Mbinu za kumuokoa kifikra mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Ukatili wa kingono unaofanywa dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tatizo hili hujitokeza katika sura tofauti na kwa nyakati zisizotarajiwa. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa idadi kubwa ya watoto wanaoathiriwa na vitendo hivi hukosa ujasiri wa kuzungumza wazi juu ya masuala haya na huenda jambo hili ndiyo hasa husababisha uwepo wa ufinyu wa takwimu mahsusi zinazohusu matukio ya kikatili wanayokumbana nayo watoto.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kupitia vyombo vya habari kuanzia Januari mpaka Juni mwaka 2019 ulionyesha kuwa asilimia 66 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalikuwa ni ya kingono, hasa ubakaji na ulawiti. Wahanga wengi walikuwa ni watoto wa shule za msingi wenye miaka kati ya 7 hadi 14. Takwimu hizi zinaiwashia taa nyekundu jamii kwa kuikumbusha kwamba inahitaji kufanya jambo ili kukomesha ukatili kwani huenda hali ikawa mbaya zaidi huko mbeleni.

Ukatili wa kingono dhidi ya watoto ni jambo la kutisha na kwakuwa mtoto anapofanyiwa kitendo hiki hupitia kipindi kigumu katika maisha yake, sisi kama wazazi, walezi, walimu mashuleni pamoja na watu wote wenye nia thabiti ya kukabiliana na janga hili, hatuna budi kujifunza viashiria vya mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho. Kwa hakika, njia hii huweza kutusaidia kumsaidia mtoto anapopatwa na janga hili.

Chuki zisizo na sababu kwa baadhi ya watu, mabadiliko ya tabia yanayoambatana na kujitenga na wenzake, upweke, kufedheheka, kupata mshtuko na uoga usio wa kawaida katika baadhi ya maeneo, vitu ama watu, kujichukia na kukosa ujasiri pindi anapokuwa na watu wengine ni baadhi ya dalili za mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono.

Mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono hupoteza imani na watu. Hujihisi amesalitiwa na jamii pale tu agunduapo kwamba mtu aliyekua akimuamini sana ndiye aliyemuingilia kimwili. Matokeo ya kitendo hicho ndiyo hasa hupelekea mtoto kukosa imani na mtu yeyote. Huwaona wote kama watu wasiofaa, waliojivika ngozi ya Kondoo kumbe ni Mbwa Mwitu.

Kwa minajili hiyo, hatua ya kwanza katika kufanya jitihada za kumuokoa kifikra mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono ni kuirejesha imani yake kwa watu. Hapa, sharti apatikane mtu anayeweza kuyafariji majuto na huzuni ya mtoto ambapo mtoto atajihisi yuko huru kuzungumza nae na kukisikia kilio chake.

Wepesi wa jambo hili utategemea zaidi uharaka wa mtu huyo katika kushughulikia uovu na huzuni ajisikiayo mtoto. Hii si kazi rahisi lakini kwani tulio wengi tusikiapo matukio na simulizi za kusikitisha, muitikio wetu wa awali huhusisha kulaumu na kuhukumu. Tunashindwa kutambua kwamba tunapofanya hivyo, mtoto hujihisi kubebeshwa mzigo wa lawama ulio na hukumu ndani yake na hivyo huona ni bora akaendelea kuitunza yake siri.

Hatupaswi kuzungumza maneno yanayoweza kuleta tafsiri mbaya kwa mtoto na kwamba tunamlaumu. Wakati mwingine hatia anayoihisi mtoto hutokana na fikra kwamba huenda ukatili aliofanyiwa tayari umeharibu maisha yake, jaribu kumuepusha na fikra hizo. Aidha, mdhibitishie kuwa maisha yake hayajaenda kombo kama afikiriavyo, mpe mifano ya watu mashuhuri waliowahi kuwa wahanga wa ukatili wa kingono lakini sasa wana mafanikio makubwa, mifano hiyo huweza kuwa chachu ya kuondoa majuto aliyonayo mtoto, kulirejesha tumaini lake na ujasiri wake.

Hatuna budi kumhakikishia mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji wa kingono kuwa, pamoja na yote yaliyomkumba, yeye ni wa thamani sana na bado ana nafasi ya kufikia ndoto zake. Wajibu wetu ndiyo maisha yake. Tuukatae udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto!

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa JamiiForums: Sema Tanzania;
 
Ni sahihi.. lakini msisahau pia watoto wanaonyanyaswa/wanaofanyiwa ukatili wa kihisia.. Hawa ndio wengi mno nchini. Wazazi na vile hawajali hata maneno ya kuongea na watoto zao..
Kila neno la hovyo mzazi anamwambia mwanae..
Habari. Ahsante sana kwa kutuandikia. Mwitiko wako ni adhimu sana kwetu.^CS
 
Sema Tanzania,
SIJAONA MKAKATI NA NGUVU KALI KUKOMESHA HAYO. HADI KUNA MUDA NAHISI LABDA WANAOPIGA HII KAMPENI WANAMASLAHI YA KIMAISHA HIVYO HAWAPENDI IISHE. USHAURI WANGU.

1. Kwa wale wanaowaingilia watoto kingono
A) hukumu ya wazi ifanyike hadharani ikithibitika ni mhusika
B) Apigwe Risasi hadharani ( mfano kama pale Taifa, CCM Kirumba etc
C) Ifanywe kwa nchi nzima kila mji walau hukumu mbili au tatu. HILO MTAONA LITAISHA IN FEW DAYS

2. Kwa wanaonyanyasa watoto kihisia, wako wengi na wa aina mbali mbali, mfano
A) kwakuwaonesha picha chafu
B) TV zinazoonesha cinenma zenye mchanganyiko na mambo zaidi ya Umri
C)mamlaka zinazoshindwa kuchukua hatua kama Basata.

Onyo litolewe hadaharani na kufungia hayo yote. Na ikithibitika wanaendelea kutokuzingatia taratibu wao wanyogwe kwa heshma tofauti na kundi la kwanza.

Mkifanya hayo mtaona mambo yatakavonyooka na watoto wa Tanzania kuishi kwa amani. Na mimi nitawaunga Mkono
 
changamoto kubwa sana ni wazazi kuficha matukio haya kwa kuogopa kuichafua familia wakati walitakiwa kushirikiana vyema na vyombo vya dola ili kusaidia kutokomeza ukatili huu.
 
changamoto kubwa sana ni wazazi kuficha matukio haya kwa kuogopa kuichafua familia wakati walitakiwa kushirikiana vyema na vyombo vya dola ili kusaidia kutokomeza ukatili huu.
Habari mdau wetu. Pongezi zikufikie kwa uamuzi wako wa kutuandikia hapa.
 
tafadhali hebu jaribu kutafakari hayo maneno niliyo yafanyia quotation

''mdhibitishie kuwa maisha yake hayajaenda kombo kama afikiriavyo, mpe mifano ya watu mashuhuri waliowahi kuwa wahanga wa ukatili wa kingono lakini sasa wana mafanikio makubwa, mifano hiyo huweza kuwa chachu ya kuondoa majuto aliyonayo mtoto, kulirejesha tumaini lake na ujasiri wake''
 
Ahsante Sana

Kingine wazazi tuwe karibu Sana na watoto wetu..tufuatilie nyendo zao na kuwasikiliza pia.
 
Mimi mtu amnyanyase mwanangu kingono sijui kama ataishi... atajiua mwenyewe
 
Back
Top Bottom