Mbinu Kabambe za kuwa Maarufu kwenye karne ya 21 - 22

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,330
51,836
MBINU KABAMBE ZA KUWA MAARUFU KWA KARNE 21 - 23​

Na, Robert Heriel

Leo Taikon sitakuwa na lumbelele nyingi hapa, kwani watu wengi hawapendi Makala ndefu. Nitajitahidi kuandika kwa kifupi sana ili kutowakwaza baadhi ya wasomaji wangu.

Umaarufu ni sehemu ya jambo la heshima katika ulimwengu wa wanadamu, hata hivyo inategemea na aina ya umaarufu, lakini umaarufu ni umaarufu uwe kwa wema au kwa ubaya. Umaarufu unaotokana na mambo mema na kazi njema hujulikana kama Umashuhuri, lakini ule utokanao na Ubaya huishia kuitwa Umaarufu tuu. Hii ni kusema, watu maarufu ni wengi ukilinganisha na watu MASHUHURI. Watu Mashuhuri hujulikana na watu wachache wenye AKILI, Lakini watu maarufu hufahamika zaidi na watu wote wajinga na werevu.

Vijana wengi wa zama hizi huupenda umaarufu, hufanya kila namna ili waweze kuwa maarufu, hujipindua wakapinduka kujipatia umaarufu uliopindukia. Hujivua wakavulika heshima na utu waliovikwa na Maulana. Hujivunia kujulikana kila kona ya hii dunia, raha iliyoje kuwa maarufu, kila upitapo jina lako lasemwa kama dawa ya njaa inayotibu tumbo la kabwela. Looh!

Sio kila mtu maarufu anapenda umaarufu, wengine kazi zao hujikuta wakiingia katika mkondo wa kujulikana kwenye jamii, mathalani kazi za Utangazaji kwenye vyombo vya habari vikubwa, kuwa mwanasiasa mkubwa kwa ngazi ya kitaifa, kuwa mhubiri kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa, kuwa mwanamuziki kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa miongoni mwa mambo mengine. Nimeshaeleza, ikiwa kazi yako unaifanya kwa weledi na kwa maadili alafu ukawa maarufu basi wewe upo kwenye kundi la watu Mashuhuri.

Hata hivyo kuwa Mashuhuri sio kazi rahisi, sio lelemama, huwezi kuwa mashuhuri kwa siku moja au mbili au kwa mwaka, ila Umaarufu unauweza ukaupata ndani ya dakika moja tuu dunia ikakujua ukizingatia dunia ya sasa ni kama kijiji.

Zifuatazo ni mbinu Kabambe za kuwa Maarufu katika karne ya 21 - 22

1. IJUE JAMII YAKO (know your community - KYC)
Hii ndio mbinu namba moja kabisa ndugu mpenda umaarufu. Ukitaka uwe maarufu ni sharti ujue jamii yako ikoje, mila na desturi, miiko, utamaduni. miongoni mwa mambo mengine. Bila kuijua jamii yako kamwe huwezi kuwa maarufu, labda utakachokifanya ni Ku-trend tuu kwa siku moja, lakini kama unataka kuwa na umaarufu endelevu(Sustainable popularity).basi lazima utumie KYC, ijue jamii yako. Ijue inataka nini kutoka kwako, ijue inakuchukuliaje na kutegemea nini kutoka kwako, fahamu inakumiliki kwa namna na kiwango gani n.k.

2. ZIMA UFAHAMU WAKO (Turn off your consciousness - TYC)
Mbinu namba mbili ni kuzima watoto wasikuhizi wanaweza wasinielewe, labda nitumie neno Ku-logout, ku-disconnect, ku-offline ufahamu wako. Ukitaka uwe maarufu basi Logout your consciousness/ mind, be out of your mind, zima ufahamu wako, fumba macho, ziba masikio, binya pua lako, ng'ata ulimi wako ukatike kabisa, chubua au ziriba ngozi yako, yaani hakikisha milango yako yote ya fahamu umei-logout, au kui-turn off, ukishaweza hivyo basi lazima uwe maarufu, kwa kufuata mbinu zingine ninazoenda kuzieleza. Sio ajabu watu maarufu karibu wote hupenda kuvaa miwani nyeusi, unajua ni kwa nini, nafikiri ushaanza kunielewa. Huwezi ukawa maarufu kama ubongo wako upo Online au umeu-turn on. Hutaweza kwani utajisikia aibu.

3. CHAGUA AINA YA UMAARUFU (select the type of popularity)
Mbinu namba tatu, chagua unataka uwe maarufu kwenye ishu gani hasa, kama ni muziki haya, kama ni siasa sawa, kama ni mwanamitindo poa, kama ni mchambaji fresh, kama ni matusi, kila la kheri, kama ni uhalifu yote sawa, wewe tuu. Kama ni uchawi na ulozi haya, Mwanaharakati haya, udalali sawa, utapeli ewala, Nabii wa upako ni wewe tuu nishasema. Japo unaweza kuwa multipurpose ili kuteka soko kubwa zaidi.

