Mbio za uongozi CCM: Sumaye amuengua Nagu, Mama Salma Hana mpinzani Lindi, UWT Dar moto......

Mi nafikiri kama wapenda nchi, wenye kutaka mambo yaundugu yasiwepo katika vyama au serikali au sehemu yeyote; hii ni faida kwetu. Nasema hivyo kwa sababu, ukigundua adui yako anafanya makosa huo unakuwa msaada mkubwa huko mbeleni kwani watu wanaona, wanaakili na wengi kama hawafurahiii hii hali lazima hatua zitachukulia.
Hakuna utawala uliowahi kudumu kwa style kama hizi za kupeana madaraka bila hata wahusika kuwa na sifa, kuna mtu anaweza kusema hao wajumbe wanaotoka kwenye familia ya M/kiti wa chama tawala, kulikuwa na ulazima wowote wa kufanya hivyo hadi kuchafua image ya chama?
 
usafi na uchafu na udhaifu wa salma niulizeni mimi niliekaa nae pale mnarani kwa babu kushoto(marehemu moledina) na pia nikasoma nae liseco kisha nachingwea ttc namjua hasa! Hawezi kukosa mpinzani lakini loo!! Kweli pesa zinavunja milima.
unatisha mwalimu...
 


TAFAKURI JADIDI

Johnson Mbwambo

Toleo la 258
12 Sep 2012



  • Ni zama za mama na mwana




TOLEO lililopita niliandika makala kwenye safu hii iliyobeba kichwa kinachosomeka: Tumsaidie Sitta kuona asichokiona CCM. Katika makala hiyo nilijaribu kueleza namna chama tawala, CCM, kilivyopoteza mvuto kwa wananchi kwa sababu ya ukaidi wake wa kukataa kubadilika na kujirekebisha.

Nilieleza kwamba CCM ya sasa ni kivuli cha CCM asilia ya enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na kwamba sasa kimepoteza kabisa mwelekeo kwa kugeuka kuwa chama cha matajiri kilichowatelekeza wakulima na wafanyakazi.


Nilijaribu kutoa mifano ya mambo ya hovyo yanayotokea hivi sasa ndani ya chama hicho, ambayo enzi za Mwalimu Nyerere usingeweza hata kufikiria kwamba yanaweza kutokea – mambo kama vile viongozi kutoleana bastola hadharani, nk!


Leo, niendeleze kidogo tafakuri hiyo kwa kutoa mfano mwingine wa sasa wa kitu kinachotokea ndani ya chama hicho na kukubalika ambacho enzi za Mwalimu hakikuonekana sana katika mienendo ya chama hicho.


Nazungumzia tabia za watawala wa sasa ndani ya chama hicho kubebana kindugu au kifamilia katika chaguzi za chama. Hali hii pia imeanza kuonekana ndani ya serikali yake, kwenye ajira muhimu za makampuni, na hata katika duru za biashara kubebana kindugu ndio umekuwa wimbo wa wakubwa.


Kilichonisukuma, kwa mara nyingine, kulizungumzia suala hili, ni taarifa za vyombo vya habari za wiki iliyopita kwamba mtoto wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, anayeitwa Ridhiwan, amepita bila kupingwa kwa kukosa mpinzani katika patashika ya kuwania ujumbe wa NEC huko Bagamoyo, na vivyo hivyo mke wa Rais Kikwete, Salma Kikwete, wilaya ya Lindi Mjini.


Yeyote mwenye kufikirisha ubongo wake aliyezisoma habari hizo bila shaka alijiuliza maswali kibao yasiyo na majibu. Je, mama (Salma) na mwana (Ridhwan) hawakupata wapinzani kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa uongozi uliowatisha hadi kunywea waliotaka kuwania nafasi hizo?


Je, wawili hao – Mama Salma na mwanawe Ridhiwan, wanajisikiaje binafsi kupita katika uchaguzi huo bila kupingwa? Je, nini hisia za wana CCM wa Lindi Mjini na Bagamoyo, na kwa hakika wana CCM kote nchini kuhusu watu hao wawili kupita bila kupingwa kwa kukosa wapinzani?


Lakini zaidi ya yote ni vigumu kukwepa kushawishika kujiuliza swali hili: Je, wawili hao walikosa wapinzani kwa sababu ni mke na mwana wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete?


Je, Rais Kikwete mwenyewe alihusika katika kuwafagilia njia ya u-NEC na kuhakikisha wanapita bila kupingwa, au ni viongozi tu wa chama wa wilaya hizo waliosuka mipango kuhakikisha hawapati wapinzani ili ‘kumridhisha' mkubwa, na kwa maana hiyo walifanya hivyo kujipendekeza tu kwa Rais?


Je, Rais Kikwete mwenyewe binafsi anajisikiaje anapopata habari kwamba mkewe na mwanawe wamepita u-NEC bila kupingwa? Anasikitika kwa sababu hawakuhenya kuupata ujumbe huo wa NEC kama wengine au anaona ni stahiki yao kwa mujibu wa uwezo wao wa kiuongozi (kisiasa) walionao?


Vyovyote vile, suala la Ridhiwan Kikwete na Salma Kikwete kupita bila kupingwa linafikirisha, na tena linafikirisha sana katika zama hizi ambapo chama hiki tawala tayari kinalaumiwa kuwa kinapendelea watoto na ndugu za wakubwa katika chaguzi zake, na kwamba huko kinakoelekea itakuwa ni vigumu zaidi kwa mtoto wa mkulima na mfanyakazi masikini kupata uongozi wa kitaifa!


Na katika hili, sina hata haja ya kutoa mifano ya majina kadhaa ya vijana ambao wamefikia nafasi za juu za uongozi kutokana na kubebwa na baba zao au ndugu zao ambao tayari ni wakubwa ndani ya chama na ndani ya serikali; maana sote tunawajua.


Hata hivyo, katika suala hili, napenda kusisitiza tena kwamba si vibaya wala ajabu kwa mtoto au mke wa kiongozi wa kitaifa kuwa naye kiongozi wa kitaifa. Kwa hakika, dunia yetu ina mifano mingi tu ya watoto au wake wa wakubwa ambao nao walikuja kuwa viongozi wa kitaifa maishani.


Kuna watu kama George W. Bush ambaye naye alikuja kuwa Rais wa Marekani kama alivyokuwa baba yake. Kuna watu kama Hillary Clinton ambaye naye alikuja kuwania kuteuliwa kugombea urais wa Marekani akifuata njia ile ile aliyotumia mume wake, Bill Clinton.


Hata hapo jirani nchini Kenya yupo Uhuru Kenyatta ambaye naye sasa ni jina kubwa katika siasa kama alivyokuwa baba yake; yaani rais wa kwanza wa nchi hiyo, Jomo Kenyatta. Yupo pia Raila Odinga ambaye anafuata nyayo za marehemu baba yake, Jaramogi Odinga.


Hata hivyo, hao wote niliowataja walithibitisha wenyewe ubora wao kiuongozi na karama walizonazo za uongozi kwa kupambana, na si kwa kuletewa uongozi kwenye kisahani cha dhahabu.


Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, ubaya kwa watoto au wake wa viongozi kuwa nao viongozi unakuja tu pale ambapo wahusika hawana uwezo wala sifa za uongozi bora; bali hupeta tu katika chaguzi kwa sababu ya ‘kubebwa' na baba zao au waume zao wenye nafasi za juu za uongozi nchini. Waingereza wana neno linalozungumzia hali hii – Nepotism.


Ndiyo maana, kama wahusika ni wachacharikaji kweli kweli na wenye kipaji na karama za uongozi, hakuna Mtanzania anayeweza kuhoji anaposikia kwamba mtoto wa mkubwa fulani amepita bila kupingwa katika chaguzi fulani.


Lakini kama wahusika huwana track records za uchacharikaji katika uongozi, na hawajapata kuonyesha dalili za kuwa na karama zozote za uongozi, lakini katika kipindi kifupi tu wanapanda ngazi za kisiasa kwa kasi, ni lazima watu wajiulize maswali kibao – ni lazima kope zipepese!


Na kwa mtazamo wangu, mazingira haya ndiyo yanayoambatana na taarifa hizo za wiki iliyopita kwamba Salma Kikwete na Ridhiwan Kikwete wamepita bila kupingwa kwenye patashika za u-NEC huko wilayani. Kama kweli wawili hao wana karama za uongozi na wana track records za utendaji uliotukuka unaowafanya wastahili kupita bila kupingwa, naomba nielimishwe.


Najua wapo watakaobeza suala hili kwa kutoa mifano ya wagombea wengine watakaopita bila kupingwa, lakini niwaambie hao mapema kwamba, kuna tofauti kubwa ya kupita bila kupingwa kwa mwananchi wa kawaida na kupita bila kupingwa kwa mtoto wa rais au mke wa rais! Asiyeelewa hilo, sijui nimsaidieje kuelewa.


Ni kwa kuzingatia yote hayo, kama ningalikuwa mimi ndiye Rais Kikwete, nisingelifurahia kamwe mke wangu na mtoto wangu kupita bila kupingwa katika patashika hizo za NEC. Ningalitaka mke wangu na mtoto wangu wapambane na kuonyesha uwezo wao ili ulimwengu uridhike kwamba wanastahili nafasi hizo kwa sababu ya karama za uongozi walizonazo, na si kwa sababu ya ‘kubebwa' na mimi rais.


Hivi ndivyo wenzetu wa nje waliokomaa kidemokrasia wafanyavyo. Kwa mfano; mwaka 2000 George W. Bush alihangaika kweli kweli na nadharia yake ya "Compassionate Conservatism" na kauli mbiu yake ya "A New Day" kwenye kampeni ya urais, na hivyo kumtoajasho kweli kweli Al Gore wa Democrat.


Kwa maana hiyo, hakuna Mmarekani anayeweza kusema, leo hii, kuwa George W. Bush alipata urais wa Marekani mwaka 2000 kwa ‘kubebwa' na baba yake, rais wa zamani, George Bush.


Hata hapo Kenya tu sote tunajua kwamba Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wamefikia ngazi za juu za uongozi wa kisiasa kwa kuchacharika wao wenyewe, na si kwa kubebwa na baba zao - Jomo Kenyatta na Jaramogi Odinga; maana walishafariki dunia kabla wao (watoto) hawajaanza kikweli kweli safari zao za kisiasa.


Kwa hiyo, inapotokea hapa kwetu Tanzania mtoto au mke anakwea haraka ngazi za kisiasa kwa sababu baba au mume amekalia ‘kiti cha enzi', ni lazima tuulizane maswali na kuhoji; kulikoni?


Kwa hakika, kwa kuwa CCM ndicho chama tawala, kitazidi kupoteza mvuto kwa wananchi endapo hakitahoji mwenendo huu mpya wa nepotism ambao haukuwapo sana enzi chama kilipokuwa chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.


Kwa kuwa CCM ni chama tawala, kisipoachana na mwenendo huu mpya tunaouona hivi sasa ndani ya chama hicho, basi huko mbele ya safari kitatoa rais wa nchi anayemteua mkewe kuwa waziri kama alivyofanya Rais Museveni kwa Janet, au anayemteua nduguye kuwa waziri kama alivyofanya hayati Rais Bingu wa Mutharika kwa Peter!

Nina wasiwasi huko ndiko Tanzania tunakoelekea.










 

Similar Discussions

Back
Top Bottom