Mbeya: Wanafunzi 1,566 kati ya 56,763 wa Darasa la 4 hawajui kuandika, kusoma na kuhesabu

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,023
1,609
Mkoa wa Mbeya umatajwa kuwa na changamoto ya kufuta ujinga, ambapo wanafunzi 1,566 kati ya 56,763 wa darasa la nne wameripotiwa kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) katika shule za msingi mkoani humo.

Ofisa elimu taaluma Mkoa, Mwalimu Denis Nyoni amesema leo Jumamosi Novemba 26, 2022 kwenye kikao cha tathimini ya taaluma na elimu Mkoa wa Mbeya kwa mwaka 2022.

Amesema kuwa idadi hiyo ya wanafunzi imetokana na tathimini ya mitihani ya majaribio, akisema inakwamisha jitihada za mkoa kufikia malengo ya kufanya vizuri na kushika nafasi ya tatu kitaifa.

“Idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika ni kubwa licha ya jitihada za Serikali kuwekeza katika elimu, huku changamoto ikiwa ni usimamizi usio mzuri kwa wazazi na ukosefu wa mlo shuleni,” amesema.

Aidha ametaja halmashauri vinara kuwa ni Wilaya ya Mbeya, akisema kati ya wanafunzi 11,663 waliofanya mtihani, 644 hawajui kusoma, huku Wilaya ya Mbarali ikiwa na wanafunzi 482 wasiojua kusoma na kuandika kati ya wanafunzi 10,214 waliofanya mtihani.

Ameitaja pia Wilaya ya Chunya aliyosema kati ya watoto 6,608 waliofanya mtihani, 145 hawajui kusoma, huku Kyela ikiwa na watoto 119 wasiojua kusoma na kuandika kati ya wanafunzi 6,786 waliofanya mtihani.

“Hii ni changamoto kubwa katika sekta ya elimu na itakuwa vigumu kwa mkoa kufikia malengo ya kufanya vizuri kitaifa, hivyo ni vyema sasa kujipanga kurekebisha kasoro zilizojitokeza mwaka 2022 na kuanza mikakati 2023,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa elimu Mkoa, Ernest Hinju amewaonya walimu kwa tabia ya kutozingatia masuala ya taaluma na kuwataka kuwa chachu kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.

“Maofisa elimu taaluma angalieni walimu ambao hawazingatii wajibu sehemu zao za kazi na kama kuna mwalimu mkuu ambaye ni kikwazo kwenye sekta ya elimu toeni taarifa lengo ni kuona kiwango cha taaluma kuwa vizuri,” amesema.

Hinju ameomba pia Wakurugenzi wa halmashauri kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri, ikiwa ni pamoja na kuwasimamia maofisa elimu kata katika fuatiliaji wa changamoto katika shule zetu na kusikiliza kero za walimu.

“Nionye tabia za baadhi ya walimu kuepuka tabia za ulevi, kufanya mapenzi na wanafunzi, kwa kweli hilo halitavumilika na tunaendelea na ufuatiliaji.
“Wakuu wa shule toeni taarifa zao sio kuwafumbia macho kwani suala hilo linavunja mwiko wa taaluma,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutoa motisha kwa walimu ili kupanua wigo mpaka wa kitaaluma na kufikia malengo ya Serikali ifikapo 2023.

“Nasisitiza kila halmashauri kutekeleza agizo la Serikali ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kwa ajili ya waliochaguliwa kujiunga mwaka 2023 pamoja na kushirikisha wazazi,” amesema.

Naye Ofisa elimu Kata ya Madibira Wilaya ya Mbarali, Evans Mwamba amesema changamoto kubwa ni uhaba wa walimu hususan katika maeneo ya vijijini kwenye shule shikizi.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom