Mbunge aliyemtwanga msaidizi wake atajwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
Mbunge aliyemtwanga msaidizi wake atajwa

Azzan%20-kinondoni.jpg

Mhe. Idd Azzan

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima

MBUNGE mmoja wa Wilaya ya Kinondoni, anayedaiwa kumpiga msaidizi wake wa zamani na kumjeruhi, sasa amejulikana.

Mbunge huyo ni Idd Azzan, wa Jimbo la Kinondoni, anadaiwa kumpiga msaidizi wake wa zamani, Shawej Mkumbuli, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kata ya Magomeni.

Sababu kubwa ya ugomvi huo, imeelezwa kuwa ni hofu ya uchaguzi, ambapo mbunge huyo anadai Shawej amekuwa akijenga mtandao na kuandaa mkakati maalumu wa kumng’oa katika jimbo lake, kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima juzi, Shaweji alisema ugomvi kati yake na mbunge huyo, ulitokea Jumatano iliyopita, katika eneo la wazi linalotumika kuegeshea magari, katika ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Akiwa ameongozana na Katibu Mwenezi wa kata hiyo, Juma Matandika na viongozi wengine waliodai kushuhudia ugomvi huo, Shawej alisema siku hiyo kulikuwa na uchaguzi wa naibu meya, ambapo mbunge huyo na naibu meya aliyemaliza muda wake, Tulian Bujugo, walikuwapo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni.

Alisema katika uchaguzi huo, yeye (Shewej) pamoja na viongozi wengine wa kata hiyo, walikuwa wakimpigia debe Diwani wa kata yao, Bujugo, ili atetee kiti chake lakini alishindwa na badala yake, Diwani wa Kata ya Goba, Ibrahim Kisoki, ndiye aliyeibuka mshindi.

“Sisi tulikuwa tumekaa kwenye sehemu ya wageni ukumbini. Wakati kura zinaendelea kuhesabiwa, ghafla nilimwona mgombea wetu ambaye muda wote alikuwa amekaa jirani na Idd Azzan, akitoka nje kwa haraka, nikaamua pia kutoka na kumfuata, lakini sikumwona.

“Badala yake nikakutana na viongozi wetu wengine wako nje, tukawa tunabadilishana mawazo, hasa baada ya kubaini kuwa mgombea wetu alikuwa anaelekea kushindwa.

“Tukiwa katikati ya mazungumzo, Idd Azzan, alikuja kuungana nasi na baada ya kusalimiana naye, akaanza kusema Shawej nimepata habari zako siku nyingi kuwa unanichimba, unanifitini eti una mgombea wako wa ubunge na unajenga mtandao wa kuniangusha,” alisema Shewej.

“Nilitaka kujibu, lakini alinibeza kwa kunitaka nisijibu chochote, lakini nami nikawa mbishi kutaka nijibu, ndipo ghafla alinirukia na kunipiga ngumi ya kichwa, kofi na kurusha teke ambalo lilinikosa.

“Kanipiga vibaya ndugu yangu, lakini sikutaka kurudishia, ingawa ninaweza kupigana naye, bahati nzuri viongozi niliokuja nao hapa ofisini kwako, walikuwapo, wakaamua kuingilia kati kuamlia ugomvi huo,” alisema Shaweji, huku akionyesha sehemu ya jicho na mkono, alivyodai kuumizwa.

Alisema malalamiko ya Azzan dhidi yake, amekuwa akiyasikia muda mrefu, lakini aliyapuuza kwa madai kuwa mbunge huyo ni mtu wake wa karibu, hivyo kama ana malalamiko angeweza kumwita na kuzungumza naye kindugu.

Shawej alimtaja mtu anayedaiwa kuanza kumpigia debe kuwa ni Tarimba Abbas, jambo ambalo alisema si la ukweli, bali inatokana na hofu ya mbunge huyo.

Akizungumzia uhusiano wake na Azzan, tangu mbunge huyo alipoingia madarakani, alisema amekuwa msaidizi wake, lakini ilipofika Mei mwaka jana, aliacha kazi hiyo kutokana na majukumu mengine aliyokuwa nayo kichama.

“Yeye mwenyewe Azzan, ndiye aliyeniambia kuwa sasa niache kuwa msaidizi wake kutokana na kazi nyingi nilizokuwa nazo kichama na tulikubaliana nimchagulie msaidizi mwingine na tangu wakati huo, nimekuwa na maelewano na mbunge wangu vizuri,” anasema.

Shawej alisema yeye ndiye aliyechangia Azzan kuwa diwani wa kata yao na hata baadaye kuwa mbunge, hivyo alielezea kushangazwa kwake na hatua ya mbunge huyo kutoa kipigo kwake kwa tuhuma zisizo za ukweli.

Hata hivyo, alisema kama mwenyekiti wa kata, ameamua kulipeleka suala hilo kwenye kamati ya siasa ya kata, inayotarajia kukutana wiki hii na kupeleka taarifa ya tukio hilo la aibu kwenye ngazi za juu za chama.

Mbali na kulipeleka kwenye chama, suala hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Magomeni, ambapo Idd Azzan, ndiye aliyefungua jalada la kudai kuwa ametukanwa na Shawej.

Habari kutoka ndani ya kituo hicho cha polisi, zilikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini mlalamikaji akiwa Idd Azzan, ambaye amedai kutukanwa na Shawej.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Tarimba juu ya kuwapo kwa malalamiko dhidi yake ya kutaka kuwania jimbo hilo, alikataa katakata huku akizitaka pande hizo mbili zinazotofautiana, zisimhusishe kwenye ugomvi wao.

“Mimi ndugu yangu haya mambo sijui yanatokea wapi. Ila wasinihusishe kwenye ugomvi wao,” alisema kwa kifupi Tarimba.

Juhudi za kumtafuta Azzan kwa simu yake ya mkononi, hazikufanikiwa, kwani muda wote ilikuwa imezimwa.

Azzan amekuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2005, baada ya kumshinda aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Peter Kabisa.
 
..Kama huyo mhanga wa kipigo ana ushahidi wa kutosha aende kwenye kwenye vyombo vya sheria haki itendeke...Nchi inamalizwa na mafisadi wao wanakandamizana mangumi mtaani??
 
ccm unatakiwa huwe na nguvu kama Tyson bila hivo utakuwa mtu wakupigwa ngumi kila siku!!!!
 
kwa sasa idd azan kashaacha ubabe!

Hawa watu wa Kiboko Msheli! Hivi hata kama huyo jamaa anampigia mtu debe ndio Azzan ampe kipondo? Kwa hiyo Azzan amejimilikisha jimbo la Kinondoni kama mfalme? Miaka 10 bado haimtoshi? Kwanza sioni kurudi kwake bungeni 2015 ni vyema angetafuta mtithi ili amuandae na yeye kutoka kwa heshima kuliko anguko la kushindwa linalomngojea.
 
Source ni Tanzania Daima.

Tuseme NO kwa magazeti ya "kikanjanja" kama hili la Tanzania Daima.
 
Hawa watu wa Kiboko Msheli! Hivi hata kama huyo jamaa anampigia mtu debe ndio Azzan ampe kipondo? Kwa hiyo Azzan amejimilikisha jimbo la Kinondoni kama mfalme? Miaka 10 bado haimtoshi? Kwanza sioni kurudi kwake bungeni 2015 ni vyema angetafuta mtithi ili amuandae na yeye kutoka kwa heshima kuliko anguko la kushindwa linalomngojea.

huyu jamaa jimbo limemshinda, anatumia fimbo ya fedha kila agombeapo. nakumbuka aliwahi kufulumushwa na takukuru katika uchaguzi ndani ya ccm.
 
Shaweji hawezi kumshitaki sababu hawa wanajuana sana na ni ndugu wa karibu!na ni watoto wa mjini hawa wanajuana kwa vilemba!
 
Shaweji hawezi kumshitaki sababu hawa wanajuana sana na ni ndugu wa karibu!na ni watoto wa mjini hawa wanajuana kwa vilemba!

Mkuu unajua tafasiri ya haraka haraka ya neno watoto wa mjini ni kwamba ni wahuni?!
 
Source ni Tanzania Daima.

Tuseme NO kwa magazeti ya "kikanjanja" kama hili la Tanzania Daima.

Ndo hapo pro ccm mnapojivua nguo, jambo hata alifanye mtu binafsi kwa utashi na udhaifu wake mwenyewe mnaibuka na kulitetea kichama. Shame on you..
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom