhubuti kama alivyosema Einstein, Tanzania itakuwa mahali pa hatari sana kuishi," alisema.

Kauli hiyo ya Mpendazoe imekuja huku wanasiasa wakongwe wakiendelea kuinyoshea vidole Serikali ya Rais Kikwete kwa jinsi inavyosita kuchukua hatua kwa watuhumiwa mbalimbali wa ufisadi wakiwamo wanasiasa wa sasa na wa zamani.
 
Hawa wabunge wa CCM wanafiki wakubwa. Labda kutoa Ana Kilango. Wengine wanafiki sana, wanajifanya wanakosoa sana serikali inapofika wakati wa kupitisha kitu hata kama hakina maslahi kwa wananchi unasiki,"naunga mkono hoja kwa 100%", wapinzani wanapopinga mambo xa msingi wa CCM wanawazomea. Acheni unafiki nyie wabunge wa chama tawala. Uwezo wa kuiadabisha serikali mnao kutokana na wingi wenu, sasa kwa nini mnaianpalia inafanya upupu halafu mnabwabwaja bungeni ili watanzania tuwaone kuwa mnatutetea. Waongo wakubwa nyie.
 
mi simini kabisa kama urafiki wa JK na EL umekufa kwahiyo siamini hata kidogo kama JK atamgunga jela shogaye na kumbuka JK ndie aliesimama kama baba wa bi harusi (mtoto wa EL) na kutoa nasaha .....
 
Back
Top Bottom