Mbio za Urais ni Kikwazo cha Demokrasia na Maendeleo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbio za Urais ni Kikwazo cha Demokrasia na Maendeleo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Nov 11, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Nov 11, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Ndugu zangu,

  Yapata miaka themanini iliyopita , mwandishi Shaaban Robert aliandika waraka kwenye gazeti la Mambo Leo juu ya mahusiano ya Merikebu na Nanga. Shaaban Robert anasema; ” Chombo huchukua nanga katika safari. Nanga nayo hukizuia chombo kisipeperushwe kwa upepo bandarini. Mwanadamu huelemewa na mshangao akipima ukubwa na chombo na wa nanga


  Chombo cha baharini, kiwe cha matanga au mashine, pasipo nanga manahodha hutindikiwa. Na nanga pekee si chombo. Vitu hivi kwa pamoja ndio chombo hutimu. Hivyo, Merikebu na nanga ndio watu na Serikali yao. ( Shaaban Robert, Mambo Leo, Septemba, 1932.)


  Na Shabaan Robert huyo huyo anaandika waraka mwingine husemao; ‘ Kama Ulaya, Kama Afrika’- Anasema; ” Nina hakika ya kuwa labda baada ya miaka mingi watakaoturithi wataweza kusema Kama Ulaya, Kama Afrika!
  Bara kubwa maskini lililokuwa katika giza kwa muda mrefu , hata Wazungu walipofika watu walikuwa wakitiana vidole machoni mchana, kila mahali palikuwa na soko la biashara ya aibu. Sasa, taa ya ustaarabu yawaka na nuru yake yaangaza” - ( Shaaban Robert , Gazeti Mambo Leo, Juni, 1932).

  Hakika, Shabaan Robert hakuwa tu mwandishi na mshairi. Maandiko yake yalijaa falsafa. Bado yanatufundisha mengi hata katika wakati tulio nao.
  Ndugu zangu,

  Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu sana kuwahi kutokea. Ni kipindi cha majaribu magumu, huenda, tunapimwa sasa uwezo wetu wa kusimama kama taifa.


  Katika umri wangu huu, miaka 45, nimebahatika kufuatilia kwa karibu siasa za nchi yetu kwa kushuhudia mwenyewe matukio ya kisiasa, kupitia simulizi na maandiko pia. Najiona ni mwenye deni kwa nchi yangu. Kwa karama , elimu na maarifa ambayo Mwenyezi Mungu na nchi yangu imenijalia kuyapata, hata kama ni kwa uchache, basi, nina deni la kuzitumia tunu hizo nilizojaliwa kwa manufaa ya nchi yangu. Na kwa mwanadamu, hakuna dhambi mbaya kama kuisaliti nchi yako uliyozaliwa.


  Hivyo, nitaanza sasa mfululizo wa simulizi ya machache ninayoyajua kwa kuyatanguliza maslahi ya nchi niliyozaliwa, Tanzania. Ni imani yangu, maandiko ni kumbukumbu ya muda mrefu. Huenda, kama yalivyo maandiko ya Shaaban Robert, miaka 80 ijayo, kuna atakayekwenda maktaba na kupekua ninachoandika sasa. Kwa vile historia ni mwalimu mzuri, basi, nami nitakuwa nimechangia katika elimu hiyo kwa vizazi vijavyo.


  Na hili mwanadamu ujue uliko sasa na unakokwenda, una lazima ya kujua ulikotoka. Maana, kuna wengi wa kizazi cha sasa hawajui kwanini tumefika hapa tulipo. Nimetafakari sana na hata kujiridhisha na hitimisho la fikra zangu, kuwa kikubwa kinachotusumbua waTanzania leo ni Mbio za Urais.


  Ndio, kwa mtazamo wangu, chanzo cha mengi tunayoyashuhudia sasa ni mbio za Urais. Ni mbio zilizopelekea Urais wa sasa wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, mbio kuelekea urais ujao wa 2015, na hata maandalizi ya mbio kuelekea urais wa kesho kutwa, 2020. Na mbio hizi ni kikwazo cha kukua kwa demokrasia na kukua kwa uchumi na hivyo basi maendeleo ya nchi. Ni imani yangu, kuwa kadri tunavyokwenda mtanielewa zaidi ninachomaanisha.

