Mbunge ODM ahutubia Dar aomba majeshi ya AU kwa Kikwete

Shukurani

JF-Expert Member
Oct 23, 2007
251
11
Mbunge ODM ahutubia Dar aomba majeshi ya AU kwa Kikwete
* Kalonzo aenda Ulaya, Marekani kurekebisha mambo

Na Waandishi Wetu

MBUNGE wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha nchini Kenya, Mohamed Dor Mohamed, amemuomba Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, kuamuru jeshi la umoja huo kwenda kulinda amani nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mohamed ambaye yuko nchini kwa ziara maalum, alisema ombi lake hilo linatokana na mapigano kukithiri Kenya, huku Wizara ya ulinzi ikishindwa kurejesha amani nchini humo.

Mkutano wa mbunge huyo na waandishi wa habari jana, uliwashirikisha pia viongozi mbalimbali wa taasisi za Kiislamu nchini, akiwamo Mwenyekiti wa Tanzania Muslim Solidarity Trust Fund, Abbas Sykes, Amiri wa Shura ya Maimamu nchini, Sheikh Mussa Kundecha na Mhadhiri wa Msikiti wa Idrisa, jijini Dar es Salaam, Maalim Ali Bassaleh.

Mohamed ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jukwaa la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu Kenya (NMLF), alisema hali hiyo inatokana na vurugu zinazoendelea nchini humo kubadilika kutoka za kisiasa na kuchukua mwelekeo wa kikabila na kuchochea ulipizaji kisasi.

Alisema pia idara ya ulinzi ya nchi hiyo, imekuwa na msimamo lemavu katika kushughulikia vurugu za Kenya kwa kuegemea upande wa serikali na kuua mamia ya raia kwa kuwapiga risasi.

"Tuna furaha kubwa kwa Rais Kikwete kuwa Mwenyekiti wa AU. Sasa ni jukumu lake kuingilia kati mzozo wa Kenya ili kuleta amani," alisema Mohamed ambaye ni mbunge wa ODM wa kuteuliwa na kuongeza:

"Kwa hiyo tunamuomba Rais Kikwete aweze kuamrisha jeshi la amani la AU liweze kwenda Kenya haraka. Au wasaidiwe na askari wa Umoja wa Mataifa (UN). Itakuwa ni makosa makubwa duniani kuona AU haijachukua hatua. Hatutaki Kenya ifikie hivi sasa kama Tchad".

Hata hivyo, alisema wana imani na mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo yanayoongozwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan.

Lakini akalaani matamshi ya Rais wa Kenya, Mwai Kibaki aliyoyatoa katika mkutano wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni akiwataka wasioridhika na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa Desemba 27, mwaka jana, waende mahakamani.

Alisema matamshi hayo hayalengi kumaliza mzozo wa kisiasa unaoigharimu hivi sasa nchi hiyo, badala yake akasema yanavunja moyo na kuchochea mzozo zaidi.

Ziara ya mbunge huyo ambaye ameongozana na Mweka Hazina wa NMLF, Sheikh Hassan Omar inalenga kuwaeleza Watanzania hali ilivyo Kenya, kujenga umoja wa taasisi za Kiislamu katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania na kusaidiana katika masuala mbalimbali, yakiwamo ya kijamii, kisiasa ili kuwa na chombo kimoja cha kupashana habari zinazohusu masuala hayo.

Msimamo wa mbunge huyo unaendana na ule wa kiongozi wa upinzani Kenya wa chama ODM Raila Odinga ambaye ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) kuisaidia nchi hiyo kwa kuingiza vikosi vya kulinda amani nchini Kenya ili kuinusuru nchi hiyo

Raila ambaye juzi aliwahutubia wafuasi wake baada ya kumaliza ibada maalum nje ya Kanisa la Bondo ACK alisema hadi sasa askari wa nchi hiyo wameshindwa kulinda usalama wa watu wan chi hiyo na kuegemea upande mmoja.

Ombi hilo la Raila limekuja huku idadi ya watu waliouawa ikiongezeka kwa kasi baada ya mauaji ya zaidi ya watu 13 kuuawa juzi katika maeneo ya Magharibi mwa nchi hiyo, katika mapigano yaliyoendela kwa usiku mzima.

Vifo hivyo vinaifanya idadi kamili ya watu waliokufa kufikia 70 katika wilaya ya Nyamira. Mauaji hayo yalitokea mara baada ya kuuawa kwa Mbunge wa David Kimutai Too Ijumaa wiki iliyopita.

