Mbona hatuonekani kujiandaa tusifikwe na Richmond nyingine? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbona hatuonekani kujiandaa tusifikwe na Richmond nyingine?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sulphadoxine, Dec 16, 2011.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Dec 16, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  TATIZO kubwa la uhaba wa umeme ndilo ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa likiiumiza kichwa Serikali na kuathiri vibaya sekta ya uchumi na kudhoofisha sekta nyingine za kimaendeleo nchini.


  Kwa asilimia kubwa tatizo hili linatokana na taifa kutegemea kupata nishati hiyo kutoka kwenye vyanzo vya maji ambavyo na vyenyewe vinapewa uhai na upatikanaji wa mvua za kutosha.

  Hakuna asiyesahau ambavyo kwa mwaka huu pekee taifa limekabiliana na uhaba mkubwa wa umeme ambao umepelekea kuwepo kwa mgawo wa muda mrefu na kusababisha athari kubwa za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.  Kama kuna awamu ya uongozi ambayo imeonja shubiri ya ukosefu wa nishati ya umeme wa uhakika nchini, basi ni Serikali ya Awamu ya Nne ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

  Ni katika awamu hiyo ya uongozi, baada ya kuwepo kwa uhaba mkubwa wa umeme, Serikali ilitafuta mpango kupata umeme wa dharura na kujikuta ikitumbukia kwenye mkataba tata na Kampuni feki ya Richmond, mkataba ambao mwaka 2006 ulisababisha Waziri wake Mkuu Edward Lowassa na Mawawiri wengine wawili, Nadhir Karamagi na Ibrahim Msabaha kujiuzulu kuitokana na kashfa hiyo.

  Hata hivyo, tukio hilo halikutoa fundisho lolote kwa Serikali kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ukosefu wa nishati ya umeme, na badala yake ilijikuta kiendeleza malumbano, kujitetea na kuchukua hatua kiduchu katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyotokana na Kamati teule ya Bunge iliyoundwa kufuatilia suala hilo.

  Mizaha ya Serikali ya kushindwa kuchukua hatua za kukomesha tatizo la uhaba wa umeme nchini ilisababisha taifa kurejea kwenye mgawo mkubwa wa umeme mwaka huu, mgawo ambao unaendelea hadi leo katika badhi ya maeneo nchini.

  Kutokana na ukweli kwamba kwa kiwango kikubwa taifa linategemea umeme utokanao na maji, huku maji yenyewe yakiwa ni yale yatokanayo na mvua ya Mwenyezi Mungu, Serikali ilipaswa kujiandaa kuyavuna maji hayo ili yatumike wakati wa kiangazi.

  Nasema hivyo kwa sababu kwa miaka mingi taifa limekuwa likuwa likipata mvua nyingi, ambazo husababisha mabwawa yote yanayotegemewa kwa kuzalisha umeme kujaa maji tena wakati mwingine kupita uwezo wake na hivyo kulazimika kuyafungulia maji hayo yaende baharini, lakini baadaye kiangazi kinapoanza mabwa hayo hukauka na kukosa uwezo wa kuzalisha tena umeme ndani ya kipindi kifupi.

  Watanzania tumekuwa tukishuhudia mito lukuki iliyopo nchini ikisomba maji ya mvua na kuyapeleka baharini, ziwani au kwingineko wakati wa masika na baadaye taifa kukosa umeme wakati wa ukame.

  Nimelazimika kuandika makala haya baada ya kuona tena mwaka huu Mwenyezi Mungu akiwa amelibariki Taifa kwa kulipatia mvua za vuli ambazo katika badhi ya maeneo zilianza mapema mno kuliko hata kawaida yake, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na Serikali za kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya baadaye ya kuzalisha umeme.

  Imekuwa kawaida ya Serikali kuandaa mipango ya dharura ya kupata nishati ya umeme punde tu taifa linapokubwa na uhaba wa nishati hiyo.

  Mipango hiyo imekuwa ikitengewa mabilioni ya fedha ambazo wakati mwingine uhishia vinywani mwa mafisadi kama ilivyokuwa kwenye mpango wa dharura uliopelekea kupatikana kwa mkataba tata wa Richimond.