  Historia inatwambia nini?
  Katiba
  Mwanasiasa Zitto Zuberi Kabwe anaandika; ” Kama kuna jambo moja ambalo huunganisha Taifa ni KATIBA ya taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo, Katiba inapaswa kuwa ni matokeo ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika.” ( Zitto Kabwe, gazeti Raia Mwema, Nov 9-17, 2011)

  Kwa maandiko hayo ya Zitto Kabwe, Katiba yaweza pia kutafsiriwa kama Mkataba wa Kijamii- Social Contract . Na katiba iwe ni msingi wa utawala bora. Kwamba Katiba ni muafaka pia wa Serikali na Wananchi. Na hapa ndipo falsafa ya Shaaban Robert ya Merikebu na nanga inapokuwa na maana kwetu.


  Madai ya Watanzania kupata Katiba Mpya ni madai muhimu, ya haki na ya kihistoria. Nimepata kuandika, kuwa Watanzania wenye mapenzi na nchi yenu, msikae mkafikiri, kuwa madai ya kupata Katiba Mpya ni kazi nyepesi.

  Ni kazi ngumu sana, hata kama mnaowataka wawasaidie kupata Katiba hiyo ni Waafrika wenzenu na si wakoloni. Ilivyo Afrika, kwanza mtaletewa na walio kwenye mamlaka, ’Katiba Mpya’ iliyofanyiwa marekebisho madogo kwa maana katiba iliyoongezewa viraka. Haitapelekea mkawa na chaguzi salama.

  Kuna kuandamana na hata watu kufa kutakakofuatia. Kuna akina Ocampo wa Mahakama za Kimataifa watakaokuja kuwanyofoa wahusika wa vurugu zitakazopelekea mauaji ya raia. Kisha itakuja Katiba Mpya. Ni njia mbaya na ya kusikitisha, lakini inaepukika, kama kuna utashi wa kisiasa. Ndio, Afrika kudai Katiba Mpya yaweza kuwa ni kazi ngumu kuliko kudai uhuru kutoka kwa mkoloni.


  Nakumbuka, Prince Bagenda, Mwakilishi wa CCM kwenye Kongamano la Katiba pale Chuo Kikuu Mlimani alipata kukaririwa na gazeti la Mwananchi akitamka; ” Msifikiri kila kitu mnapewa tu, lazima mdai”. (Mwananchi Aprili 3, 2011). Ndio, Prince Bagenda alitamka; kuwa hoja ya Katiba haikuwa ya CCM. Kwamba CCM ilikubali kwa kuwa Serikali huongozwa kwa maoni ya wananchi.


  Na Afrika safari ndefu huamuliwa na hatua ya mguu wa kwanza. Ukiianza safari na ’ mguu mbaya’, basi , hiyo haitakuwa safari njema. Ina maana moja kubwa, namna ulivyojipanga na safari yako kuanzia mwanzo. Nilivyofuatilia Kongamano lile la Katiba pale Chuo Kikuu Mlimani, nasikitika kusema, hata wakati ule, tuliianza safari yetu na mguu mbaya.

  Tafsiri yangu juu ya alichokitamka Bagenda ni hii; Katiba ni suala la ’ Sisi na Wao’. Ni mapambano. Hapa kuna tatizo kubwa. Maana, kuna hali ya kutafuta mshindi na mshindwa. Ndio, unatafutwa ushindi na ufahari, le prestige, kama wasemavyo Wafaransa. Ninachokiona, kama tutachagua njia ya kushindana katika kuifanyia marekebisho katiba yetu, basi, hakutakuwa na mshindi. Sote tutashindwa.

  Hakika, pale Chuo Kikuu Cha Mlimani ndio tulianza rasmi safari hii ya mchakato wa Katiba kwa wadau kuutolea maoni Muswaada wa Katiba uliorudishwa Bungeni sasa na tunaambiwa utasomwa kwa mara ya pili ingawa ulipaswa usomwe kwa mara ya kwanza.

  Kuusoma muswaada huo kwa mara ya pili kutakuwa na maana moja; kuwa muswaada huo utajadiliwa na wabunge ambao wengi ni wa CCM. Ni kwa siku tatu, kuanzia Jumatatu hadi Jumatano. Hatimaye utapitishwa ‘ kishabiki’. Hivyo basi, kwa jinsi hadidu rejea zilivyopangwa, WaTanzania watakuwa wamepatiwa Katiba Mpya ndani ya saa 72!

