SoC02 Mbinu 12 za kulea watoto wanaojiamini (6 za kwanza zitaibua kizazi cha ‘Ma-genius’!)

Stories of Change - 2022 Competition

Uncle Joe

New Member
May 24, 2013
1
4
Sisi sote ni zao la malezi tuliyoyapata kwenye familia na jamii zetu. Wataalamu wengi wa makuzi ya watoto hukubaliana kwamba miaka sita ya kwanza ya malezi ndiyo hujenga haiba, tabia, na kukamilisha ujenzi wa utambulisho wa mtoto! Sisi ambao tumepewa wajibu wa kulea au kuwa na mchango kwenye maisha ya watoto tuna wajibu na fursa kubwa namna gani?!

Makala hii itajikita na umuhimu wa kuwekeza kwenye watoto chini ya miaka sita katika kujenga tabia na mitazamo itakayoibua kizazi kipya kitakacholeta mageuzi makubwa kwenye nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi Tanzania na duniani. Sababu kipaji ni jambo moja, ila kujiamini ni kila kitu kwenye safari ya mafanikio!

1. TUWAACHE WATOTO WAWE WACHUNGUZI (EXPLORERS)

Tujaribu kuwapa fursa nyingi iwezekanavyo watoto wakiwa chini ya uangalizi-- wajifunze kupitia milango yao mitano ya fahamu. Kusikia, kunusa, kugusa, kuonja, na kuona. Kuna mifano ya shughuli chache ambazo watoto wakipewa fursa ya kuzijua wanaweza kupenda kujitolea kuzichunguza kwa kina zaidi mfano:
  • Kazi mbalimbali za mikono kama useremala, kupika, usafi, bustani, kushona, kuchora, kuandika, kuchonga, kushona au kufuma.
  • Mziki: Kuimba, kucheza, kutunga, kupiga gitaa, piano, ngoma, ku-prodyuzi.
  • Kusafiri au kutalii.
  • Michezo: karate, taekwondo, ndondi, kuogelea, sarakasi, soka na riadha.
  • Vitabu: Kusoma, kuandika, kuchora.
  • Kompyuta: Ku-program kompyuta.
  • Kujifunza lugha mbalimbali.
2. UDADISI NA KUPENDA KUJIFUNZA MAMBO MAPYA

Kuna mfano wa Finland ambapo inasemekana kwamba mtoto wa shule ya awali hafundishwi mambo ya taaluma hadi afikishe miaka saba. Shule hutumia muda huu kuwajengea watoto udadisi kwa njia za kutalii mazingira yao, nyimbo, michezo. Karibu kila mradi wa kujifunza umewekwa kwenye mazingira rafiki kwa mtoto nje ya darasa. Wengi wao wafikapo miaka saba huwa tayari wanajua kusoma na kuandika!

Watoto hupenda kujifunza kwa njia ya vitendo, mifano, picha, nyimbo na michezo na hadithi. Zawadi za vitabu na michezo ya kupanua upeo wao ni muhimu sana.

3. WAJENGEWE UTAMADUNI WA KUWAJIBIKA

Mtoto wa miaka mitano anatelekeza vifaa vyake vya kuchezea, mzazi au dada wa kazi na anamkusanyia na kumuhifadhia sehemu inayostahili. Matendo haya yawezaonekana ni kumpenda na kumjali mtoto, lakini ukweli ni kwamba mtoto anapokea ujumbe kwamba hapaswi kuwajibika kwa mambo anayofanya, pia kwamba hakuna madhara ya moja kwa moja kwa matendo yake. Mtoto anafaa kukumbushwa wajibu wake sawa na umri wake.

4. USIMWAMBIE, ‘’UNA AKILI SANA…!’’ SIFIA JUHUDI ZAKE

Badala ya kusifia kipaji chake, tusifie juhudi zake kwenye jambo alilofanya likazaa matunda mazuri. Mwanasaikolojia mashuhuri, Dr. Angela Duckworth, kwenye kitabu chake Grit, anasema kusifia kipaji hudumaza juhudi, sababu mtoto hujenga dhana kwamba hiyo ndiyo asili yake na akapuuza umuhimu wa kufanya bidii. Hivyo mzazi aweke msisitizo kusifia bidii ya mtoto badala ya uwezo wake.

5. TUJIFUNZE KUWASIKILIZA KWA DHATI

Kusikiliza watoto sio moja ya desturi za tamaduni nyingi za Ki-Africa. Sisemi watoto wapewe nguvu za kutawala na kuendesha wazazi. La hasha! Wapewe sikio la kuoneshwa kwamba ajenda zao zinasikika na kueleweka, hata zisipopata ufumbuzi wa ghafla. Mzazi kusoma gazeti, kutazama runinga huku ukisikiliza nusu-nusu huvunja moyo na kuvuruga mawasiliano.