Hata hivyo Raila alieleza kuwa ni wazi askari wa nchi hiyo wanaonekana kulinda maslahi ya bwana wao hivyo kuwaacha wananchi wengi wakiendelea kupata taabu na wengi kupoteza maisha na mali zao.

Majibizano hayo yaliendelea baada ya Rais Kibaki kukaririwa kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika mwishoni mwa wiki akidai kuwa matatizo ya Kenya yanaweza kumalizwa kwa kutumia mahakama za nchi hiyo na kukilaumu chama cha ODM kuwa ndicho kinachochochea mauaji yanayoendelea nchini humo.

Raila alimtaka Kibaki kukanusha kauli yake kuwa ameshinda kihalali na kuwaomba samahani wananchi wa Kenya kwa kuwa yeye ndiye aliyepora ushindi wake wa kiti cha urais katika matokeo ya kura ziliopigwa Disemba 27 mwaka jana.

Raila alisisitiza kuwa msimamo huo wa Kibaki unaonyesha wazi nia yake ya kutaka kuvuruga mazungumzo ya amani yanayoendelea baina ya vyama hivyo chini ya mpatanishi Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa.

Hii inaonyesha wazi nia yake mbaya dhidi ya mazungumzo yanayoendelea kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yaliyoikumba nchi yetu, ni lazima akanushe na kubadili kauli hiyo ambayo inaonekana kuchochea zaidi matatizo, alisema Raila.

Aliongeza kuwa kutokana na upendeleo unaoonyeshwa na vikosi vya usalama vya ndani kwa kulinda makundi ya watu wachache, chama chake cha ODM kitaendelea kusisitiza umuhimu wa kuingizwa kwa vikosi vya kulinda amani hasa kutokana na mauaji yanayoendelea hata baada ya tamko rasmi la kamati ya mazungumzo ya upatanishi chini ya Kofi Annan.

Kuendelea kwa machafuko hayo kuemeleta hofu juu ya kuharakishwa kwa mafanikio ya kikosi cha mzungumzo ya upatanishi chini ya Kofi Annan ambacho kililazimika kuendelea na hatua nyingine ya mazungumzo jana baada ya machafuko na mauaji mwishoni mwa wiki.

Annan anayesaidiwa na Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na mke wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini Graca Machel, alitarajiwa kuanza kumshirikisha Cyril Ramaphosa kuwasili nchini humo Jumamosi wiki iliyopita, kwa ajili ya kuwa msimamizi mkuu wa mazungumzo hayo.

Wakati hali ya usalama ikiendelea kuwa tete katika maeneo mengi nchini humo, Makamu wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka ameondoka juzi kwa ziara ya siku nne katika nchi za Ulaya na Marekani.

Ilielezwa kuwa katika ziara yake hiyo ya kwanza tangu kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Kalonzo ana jukumu la kuendelea kuwaweka sawa washirika wa kimaendelea wa nchi hiyo.

Pia ilielezwa kuwa atakutana na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Madola anayemaliza muda wake, Donald McKinnon na wajumbe waBunge la Makabwele nchini Uingereza, kuwaeleza kuhusu mazungumzo yanayoendelea na mpango wa kufikia amani ya kudumu nchini Kenya.


Imeandaliwa na Muhibu Said, Andrew Msechu na Mashirika ya habari.
 
"Tuna furaha kubwa kwa Rais Kikwete kuwa Mwenyekiti wa AU. Sasa ni jukumu lake kuingilia kati mzozo wa Kenya ili kuleta amani," alisema Mohamed ambaye ni mbunge wa ODM wa kuteuliwa na kuongeza:

Si amesea AU haiwezi kupoteza muda na mgogoro wa kenya, kuwa kuna mambo muhimu zaidi.

Huu ujio wa huyu mbunge kama ulikuwa wa kidini zaidi.
 
Kasana kama kila jambo unalitafsiri hivyo basi hatutafika...Raila kazungumza na wafuasi wake Nje ya Kanisa baada ya Ibada...hukuiona hio?

Hizo ni platform tu kufikisha ujumbe juu ya Kenya..AMAN haiwahusu waislam pekee au wakristo pekee au wakikuyu pekee or yoyote..WOTE wanahusika kujenga AMAN.pia kama kungalikuwa na mkutano wa kikabila..bado subject ya AMAN KE inabakia palepale..
 
Back
Top Bottom