  Nionavyo, kama Serikali yetu ni sikivu kweli, na inasoma alama za nyakati, haina kingine, bali kusitisha kuharakisha muswaada huu hadi pale utakapopatikana muafaka wenye kuihusisha jamii pana zaidi ya WaTanzania.

  Ndio, safari hii ya kuitafuta Katiba yetu iwashirikishe wadau muhimu katika nchi . Na wadau hao tunao. Nayasema haya kama Mtanzania ninayeiangalia na kuitafakari nchi yetu na bendera ya taifa letu . Si chama cha siasa wala bendera yake.

  Katika dunia hii, chama na bendera yake huja na kupotea. Nchi na wananchi hubaki pale pale. Si kuna Msajili wa vyama, na anaweza kukifuta chama? Kikapotea chama na wanachama wake. Lakini, duniani hakuna Msajili wa Nchi wala wanachama wake. Ukizaliwa kwenye nchi tayari umeshapata usajili wa kudumu kama mwananchi. Ndio maana, katika nchi za wenzetu, hata raia wao akijiandikisha uraia wa nchi nyingine, bado nchi aliyozaliwa haiwezi kuufuta uraia wa nchi yake aliyozaliwa. Siku yeyote anaweza kurudi nyumbani alikozaliwa na kukaribishwa, awe na hati ya kusafiria ya nchi yake au ameipoteza.

  Rai yangu; ” Tutangulize Maslahi Ya Taifa.” Mifano mingine ni hai na tunaishi nayo. Si tumeyaona yaliyotokea hata kwa jirani zetu Kenya na hata Zanzibar. Ni matokeo ya wanasiasa kutotanguliza maslahi ya taifa.

  Watu wanapoteza uhai kutokana na utata wa matokeo ya Uchaguzi. Chanzo hasa ni mapungufu ya Katiba ya nchi . Sababu hasa ni wanasiasa wetu kutanguliza maslahi binafsi, ya vyama na makundi yao. Wanasiasa wetu si wepesi wa kujifunza. Ni jukumu letu kuweka shinikizo. Tuweke wazi tunayoyataka kwa nchi yetu. Tusikubali kupitishwa kwenye njia yenye maafa na kubaki kimya. Tuanze kupiga kelele, sasa.

  Ni vema na ni busara, kwa kazi ya kuandaa Katiba ya nchi ikaridhiwa na wadau muhimu katika nchi. Inahusu imani. Kukosekana kwa imani kwa maana ya wadau wa Katiba wasipokuwa na imani na dhamira za walioandaa Katiba, basi, hicho huwa ni chanzo cha kinyongo, chuki na machafuko katika nchi.

  Haiyumkini mechi ya kandanda ikawa na matokeo ya haki pale timu moja inapojibebesha jukumu la kuamua uwanja, mwamuzi na taratibu za mchezo. Mwamuzi wa kandanda anaweza kuwa chanzo cha wachezaji kupigana uwanjani na hata mashabiki kupigana pia.

  Mara nyingi chanzo ni upande mmoja kukosa imani na mwamuzi. Kinyume chake, timu zote mbili zikiwa na imani na mwamuzi, basi, mara nyingi mechi humalizika kwa hata aliyeshindwa kutangulia kumpa mkono mshindi na mwamuzi pia. Katiba, mbali ya mambo mengine, iwe pia msingi wa chaguzi za kiungwana ili, kama taifa, tuepukane na yaliyotokea Kenya na kwingineko.

  Kama nchi tumedhamiria kuifanyia marekebisho makubwa Katiba yetu. Tufanye hivyo tukiwa na dhamira njema na mapenzi kwa nchi yetu. Nimepata kuandika, kuwa katika hili la Katiba tujiulize; Je, Katiba yetu ya sasa, na kwa wakati uliopo, inakidhi matakwa ya shabaha na malengo yetu kama taifa? Jibu langu ni HAPANA.