6. KUWAJENGEA UTHUBUTU MAPEMA

Kuwajengea ujasiri wa kuthubutu ni mbinu muhimu sana kwenye mafanikio na maendeleo ya watoto kwenye maeneo yote ya ukuaji wao. Wajibu wako hapa ni kuwatia moyo na kuwapa msaada wanaohitaji kwenye kufanikisha ndoto zao. Unaweza tafuta msaada nje ya uzoefu wako pale inapohitajika. Mfano mtoto anahitahi kujifunza lugha mpya, au ujuzi mpya. Au utampiga marufuku na kutoa vitisho luluki kama wale wazee wetu wa zamani, kwamba aachane na mambo hayo hadi atakapo maliza shule na kujitegemea?

7. TUFIKIRI KUHUSU DHANA YA KUJITOLEA

Mifano ya sehemu tunazowezajitolea ni kama kwenye nyumba za watoto yatima, kwenye jamii zilizopatwa na maafa, maktaba, mashuleni, kwenye taasisi za dini, na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na ya misaada ya kijamii.

Kujitolea huleta furaha, hutengeneza mahusiano ya utu, hujenga kujiheshimu, humfanya mtu anayejitolea awe na moyo wa shukrani. Watoto wapate nafasi nyingi za kujitolea kwenye kazi za mikono, kwa kufanya hivyo kunawapa watoto uzoefu wa kutosha kwenye shughuli mbali-mbali tofauti za kijamii zitakazo waandaa vema kuchagua kazi watazofanya kwa ufanisi.

8. KUFIKIRI IWE TABIA

Mtoto anafaa kuwa na maswali mengi yanayochochea fikra zake na kumwandaa na safari yake ya kujifunza kuhusu dunia. Nani? Lini? Nini? Wapi? Kwa nini? Kwa namna gani? Ni funguo za maarifa mapya anazotakiwa kuzitumia kila mara. Ile kasumba ya kufananisha kufikiri na ‘kupasua kichwa’ ifutiliwe mbali. Fanya kufikiri kuwa jambo la kufurahisha!

Mara kadhaa tafuta kujua mawazo na maoni ya mtoto kuhusu changamoto zinazomzunguka. Lengo ni kuwazoesha kuwa wabunifu na watatuzi wa matatizo ya jamii!

9. AKILI-HISIA NI MWAROBAINI WA SHIDA NYINGI ZA KISAIKOLOJIA (EMOTIONAL INTELLIGENCE)

Wazazi huweka nguvu nyingi kwenye kutafutia familia zao ‘ugali’, mali na elimu. Mwisho wa siku matatizo yatokanayo na hisia na afya ya akili yaliyopuuzwa huibuka au kuripuka na kuleta heka-heka nyingi kwenye familia.

Akili hisia ni kumfundisha mtoto kutambua hisia na kuzijua kwa majina, kujitawala kihisia, kujua namna ya kujihamasisha kufikia malengo hata anapokosa hamasa, kusoma hisia za wengine na kujua namna kuhusiana na wengine kwenye jamii.

10. WAZIISHI NDOTO ZAO MAPEMA (ACHIEVEMENT CULTURE)

Hakuna hisia inayojenga kujiamini kama kufanikisha jambo maishani. Ulipojifunza kuendesha baiskeli, gari, au pikipiki uliongeza kujiamini kwako. Utakapojifunza gitaa, piano na kurusha ndege, kiwango chako cha kujiamini kitapaa kama roketi iendayo mwezini.

Watoto wakiwezeshwa kujifunza na kumudu mambo mbalimbali wanayoyapenda mapema, tutafyatua kizazi chenye vijana wasiozuilika!

11. ELIMU YA KUMILIKI NA KUTAWALA FEDHA

Mbinu zilizotangulia bila wasiwasiakuna zitafanya watoto wetu wavutie pesa nyingi sana popote walipo. Hivyo ni jambo la msingi sana kuwaandaa na maarifa ya msingi kuhusu pesa.

Kwa kiwango chao watahitaji kufunguliwa akaunti ya benki na kumilikishwa. Pia wanapopewa pesa za matumizi wapewe wajibu wa kutoa hesabu au repoti wamezitumiaje.

12. FALSAFA YA HESHIMA NA UTU

Ili tujenge taifa lenye afya bora kabisa na kivutio cha dunia ‘utu’ ni lazima! Ndani yake kuna wema wote. Wanafalsafa wengi wa kale walipofundisha kuhusu utu walitumia sana kanuni hii: ‘’Fanyia wengine vile ambavyo ungependa ufanyiwe’’ au “Usiwafanyie wengine vile ambavyo usingetaka ufanyiwe wewe”. Tutawalea watoto kwa kipimo hiki na kuwakumbusha kuwafanyia wengine mema, sisi tukiwa mifano kwao.

HITIMISHO

Wazazi, walezi hapa nyumbani Tanzania (na hata nje ya mipaka) wote wenye mapenzi mema na watoto wanawezatumia mbinu hizi kusaidia kujenga Tanzania bora kuliko tunayoijua leo. Tanzania ya tuzo luluki za nobeli, Tanzania ya vijana wavumbuzi, wabobevu na wabunifu wa kiwango cha dunia. Taifa ambalo, raia wote wa sayari ya dunia wanatamani kuhamia na kuwekeza humo.

Tuisambazie dunia furaha!





Uncle Joe​

Josephan07@gmail.com

0625762505​

 
Back
Top Bottom