Mbunge ashitakiwa kwa Pinda

Msharika

JF-Expert Member
May 15, 2009
947
69
MBUNGE wa Bukene, Teddy Kasela-Bantu (CCM), amejikuta katika wakati mgumu baada ya wakazi wa jimbo hilo kumshitaki kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba ametwaa ekari 40 za ardhi katika kijiji cha Mwalyenze, ili kujenga kiwanda bila kuwalipa fidia.

Kasela-Bantu pia alishitakiwa kuwa, tangu alipochaguliwa ubunge haonekani jimboni na hivyo hajatekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni ukiwamo ukarabati wa barabara na ujenzi wa shule.

Mkazi wa kijiji hicho, Antony Machibya, amemwambia Waziri Mkuu kwamba, Kasela-Bantu na Serikali ya kijiji walitwaa ardhi hiyo bila kushirikisha wananchi wala kuwalipa fidia yoyote.

“Serikali imechukua ardhi yetu ili kujenga shule ya sekondari, shule ya mchepuo wa Kiingereza ya CFS ya Kitindi na kiwanda cha Mbunge bila kutushirikisha na kutulipa fidia kwa maeneo yetu,” amesema Machibya.

Mashitaka hayo yalimfanya Waziri Mkuu, kumwita Kasela-Bantu atoe maelezo kuhusu tuhuma hizo.

Kabla ya Mbunge kujieleza,Pinda alisema utaratibu unaelekeza kuwa Serikali au mtu yeyote anapotaka kuchukua ardhi ambayo inamilikiwa na watu, ni lazima yawepo mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

“Unapochukua ardhi ya mtu yeyote zungumza naye, mpe maelezo ayaelewe kama ni Serikali inataka kujenga shule, zahanati, soko au miundombinu yoyote yenye maslahi kwa wananchi na inapaswa kuwaelimisha wananchi hao ili waridhie ardhi yao kuchukuliwa ili itumike kwa huduma hizi muhimu kwa jamii.

“Inapokuwa ni mtu binafsi anataka kujenga kiwanda au shule ili aje atutoze ada au kitu kingine chochote kile hali ni tofauti. Mtu huyu ni lazima azungumze na wamiliki wa ardhi na ni lazima awalipe wahusika iwe ni fidia au kifuta jasho,” amesema Waziri Mkuu.

Kuhusu Mbunge huyo kutoa ahadi hewa na kutoonekana jimboni kwa muda mrefu, swali lililoulizwa na Salum Mabula, Waziri Mkuu alisema inawezekana Mbunge alitoa ahadi nyingi zilizokuwa nje ya uwezo wake, alipokuwa akiomba kura, lakini kwa upande wa CCM ahadi ilizoahidi ni zile zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi.

Alipotakiwa kutoa maelezo na Waziri Mkuu kuhusu kutwaa ekari hizo 40, Mbunge Kasela-Bantu alisema hivi karibuni kulifanyika harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Bukene, ambapo serikali ya kijiji cha Bukene iliahidi kuwa mtu yeyote atakayetoa mifuko miwili ya saruji, atapewa ekari moja ya ardhi kama zawadi kutokana na mchango wake.

“Kutokana na hamasa hiyo, mimi nilitoa mifuko 80 ya saruji nikapewa ekari 40 za ardhi. Hata hivyo, Serikali ya kijiji ilipotugawia eneo hilo la ardhi wananchi walilalamika kuwa ni maeneo yao.

“Kutokana na malalamiko hayo ilibidi tuiulize Serikali ya kijiji kulikoni, lakini hadi sasa ardhi hatujapewa wakati saruji yangu imeshatumika kujengea shule,” alisema Kasela-Bantu na kumwomba Ofisa Mtendaji kumsaidia kutoa maelezo ya ziada kwa Waziri Mkuu ili kumpa picha kamili ya suala hilo.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji huyo ambaye hakutaja jina lake alimwambia Waziri Mkuu kuwa kutokana na utata wa suala hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ilitoa waraka wa kuzuia ugawaji wa ardhi kwa Mbunge huyo na watu wengine waliogawiwa ardhi hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, aliwauliza wakazi wa kijiji cha Shila kama wanampenda Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii na wanakijiji hao walijibu kwa sauti “tunampenda”.

“Kwa kweli nimeamini kuwa mnampenda sana Selelii … sijui ni kwa sababu anapambana na ufisadi? Lakini hata mimi nampenda sana Selelii ni rafiki yangu na hivi karibuni tumeamua kumpa Halmashauri ya Mji wa Nzega ili muwe na halmashauri mbili ya Mji na ya wilaya ili zote mbili ziwe na bajeti yake, ili kuharakisha usukumaji wa maendeleo,” alisema Pinda.
 
Back
Top Bottom