4. UNDA MTANDAO (Create a network)
Tayari unaijua jamii yako, umeshazima ufahamu wako, kazi ya kuunda mtandao itakuwa rahisi sasa. Huna aibu, unaouwezo wa kumfuata yeyote na kufanya lolote. Mbinu namba mbili ya TYC itakusaidia kuunda mtandao, hutaona shida kujipendekeza kwa watu maarufu waliokwenye game kitambo, hutaona aibu kushobokea wanasiasa, kushobokea vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mtandao muhimu hapa ni hakikisha unateka baadhi ya watu maarufu, jifanye kuwa wewe ni shabiki yao tangu ukiwa chekechekea huko Mwakareli. Chukua simu kubwa, simu janja anza kufanya mambo, usikose kwenye matukio ya kijamii kama matamasha ya wasanii na watu mashuhuri.

5. TUMIA KANUNI YA UNYUME NYUME (Use the reverse principle- Rp Laws)
Taikon nakushauri wewe mpenda Umaarufu utumie Rp Laws, hii ni hatua kubwa na muhimu kwa watu wote wapenda umaarufu duniani. Na ili kanuni hii uifanye basi lazima uzingatia kanuni nilizozitaja hapo juu hasa kanuni ya KYC na TYC. Rp laws nimeielezea zaidi katika kitabu changu chenye jina "The Middle Page" Hata kwenye Umaarufu pia Rp laws inatumika tena ndio muhimu zaidi.
Nenda kinyume na jamii yako.

Kwa mfano, kama wewe ni mwanaume, basi vaa sketi au toboa masikio, au suka nywele, au fanya jambo lolote lililokuwa kinyume na Uanaume wako. Na kama ni mwanamke, basi andaa project, mtolee mahari mwanaume ukiwa kwenye jamii yetu ambapo ni kinyume cha jamii yetu.

Mwanamke, tembea ukiwa uchi(nguo zisizositiri) kwani hiyo ni kinyume na jamii, wanawake wanapaswa wajisitiri
Nenda kinyume na jamii yako, hiyo ni sehemu ya kozi za umaarufu.

Kwa Wanaharakati, lazima nawe utumie Rp laws, uende kinyume na jamii yako, mathalan kwenye jamii ni jambo jema kuongea kwa adabu, kukosoa kwa adabu hasa unapomkosoa mtu mkubwa aliyekuzidi umri au cheo, lakini mwanaharakati ili uwe mashuhuri lazima uvunje kanuni hiyo na kwenda kinyume chake, lazima umkosoe vikali tena bila adabu pasipo kuogopa. Hapo lazima uwe maarufu. Sishangai wanaharakati wengi wakiwa hivi walivyo, ndio scripts yao inavyowataka wawe.

Sishangai wasanii wa muziki na bongo fleva wakifanya wanayoyafanya, ndio mambo ya umaarufu hayo, hiyo ni tofauti na kuwa mashuhuri ambapo hauhitaji kufanya upuuzi wa namna hiyo. Usishangae wasanii wakirekodi picha za uchi na kuzirusha mtandaoni alafu wanajifanya ati wanapelekana polisi, huo ni uongo kwani ni mambo wanayoyapanga kwa makusudi kabisa. Jamii yetu, kufanya mapenzi hufanyika kwa siri, lakini watu maarufu hufanya makusudi kuvujisha picha zao kuvunja kanuni ya ufaragha wa tendo la ndoa na kuleta tension kwenye akili za watu.

Niliahidi nitaandika kwa kifupi, ngoja niishie hapa, nafikiri utakuwa umepata kitu. Hata hivyo nashauri, usitake umaarufu, taka Umashuhuri.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa, Mlali, Morogoro
 
Hapo unaongelea umaarufu kama wa dokta Shika au Pierre Liquid...
Dk. Shika alikua mashuhuri ila pierre liquid ndo maarufu.

Turudi kwenye uzi;

Aisee ni kweli bna wasanii wengi siku izi wanapenda huo wa kuitwa umaarufu yaani mtu anakua na team yake ya kumzushia mambo hata kifo anazushiwa na iyo team yake afu mwisho wa siku aje kukanusha kwenye vyombo vya habari. Ati ooh mimi sijafa ni watu tu wasionipenda wananizushia ilhali ni yeye yeye aliejizushia.
 
Dk. Shika alikua mashuhuri ila pierre liquid ndo maarufu.

Turudi kwenye uzi;
Aisee ni kweli bna wasanii wengi siku izi wanapenda huo wa kuitwa umaarufu yaani mtu anakua na team yake ya kumzushia mambo hata kifo anazushiwa na iyo team yake afu mwisho wa siku aje kukanusha kwenye vyombo vya habari. Ati ooh mimi sijafa ni watu tu wasionipenda wananizushia ilhali ni yeye yeye aliejizushia
Huo ndio Umaarufu mzee, kuwa maarufu lazima ujitoe akili kwanza.
 
Back
Top Bottom