  Na katika hili hatuna sababu za kugombania fito ilihali nyumba tunayojenga ni moja na ni yetu sote. Ni busara kutambua, kuwa wakati umebadilika. Mtanzania wa mwaka 1977 si Mtanzania wa mwaka 2011. Hoja hii ya Katiba si kama nzi anayetua na kuruka. Hoja ya Katiba kwa sasa inaongozwa na kundi kubwa la vijana wanaotaka mabadiliko. Hawa si nzi wanaotua na kuruka, ni siafu wanaokuja kwa kuongezeka idadi yao.

  Na harakati za Watanzania kutaka marekebisho ya Katiba zina muda mrefu. Hizi si harakati mpya. Si harakati za chama au kikundi kidogo cha ’wapinzani’ wasioitakia mema nchi hii. Siku zote, yamekuwa ni madai ya msingi ya Watanzania, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini, rangi na makabila.

  Kama ni shauri mahakamani, basi, lilishafunguliwa zamani. Kinachofanyika sasa ni mwendelezo wa shauri. Si wengi, miongoni mwa vijana wa sasa, wenye kumbukumbu ya ukweli huu. Kuwa tayari mwaka 1991 vuguvugu la kudai vyama vingi na Katiba mpya lilishaanza. Wakati huo madai makubwa yalikuwa mawili; vyama vingi na Marekebisho ya Katiba. Kuna mnaokumbuka ’ KAMAKA’- Kamati ya Marekebisho ya Katiba iliyoundwa na wanaharakati. Ikumbukwe, kuwa hayo yalikuwa ni madai ya Watanzania ndani ya mfumo wa chama kimoja.

  Marehemu Chifu Abdalah Fundikira aliongoza Kamati iliyoundwa, si na Serikali, bali wanaharakati, kuratibu mchakato wa kudai vyama vingi na Katiba mpya.

  Hata wakati huo, Mzee Mwinyi, kama Rais, aliweka ‘ mkwara’, kuwa madai hayo yasiendeshwe na watu au makundi ya watu bila kibali cha Serikali. Presha ya madai ilipoongezeka, tunakumbuka, kuwa Mzee Mwinyi aliweza kusoma alama za nyakati. Aliongea pale Chuo Kikuu Mlimani na kuweka bayana dhamira ya Serikali ya kuunda ‘ Tume ya Nyalali’ . Tume hiyo ilizunguka nchi nzima kuwauliza Watanzania kama wanataka kuendelea na Chama kimoja au Vyama vingi.

  Itakumbukwa, Chifu Fundikira alipata kutamka; kuwa huko ni kupoteza muda na fedha za wananchi. Itakumbukwa pia, Mabere Marando alikuwa Katibu wa Kamati ile ya wanaharakati ya kuratibu mchakato wa madai ya kuwepo na vyama vingi na marekebisho ya Katiba. Marando alipata kutamka na kunukuliwa na Daily News, April, 12, 1991; “ We have a bad political system because our Constitution embraces political discrimination. What we want is that all of us should shout out that our Constitution is bad.” ( Mabere Marando, Daily News, April 12, 1991)

  Tafsiri; “ Tuna mfumo mbaya wa kisiasa kwa sababu Katiba yetu ina ubaguzi wa kisiasa. Tunachotaka, ni sote, tupige kelele, kwamba katiba yetu ni mbaya.”)

  Marando aliyasema hayo katika Semina ya kwanza ya Kamati ya kuratibu mchakato wa madai ya vyama vingi na Katiba mpya iliyoongozwa na Chifu Fundikira. Semina hiyo iliudhuriwa na watu wapatao 800 kwa mujibu wa taarifa ya Daily News la April 12, 1991.

  Na akina Chifu Fundikira waliandamwa sana na Serikali na Chama Tawala. Kwa mujibu wa Daily News la April 26, 1991, Mbunge wa Shinyanga, Ndugu Paulo Makolo alimshambulia Fundikira kwa kusema kuwa , katika hilo la kuwa na vyama vingi na katiba mpya , Chifu Fundikira hakuwakilisha mawazo ya Wasukuma na Wanyamwezi wenzake; “ This is not a Wanyamwezi and Wasukuma movement. It is the selfish interests of Fundikira and his ten colleagues. Our people are not after parties. They want food, water, education and health care.” ( Paulo Makolo, MP, Shinyanga, Daily News, April 26, 1991).

  Mwenyezi Mungu umrehemu Chifu Abdalah Fundikira….. Itaendelea.

  Maggid Mjengwa
  Iringa,
  11.11.11
  MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
   
Loading...