  Nadhani kama Serikali ingekuwa na nia ya dhati ya kukomesha tatizo la uhaba wa umeme nchini, katika kipindi hiki cha mvua za vuli na kuelekea katika msimu wa mvua za masika ambazo kwa kawaida hunyesha nchini kati ya Machi na Mei, basi ingeandaa mpango wa dharura hivi sasa na kuutengea fedha za kutosha kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua jirani na mabwawa yetu ya kuzalisha umeme ili maji hayo yaje kutusaidia wakati wa ukame.

  Siioni busara ya Serikali kukaa kimya katika kipindi hiki ambacho maji ya mvua yanaendelea kumwagika baharini na kwenye maziwa, huku ikisubiri kiangazi ipeleke mpango wenye mabilioni ya fedha bungeni kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura.

  Sitaki kuamini kuwa kwa sasa wataalamu wa kuandaa mipango endelevu kama hiyo hawapo Serikali na kuwa waliopo wanao uwezo wa kuandaa mipango ya dharura kwa ajili ya kwenda kusaka mitambo chakavu ya kuzalisha umeme wa mafuta ama gesi nje ya nchi, mipango ambayo pia inatoa mwanya kwa mafisadi kutumbukiza mirija yao.

  Kama kweli Serikali ya CCM ipo makini na inahitaji kujikwamua na tatizo la uhaba wa umeme nchini inapaswa sasa kufikiria ama kujiandaa na kujidhatiti kuhifadhi maji ya kutosha kuzalisha umeme kwa kipindi chote cha mwaka au kuachana kabisa na umeme wa nguvu za maji na badala yake kuwekeza zaidi kwenye matumizi ya gesi na makaa ya mawe ambayo kwa bahati nzuri yanapatikana kwa wingi nchini.

  Aidha napenda kutoa rai kwa Serikali kutazama upya vyanzo vyake vya upatikanaji wa umeme katika kipindi hiki ambacho naamini mgawo wa umeme utakwisha kwa muda kutokana na Mungu kujaza maji kwenye mabwawa badala kukaa na kubweteka ikisubiri maji yaishe kwenye mabwawa ili ituletee mpango wa dharura wa kukabiliana na mgawo wa umeme.

  Ifahamike kwamba kila linapotokea tatizo la mgawo wa umeme nchini, athari zake haziishii kwenye sekta za uchumi, jamii na siasa pekee, bali pia zisababisha wananchi walio wengi kuichukia Serikali yao kutokana na maisha kuwa magumu na hivyo kuiweka pabaya wakati wa uchaguzi unapofika.

  Kama Serikali ya Sasa ambayo ipo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inahitaji kujisafisha kwa wananchi wake na kutaka CCM iendelee kubaki madarakani kwa miaka mingi ijayo, basi haina budi kutafuta mipango kabambe na endelevu kwa ajili ya kukomesha kabisa tatizo sugu la uhaba wa umeme.

  Wanachi tumeshuhudia jinsi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilivyojizolea umaarufu kwa kuikosoa na kuishambulia Serikali ya CCM kuhusiana mafisadi waliozalishwa na mipango ya dharura ya kukabiliana na mgawo wa umeme nchini na chama hicho kikafikia hata hatua ya kuwataja kwa majina watuhumiwa vinara wa ufisadi huo.

  Sio nia yangu katika makala hii kuwataja watuhumiwa wote wa ufisadi katika sekta ya umeme walioorodheshwa na Chadema, lakini ninachoweza kusema ni kwamba kama watuhumiwa wote hao wangekuwa na utamaduni wa kujiuzulu kutokana na kuchafuliwa na kashfa hizo, basi hivi leo Serikali yote ya CCM ingekuwa imeangushwa kama sio viongozi wake wote kujiuzulu.

  Kama hali ipo hivyo ni dhahili kwamba tatizo la upungufu wa umeme nchini linaiumiza zaidi Serikali pengine hata kuliko wananchi na hivyo sio tatizo la kubeza na badala yake linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu na kumalizwa kabisa nchini.

  Naamini kuwa kama Serikali ilikuwa imeuchapa usingizi ama imepumzika ikidhani kuwa mvua za vuli zilizofunguliwa na Mwenyezi Mungu zinaweza kuwaepusha au kuwanusuru na tatizo na uhaba wa umeme, huku ikiangalia maji ya mvua yakiendelea kumwagika baharini, inajidanganya kwani tatizo hilo linakuwa limeahilishwa kwa muda na huwenda likarejea kwa nguvu zaidi miezi michache ijayo.
   
Loading...