Mei Mosi 2021 itukumbushe wafanyakazi wa Tanganyika chini ya mkoloni

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,908
30,249
MAY DAY TUWAKUMBUKE WAFANYAKAZI WA TANGANYIKA YA MKOLONI

Toka jana nilikuwa nawaza niandike nini kuhusu May Day na Wafanyakazi.
Ikawa nimekwama.

Siku hizi kuna Kiswahili vijana wanasema, ''mara paa,'' nikaona video ya Paul Makonda anasema kama katika maandamano ya May Day angeona bango la kudai mishahara angewatandika viboko wafanyakazi wale.

Sasa ndiyo na mimi nikapigwa na ile ''paa,'' ikawa nimepata la kuandika.

Babu yangu Salum Abdallah alikuwa mmoja wa viongozi wa wafanyakazi wa Tanganyika wakati wa ukoloni hadi uhuru na hadi vyama huru vya wafanyakazi vilipovunjwa mwaka wa 1964 na kuundwa NUTA.

Babu yangu aliunganisha harakati zake za kutafuta haki ya Mwafrika na mfanyakazi katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Baada ya kuhamia Tabora kutoka Dar es Salaam mwaka wa 1947 kufuatia Loco Shed ya Tanganyika Railways kuhamishiwa Tabora, Salum Abdallah aliongoza mgomo wa Railway wa mwaka huo mgomo ambao uliungwa mkono nchi nzima.

Miaka miwili baadae mwaka wa 1949 aliongoza mgomo mwingine wa Railway na ukafuatia na mwingine mwaka wa 1960 uliodumu siku 82.

Kwa wale ambao wamekuwa wakinisoma historia hii watakuwa wameshakutana nayo mara kadhaa.
Turudi kwa Makonda na tishio lake la kuwapiga viboko wafanyakazi waliobeba bango la kudai nyongeza ya mshahara.

Si kuwa atawapiga viboko wafanyakazi kwa kugoma, la hasha, atawacharaza henzerani kwa kubeba bango la kuomba nyongeza ya mshahara.

Wananchi wa Tanganyika walipigwa viboko hadharani na Wajerumani na kwa ajili ya fedheha hii akina Abdulrauf Songea Mbano maarufu wa jina la Songea Mbano walinyanyua silaha na kupigananae katika Vita Vya Maji Maji (1905 - 1907).

Namkumbuka babu yangu Mwenyekiti Muasisi wa Tanganyika Railways African Union (TANU) mwaka wa 1955 Katibu Kassanga Tumbo.
Viongozi wa wafanyakazi wamepotelea wapi?

Salum Abdallah kasimama, kapanda juu futi sita mrefu na ana sauti kali akihutubia kila mtu anamsikia.
Anawaambia wagomaji waliokaa chini wakimsikiliza, ''Punda nyuma kwama mbele.''

Hapo anapokelewa kwa kibwagizo kama hicho kutoka kwa wafanyakazi waliokusanyika chini ya miembe iliyojaa kila mahali Tabora ya miaka ile ya 1940.

Umbo lake matambo ya Kimanyema miili mikubwa peke yake ilitosha kuwapa wafanyakazi aliokuwa akiwaongoza moyo wa ushujaa wa kupambana na dhulma za Waingereza.

Sikuambii hiyo sauti yake.

Sauti hii iko siku mimi niliisikia lakini ilikuwa miaka mingi sana baada ya harakati za vyama vya wafanyakazi kufa kwa kufutwa vyama vyote huru ikaundwa NUTA chini ya Alfred Tandau.

Siku hiyo nilikuwa nimesimama Mwanza Road mimi na watoto wenzangu tunasubiri Julius Nyerere apite.
Ilikuwa wakati wa likizo nimetoka Dar es Salaam nimekwenda Tabora kwa babu.

Nikasikia nyuma yangu sauti kali inaita jina langu, ''Mohamed Mohamed toka huko wewe huyo humjui? Wewe si unatoka Dar es Salaam?''

Nimegueka kuangalia nyuma babu kasimama katika ''full height,'' yake sura yake imebadilika kwa hamaki.
Taratibu nikatoka katika lile kundi nikaelekea nyumbani na si mbali ilipo barabara.

Ilichukua miaka mingi sana kwangu kufahamu kwa nini babu alihamaki kuona mimi nasimama kumpokea Nyerere Tabora.

Ugomvi wake na Nyerere ulianza miaka ya awali baada ya uhuru kwa Nyerere kutaka kuvunja vyama huru vya wafanyakazi na kuwa na chama kimoja chini ya TANU.

Salum Abdallah alimpinga Nyerere katika hili akidai kuwa vyama huru vya wafanyakazi ni muhimu na alihitimisha kwa kumwambia uso kwa macho, ''Mheshimiwa wewe kuwa serikalini tuache sisi na vyama vyetu utakapokosea tutakurekebisha.''

Hii kauli ndiyo inayosemekana iliyomfanya Nyerere awatie kizuizini viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi baada ya maasi ya Tanganyika Rifles (TR) tarehe 20 Januari 1964 na wakiwa jela akaunda NUTA.

Babu yangu alipopata taarifa kuwa huko Dar es Salaam viongozi wa TRAU akina Abdallah Mwamba na wengine katika TFL kama Paul Pamba walikuwa wamekamatwa, yeye ghafla akapotea akawa haonekani na hakuna aliyejua yuko wapi ila mtu mmoja katika nyumba yake.

Kassanga Tumbo alitorokea Mombasa.
Mwishowe hawa wote walikamatwa na wakawekwa kizuizini.

Siku Salum Abdallah alipotoka mafichoni alikwenda moja kwa moja hadi Kituo Kikuu cha Polisi Tabora.
Alimkuta Mkuu wa Kituo Singasinga akajisalimisha.

Mkuu wa kituo alipomwambia aingie ndani nyuma ya counter ya kituo, Salum Abdallah alitaka kwanza aelezwe kosa lake analokamatiwa.

Mkuu wa Kituo akamwambia kuwa yeye amepewa amri ya kumweka ndani na wapo wenzake tayari keshawakamata.
Hapa ukazuka ubishi mkubwa.

Ilimchoma sana babu yangu hadi anaingia kaburini kuwa juu ya kujitolea kwake kwa hali na mali kupigania haki ya Mwafrika chini ya TANU na TRAU leo jaza yake ni kusakwa na polisi kutupwa gerezani kama mhalifu jambo ambalo hata Gavana Edward Twining hakuthubutu kulifanya.

Lakini yule Mkuu wa Kituo alikuwa mtu anaejua kazi yake vyema.
Alikuwa akimjua babu yangu vizuri sana toka enzi za migomo wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika na akimstahi kama kiongozi.

Hakutaka kutumia nguvu kwani alijua madhara yake yangekuwa makubwa kwani alijua hakuna askari wake yoyote ambae angeweza kukapambana na Salum Abdallah uso kwa uso hata kama wangekuja watatu kujaribu kumkamata.

Yule Singasinga alikaa kitako na babu yangu na wakazungumza kwa kuheshimiana na mwishowe baba yangu alinyanyuka mwenyewe akaingia ndani nyuma ya counter ya kituo na hapo taratibu za kumweka mtu chini ya ulinzi zikafanyika.

Paul Makonda au awae yoyote yule angeweza kweli kumkabili mtu kama Salum Abdallah akamtishia viboko?

PICHA:
Salum Abdallah ni huyo anavishwa mgolole na viongozi wenzake wa TRAU kama ishara ya uongozi wa mapambano dhidi ya wakoloni, kulia wa kwanza ni Kassanga Tumbo.

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom