Mbunge maarufu CCM matatizoni

Kitia

JF-Expert Member
Dec 2, 2006
418
74
Mbunge maarufu CCM matatizoni

na Martin Malera


MBUNGE wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM), anasakwa na polisi kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya sh milioni 191 kwa njia ya udanganyifu, kutoka kwa mfanyabiashara Joseph Mushi.

Mfanyabiashara huyo ambaye ni Mtanzania anayeishi China kwa shughuli za kibiashara, amewasili nchini na kupitia mawakili wake, anakusudia kufungua kesi ya wizi kwa njia ya udanganyifu na tayari Msindai amefunguliwa RB namba OB/RB/15896/07.

Mbali ya madai hayo kufikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo juzi aliwasilisha barua yake ya malalamiko katika ofisi ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, akitaka ofisi hiyo imsaidie kupata haki yake kutoka kwa mbunge huyo.

“Januari mwaka huu, nilikutana na Mh. Msindai na kunishawishi kuwa kutokana na nafasi yake ya ubunge na ushawishi alionao, anaweza kupata tenda (zabuni) ya kusambaza vibao vya shule katika halmashauri mbalimbali. Baada ya kuangalia gharama, niliweza kutuma kontena tatu za vibao hivyo na naamini ameshasambaza na kulipwa fedha zake kutoka kwenye halmashauri alizosambaza.

“Nasikitika kukuambia kuwa Msindai amegoma kunilipa pesa zangu na tangu Agosti 22 mwaka huu, amekuwa akinipa ahadi zisizotekelezeka na hakuna namna naweza kupata pesa zangu.

“Nimeamua kukuandika barua hii nikiamini kuwa ofisi yako inaweza kunisaidia kupata fedha zangu,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Oktoba 8 iliyogongwa muhuri wa Ofisi ya Bunge kuonyesha ilipokewa na Ofisi ya Bunge Jumanne wiki hii.

Vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika vinadai kuwa Msindai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, alifahamiana na mfanyabiashara huyo alipokuwa kwenye ujumbe wa ziara ya Wabunge wa Tanzania nchini China, Januari mwaka huu, ambapo alimshawishi kufanya naye biashara.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, inadaiwa kuwa, Msindai alimshawishi mfanyabiashara huyo kuingia naye mkataba wa kusambaza vibao vya wanafunzi kutoka China.

Kutokana na makubaliano hayo kati ya Msindai na mfanyabiashara huyo, Msindai alipokea kontena tatu za vibao hivyo kupitia kampuni ya Msindai ya MSIMU Co na vibao hivyo vilikuwa na thamani ya sh milioni 191.

Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya kontena hizo kuwasili nchini kwa nyakati tofauti, Msindai kupitia kampuni yake ya MSIMU, ilianza kazi ya kusambaza vibao hivyo katika halmashauri kadhaa nchini.

Katika kuthibitisha kupewa zabuni hiyo, Kampuni ya MSIMU ilikabidhiwa hati ya idhibati namba 631 Januari 8, mwaka huu ya Wizara ya Elimu na Utamaduni.

Akizungumza na Tanzania Daima, Mushi alisema tangu kuwasili kwa kontena hizo na biashara kufanyika vizuri, hajawahi kupata malipo na amejitahidi bila mafanikio kumtafuta Msindai ili alipwe pesa hizo.

“Tangu nimefika hapa Dar es Salaam, nimejitahidi sana bila mafanikio kumtafuta Mzindai, lakini mara ya mwisho nilipompata kwenye simu yake ya mkononi alinijibu kwa kejeli kuwa niende mahakamani kutafuta haki yangu,” anasema Mushi.

Hata hivyo, alisema kuna wakati Msindai aliwahi kumtumia muhtasari wa kikao cha Kampuni ya MSIMU unaoonyesha mchanganuo wa mgawo wa vibao hivyo, wilaya zilizosambazwa, kiasi cha fedha kilichokusanywa na matumizi ya MSIMU wakati wa kazi ya kusambaza vibao hivyo.

Kwa mujibu wa muhtasari wa kikao hicho cha kujadili mapato na matumizi ya kampuni hiyo, kilichoongozwa na Msindai mwenyewe kama mwenyekiti, ambao Tanzania Daima ina nakala yake, vibao hivyo vilisambazwa katika halmashauri tisa.

Halmashauri hizo ni pamoja na Moshi, Mbarali, Mbeya, Kilosa, Bagamoyo, Iringa, Mufindi, Handeni na Kilombero na kukusanya sh 101,649, 800. Hata hivyo Kampuni ya MSIMU ilikuwa haijapokea malipo kutoka halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo na Kilombero.

Idadi ya vibao na kiasi cha fedha kilichokusanywa kutoka kwenye halmashauri hizo kwenye mabano ni Moshi vibao 1459 (sh 4,375,000), Mbarari vibao 5,000 (sh 13,000,000), Mbeya vibao 3,650 (9,125,000), Kilosa vibao 9,537 (sh 25,750,000), Bagamoyo vibao (sh 14,125,000), Iringa vibao 5900 (sh 18,750,000), Handeni vibao 6913 (sh 15,899,000) na Kilombero vibao 5323 (sh 13,082,500.)

Kwa upande wa matumizi, muhtasari huo unaonyesha kuwa kampuni hiyo ilitumia sh milioni 131, ikiwemo asilimia 10 ya kila fedha zilizotolewa na wilaya kununua vibao hivyo, na sh milioni moja kama asante kwa wizara iliyotoa tenda hiyo.

Alipohojiwa na Tanzania Daima juu ya madai hayo, Msindai alisema kwa kifupi kuwa, analijua suala hilo na kwamba liko polisi, lakini hawezi kulizungumzia kwa madai kuwa atakwenda kukutana nalo polisi.

“Hilo suala liko polisi, nami niko njiani kuja Dar es Salaam, hivyo nitakutana nalo polisi ila siwezi kuzungumzia suala hilo ila nashukuru kwa kunipigia,” alisema Msindai na kukata simu.

Hata hivyo Spika Sitta hakuweza kupatikana jana kuthibitisha kupokea barua hiyo na msaada atakaoweza kutoa kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapata haki yake.
 
Kila mtu ndani ya CCM ni Mfanyabiashara? OOOh naikumbuka ile CCM ya Marehemu Mwalimu,Mzee Abood Jumbe na Msekwa ule mwaka 1977 walipotuambia kuwa wameunda Chama cha Wafanyakazi na Wakulima!,Naona CCM hii ya sasa ina mwelekeo Mpya!!!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom